Huyu Ndie Maggid Mjengwa akiwa ughaibuni nchini Sweden, mjasiri haachi asili..
Na: Maggid Mjngwa,
WATANZANIA tumekumbwa
tena na balaa la ajali kubwa ya meli kuzama. Ni wakati sasa wa kujifunza
kutokana na yaliyotokea huko nyuma.
Maana ajali ya Mv Skagit
inaonekana dhahiri kuchangiwa na uzembe. Na uzembe kwa nchi yetu unalelewa na
mfumo mbovu. Na mfumo mbovu unatokana na Katiba mbovu.
Maana, ni katika
mazingira haya ya kufanya mambo ya hovyohovyo ndipo tunapokuwa na wanasiasa wa hovyohovyo
wenye kuhusika pia na biashara ya uchukuzi na usafirishaji wa abiria.
Ni vigumu kwa mfumo wetu
wa sasa, kwa watendaji wa vyombo au taasisi zisizo huru kikatiba na kisheria
kuweza kuwasimamia wafanyabiashara dhalimu ambao miongoni mwao wamo baadhi ya
wanasiasa wetu.
Tuna lazima sasa kupitia
Katiba yetu ijayo, kuvipa nguvu za kisheria vyombo na taasisi zetu muhimu kwa
nchi yetu. Tuwe na vyombo na taasisi huru ambazo utendaji wake hauwezi
kuingiliwa kirahisi na mamlaka nyingine.
Fikiri leo kama
tungekuwa na utaratibu wa kwamba mmiliki wa chombo cha majini au angani na
atakayebainika kuingiza nchini chombo kilicho chini ya viwango vinavyokubalika
kimataifa na hata chombo hicho kikasababisha ajali ya kuua raia kuwa mmiliki
huyo atafungwa jela na kufilisiwa mali zake? Naamini, tungekuwa na vyombo
madhubuti na ajali zingetokea kwa bahati mbaya kwa maana yake halisi.
Ni nini basi cha
kujifunza kutoka kwenye ajali iliyopita ya Mv Spice Islanders?
Ikumbukwe, Ripoti ya
Tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa Meli ya Mv Spice Islanders ilipendekeza
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari, Mustafa Aboud Jumbe pamoja na wahusika
wengine wachukuliwe hatua za kisheria na kinidhamu kutokana na uzembe
waliofanya na kusababisha kuzama kwa Meli hiyo. Mpaka leo hii hatujasikia
adhabu walizopewa wahusika wa ajali ile.
Maana, bado tunakumbuka
kuwa, ripoti ile ilibainisha kuwa miongoni mwa watu ambao walibainika na makosa
katika ajali ya Mv Spice Islanders ni pamoja na Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Usafiri wa Baharini Zanzibar, Haji Vuai Ussi, Mkuu wa kituo cha usimamizi wa
usalama wa vyombo vya baharini wa Shirika la Bandari, Usawa Khamis Said na
Kaimu Mdhibiti wa Bandari ya Malindi, Sarboko Makarani Sarboko.
Wengine ni pamoja na
Wanahisa wa Kampuni inayomiliki meli hiyo Jaku Hashim Ayub ambaye ni Mwakilishi
na Mbuge wa Jimbo la Muyuni, Salim Said Mohammed, Makame Hasnuu Makame na
Yussuf Suleiman Issa.
Alikuwamo pia nahodha wa
meli Said Abdallah Kinyanyite na wasaidizi wake, Ofisa usafirishaji wa Shirika
la Bandari Hassan Mussa Mwinyi na Mkaguzi wa Meli wa Mamlaka ya Usafiri wa
Baharini, Juma Seif Juma.
Ndiyo, wakati bado
hatuna hakika ya hatua zipi zilichukuliwa dhidi ya wahusika hawa leo
tunaomboleza msiba mwingine kwa taifa.
Hakika, inasikitisha sana , kuwa hata mwaka
haujatimu kukumbuka ajali iliyopita ya Septemba 9, 2011, Watanzania tunapatwa
na msiba mwingine. Na misiba yote miwili inatokana na uzembe na wala si ya
kusingizia ‘Kazi ya Mungu’.
Watanzania sasa tunataka
kuona hatua kali za kisheria na kinidhamu zinachukuliwa, tena kwa haraka dhidi
ya wahusika waliochangia kwenye ajali ile ya Mv Skagit.
Kwa kuanzia jina la
mmiliki wa meli liwekwe hadharani. Na Tume itakayochunguza ajali hii itabaini
kuwa mwenye meli ameingiza chombo chakavu, basi, awe wa kwanza kutolewa mfano.
Maana, kama
taifa, bila kuwa wakali katika haya ya msingi, basi, tunahatarisha usalama wa
taifa letu pia. Kamwe tusiruhusu hilo
kutokea. Nahitimisha.

No comments:
Post a Comment