Kamati ya kimataifa ya kuwalinda waandishi wa habari, CPJ, imesema waandishi kiasi 60 waliuwawa kazini 2014 au kwa sababu ya
kazi yao. Asilimia 44 ya waandishi walilengwa katika mauaji.
Kamati ya CPJ yenye makao yake makuu mjini New York nchini Marekani,
imesema katika ripoti yake mpya iliyochapishwa leo kwamba idadi kubwa
isiyo ya kawaida au takriban asilimia 20 ya waandishi waliouwawa
walikuwa ni wa kimataifa, ingawa idadi kubwa ya waliotishwa iliendelea
kuwajumuisha waandishi katika nchi zao za asili.
Miongoni mwa waandishi waliouwawa mwaka huu ni Anja Niedringhaus,
mpiga picha wa shirika la habari la Associated Press aliyepigwa risasi
alipokuwa akiripoti kuhusu uchaguzi wa Afghanistan.
Ripoti ya Kamati ya CPJ imesema idadi ya waandishi wa habari
waliouwawa mwaka huu ilipungua kutoka 70 mwaka uliopita, lakini miaka
mitatu iliyopita imekuwa mibaya zaidi tangu shirika hilo lilipoanza
kuorodhesha matukio ya aina hiyo mnamo mwaka 1992.
Anja Niedringhaus
Mzozo unaoendelea nchini Syria ambao sasa umeingia mwaka wa nne,
umechangia kwa kiwango kikubwa. Ripoti hiyo imesema waandishi wapatao 17
waliuwawa mwaka huu, huku wengine wapatao 79 wakiwa wameuwawa tangu
mapigano yalipoanza mwaka 2011.
Waandishi wa kigeni walilengwa
Syria imehusishwa na visa viwili vya kutisha vya mauaji ya waandishi
wa habari mwaka huu, kuchinjwa kwa waandishi huria wa kimarekani James
Foley na Steven Sotloff na kundi linalojiita Dola la Kiislamu. Wote
wawili walikuwa wamepotea wakati wakiripoti kuhusu mzozo huo wa Syria.
Mzozo nchini Ukraine kati ya serikali mpya na wanamgambo wanaoungwa
mkono na Urusi ulisababisha waandishi watano na wafanyakazi wawili wa
vyombo vya habari kuuwawa wakati mahusiano kati ya Urusi na mataifa ya
magharibi yalipoporomoka na kufikia kiwango cha chini kabisa tangu
kumalizika kwa vita baridi. Mauaji hayo yalikuwa ya kwanza kurekodiwa na
kamati ya CPJ nchini Ukraine tangu mwaka 2001.
Siku 50 za vita katika Ukanda wa Gaza kati ya Israel na Wapalestina
wakati wa msimu wa kiangazi zilisababisha waandishi wapatao wanne na
wafanyakazi wengine watatu wa vyombo vya habari kuuliwa, akiwemo mpiga
picha wa shirika la habari la Associated Press, AP, Simone Camili na
mkalimani Ali Shehda Abu Afash, waliouwawa na mlipuko wa mabaki ya bomu.
James Foley
Takwimu kuhusu vifo
Nchini Iraq, waandishi wasiopungua watano waliuwawa, watatu kati yao
walipokuwa wakiripoti mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu,
wakati lilipokuwa likiyateka maeneo ya kaskazini magharibi mwa nchi
hiyo.
Ripoti ya CPJ inazungumzia mauaji ya kwanza ya waandishi wa habari
katika kipindi cha miaka kadhaa katika baadhi ya nchi, zikiwemo
Paraguay, ambako vifo vitatu viliripotiwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka
2007 na Myanmar, ambako kuuliwa kwa mwandishi wa habari aliyekuwa
akizuiliwa, ni kifo cha kwanza tangu mwaka 2007.
Kamati ya CPJ pia imeripoti mauaji ya kwanza ya mwandishi wa habari
katika Jamhrui ya Afrika ya Kati, ambayo imegawanyika kutokana na
machafuko kati ya Wakristo na Waislamu. Na hata kuripoti mapambano dhidi
ya ugonjwa hatari wa Ebola kumesababisha vifo vya waandishi huku maiti
za mwandishi na wafanya kazi wawili wa vyombo vya habari ikipatikana
katika kijiji kimoja nchini Guinea, ambako walikuwa wamekwenda kuripoti
kuhusu kampeni ya uhamasishaji wa umma.
Kamati ya Kimataifa ya kuwalinda waandishi wa habari CPJ, inasema
inachunguza vifo vya waandishi wapatao 18 mwaka huu. Shirika hilo
halihesabu vifo vinavyotokana na magonjwa au ajali ya magari au kuanguka
kwa ndege mpaka ajali hizo ziwe zilisababishwa na hatua za uchokozi.