Thursday, April 17, 2014

Dhiki ya mnyonge




1.      Bega langu la unyonge, nalibwaga kama mwewe
               Nisemalo mnipinge, dua langu nistiriwe
               Ninachopata niringe, nitoe sadakalawe

2.      Najikaza kisabuni, huku natoka mapovu
               Mkono wangu shavuni, nimeupinda ubavu
               Mara hutia ubani, manani anipe nguvu

3.      Nashukuru kwa kidogo, nikipatacho kwa jasho
              Sitegemei vigogo, wenye karadha ya posho
              Nabeba yangu mizigo, kwa ada ya machapisho

4.      Sipendi vibanda hodi, nilikatazwa zamani
              Baba yangu maridadi, mtukufu athumani
              Napenda yake marudi, huniongeza thamani

5.      Sikinyooshi kiganja, hovyo hovyo mitaani
              Bali kwa kusudi moja, kusaidia masikini
              Ulua sitoufuja, nimeshaila yamini

6.      Stara vazi la wachache, wenye akili timamu
              Ambao hungoja kuche, waondoe udhalimu
             Si tamaa ya vicheche, wanyonyao kuku damu
HAFIDH KIDO
KIJITONYAMA, ALIMAUA
DAR ES SALAAM
17 APRIL, 2014


Msichana aliyeteswa kinyama kwa miaka 9


 
Msichana huyo aliishi na Tumbili kwenye chumba cha kueegesha magari
Polisi nchini Argentina wamemwokoa msichana mwenye umri wa miaka kumi na mitano ambaye alifungiwa katika chumba cha kuegesha magari na kunyimwa chakula pamoja na kupigwa na wazazi waliokuwa wamemuasili, kwa kipindi cha miaka tisa.
Msichana huyo alikuwa na uzani wa kilo ishirini pekee.
Viumbe wa pekee walioishi naye ni mbwa pamoja na Tumbili. Msichana huyo amesema alipigwa kila mara iwapo angejaribu kula mabaki ya chakula kilichotupwa kwa wanyama hao.
Amesema alifanikiwa kuondoka katika eneo hilo la kuegesha magari mara mbili tu katika kipindi cha miaka tisa.
Walezi wake wamekamatwa na kufunguliwa mashItaka ya kumdhulumu na kumweka kama mtumwa msichana huyo.
Msichana huyo ambaye amelazwa hospitlaini, alipatikana na dadake wa kuzaliwa naye mjini Buenos Aires.
Kwa mujibu wa maafisa wakuu, wazazi hao walimuasili mwaka 2001 baada ya mahakama kuamua kuwa wazazi wake wa kumzaa hawakuwa na uwezo wa kifedha kuweza kumlea.
Walikuwa wanasubiri stakabadhi za kukamilisha mpango wa kumuasili mtoto huyo.
Chanzo: BBC Swahili

Wasomi wetu wasiishie kuhangaikia ajira: Watengeneze.




Na Hafidh Kido
NINAPENDA kuangalia na kusikiliza vichekesho katika luninga ama redio, ni vitu vinavyonipa maarifa na utulivu wa fikra.
Wiki chache zilizopita niliangalia kipindi cha ucheshi cha Churchill Show kinachorushwa na kituo cha luninga cha KTN, nchini Kenya. Katika kipindi hicho kulikuwa na mchekeshaji anaitwa Owago Nyiro, kijana mdogo lakini hutumia maneno ya busara kuwafanya watu wacheke na wakati huohuo waelimike kuhusiana na masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Alikuwa akizungumzia umuhimu wa vyuo na faida ya wahitimu nchini Kenya, mathalan alizungumzia chuo kikuu cha Nairobi, ambacho kinasifika kwa masuala ya uhandisi. Kama ambavyo kipindi cha ushirikiano wa Afrika Mashariki nchi tatu Kenya, Uganda na Tanzania kila moja ilisifika kwa utaalamu wake.
Uganda katika chuo kikuu cha Makerere walitoa wataalamu wa masuala ya udaktari, Tanzania katika chuo kikuu cha Dar es Salaam walitoa wataalamu wa sheria, na Kenya katika chuo kikuu cha Nairobi walitoa wataalamu wa uhandisi.
Hivyo, Owago, alisema mbali ya kuwa chuo hicho kinafundisha uhandisi tena uhandisi wa ujenzi (architect), lakini majengo ya chuo hicho yanajengwa na kampuni kutoka China. Watu walicheka lakini nilihuzunika badala ya kucheka kutokana na dhihaka hiyo.
Wasomi wetu wanafanya nini, serikali za nchi zinazoendelea zinawasaidia vipi wasomi wetu ili wazitumie vizuri elimu zao kwa manufaa ya umma?
Kwa sasa Tanzania ina vyuo vikuu vingi vya kila namna, kuna vyuo vya uhandisi, ualimu, sheria, udaktari, vyuo vya maendeleo ya jamii na kila namna. Lakini kila siku wahitimu wanahangaika mitaani na bahasha za kaki kutafuta ajira.
Kwa namna gani elimu zetu zitatusaidia kutengeneza watanzania watakaopata mwamko wa kutumia elimu zao kunufaisha umma na si matumbo yao? Kwasababu msomi tunaetumia gharama kubwa kumsomesha kwa fedha za walipa kodi, lakini anaishia kujinufaisha yeye na familia yake kwa kufanya kazi kinyume na ile tuliyosomesha.
Niliwahi kuhudhuria mkutano wa waandishi wa habari wakati ( ) wa Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB). alipozungumza kuhusu matatizo wanayoyapata kwa wanafunzi kushindwa kurudisha mikopo kwa wakati.
Bodi hiyo inadai zaidi ya Sh trilioni moja, hazijalipwa na wanafunzi waliohitimu. Moja ya matatizo yanayosababisha kuchelewa kulipwa kwa mikopo hiyo ni wahitimu kukosa ajira.
Mifumo ya elimu nchini itaendelea kutengeneza wasaka ajira mpaka lini? Ipo haja kuangalia upya aina ya wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza, yaani mitihani ya darasa la saba isaidie kujua mwanafunzi gani anataka kuwa nani.
Turudishe mifumo ya zamani ambapo shule ziligaiwa kutokana na sekta, mathalani tuwe na shule za sekondari zinazoandaa madaktari tu mpaka watakapoingia vyuoni. Vilevile kuwe na shule za sekondari zinazoandaa wahasibu, watafati na taaluma nyingine zenye manufaa kwa watanzania.
Hii itasaidia kuondoa uvivu wa kufikiri, kijana wa kitanzania anataka kuwa nani, kwasababu nimeshashuhudia mwanafunzi anamaliza kidato cha sita yaani ameshakaa darasani kwa miaka 13, lakini hajui anataka kuwa nani.
Anahangaika na fomu ya kujiunga na chuo kikuu kuuliza wakubwa wake, achukue kozi gani. Ni kichekesho hata kuona mwanafunzi wa ‘diploma’ hajui masomo yake ya shahada atafanya kozi gani. Tunaanza kupoteza umakini kabla hatujaingia kwenye soko la ajira, unadhani nani atamuajiri mtu katika kampuni yake ambae hajitambui?
Hafidh Kido
Kijitonyama, Alimaua
Dar es Salaam, Tanzania
17 April, 2014 

Sunday, April 13, 2014

Uchaguzi Guinea Bissau



Raia wa Guinea Bissau kuchagua rais mpya

Bissau, Guinea-Bissau
Ni uchaguzi wa Kwanza tangu kufanyika kwa mapinduzi miaka miwili iliopita -ikiwa ni hatua ya hivi karibuni ya kijeshi ambayo imesaidia kuhakikisha kwamba hakuna raisi aliyechaguliwa ambaye amefanikiwa kuiongoza Guinea Bissau kwa kipindi chote alichochaguliwa tangu taifa hilo lijipatie Uhuru wake kutoka kwa Ureno mnamo mwaka 1974.
Kiongozi wa mapinduzi hayo Antonio Indjai aliikabidhi mamlaka serikali ya raia mnamo mwaka 2012 iliopewa wajibu wa kuandaa Uchaguzi huo.
Indjai alifunguliwa mashtaka nchini marekani kwa madai ya kufanya biashara ya mihadarati pamoja na kuwauzia silaha waasi wa Colombia.Wagombea 13 wanawania wadhfa wa urais.
Iwapo mmoja wao hatashinda kwa wingi wa kura basi uchaguzi huo utaenda kwa awamu ya pili mnamo mwezi May.


Marekani yaionya Urusi kuhusu Ukraine.

Kiev, Ukraine

Marekani imeonyesha wasiwasi wake kuhusu kile ilichokitaja kama harakati za kundi fulani linalotaka kujitenga ambalo limekuwa likisaidiwa na Urusi kuchochea ghasia mashariki mwa Ukrain.
Kufuatia kutekwanyara kwa vituo vya polisi katika miji kadhaa ya mashariki mwa Ukrain ,waziri wa maswala ya kigeni nchini marekani John Kerry amesema kuwa mashambulizi hayo ya watu waliojihami na silaha za Urusi yalifanyika kwa mpangilio.
Katika mazungumzo yao ya simu na waziri wa maswala ya kigeni nchini Urusi Sergei Lavrov,Kerry ameitaka Urusi kusitisha mashambulizi kama hayo la sivyo ikabiliwe na vikwazo zaidi.
Urusi imeonya kuwa utumiaji wowote wa nguvu nchini Ukrain utahujumu harakati za kidiplomasia kumaliza mgogoro huo.


Boko Haram ladaiwa kuwaua watu laki moja

Abuja, Nigeria
Sasa imebainika kuwa wanamgambo wa kiislamu kazkazini mwa Nigeria wamewaua zaidi ya watu laki moja na arubaini na tano katika misururu ya mashambulizi juma lililopita.
Sineta wa jimbo la kazkazini mashariki la Borno Ahmed Zannah ameiambia BBC kwamba mauaji hayo yalifanyika katika maeneo matatu tofauti yaliopo mashambani.
Amesema kuwa taassi moja ya kutoa mafunzo ya elimu ndio iliokuwa ya kwanza kulengwa ambapo wanamgambo hao waliwaua walimu watano kabla ya kuwatekanyara wake zao kadhaa.
Wapiganaji hao wanaoshukiwa kutoka katika kundi la wanamgambo wa Boko haram baadaye walivamia vijiji viwili katika eneo la mashambani karibu na mpaka na Cameroon.

Chanzo: BBC Swahili