Sunday, March 31, 2013

Makanisa ya Afrika Kusini yamemuombea rais mstaafu Nelson Mandela ambaye anatibiwa homa ya mapafu, pneumonia.




Bwana Mandela aliishi mtaa wa Soweto, Johanneburg, kwa miaka mingi.Jumamosi msemaji wa rais, Mac Maharaj, alieleza kuwa Bwana Mandela aliweza kuvuta pumzi bila ya shida na amepata nafuu, lakini bado wasi-wasi ungaliko kuhusu kiongozi huyo wa zamani wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 94.
Mkaazi mmoja wa Soweto, Eddie Vilakazi, aliyemuombea Bwana Mandela katika ibada ya Pasaka Jumapili, anasema anatumai mzee huyo ataishi muda mrefu:
"Mandela ni kiongozi wetu.
Tunamuona kuwa mkombozi wetu.
Ni kila kitu kwetu.
Tunamtakia afya njema haraka.
Mungu amuangalie, ambariki kwa sababu tayari ameshabarikiwa.
Lakini tunamtakia maisha marefu zaidi, awe nasi."
chanzo: bbc swahili

Hata Wachina wameshangazwa na aina ya zege lililochanganywa kwenye jengo lililoanguka Dar es Salaam.

 Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa(JKT)wakiwa wamejipanga kupokea miili inayofukuliwa kwenye kifusi cha jengo ghorofa 16 lililoanguka jana.Picha na Fidelis Felix.


Rais Jakaya Kikwete akiwa na baadhi ya viongozi wa Dar es Salaam, wakati alipokwenda kuangalia athari zilizosababishwa na kuanguka kwa jengo hilo juzi.

 Zoezi la kutafuta miili iliyokwama katika vifusi inaendelea, zaidi ya maiti 22 zapatikana.
Dar es Salaam. Idadi ya watu waliokufa kutokana na kufukiwa na kifusi cha jengo la ghorofa 16 lililoporomoka juzi asubuhi jijini Dar es Salaam, imefikia 22.

Habari zilizopatikana kutoka eneo la uokoaji na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova zinaeleza kuwa miili iliyopatikana imepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Jengo hilo lililokuwa likijengwa mkabala na Msikiti wa Shia Ithnasheri ulioko Barabara ya Indira Gandhi na Kampuni ya Lucky Construction Limited liliporomoka saa 2.30 asubuhi wakati mafundi na vibarua wakiendelea na ujenzi huku chini watoto wakicheza mpira na mama lishe wakiendelea na biashara zao kama kawaida.

Rais Kikwete
Rais Jakaya Kikwete ambaye jana pia alifika katika eneo la tukio, kama ilivyokuwa juzi, alipata taarifa fupi ya maendeleo ya uokoaji kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadik na Kamanda Kova.

Baada ya kupewa taarifa hiyo, Rais Kikwete alimwagiza Kamanda Kova kuhakikisha wahusika wanakamatwa akiwamo Mkadiriaji Majengo (Quantity surveyor), mchora ramani za majengo (Architecturer), Mhandisi Mshauri (Consultant) na Mhandisi wa Jiji la Dar es Salaam. Juzi baada ya kutembelea eneo la tukio, Rais Kikwete aliagiza wahusika wote wa ujenzi huo wachukuliwe hatua kali.

Habari zilizopatikana jana zilidai kuwa Diwani wa Kata ya Goba, Wilaya Kinondoni, Ibrahim Kisoka ambaye ndiye mmiliki wa kampuni ya ujenzi, na Mhandisi Mshauri kwa pamoja wamejisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi na hadi saa 8:00 jana mchana walikuwa wakihojiwa.

Awali Kamanda Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa amemtaka mmiliki wa Kampuni ya Lucky Construction Limited ambaye ni Diwani wa Kata ya Goba, Kisoka na wahusika wengine kujisamilisha kituo cha polisi, kabla hawajaamua kutumia nguvu kumtafuta.

Pinda atembelea eneo la tukio
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifika eneo hilo saa 3:41 asubuhi, kujionea hali ilivyo, lakini hakutoa tamko lolote. “Sina la kusema,” alisema Waziri Mkuu alipoulizwa na waandishi wa habari kutoa kauli ya serikali kuhusiana na tukio hilo.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi aliyefuatana na Pinda, alisikika akimwagiza Kamanda Kova kuhakikisha mchora ramani wa jengo hilo naye anatiwa nguvuni kwa kuwa jengo hilo lilikuwa la ghorofa 10, lakini likajengwa hadi 16. Mtu mwingine ambaye anatafutwa na jeshi la polisi kukamatwa ni Mhandisi Mshauri.

Lukuvi alimwagiza Kova kuwa watu waliokuwa karibu na jengo jingine la ghorofa 15 lililojengwa na mkandarasi huyo, kuhama mara moja na ubomoaji ufanyike bila kuleta madhara.

Mwenyekiti wa CUF
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alitumia fursa hiyo kuitaka Serikali kuwabana makandarasi wasio na sifa kwani wanahatarisha maisha ya watu.
“Huu ni uzembe, wahandisi wa jiji walikuwa wapi? Wasimamizi na washauri walikuwa wapi hadi jengo linafikia ghorofa 16?” Alihoji Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba aliitaka Bodi ya Makandarasi (CRB) kufuta leseni ya kampuni hiyo, kwani imeonyesha kuwa haiwezi kusimamia ujenzi na hivyo kusababisha vifo.

Huzuni, vilio na simanzi
Vilio na huzuni viliendelea kutanda jana katika eneo hilo ambapo waokoaji walikuwa wakijitahidi kufukua vifusi na kuzingirwa na watu waliokuwa wakisubiri ndugu zao waliofukiwa na kifusi kutolewa.

Watu wengi tangu asubuhi walikuwa wamesimama karibu na eneo hilo huku wengi nyuso zao zikiwa zimegubikwa na simanzi na wengine wakilia. Mama mmoja aliyekuwa akilia mapema asubuhi katika Mtaa wa Mshihiri, alisema mwanawe ni fundi na jana hakurudi, lakini pamoja na kilio, alisema bado haamini kama mwanawe amepoteza maisha.

Mwingine aliyekuwa ameshikiliwa na wenzake, alisikika akisema miongoni mwa waliopotea ni mume wake aliyemuaga asubuhi kuwa anakwenda kibaruani lakini hadi usiku wa manane hakurudi hivyo ilibidi afike eneo hilo.

Mama mwingine wa jamii ya Kihindu aliyekuwa akilia, alizirai kabla ya kuzinduka baada ya kupatiwa huduma ya kwanza. Mama huyo alisema mtoto wake ni miongoni mwa waliokwama kwenye kifusi hicho.

Barabara zafungwa
Mbali ya watu hao barabara zote zinazoingia katika eneo hilo zimefungwa.
Barabara hizo ni Mshihiri na Morogoro, Hazrat Abbas, Mali -Asia, Mali-Zanaki, Mtaa wa Zanaki, India na Indira Ghandhi.

Wachina walishangaa ‘zege’
Wachina wa Kampuni za ujenzi za China zilizopo nchini, Beijing Construction Engineering Group, BCEG iliyojenga Uwanja wa Taifa, na ile ya China Civil Engineering Construction Company (CCECC) inayojipanga kwa ujenzi wa Daraja la Kigamboni, ni miongoni mwa waliofika kusaidia uokoaji.
Mmoja wa Wachina hao alichukua kipande cha zege kilichotoka kwenye jengo hilo, na kukisaga kwa kutumia mkono, kikapukutika.

“Hii mchanga mingi..., hakuna zege kama hii,” alisema Mchina huyo kutoka Kampuni ya CCECC ambaye hata hivyo alikataa kutaja jina lake.
Wachina hao walitoa kijiko ambacho ndicho kilichosaidia kwa kiasi kikubwa katika uokoaji huo.

Huduma za kijamii
Mashirika mbalimbali ya hisani, yalikuwa na kazi ya kuleta vyakula, maji na vitu vingine kwa waokoaji ili kazi iendelee bila kusimama.

Malori ya Kampuni ya Strabag yanayotumika kwa ujenzi wa Barabara ya Morogoro kwa mabasi yaendayo kasi, yalishiriki kikamilifu saa 24 kuzoa kifusi hicho kilichokuwa kimejaa nondo za kila saizi.

Vikosi vya uokoaji pamoja na manesi wa Hospitali ya Mwananyamala, Hospitali ya Ibrahim Hajj na Chama cha Msalaba mwekundu, wameweka kambi wakiwa na dawa, dripu, na vitu mbalimbali vya huduma ya kwanza.

Matukio mengine
Hii ni mara ya pili kwa mwaka huu jengo kuanguka, kwani Februari jengo la ghorofa nne lilianguka maeneo ya Kijitonyama Mpakani jijini Dar es Salaam na kusababisha kifo cha mtoto wa miaka 9.

Licha ya ujenzi wa jengo hilo kusimamishwa miaka 10 iliyopita, familia ya marehemu iliendelea kuishi katika jengo hilo.

Juni 21, 2008 jengo la ghorofa 10 lilikuwa likiendelea kujengwa na Kampuni ya NK Decorators katika Mtaa wa Mtendeni Kisutu jijini Dar es Salaam liliporomoka na kuua mtu mmoja.

Mwaka 2006 jengo la ghorofa lilianguka eneo la Chang’ombe Village Inn na kuua mtu mmoja, baada ya tukio hilo aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa aliunda tume kuchunguza tukio hilo ambayo ilibaini kuwa zaidi ya maghorofa 100 jijini Dar es Salaam yalikuwa yamejengwa kinyume na taratibu za ujenzi.
Imeandikwa na Ibrahim Bakari, Ibrahim Yamola, Nuzulack Deusen
Chanzo: Gazeti Mwananchi.

Thursday, March 28, 2013

Kifo cha Mbunge wa Chambani chaacha huzuni kubwa, Rais Kikwete atoa ndege ya Rais kusafirishia maiti kuelekea Pemba.


Mbunge wa Chambani (CUF),marehemu Salim Hemed Khamis akiwa amebebwa na baadhi ya wabunge na watumishi wa Bunge baada ya kuanguka ghafla wakati akihudhuria vikao vya kamati za Bunge juzi.Picha na Nuzulack Dausen.  

Mbunge wa Chambani (CUF), Salim Hemed Khamis (60) amefariki dunia jana katika hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa baada ya kuanguka ghafla juzi kwenye Ofisi za Bunge, Dar es Salaam.
Kifo cha mbunge huyo kimewagusa wengi akiwamo Rais Jakaya Kikwete ambaye ametoa ndege yake ili kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Pemba. Ofisi ya Bunge imethibitisha kutokea kwa kifo hicho cha mbunge huyo na kueleza kuwa, alipatwa na ugonjwa wa kiharusi uliosababishwa na ugonjwa wa moyo (Hypertension).

Khamis anatarajiwa kusafirishwa kisha kuzikwa leo kijijini kwao Chambani, Pemba baada ya jitihada za kumsafirisha jana kushindikana na wabunge wengi kuomba kushiriki kumuaga.
Mbunge huyo atasafirishwa leo saa tatu asubuhi baada ya shughuli ya kuaga itakayofanyika kwenye Viwanja vya Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Anne Makinda ametangaza kusitishwa kwa shughuli zote za Kamati za Bunge hadi Jumanne Aprili 2, kutokana na msiba huo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Makinda alisema: “Ninatoa pole kwa familia ya marehemu, wananchi wa Chambani, Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, wabunge wote na Watanzania wote kwa jumla”.

Khamis alianguka juzi saa 10.50 asubuhi wakati akishiriki kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kilichofanyika katika ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam.

Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema wamepokea taarifa za kifo hicho kwa masikitiko ambacho kilisababishwa na kupasuka kwa mshipa wa damu kichwani.

“Tumeelezwa na daktari kuwa Mbunge Salim amefariki kutokana na kupasuka kwa mishipa ya damu ambayo ilimiminikia kwenye ubongo wake na kuenea kichwani,” alisema Joel. Alisema kutokana na hali hiyo shughuli zote za uchambuzi wa bajeti zilizokuwa zikifanywa na kamati za Bunge, zimeahirishwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo hadi tutakapomaliza shughuli za mazishi.

Joel alisema kwa upande wa Bunge, shughuli za msiba zitaongozwa na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ambayo marehemu alikuwa mjumbe.

Alisema Bunge linamshukuru Rais Kikwete kwa kutoa ndege yake kwa ajili ya kupeleka mwili huo Pemba na kwamba hatua hiyo itatoa fursa kwa wabunge wengi kushiriki mazishi.
Alisema kutokana na hali hiyo wabunge 12 wakiongozwa na Lowassa watakwenda kushiriki kwenye msiba.

Wabunge, CUF waomboleza
Baadhi ya wabunge jana walionekana kuchanganyikiwa baada ya kupata taarifa za msiba huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema kuwa kifo hicho ni cha ghafla kwa sababu Salim alikuwa kwenye vikao vya Bunge tangu walipoanza vikao vya kamati.

“Tangu tuanze vikao vya kamati tulikuwa naye na alionekana kuwa mwenye afya, kwangu mimi ni pigo nimepata kwa sababu alikuwa mwalimu kisiasa katika Chama cha CUF,” alisema Rajab Mohamed Khamis, ambaye ni Mbunge wa Ole (CUF).

Kwa upande wake, Mbunge wa Peramiho CCM, Jenister Mhagama alishtuka na kuonekana kutoamini taarifa hizo, jambo ambalo lilimfanya ashindwe kuzungumza chochote.
Wabunge wengi walionekana wakihaha kutafuta usafiri ili wawezekwenda Muhimbili huku baadhi yao wakienda kujiandaa na safari ya kwenda Pemba.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema chama chake kimepata pigo kubwa kutokana na kifo cha Mbunge, ambaye amemwelezea kwamba alikuwa nguzo muhimu kwa chama hicho.

Mtatiro alisema marehemu alikuwa na mchango mkubwa kwa chama chake kutokana na shughuli mbalimbali alizokuwa akizifanya katika chama hicho.

Alisema kuwa marehemu ndiyo alikuwa Mnadhimu Mkuu wa Wabunge wa CUF, pia alikuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho kuanzia mwaka 2010 hadi 2012.
“Pia alikuwa anatusaidia sana wakati tukiwa na migogoro kwani kutokana na busara zake alikuwa anaheshimika sana,” aliongeza Mtatiro.

Kuumwa kwake
Alianza kujisikia vibaya akiwa kwenye kikao cha kamati juzi na alianguka hivyo wabunge wenzake kwa kushirikiana na Ofisi ya Bunge walimchukua na kumpeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu.

Alilazwa kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu, hadi alipokutwa na mauti jana.

Miezi mitatu iliyopita alikuwa nchini India katika Hospitali ya Apollo kwa ajili ya matibabu na alirejea nchini na kuendelea kushiriki shughuli za Bunge na za chama chake.

Hoja ya mwisho kuchangia katika vikao vya kamati ni ile ya Machi 26, mwaka huu, pale alipoukosoa Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) kwa kushindwa kutoa taarifa za kweli kuhusu rushwa kwenye taasisi nyeti zikiwemo polisi, magereza na hospitali.

Rekodi Bungeni
Khamis aliingia bungeni kwa mara ya kwanza 2005 na kuchaguliwa tena 2010. Katika Bunge la 10 aliuliza maswali ya msingi matano, ya nyongeza saba na alichangia hoja mbalimbali mara 18.

Historia yake
Mbunge huyo, ambaye alizaliwa mwaka 1952, alisoma Shule ya Msingi Pandani kati ya 1959 na 1960 na kumalizia katika Shule ya Msingi Kengeja kati ya 1960 na 1967.
Elimu ya sekondari aliipata kati ya 1968 mpaka 1969 katika Shule ya Chambani na kuhamia Shule ya Fidel Castro aliposoma kati ya 1970 mpaka 1971. Kati ya 1972 hadi 1973 alikuwa katika Chuo cha Lumumba kwa shahada yake ya kwanza ya Kilimo.

Alisoma shahada yake ya uzamili katika Chuo cha Commonwealth Mycological cha Uingereza kati ya 1988 hadi 1989.

Kabla ya kuwa mbunge alifanya kazi sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa Mwalimu kati ya 1974 mpaka 1978, huku 1984 mpaka 1996 akifanya kazi katika Kampuni ya Mohamed Sugar.

1997 alijiunga na Kampuni ya SAS Ltd alipofanya kazi mpaka 2001 kabla ya kupata Ubunge 2005 hadi mauti ulipomkuta.
Salim ni mbunge wa kwanza kufariki kwa mwaka huu, ingawa katika Bunge hili anakuwa Mbunge wa nne.

Wabunge wengine waliofariki ni Mussa Khamisi Silima wa Zanzibar, Mbunge wa Viti Maalumu wa Chadema Regia Mtema pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Jeremia Sumari.

Chanzo: Gazeti Mwananchi.



Waziri Kigoda azomewa Mtwara...


Kigoda na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba, walikutwa na kadhia hiyo walipokuwa wakihutubia wananchi wa Mtwara katika Uwanja wa Umoja.

Mawaziri hao pamoja na Balozi wa Nigeria Nchini, Nshaya Manjabu walikuwa mkoani Mtwara kwa ajili ya makabidhiano ya vifaa vya ujenzi wa kiwanda cha saruji kinachotarajiwa kutumia malighafi ya gesi asilia.

Itakumbukwa kuwa Januari 30, mwaka huu Waziri Mkuu Mizengo Pinda alituliza jazba za wakazi wa Mkoa wa Mtwara baada ya kueleza jinsi watakavyonufaika na gesi itakayozalishwa mkoani humo kabla ya kusafirishwa kwa bomba hadi Dar es Salaam.

Katika mkutano wa majumuisho, Pinda alisema gesi ghafi haitosafirishwa kwa njia ya bomba na kwamba kiwanda cha kusindika gesi kitajengwa mkoani humo ili mabaki yatumike kama malighafi ya viwanda.

Hata hivyo, jana ilionekana kama wakazi hao wamekwishasahau mipango waliyoelezwa na Pinda, hivyo kusababisha kadhia hiyo kwa RC na mawaziri katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Mashujaa.

Mkutano huo ulitanguliwa na hafla ya Dk Tizeba kumkabidhi Dk Kigoda makontena 38 yenye vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kuanza rasmi ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Dangote pamoja na magari ya kubebea mizigo.

Halfa hiyo ambayo ilifanyika kwenye Bandari ya Mtwara pia ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Dangote, Deva Kumar. Ujumbe huo pia ulitembelea Kijiji cha Msijute, Kata ya Namayanga kitakapojengwa kiwanda cha Dangote, kisha kuzungumza na wanakijiji.
Viwanja vya Mashujaa.

Mkuu wa Mkoa, Simbakalia ndiye aliyefungua pazia la kuzomewa baada ya kupanda jukwaani kwa lengo la kutoa utangulizi wa ziara hiyo. Wananchi walianza kutawanyika na kwenda kusimama mbali na eneo la mkutano huku wakipaza sauti: “hatukutaki…haitoki.”

Hata pale alipojaribu kusema; “Mtwara oyee” alijibiwa, “Haitokiii” na wengine wakisema: “hatukutakii...” hali iliyompa ugumu kiongozi huyo kuendelea na hotuba yake.

Kuona hawezi tena kuendelea, alimkaribisha Dk Tizeba ambaye naye alikutana na kadhia hiyo, kwani alipoanza kusalimia wakazi wa Mtwara, alipokewa kwa majibu “haitoki...”. Baada ya majibu hayo, akasema “Mtwara oyeee”,ndipo kukaibuka kikundi cha wananchi waliokuwa wakiimba “Haitokiii…Haitokiii…Haitokiii”

Zomea zomea hiyo iliyoambatana na mabango yenye ujumbe wa kupinga mradi wa kusafirisha gesi, ulisababisha kukosekana kwa utulivu wakati wote wa hotuba yake.
Pamoja na kelele za wananchi hao, hakukupoteza mwelekeo kwani aliendelea kuwaeleza wananchi kwamba hivi sasa Serikali inaendelea kuboresha barabara zinazoingia mkoani humo ili bandari iweze kufanya kazi vizuri.

Dk Tizeba alisoma moja ya mabango lililoandikwa “Gesi ndiyo roho yetu Wanamtwara” na alionyesha kuunga mkono madai ya wananchi ya kutaka kufaidika na rasilimali hiyo. Hata hivyo alijibiwa “siasa hizoo...hatutakiii”
Dk Tizeba alisema tayari wawekezaji 12 wameomba kuwekeza katika Bandari ya Mtwara na kutoa wito kwa wengine wenye nia ya kufanya hivyo kujitokeza.

Dk Kigoda kwa upande wake lipopanda jukwaani mambo yakawa kama ilivyo kwa watanguzi wake, hali iliyomlazimu kuongea kwa muda mfupi kutokana na kukosekana kwa utulivu.

“Madai ya wananchi wa Mtwara ni ya msingi sana, wanataka kufaidika na rasilimali inayotoka katika eneo lao… Serikali tumeamua kushawishi wawekezaji kujenga viwanda Mtwara ili wananchi wafaidike…lakini suala la kuzuia gesi kwenda Dar es Salaam siyo sahihi kwa sababu gesi ipo nyingi,” alisema Kigoda huku wananchi wakimpinga hali iliyomlazimu kukatisha hotuba yake.

Imeandikwa na Abdallah Bakari, Mary Sanyiwa na Haika Kimaro
Chanzo: Mwananchi.
; ma4 � -

Marehemu Khamis kuzikwa kesho Pemba.


MAZISHI ya aliyekuwa Mbunge wa CUF, Jimbo la Chambani Pemba kisiwani Zanzibar, Marehemu,  Salim Hemed Khamis, yanatarajiwa kufanyika kesho mchana mjini Pemba.

Taarifa za awali kutoka Chama cha Wananchi (CUF), zinasema Mwili wa Marehemu, Khamis utaagwa kesho asubuhi kuanzia majira ya saa 2:30-4:00  katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam ambapo Viongozi mbalimbali wa kitaifa na Kimataifa pamoja na wananchi na Wanachama wa CUF watapata fursa ya kutoa heshima za mwisho kwa Marehemu.

Taarifa hiyo ya Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julis Mtatiro inasema kuwa Msafara utaondoka Karimjee saa 4:00 kuelekea uwaja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo Msafara wa Ndege 2 utaondoka kwenda Pemba.

Saa saba mchana mazishi yatafanyika huko Pemba na maazishi hayo yataongozwa na Viongozi wa serikali, Chama cha CUF na Wabunge.

Mtatiro amewaomba wanachama na wafuasi wa CUF jijini Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kuuaga mwili wa Mbunge huyo aliyefikwa na umauti akiwa kazini katika vikao vya Kamati za Bunge, ambapo Marehemu alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
 Chanzo: FK blogspot.com

Wednesday, March 27, 2013

Mwanafunzi wa kitanzania Afariki Airport ya China akirudi nchini.


Dar es Salaam. Mwanafunzi wa Kitanzania aliyekuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Huazhong nchini China, Leonard Peter Tambalu amefariki dunia ghafla katika mazingira ya kutatanisha wakati akiwa anajiandaa kurejea  nchini.
Tambalu aliyekuwa mwaka wa pili katika chuo hicho kilichopo kwenye mji wa Wuhan, alifikwa na mauti hayo Machi 17 mwaka huu wakati akiwa katika Uwanja wa Ndege mjini Beijing. Marehemu alikuwa Ofisa Kilimo Mwandamizi kutoka wilayani Iramba mkoani Singida.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Christina Midelo hakukubali wala kukanusha kuwapo kwa tukio hilo. “Sina taarifa za kifo cha kijana huyo, wanaoweza kuzungumza ni Ubalozi wa China kwa kuwa ndio waliokuwa wakimsomesha.”
Balozi wa Tanzania nchini China, Philip Marmo, ambaye yupo nchini kutokana na ushiriki wake katika mapokezi ya Rais wa China,  Xi Jinping, alikiri kufahamu suala hilo. Katibu wa Umoja wa Wanafunzi wanaosoma vyuo mbalimbali katika mji wa Wuhan (Wtasa), Humphrey Sikauki, alithibitisha kifo cha Tambalu na kwamba mwili wake ulikuwa unafanyiwa uchunguzi na maofisa wa serikali ya China wakishirikiana na wale wa Tanzania.
“Tangu alipofariki madaktari walisema ripoti ingetolewa baada ya siku saba ambazo ziliisha Jumatatu, mpaka sasa hiyo ripoti hatujaipata lakini Mwambata wa Elimu katika Ubalozi wa Tanzania nadhani atakuwa ameipata kwa sababu ndiye alikuwa akiiwakilisha Tanzania katika uchunguzi huo,” alisema Sikauki.
Gazeti hili lilijaribu mara kadhaa kuwasiliana na Mwambata wa Elimu katika Ubalozi wa Tanzania nchini China, George Manongi lakini  mawasiliano yalikuwa magumu, kutokana kushindwa kusikilizana.
Kifo cha Tambalu
Tambulu ambaye alifika China Septemba  2011 kwa ajili ya masomo yake ya fani ya Kilimo, alifariki dunia akiwa katika Hospitali ya Chinese -Japanese Friendship.
Habari zaidi zinaeleza kuwa, baada ya kufika Uwanja wa Ndege wa Beijing alianguka, kabla ya kupelekwa hospitalini, ambako ilibainika kwamba alikuwa amekwishafariki.
Chanzo chetu kilidokeza kuwa, uongozi wa hospitali ulitoa siku saba za uchunguzi kabla ya kutoa mwili wa marehemu, lakini tatizo kubwa limekuwa ni uwezo wa kuusafirisha mwili huo.
Habari zinasema Wizara ya Kilimo haiwezi kuwajibika moja kwa moja kuusafirisha mwili wa marehemu isipokuwa  halmashauri yake.
Marmo kwa upande wake alisema ni vigumu kwa Serikali kusafirisha mwili huo kwani haina bajeti ya masuala hayo na kwamba yeye atachangia kama Watanzania wengine.
Habari zaidi zinasema Serikali ya China imekataa kumsafirisha marehemu kutokana na kifo hicho kutokuwa cha kawaida (natural death).
“Manongi aliwaambia ndugu wa marehemu Tanzania kuwa kampuni aliyowasiliana nayo inaweza kusafirisha mwili huo kwa Dola za Marekani 40,000 au 45,000,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kinapasha pia kuwa,  Mwambata huyo aliwasiliana na mwajiri wa marehemu (Wizara ya Kilimo) kuhusu kumsafirisha na mwajiri akakataa kwa sababu marehemu alikuwa mikononi mwa Serikali ya China.
“Alitaka ndugu wawajibike kuusafirisha mwili hadi nyumbani kwao Shinyanga kwa mazishi,”kilisema.
Chanzo hicho kinaeleza kuwa, Mwambata pia aliwaeleza ndugu kuwa chuo alichokuwa akisoma kilisema hakiwezi kuusafirisha mwili kutokana na ukubwa wa gharama lakini kinaweza kuuchoma na kusafirisha majivu.
Gazeti hili liliwasiliana na Mwambata huyo, lakini alipokuwa akipokea simu yake  na mwandishi anamsikia lakini kwa upande wake alikuwa hasikii hivyo kuitika tu “haloo, haloo…”
Alipotumia ujumbe mfupi wa maneno, alijibu kuwa simu yake imeshindwa kuutambua ujumbe huo kwani maandishi yalikuwa hayasomeki.
Chanzo: Mwananchi.

</

UJUMBE WA FIFA KUSIKILIZA WAGOMBEA TFF APRILI 16




SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambalo lilisimamisha mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na baadhi ya wagombea kulalamika kuenguliwa sasa litatuma ujumbe wake nchini katikati ya mwezi ujao.

Ujumbe huo ambao moja ya shughuli zake kuwasikiliza wote walioenguliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na hawakuridhika na uamuzi huo, utakuwepo nchini Aprili 16 na 17 mwaka huu.

Kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, kazi ya ujumbe huo ni kubaini tatizo lililopo na kutoa ripoti kwa mamlaka zinazohusika ndani ya FIFA kwa ajili ya kutoa mwongozo.

Ujumbe huo utakutana na pande mbalimbali zinazohusika wakiwemo wagombea, kamati za uchaguzi za TFF. Lakini pia ujumbe huo unatarajia kumtembelea Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara pamoja na watendaji wake wizarani.

Uchaguzi wa viongozi wa TFF ulikuwa ufanyike Februari 24 mwaka huu, lakini ukasimamishwa na FIFA baada ya baadhi ya wagombea walioenguliwa kulalamika kuwa hawakutendewa haki na wangependa shirikisho hilo liingilie kati.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Mahakama ya rufaa nchini Misri, imeamuru kiongozi mkuu wa mashtaka aliyefutwa kazi na rais Mohammed Morsi kurejeshwa kazini mwezi Novemba.



 27 Machi, 2013 - Saa 14:08 GMT
·                              

Mahakama hiyo imefutilia mbali uamuzi wa rais Mosri kumteua mwendesha mkuu wa mashtaka mwingine Talat Ibrahim.
Hatua ya Bwana Morsi kumfuta kazi Abdel Maguid Mahmoud, iliwaudhi sana majaji wakuu walioina kama hatua ya kuhujumu mamlaka yao.
Hii ilikuwa hatua ya kwanza kama hii kutokea baada ya rais Mosri kujiongeza mamlaka makubwa.
Hatua ya rais Morsi iliindolea idara ya mahakama mamlaka yake ya kuweza kubatilisha uamuzi wowote tatanishi alioutoa . Lakini rais Morsi baadaye alibatilisha uamuzi wake baada ya maandamano makubwa kumpinga.
Kiongozi wa mashtaka wa sasa bwana Mahmoud, aliteuliwa na rais wa zamani Hosni Mubarak.
Aidha Talaat Ibrahim naye alitakiwa kudurusu uchunguzi kuhusu vifo vya waandamanaji waliopinga serikali ya Mubarak.
Afisaa mkuu wa serikali aliambia BBC kuwa serikali itakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya juu zaidi nchini Misri.
Bwana Morsi amekabiliwa na matatizo chungu nzima tangu kuchukua mamlaka mwezi Juni mwaka 2012 baada ya uchaguzi wa kwanza kufanyika tangu kuondolewa mamlakani kwa Mubarak.
 Chanzo: BBC Swahili.

Dereva aliemgonga Traffic Bamaga huyu hapa...



Dereva Jackson Simbo (43), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, kujibu shtaka la kusababisha kifo cha askari wa Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani, Elikiza  Nnko.
Mshtakiwa huyo, alifikishwa mahakamani jana.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Ladislous  Komanya, alidai kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo Machi 18 mwaka huu, katika  eneo la Bamaga, Barabara ya Bagamoyo.
Wakili Komanya alidai kuwa  pamoja na shtaka  hilo, mshtakiwa  pia anakabiliwa na shtaka la kuingilia msafara wa kiongozi, kinyume na sheria. Wakili alidai kuwa akiwa katika sehemu hiyo ya  Bamaga, mshtakiwa  aliingilia msafara wa kiongozi na kushindwa kuheshimu maelekezo yaliyokuwa yakitolewa kwa ishara na askari huyo.
Komanya  aliendelea kudai,  Simbo pia anakabiliwa na  shtaka la  shindwa kutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi hadi alipo tafutwa na vyombo vya dola.
Hata Hivyo kwa upande wake, mshtakiwa alikana tuhuma dhidi yake na Hakimu  Kwey  Lusemwa aliahirisha kesi hiyo hadi  Aprili 15, mwaka huu.
Mshtakiwa yuko nje kwa dhamana baada ya wakili wake Edward  Chuwa, kuomba  mteja wake adhaminiwe kwa kuwa  ametimiza masharti ya dhamana.
Chanzo: Gazeti Mwananchi.

Kitabu cha 'Kifo ni haki yangu' cha Eric Shigongo chazinduliwa leo rasmi.

Mtunzi mashuhuri wa vitabu kutoka kampuni ya Mkuki na Nyota, Mzee Walter Bgoya, akikata utepe pamoja na mtunzi wa kitabu cha ‘Kifo ni Haki Yangu’, Eric James Shigongo (kulia) wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho uliofanyika katika duka la vitabu la Tanzania Publishing House lililopo mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam.

 Wapenzi wa vitabu vya Eric Shigongo wakipitia kitabu cha 'Kifo ni Haki yangu' wakati wa uzinduzi wake leo, pembeni mtunzi wa kitabu hicho akiwa anawatazama wasomaji wake walio pembeni namna wanavyofurahia matunda ya kazi yake.

Eric shigongo akiweka saini katika kitabu chake kipya 'Kifo ni Haki yangu' wakati wa uzinduzi leo.

Chanzo: Mjengwa website.

Rais afunga rasmi mafunzo ya JKT kwa wabunge na wananchi wengine.

Mbunge wa viti maalum (CCM) Ester Bulaya akipokea cheti cha kuhitimu mafunzo hayo jana kutoka kwa amiri jeshi mkuu Rais Jakaya Kikwete katika kambi ya Ruvu mkoa wa pwani.

Halima Mdee mbunge wa Kawe (Chadema, wa kwanza kushoto )akiwa na Mbunge wa viti maalum (CCM) Ester Bulaya (wa pili kutoka kushoto) wakati wakila kiapo cha utii baada ya kuhitimu mafunzo ya jeshi na ukakamavu kambi ya Ruvu.

Wabunge wengine waliohitimu katika kambi hiyo ni Neema Hamid, David Silinde, Murtadha Mangungu, Livingston Lusinde, Yusuph Khamis, Said Mtanda na Mendrad kigola.

Chanzo: Mjengwa website.

Tuesday, March 26, 2013

Vyama vya ndondi vyamcheka Cheka




Na Hafidh Kido

VYAMA vinavyosimamia ndondi za kulipwa nchini, katika hali isiyokuwa ya kawaida, vinamcheka bondia Francis Cheka badala ya kumsikitikia kwa hujuma anazodai alifanyiwa nchini Ujerumani hivi karibuni.

Wakizungumza na kidojembe kwa nyakati tofauti, viongozi wa vyama vya PST na TPBO wameeleza ya kuwa hawashangai kusikia Cheka alihujumiwa na Promota wa Kenya, Thomas Mutua aliyekwenda naye Ujerumani  kucheza pambano la kusaka ubingwa wa Shirikisho la Ndondi la Kimataifa (IBF).

Katika pambano hilo Cheka anadai ya kuwa Promota huyo aliyekuwa kwenye kona yake kama kocha , alitupa taulo ulingoni kuashiria mwamuzi asimamishe pambano kumwokoa ilhali alikuwa yuko ‘fiti’kuendelea kupambana na Mjerumani, Uensal Arik aliyekuwa akichuana naye. Hiyo ilikuwa kwenye raundi ya saba.

“Hii si mara ya kwanza kupata malalamiko yanayomuhusu huyu ‘promota’ Thomas Mutua kutoka Kenya kuwahujumu mabondia wa Tanzania. Tulishakubaliana tusimpe kibali cha kuondoka na mabondia wetu, mimi nashangaa sana amepata wapi kibali cha kuondoka na Cheka,” alisema Emmannuel Mlundwa, muasisi wa ndondi hizo nchini anayekiongoza chama cha PST.

kidojembe ilipowasiliana na Yassin Abdallah ‘Ustadh’ Rais wa chama kingine cha ndondi za kulipwa cha TPBO naye aliungana na Mlundwa kwa kuondoka  na mtu ambaye hana baraka zozote nchini.

“Muulize Cheka aliondoka kwa kibali cha nani. Kama aliondoka kienyeji hatuhusiki. Cheka ameondoka bila kufuata kanuni za ngumi hivyo hana msaada. Katiba ya Tanzania inaruhusu mtu kusafiri popote anapotaka kama amefuata katiba ya nchi ni sawa alikuwa na haki kuenda Ujerumani lakini kwa mujibu wa kanuni za ngumi amefeli, na hili litakuwa funzo kwa mabondia wote wanaofuata mapromota kutoka Kenya,” alisema Yassin.

Cheka mwenyewe, Francis Cheka ‘SMG’ ambaye ni bingwa wa IBF Afrika uzani wa Super Middle, alikiri kutopewa ushirikiano na chama chochote cha ngumi za kulipwa Tanzania kwa ajili ya safari yake ya Ujerumani ingawa alidai kutoa taarifa kwa Rais wa kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBC), Onesmo Ngowi.

“Nilizungumza na Ngowi kuhusiana na hujuma nilizofanyiwa lakini naye aliniambia hili litakuwa funzo kwangu, simuelewi kwa kweli,” alisema.

Kuhusu ni nini hasa kilichotokea, Cheka anasema kwamba aliombwa kupokea rushwa ili apoteze pambano hilo lakini akakataa.  “Ndugu yangu nilifuatwa hotelini mara tano wakitaka niuze pambano kwa Euro 6,000 nikakataa,” alisema Cheka.

“Nadhani baada ya kuona nimekuwa mbishi, walimfuata Mutua pamoja na mwamuzi, maana taulo lilirushwa na Mutua kutoka kona yangu, nilikuwa fiti na yule jamaa alishaanguka mara moja. Nashangaa kwanini mwamuzi alikubali kumaliza pambano,” aliongeza.

Cheka alisema ya kuwa mpaka sasa hajalipwa pesa zake zote. “Mkataba unasema nilipwe (Euro 11,000), lakini mpaka sasa nimelipwa Euro 4,500.

Kuhusu vyama vya ndondi za kulipwa nchini, Cheka  aliviponda. “Mimi naona kama vya kinafiki tu hasa chama cha ‘Ustadh’ (TPBO),” alisema bila kufafanua ni kwa nini hicho ndicho anachokiponda zaidi.

kidojembe ilipowasiliana na Mutua kwa njia ya simu kutoka Nairobi  alisema aliamua kutupa taulo ulingoni kumuokoa Cheka baada ya kumuona amepatwa na tatizo.

“Niliamua kurusha taulo kwa sababu niliona bondia wangu ameumia mkono wa kulia hivyo sioni kama kuna tatizo lolote kufanya hivyo kwani ni kitu cha kawaida sana kumsaidia bondia anapozidiwa,” alisema Mutua anayedai pia kwamba alipata kibali cha kumchukua nchini kutoka kwa Ngowi.

Kuhusu Cheka kufuatwa mara tano kutakiwa auze pambano, Mutua alisema hajaambiwa kitu kama hicho na bondia wake kwani ikiwa alifuatwa basi mtu wa kwanza kujua ilipasa kuwa ni yeye lakini hajui chochote na kuongeza kuwa mabondia wengi wa Tanzania wanapenda kupotosha umma wanaposhindwa.

“Kitu ambacho hatujamalizana na Cheka ni pesa zake mkataba unasema anatakiwa kulipwa Euro 11,000 lakini mpaka sasa amelipwa Euro 5,500 na sababu kubwa ni matatizo ambayo yalitokea bana yetu na promota Eva Arole ambaye aliandaa pambano lile lakini mpaka sasa tunajitahidi kuwasiliana naye kuhakikisha pesa hizo zinatumwa,” alisema Mutua.

kidojembe ilijaribu kuwasiliana na Onesmo Ngowi, ili kupata ukweli kuhusu yeye kutoa kibali kwa Mutua kumchukua Cheka  lakini simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa.

Mwandishi alituma ujumbe kwenye simu uliomtaka kutoa ufafanuzi juu ya chama chake kuhusika kutoa ama  kutotoa kibali kwa Cheka lakini hakujibu ujumbe huo ingawa ulionyesha kumfikia.

 kidojembe@gmail.com
Dar es Salaam, Tanzania
26 March, 2013

Tanzania yawa nchi ya kwanza Afrika kutembelewa na Rais mpya wa China Xi Jinping.


Rais Xi Jinping wa China ameahidi kuendelea kuipiga jeki Afrika ili kukabiliana na changamoto za kimaendeleo, huku akisema kuwa suala la utoaji misaada yenye masharti magumu siyo ajenda ya Serikali yake.

Jinping akitumia jukwaa la Tanzania kutambulisha sera yake kwa nchi za Afrika alisema kwamba bara hilo limepiga hatua kubwa kimaendeleo na kwamba nchi yake itaimarisha uhusiano uliopo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Alisisitiza kwamba ushirikiano wenye tija ni ule unaozingatia “majadiliano na maridhiano” na kwamba Serikali yake imetenga kiasi cha Dola za Marekani 20 bilioni kufadhilia miradi mbalimbali ya maendeleo Afrika.

China haitakuwa tayari kutoa masharti kwa taifa lolote… Tunataka kutoa fursa zinazofanana,” alisema Rais, ambaye alishika rasmi wadhifa huo Machi 14, mwaka huu.
Alisema China haitaingilia masuala ya ndani ya nchi, huku akisisitiza kwamba shabaha ya nchi yake ni kuendelea kupalilia ushirikiano mwema uliodumu kwa miongo kadhaa na siyo kujihusisha na migogoro.

Baadhi ya wachunguzi wa mambo wanadai kuwa, kauli ya kiongozi hiyo ni kama ujumbe wa onyo kwa baadhi ya nchi za Magharibi ambazo zinalalamikiwa kuendesha sera zinazominya ustawi wa Afrika.

Mhadhiri katika Chuo cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa (CFR), Dk Ahmed Mtengwa alisema: “Ni hotuba inayofungua njia kwa Afrika..., amezungumzia ushirikiano unaolingana yaani `win win situation’ (kila upande ufaidike), hivyo kwangu ninayaona matumaini.”
Rais Jinping, aliyekuwa katika ziara ya siku mbili nchini na juzi usiku alisaini mikataba 17 inayohusu sekta za kilimo, afya na miundombinu.

Mkataba wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani ni kati ya miradi mikubwa iliyomo kwenye makubaliano hayo na ujenzi wake utafanywa na Kampuni ya Merchants Holding ya China na utakwenda sanjari na ujenzi wa barabara inayounganisha bandari hiyo.

Pia katika bandari hiyo itaunganishwa na Reli ya Kati na na ile ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) ili kurahisisha usafiri wa mizigo ndani na nje ya nchi.
Mikataba mingine itahusiana na uboreshaji wa sekta ya viwanda, kilimo hasa kile cha tumbaku ikiwamo kuwatafutia soko wakulima kutoka Mikoa ya Tabora na Ruvuma ili waweze kuuza zao hilo katika soko la China pamoja na kulipatia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) zana za kufanyia kazi.

Rais huyo, ambaye Tanzania ndiyo nchi ya kwanza barani Afrika kuitembelea, alizindua na kukabidhi rasmi Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere kilichoko jijini Dar es Salaam ambalo ni jengo la ghorofa tatu na lenye kumbi nne za mikutano zenye uwezo wa kuchukua watu 1,800 kwa wakati mmoja.

Ujenzi wa kituo hicho uligharimu Dola za Marekani 29.7 milioni zilizotolewa na Serikali ya China kwa lengo la kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Rais huyo alisifu ushirikiano wa muda mrefu baina ya taifa lake na Tanzania na kusisitiza kuwa nchi hizo zitaendelea kusaidiana kama sehemu ya kuenzi misingi iliyowekwa na waasisi wa mataifa haya mawili, Mwalimu Julius Nyerere na Mao Tse Tung.

Rais Jinping aliondoka jana jioni kwenda Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa tano wa Wakuu wa Nchi zinazokua kwa kasi kiuchumi ikiwamo Brazil, Urusi, India, China na Afrika ya Kusini (BRICS).
Chanzo: Mwananchi

Jina la aliemsaidia vyeti Mulugo lajulikana.



Imebainika kuwa mmoja wa watu ambao Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, anadaiwa kutumia jina lake kutafuta kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari ya Southern mkoani Mbeya ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu kishiriki cha elimu Mkwawa (Muce), kilichopo mkoani Iringa.

Mhadhiri huyo ni Dick Aron Mulungu ambaye alisoma na Mulugo katika Shule ya Sekondari ya Songea Wavulana kati ya 1994 na 1996 na alijiunga na shule hiyo baada ya kuhitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Kafule, ambayo iko mkoani Mbeya.

Taarifa zinaonyesha kuwa Mulungu alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupata Shahada ya kwanza katika Elimu (BA Education) 2001 na baadaye alisoma na kupata Shahada ya Uzamili (MA Development studies ) 2007.

Alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi, mahojiano yalikuwa hivi:
Mwandishi: Hallow…(mwandishi akajitambulisha)
Mulungu: Sawa, unasemaje?
Mwanishi: Nazungumza na Dick Mulungu?

Mulungu: Ndiyo mimi.
Mwandishi: Hivi unamfahamu mtu anayeitwa Hamimu Agustino?
Mulungu: Aah… hivi ulisema unaitwa nani?
Mwandishi: Si nimeshajitambulisha jina na ofisi ninayotoka?
Mulungu: Nipigie kesho naona hapa kuna kelele.

Mwandishi: Mbona nakusikia vizuri tu?
Mulungu: Nipigie baada ya nusu saa basi.
Baada ya nusu saa…….
Mwandishi: Haloo… naona nusu saa imekwisha, uko tayari kuzungumza?
Mulungu: Huyo simfahamu.
Mwandishi: Kwani wewe si ulisoma Songea Boys?

Mulungu: Ndiyo
Mwandishi: Kwa hiyo humkumbuki mtu aliyekuwa akitumia jina hilo?
Mulungu: Huyo mtu namkumbuka ndiyo.
Mwandishi: Kwa sasa yuko wapi?
Mulungu: Siwezi kujua, si unajua tumesoma siku nyingi sasa huwezi kujua mtu amekwenda wapi… ni siku nyingi mno.
Mwandishi: Ahsante.

Chuo Kikuu na siasa
Taarifa zinaonyesha kuwa Waziri Mulugo alijiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania 2002 akitumia majina ya Philipo Hamimu Augustino na alisomea Shahada ya Sanaa katika Elimu (BA. Ed). Namba yake ya usajili chuoni hapo ni 08652/T.02.
Alipokuwa akiendelea na kazi ya ualimu Mulugo alianza harakati za kisiasa na ndipo alipoamua kwenda kugombea ubunge katika majimbo ya wilaya ya Chunya.

Kada wa chama cha NCCR Mageuzi wilayani Chunya, Nyawili Kalenda aliyejitambulisha kama mlezi wa siasa wa Waziri huyo alisema walifahamiana naye 2004 wakati Mulugo na rafiki yake walipokwenda kumtaka ushauri wa kugombea ubunge katika jimbo la Songwe.
Katika nakala za wasifu wake zinaonyesha kuwa 2008 alishika nafasi ndani ya CCM ambazo ni pamoja na mjumbe wa baraza la jumuiya ya wazazi wilaya ya Chunya, Katibu wa Elimu, Uchumi, Malezi na mazingira wa jumuiya ya wilaya hiyo na mjumbe wa baraza la wazazi mkoa wa Mbeya.

Kauli yake
Mulugo anasema madai hayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na amekuwa akiyajibu kwa kuwaonyesha vyeti vyake halali vya shule. “Hayo madai ni ya muda mrefu, wewe sijui utakuwa mtu wa 20 kuuliza swali kama hilo. Mimi vyeti ninavyo na hata ukitaka ushahidi nitakuonyesha,” alisema Waziri Mulugo.

Licha ya kukiri kurudia darasa la saba, Waziri Mulugo alisema jina la Hamimu amekuwa akilitumia katika elimu tangu awali na kwamba hakuvunja sheria kufanya hivyo.

“Jina la Hamim ni la nyumbani Philipo ni jina langu la ubatizo, nadhani haya ni mambo ya kawaida na kweli nilipokuwa shule watu walikuwa wananifahamu kama Hamimu pia Philipo ni jina langu la ubatizo na kumbuka tukifika chuo huwa tunatumia jina la baba.

“Na pia ni kweli nilirudia shule kwa sababu wakati ule wa Mwalimu Nyerere na Mwinyi (Ali Hassan), sheria ilikuwa inaruhusu maana wanafunzi walikuwa wachache mno, fikiria katika darasa letu la saba tulimaliza watu saba tu. Baadaye sheria hiyo ilibadilishwa,” aliongeza.

Kuhusu jina la Dick Mulungu, alikiri kumfahamu mtu huyo na kwamba walisoma wote shule ya Sekondari ya Songea Boys. Hata hivyo, alipinga kutumia vyeti vyake.

“Ni kweli Dick Mulungu tulisoma wote Songea Boys. Lakini hili jina la Mulungu ni jina letu la ukoo. Babu yangu alikuwa akiitwa Filipo Milambo Mulungu, kwa hiyo niliendelea kulitumia hivyo hivyo na hata jina la Mulugo ni letu pia,” alisema.

Chanzo: Gazeti Mwananchi.

Monday, March 25, 2013

Naibu waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi Philip Mulugo adaiwa kughushi vyeti vya elimu yake.



Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo anadaiwa kutumia ujanja katika wasifu na elimu yake ambapo katika maisha yake ya kielimu ametumia majina manne tofauti.
Philipo Augustine Mulugo ndiyo jina lake halisi ambalo alilisomea mpaka alipohitimu darasa la saba kwa mara ya kwanza 1988, lakini kutokana na kwamba hakufaulu kwenda sekondari alirudia darasa hilo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa takriban miezi mitatu sasa umebaini kuwa 1989, Mulugo alirudia darasa la saba katika Shule ya Msingi Rukwa ya mkoani Mbeya akitumia jina la Hamimu Hassan.
Imebainika kuwa kabla ya kuhitimu darasa la saba kwa mara ya pili, alibadili jina hilo (kutoka Hamimu Hassan) na kuwa Hamimu Augustino ambalo aliendelea nalo wakati akisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari kutwa ya Mbeya (Mbeya Day) mwaka 1990.
Hata hivyo, Mulugo mwenyewe akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam alipuuza tuhuma hizo kwa kusema kuwa ni njama za kisiasa zinazofanywa na maadui zake. Mulugo anasema madai hayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara na amekuwa akiyajibu kwa kuwaonyesha vyeti vyake halali vya shule.
“Hayo madai ni ya muda mrefu, wewe sijui utakuwa mtu wa 20 kuuliza swali kama hilo. Mimi vyeti ninavyo na hata ukitaka ushahidi nitakuonyesha,” alisema Waziri Mulugo na kuongeza:
“Haya mambo kabla hata sijachaguliwa kuwa Mbunge, tulivyokuwa bado kwenye mchujo wa ndani, usiku wa manane watu walisambaza huu uvumi na nilivyoenda kwenye kikao nikatoa vyeti vyangu, wakaviona.”
Waliomfundisha
Baadhi ya walimu waliomfundisha Mulugo, watu waliofanya kazi naye pamoja na wakazi wa Kijiji cha Udinde alikozaliwa, maelezo yao yanathibitisha mabadiliko ya majina ya Mulugo kwa nyakati tofauti pia ngazi mbalimbali za kielimu.
Uchunguzi unabainisha kuwa baada ya kuhitimu kidato cha nne, alifaulu kwenda Shule ya Sekondari ya Wavulana, Songea ambako alisoma kati ya 1994 na 1996 akiendelea kutumia jina la Hamimu Mulugo.
Baada ya kuhitimu kidato cha sita, uchunguzi ulibaini kuwa Mulugo alirejea Mbeya na 1998 alilazimika kubadili tena jina pale alipotumia cheti cha mtu aitwaye Dickson Mulungu, kuombea kazi ya kufundisha katika Shule ya Sekondari ya Southern Highlands.
Habari zinasema Mulugo alichukua hatua hiyo ili kumshawishi mmiliki wa shule hiyo mfanyabiashara, Gulnoor Dossa (sasa ni marehemu), kumpa nafasi ya kufundisha shuleni hapo.
“Mulugo alilazimika kutumia cheti cha rafiki yake aliyekuwa akiitwa Dick Mulungu ambaye alipata daraja la pili katika Shule ya Sekondari ya Songea Boys, hivyo ikawa rahisi kwake kupata kazi ya ualimu katika shule hiyo,” alisema mmoja wa waliofanya kazi naye shuleni hapo (jina tunalihifadhi kwa sasa).
Aliongeza kuwa Mulugo alianza kama mwalimu wa kawaida, lakini baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Shule (headmaster) wakati hakuwa hata na cheti cha ualimu. Alichukua nafasi hiyo ya ukuu wa shule baada ya aliyekuwapo kufariki dunia.
“Unajua wale wahindi (wamiliki) walikuwa ni wafanyabiashara kwa hiyo hawakufuatilia kiwango cha elimu ndiyo maana walimpandisha tu madaraja bila kujali kuwango cha elimu,” alisema rafiki yake huyo na kuongeza:
“Nilimshauri aachane na cheo hicho kwani kama ungefanyika ukaguzi wa Serikali na kumkuta bila vyeti vya ualimu angechukuliwa hatua, hivyo alinisikiliza na akaachia nafasi hiyo na kujipa cheo cha umeneja wa shule.”
Suala la uwezo na elimu ya Mulugo liliibua mjadala siku chache zilizopita baada ya kutoa kauli nchini Afrika Kusini aliponukuliwa akisema Tanzania ni muungano wa nchi mbili ambazo ni Tanganyika na Zimbabwe badala ya Zanzibar.
Alikotokea
Uchunguzi wa gazeti hili ulianzia katika kijiji alichozaliwa cha Udinde, Kata ya Kapalala wilayani Chunya mkoani Mbeya na alisoma Shule ya Msingi ya Rukwa.
Mmoja wa walimu waliomfundisha aliyejitambulisha kwa jina la Nyoni anasema anakumbuka kwamba Naibu Waziri huyo 1989 na wakati huo alikuwa akijulikana kwa jina la Hamimu Hassan.
“Mimi nilihamia hapa 1989 nikitokea Shule ya Msingi Kapalala. Kulikuwa na mwalimu mmoja tu kwa hiyo nikawa wa pili. Namfahamu Mulugo wakati huo akiitwa Hamimu Hassan. Sijui kabla hapo alikuwa akitumia jina gani,” alisema Nyoni anayetarajia kustaafu kazi ya ualimu mwakani.
Mmoja wa ndugu wa karibu wa Waziri Mulugo anayeishi kijijini hapo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini alikiri kuwa awali waziri huyo alikuwa akiitwa Philipo Augustino Mulugo.
“Philipo amesomea hapo Rukwa, ambayo ni Shule ya Msingi na alikwenda Kijiji cha Mkulwe kabla ya kwenda Mbeya kuwa Mwalimu. Sijui kama alirudia shule,” alisema ndugu huyo.
Mkazi mwingine wa kijijini hapo, Peter Kayuti alikiri kumfahamu Waziri Mulugo tangu enzi za utoto na kwamba alirudia darasa la saba, lakini alisema hakumbuki jina la pili alilolitumia. “Ni kweli Philipo alirudia shule, lakini sijui kama alitumia jina jingine zaidi ya hilo la sasa,” alisema Kayuti.
Mwalimu aliyemfundisha katika Shule ya Sekondari Mbeya ambaye pia aliomba jina lake lihifadhiwe, alikiri kumfahamu kwa jina la Hamimu Augustino, lakini akasema hafahamu lilibadilika lini.
“Ni kweli, nilimfundisha Waziri Mulugo na alikuwa akiitwa Hamimu Agustino. Sidhani kama ni jambo geni kwa wanafunzi hasa wa zamani kurudia shule… Zamani ilikuwa kawaida kwa kuwa shule zilikuwa chache. Sijui alibadilisha jina hilo lini, lakini hilo ni suala la kisheria tu,” alisema mwalimu huyo.
Utata wa majina
Mwalimu mwingine aliyewahi kufanya kazi na Waziri Mulugo katika Shule ya Southern Highlands alisema waziri huyo alikuwa na tabia ya kuchanganya majina yake ya awali ili kuficha cheti alichoombea kazi.
“Yule alikuwa mjanja sana, ndiyo maana ukiangalia kadi zake zilikuwa na majina mengi tu na yana badilika. Leo atasaini barua kwa jina hili kesho lile. Mara utaona ameandika kifupisho cha PHDA, yaani Philip Hamimu Dick Agustino, mara Mulungu EDM, mara Mulugu D. Philip,” alisema mwalimu huyo na kuongeza:
“Amekuwa akijaribu kulibadilisha jina la Mulungu kuwa Mulugu mwisho amelipeleka kuwa lake la awali la Mulugo. Yote hayo ni kuficha tu ukweli kwamba alitumia cheti cha Dick Mulungu,” alisema mwalimu huyo.
Mmoja wa wakuregenzi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (jina tunalihifadhi) alisema: “Ili mwalimu wa sekondari awe headmaster (mkuu wa shule) ni lazima awe na shahada ya kwanza kutoka kwenye chuo kikuu kinachotambulika. Anatakiwa pia kuwa na uzoefu wa kazi wa miaka isiyopungua minane.”
Kuhusu kughushi vyeti mkurugenzi huyo alisema, ikigundulika kuwa mwalimu ameghushi cheti anafukuzwa kazi mara moja, lakini alikiri kwamba katika shule binafsi inawezekana walimu wasio na sifa wakapenya, lakini wakaguzi wakibaini hutoa maelekezo wafukuzwe.
Kwanza siku hizi ili mwalimu aajiriwe ni lazima akabidhi vyeti vyake wizarani na hupelekwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) ili kuhakikiwa. Zamani ukaguzi haukuwa makini kwa hiyo inawezekana kuna watu wasio na sifa walipenya,” alisema.
Kuhusu kurudia darasa la saba, alisema sheria haijawahi kuruhusu watu kurudia darasa la saba na kwamba wale waliorudia hutumia mbinu zao kufanya hivyo.
“Sheria haijawahi kuruhusu watu kurudia darasa la saba. Ni kweli wengi wamerudia sijui wanatumia mbinu gani, lakini hairuhusiwi. Ukishafanya mtihani wa darasa la saba mara moja ndiyo basi,” alisema mkurugenzi huyo.
Msemaji wa wizara hiyo, Mtandi Bunyanzu kwa kila swali aliloulizwa alisema hana uhakika hivyo asingeweza kutoa jibu lakini kwa suala la kughushi vyeti, alisema ni kosa la jinai siyo kwa walimu tu bali kwa kila mtu atakayebainika.
“Kughushi vyeti ni kosa la jina siyo kwa walimu tu, hata waandishi wa habari,” aliongeza Bunyanzu.
Kwa upande wake, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) halikuwa tayari kutoa matokeo ya mitihani ya Mulugo na badala yake msemaji wa baraza hilo John Nchimbi alisema matokeo hayo ni siri ya mtahiniwa na hawezi kupewa mtu mwingine.  
Chanzo: Gazeti Mwananchi