Nimepokea
mwaliko wa kikao maalumu cha kikao cha fedha na uongozi wa tarehe 3/01/2014
kikao kufanyika tarehe 06/01/2013 saa nane mchana kujadili mapendekezo ya
kuongeza maeneo mapya ya utawala katika Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na ajenda
zingine.
Nimeonelea
tija kuwasilisha mapendekezo yangu kwa maandishi kwa umma na baadae katika
kikao tajwa. Kwa hatua hii, ni fursa kwa kila mwananchi kutoa maoni yake juu ya
haya;
Kwa
ukuaji wa kasi wa Dar es Salaam ambao ndiyo mji mkubwa nchini Tanzania, jiji
kitovu cha biashara na viwanda ambalo kadiri ya takwimu linakadiriwa kuwa na
idadi ya watu milioni nne na nusu. Jiji hili limeshika nafasi ya tatu katika
miji inayokuwa kwa kasi barani Afrika na miongoni mwa miji kumi inayokuwa kwa
kasi duniani.
Ifahamike
pia, Jiji la Dar es Salaam ndilo linashikilia asilimia themanini na tatu (83%)
ya mapato ya serikali kitaifa na takribani asilimia sabini (70%) ya kodi zote
zinazokusanywa nchini Tanzania.
Yafuatayo
ndiyo mapendekezo yangu ya wasilisho la nyaraka ya mapendekezo yaliyoletwa
katika ofisi yangu toka Manispaa ya Kinondoni;
Mosi,
Pendekezo la kutumia “Manispaa” badala ya “Wilaya”:
Kadiri
ya wasilisho, imetumika pendekezo la “wilaya”. Ningeshauri na kupendekeza
kutokana na uhalisia na ukuaji wa kasi kutumika kwa “Manispaa” badala ya wilaya.
Pili,
Pendekezo bora la mgawanyo wa Manispaa:
Katika
wasilisho lenye uwepo wa mapendekezo saba. Ninaungana na kuafiki utumiaji wa
pendekezo la pili lililowasilishwa la kuwa na Manispaa tano (5) ambazo ni;
i.
Manispaa ya Ilala
ii.
Manispaa ya Temeke
iii.
Manispaa ya Kinondoni
iv.
Manispaa ya Kigamboni
v.
Manispaa ya Ubungo
Sababu
muhimu:
1.
Ukubwa kijiografia: Kwa
kuongeza wilaya mbili mpya yaani Manispaa ya Kigamboni na Manispaa ya Ubungo
hii itasaidia wilaya hizi kuweza kuhimili ukubwa wa eneo wa kijiografia ambalo
kwa sasa inaelemea wilaya hizi za sasa yaani Manispaa ya Kinondoni na Manispaa
ya Temeke.
2.
Ukuaji wa kasi wa jiji:
Katika ukuaji wa kasi unaoendelea jiji la Dar es Salaam maeneo yaliyopo katika
wilaya hasa ya Kinondoni na Temeke ndiyo ambayo yanaongoza pia katika ukuaji
huo wa kasi wa kimakazi na shughuli za kiuchumi kama viwanda na uwekezaji.
Hivyo kwa kuwa na Manispaa mpya mbili(Manispaa ya Ubungo na Manispaa ya
Kigamboni) zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kusimamia vyema mipango miji,
kuujenga vyema mji na kusimamia kihuduma.
3.
Uwepo wa mipango ya
kuimarisha ukuaji wa jiji kupitia miji ya pembezoni “satellite cities”:
tayari serikali imeweka dhamira ya kuimarisha ukuaji wa jiji kupitia satellite
cities. Hivyo uwepo wa wilaya mbili yaani Kigamboni (Satellite city
Kigamboni) na Ubungo (“Luguruni Satellite City” ndani ya Kata ya
Kwembe na Kata ya Kibamba) zitamudu kusimamia vyema ujenzi imara wa satellite
cities na pia kuwezesha wilaya zitakazoachwa kama wilaya ya Kinondoni kuwa
na ahueni ya kuelemewa na kazi hivyo nazo kusimamia vyema mipango ya ujenzi wa satellite
cities zilizomo ktk maeneo hayo
Tatu,
Ugawaji wa kata ndani ya Manispaa mpya na kusimamia kata zilizopo:
Katika
mapendekezo yaliyowasilishwa, kumekuwa na mgawanyo mpya unaonyang’anya kata
ambazo tayari zilikwisha kuwapo katika baadhi ya maeneo mathalani ndani ya
Manispaa ya Kinondoni. Mfano wa maeneo kama Kisopwa, Mloganzila. Maeneo
tajwa yamekuwa yakihamishwa toka Manispaa ya Kinondoni na kupelekwa Mkoa wa
Pwani. Hivyo kukizana hata na dhamira ya kujaribu kuchukua baadhi ya kata na
maeneo ambayo yapo katika miji inayokaribia jiji la Dar es Salaam katika
dhamira ya kupanua jiji.
Pia,
kwa nyakati tofauti tumeshuhudia viongozi wa kitaifa wakitaja mara kwa mara
katika hotuba zao na matamko yako maeneo yaliyopo ndani ya Manispaa ya
Kinondoni kama eneo la Mloganzila kuyataja kuwa katika Mkoa wa Pwani. Jambo
hili si sahihi. Jambo hili limekuwa likiacha maswali mengi kwa wananchi.
Ifahamike tu, wananchi hawa wanatambulika chini ya mifumo rasmi tuliyojiwekea
inayowatambua kama wakazi wa Manispaa ya Kinondoni.
Kuna
umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha ufafanuzi mpana unawekwa na kusimamia uwepo
wa maeneo haya yaendelee kuwapo katika wilaya za Dar es Salaam.
Sambamba,
kuna hitaji la haraka na muhimu katika mchakato huu kuhakikisha migogoro ya
ardhi ndani maeneo ya Kisopwa na Mloganzila yapatiwe ufumbuzi wa kudumu. Pia
kuhakikisha maeneo hayo yanabaki katika kata ya Kwembe kwenye Manispaa
inayopendekezwa ya Ubungo.
Nne,
Kujifunza toka miji na nchi zingine:
Kuna
umuhimu mkubwa wa kupanua wigo wa miji na nchi ambazo tunaweza kuchota uzoefu
katika zoezi la kugawa wilaya mpya na kupanua jiji la Dar es Salaam. Mifano
minne kadiri ya wasilisho pekee haitoshi. Napendekeza na kushauri kuongeza miji
iliyopo katika nchi ifuatayo, miji ambayo inashabihiana na sifa za jiji la Dar
es Salaam la ukuaji wa kasi, mifumo wa kiutawala, hali za kiuchumi na
kimaendeleo ;
i.
Lagos-Nigeria
ii.
Johannesburg-South Africa
iii.
London-Uingereza
iv.
New Delhi-India
v.
Shangai, China
Katika
kusoma na kuchukua uzoefu toka katika miji iliyowasilishwa katika pendekezo na
hii mingine, tusiishie kuangalia mifumo ya ugawaji, ukuzwaji na usimamizi bali
pia twende hatua ya kuangalia muundo wa utendaji wa miji hii ambayo yatasaidia
sana katika kuboresha muundo wa kiutendaji wa jiji la Dar es Salaam.
Tano,
Mapendekezo katika Muundo wa Kiutendaji wa Jiji la Dar es Salaam:
Nakubaliana
na hitaji la kuwepo kwa Jiji la Dar es Salaam kama chombo kikuu juu ya Manispaa
zote tano zinazopendekezwa zitakazokuwapo Dar es Salaam.
Pia,
nakubaliana na kuunga mkono hitaji la Meya wa Jiji la Dar es Salaam kuchaguliwa
na wananchi. Hii itatoa fursa katika utendaji na uwajibikaji imara ambayo
unaweza kupimwa na wananchi.
Hivi
ndivyo majiji ambayo yamepiga kasi ya kimaendeleo kama London (Uingereza)
yanajiendesha. Pia hata majirani zetu kama Kenya; nao wametambua mfumo huu na
kuuchukua katika Katiba yao mpya.
Pendekezo
muhimu; kuna haja ya Jiji la Dar es Salaam likawa juu ya manispaa zote tano
zinazopendekezwa na hivyo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa isiwe na mamlaka na nguvu
kulinganisha na Jiji la Dar es Salaam.
Kuna
umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha pia Jiji la Dar es Salaam linapatiwa mamlaka
na madaraka ambayo hayaingiliwi na kuzuiwa na wilaya nyingine zozote zilizopo
chini yake.
Sita,
kuunganisha mapendekezo ya Muundo wa Mkoa wa Dar es Salaam na mchakato wa
Katiba Mpya ya Tanganyika:
Kwa
kutambua nchi ipo katika mchakato wa kuandika katiba mpya ya Tanzania. Mchakato
ambao utatoa fursa ya uandishi wa katiba mpya ya Tanganyika kuna umuhimu mkubwa
wa kuanza kuandaa kisheria hoja za kuwapo ndani ya katiba ya Tanganyika zenye
kusimamia Muundo wa Jiji la Dar es Salaam. Huu ukawa ni mfumo wa mfano “modal”
katika ngazi za jiji zenye kuhitaji kuwapo katika mfumo wa kikatiba. Hii
ikiwamo na suala la Meya wa Jiji kubwa kuchaguliwa na wananchi na mengineyo
muhimu.
Kuna
umuhimu pia wa kuwepo wa hoja ya kikatiba katika upanuzi na ukuaji wa Manispaa
na ngazi nyingine za miji ndani ya Katiba. Hivyo, Katiba ya Tanganyika
inahitaji kuwa nguzo muhimu.
Hitimisho:
Naomba
wananchi wa Jimbo la Ubungo na wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kwa ujumla
kutoa maoni yenu ili hatimaye tupate mfumo bora wa kiutawala kwa maslahi na
ukuaji wa Jiji letu.
Wenu katika utumishi,
John J. Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo
06 Januari, 2013