Friday, December 26, 2014

Ligi Kuu Tanzania Bara kuanza leo

Ligi kuu ya Tanzania bara, maarufu kama Ligi Kuu ya Vodacom inaanza rasmi mzunguko wa pili leo, Ijumaa baada ya kusitishwa tangu Novemba 7, 2014.
Hadi ligi hiyo ilipositisha mzunguko wa kwanza, tayari timu 14 zinazoshiriki ligi hiyo zilikuwa zimecheza michezo saba kila moja.
 
 
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Kandanda nchini Tanzania, TFF, Simba ambayo ni miongoni mwa timu kongwe za ligi hiyo na ambayo katika mzunguko wa kwanza haikuwa na matokeo mazuri baada ya kwenda sare mara sita na kushinda mchezo mmoja na kujikusanyia pointi tisa ikishika nafasi ya saba katika msimamo wa ligi hiyo, leo inaikaribisha Kagera Sugar inayoshikilia nafasi ya tano katika pambano litakalofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Michezo mingine itafanyika katika viwanja mbalimbali kuanzia Ijumaa, Jumamosi na Jumapili wiki hii.
 
 
Mpaka sasa Mtibwa Sugar ndiyo inayoongoza ligi hiyo ya Vodacom baada ya kujikusanyia pointi 15, ikifuatiwa na Young Africans(Yanga) kwa kuwa na pointi 13 sawa na Azam mabingwa watetezi.
Mbeya City iliyotikisa msimu uliopita na kupata mashabiki wengi nchini Tanzania, imejikuta ikizibeba timu zote baada ya michezo saba ikiwa na pointi tano tu ikitanguliwa na timu za Ndanda na Tanzania Prisons zenye pointi sita kila moja.
 
Hata hivyo mzunguko huu wa pili utakuwa na kivutio cha aina yake baada ya timu hizo kuruhusiwa kusajili katika dirisha dogo, ambapo Simba imeweza kusajili wachezaji wapya ndugu mahiri kutoka Uganda kina Sserunkuma.
Nao wapinzani wao wa jadi Yanga, imemtimua aliyekuwa kocha wake kutoka Brazil Marcio Maximo baada ya kufungwa mabao 2-0 na Simba katika mchezo wa Nani Mtani Jembe. Pia Yanga imesajili wachezaji mahiri akiwemo Amisi Tambwe ambaye katika mzunguko wa kwanza alichezea timu ya Simba lakini akaenguliwa katika usajili wa dirisha dogo.
Kinachosubiriwa na wapenzi na mashabiki wa timu hizo ni kwa kila timu kupata ushindi, kufikia ubingwa.

No comments:

Post a Comment