WAKATI vitendo vya
uhalifu vikizidi kuongezeka sehemu mbalimbali nchini, sasa silaha kutoka nchi
jirani zinadaiwa kuingia kwa wingi na kuuzwa mitaani na baadhi yake
kubadilishwa na mahindi, Mwananchi Jumapili limegundua.
Uchunguzi uliofanywa
unaonyesha kuwa, kutokana na kushamiri kwa biashara hiyo ya silaha nchini,
bunduki moja aina ya Short Machine Gun (SMG) sasa inauzwa kati ya Sh300,000
hadi Sh500,000, huku bunduki aina ya AK 47 ikiuzwa kwa Sh700,000 hadi Sh1
milioni.
Wakati vijiji kadhaa
mkoani Tabora vilipokumbwa na uhaba wa chakula, bunduki aina ya SMG katika
Kijiji cha Usinge wilayani Urambo zilibadilishwa kwa gunia moja la mahindi,
huku AK 47 ilibadilishwa kwa magunia mawili ya mahindi.
Gazeti hili huko nyuma
liliwahi kuripoti kuuzwa kwa bastola holela mitaani katika miji mikubwa ikiwamo
Arusha, Mwanza, Moshi ambapo silaha hiyo ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh800,000 hadi
shilingi milioni moja.
Uchunguzi wa muda mrefu
uliofanywa na Mwananchi Jumapili katika mikoa mbalimbali iliyopo mipakani
umebaini kuwa, mtandao huo wa uingizaji silaha ni mkubwa na unawashirikisha
matajiri na baadhi ya askari polisi wasiokuwa waaminifu.
Silaha hizo huingizwa
nchini kupitia mkoani Kigoma, mpakani mwa Rwanda, Kenya, na Burundi kwa kutumia
njia mbalimbali ikiwamo, magari, pikipiki na boti kupitia Ziwa Victoria pamoja
na baiskeli ambapo bunduki hizo hufungwa kama mzigo ya kawaida.
Chanzo kimoja cha
uhakika kililiambia Mwananchi Jumapili kuwa eneo la Usinge ndiyo kituo kikuu
cha kupokelea silaha kutoka Burundi
na Rwanda
ambazo husambazwa mikoa mbalimbali nchini.
Mawakala
Mmoja wa watu ambao
wamewahi kufanya biashara alisema kuwa mawakala wa silaha hizo wapo katika
mikoa ya Kigoma na Tabora na kwamba ni wafanyabiashara, huku baadhi wakidaiwa
kuwa watu wenye asili ya kabila la Kitutsi.
Lakini kwa Usinge
alimtaja mfanyabiashara mmoja ambaye pia hukopesha fedha kwa riba (jina tunalo)
ambaye inadaiwa kuwa biashara hiyo haramu anayoifanya inajulikana na mamlaka
mbalimbali za juu serikalini.
Habari hizo zilieleza
kuwa mfanyabiashara huyo amekuwa akinunua SMG kati ya Sh300,000 hadi Sh500,000,
na kwamba huzisafirisha kwa kutumia mtandao wake hadi mikoa ya Kanda ya Ziwa na
huziuza kati ya Sh800,000 hadi Sh1,000,000.
Mbali na kutumia silaha
hizo kwa ujambazi pia huzitumia kufanya uwindaji wa tembo kwenye hifadhi za
taifa na mapori ya akiba.
Habari hizo zinaeleza
kuwa baada ya kuyapata meno hayo ya tembo na kukatwa vipande, husafirisha kwa
kusaidiwa na maofisa wa maliasili na askari polisi wasiokuwa waaminifu.
Chanzo: www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment