Na: Elvan Limwagu wa www.limwagu.blogspot.com
Kutokana na tukio la
vifo vya watu waliokunywa Pombe kali ya Gongo hivi karibuni, binafsi
napenda kuwaletea picha chache tu kuonyesha namna pombe hiyo inavyoandaliwa.
Kule kwetu Pombe hii
huitwa kwa jina la NIPA wengine kwa kuipendezesha wakalirefusha jina hilo kuwa "New Internationa Pure Alcohol" na kwa
hakika viongozi wengi waliotokana na makabila ya Wayao na Wamakuwa walisoma
kutokana na ADA
ya mapato ya pombe hiyo kali.
Itakumbukwa kuwa kwa
mara ya kwanza katika kampeni za uchaguzi za mwaka 1995 Mgombea mmoja alidiriki
kuwaahidi wananchi wa makabila hayo kuwa wakimchagua ataruhusu pombe hiyo na
kuiwezesha iwe inaandaliwa kitaalamu, ingawa kura hazikutosha.
Pombe ya Gongo au Nipa
kule kwetu hutokana na Mabibo (tunda la mkorosho) ambalo hukaushwa juani na
hatimaye kuweza kuhifadhiwa hata kwa zaidi ya miezi sita. Mabibo unayoyasikia
yakishakauka hubadilika jina na kuitwa KOCHOKO ambazo inapofika wakati wake (ni
baada ya msimu wa mauzo ya korosho kupita) hupatikana kwa adimu sana na waandaaji wake
huitafuta hata kwa maili zaidi ya 60.
Kochoko hizo baada ya
kuchambuliwa na kuondoa takataka hulowekwa kwa wiki nzima ndani ya pipa au
mtungi (chungu kikubwa) na maji yake yakipata ladha ya juisi inayoweza kulevya
(staili ya mnazi au ulanzi), ndipo huwa tayari kwa kupikwa kama
unavyoona hizo picha.
Vifaa vilivyosababisha
jungu hilo ni:
Mtungi, mtutu uliounganishwa na ngalawa, chungu kidogo cha kufunika mtungi kwa
ajili ya kuzua mvuke usitoke nje, udongo wa mfinyanzi kwa ajili ya kusiliba
maunganisho ya mtungi na chungu na tundu la mtutu kutolea mvuke hadi kwenye
chupa.
Mvuke unaotoka hupozwa
ndani ya mtutu kwa maji baridi na kuwa maji yanayoitwa NIPA (Gongo). Ile Pure
huitwa IPACHO ambayo ni Spiriti kabisa kwa kuwa inawaka wanapoijaribia wenyewe,
ile ya mwisho inaitwa ALEKA ambayo kwa wanaojifunza huweza kuitumia. Ili kupunguza makali ya IPACHO huwa inachanganywa na
ALEKA, hata hapo Konyagi ni cha mtoto.


No comments:
Post a Comment