Uhuru Kenyatta
Kiongozi wa mashitaka katika
mahakama ya kimataifa ya ICC, Fatou Bensouda, ameiomba mahakama hiyo kuahirisha
kesi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kwa muda usiojulikana.
Hii ni baada ya malalamiko kutoka
kwake kuwa Kenya imekataa kushirikiana na mahakama hiyo katika kuikabidhi
ushahidi unaohitajika kuendesha kesi kwa hiyo ina maana kuwa hana ushahidi wa
kutosha dhidi ya Kenyatta.
Serikali ya Kenya ilitakiwa
kuikabidhi mahakama taarifa za kifedha za Rais Kenyatta pamoja na maelezo
kuhusu mali yote anayomiliki.
Katika uamuzi uliotolewa na mahakama
hiyo Fatou Bensouda amesema kuwa hana ushahidi wa kutosha kumfungulia mashitaka
Rais Kenyatta ambaye anadaiwa kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu
nchini Kenya mwaka 2007.
Zaidi ya watu 1,000 walifariki
katika ghasia hizo. Bensouda amenukuliwa akisema kuwa halitakuwa jambo la
busara kufutulia mbali kesi hiyo hasa ikizingatiwa kuwa Kenya haitaki kutoa
ushahidi unaohitajika na mahakama hiyo.
Badala yake aliomba mahakama
kuiahirisha kesi hiyo hadi pale Kenya itakapokubali kutoa ushahidi
unaohitajika.
Kesi dhidi ya Kenyatta ilipaswa
kuanza mapema mwezi Oktoba.
CHANZO: BBC
SWAHILI
No comments:
Post a Comment