Thursday, April 17, 2014

Dhiki ya mnyonge
1.      Bega langu la unyonge, nalibwaga kama mwewe
               Nisemalo mnipinge, dua langu nistiriwe
               Ninachopata niringe, nitoe sadakalawe

2.      Najikaza kisabuni, huku natoka mapovu
               Mkono wangu shavuni, nimeupinda ubavu
               Mara hutia ubani, manani anipe nguvu

3.      Nashukuru kwa kidogo, nikipatacho kwa jasho
              Sitegemei vigogo, wenye karadha ya posho
              Nabeba yangu mizigo, kwa ada ya machapisho

4.      Sipendi vibanda hodi, nilikatazwa zamani
              Baba yangu maridadi, mtukufu athumani
              Napenda yake marudi, huniongeza thamani

5.      Sikinyooshi kiganja, hovyo hovyo mitaani
              Bali kwa kusudi moja, kusaidia masikini
              Ulua sitoufuja, nimeshaila yamini

6.      Stara vazi la wachache, wenye akili timamu
              Ambao hungoja kuche, waondoe udhalimu
             Si tamaa ya vicheche, wanyonyao kuku damu
HAFIDH KIDO
KIJITONYAMA, ALIMAUA
DAR ES SALAAM
17 APRIL, 2014


No comments:

Post a Comment