Thursday, April 17, 2014

Wasomi wetu wasiishie kuhangaikia ajira: Watengeneze.
Na Hafidh Kido
NINAPENDA kuangalia na kusikiliza vichekesho katika luninga ama redio, ni vitu vinavyonipa maarifa na utulivu wa fikra.
Wiki chache zilizopita niliangalia kipindi cha ucheshi cha Churchill Show kinachorushwa na kituo cha luninga cha KTN, nchini Kenya. Katika kipindi hicho kulikuwa na mchekeshaji anaitwa Owago Nyiro, kijana mdogo lakini hutumia maneno ya busara kuwafanya watu wacheke na wakati huohuo waelimike kuhusiana na masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Alikuwa akizungumzia umuhimu wa vyuo na faida ya wahitimu nchini Kenya, mathalan alizungumzia chuo kikuu cha Nairobi, ambacho kinasifika kwa masuala ya uhandisi. Kama ambavyo kipindi cha ushirikiano wa Afrika Mashariki nchi tatu Kenya, Uganda na Tanzania kila moja ilisifika kwa utaalamu wake.
Uganda katika chuo kikuu cha Makerere walitoa wataalamu wa masuala ya udaktari, Tanzania katika chuo kikuu cha Dar es Salaam walitoa wataalamu wa sheria, na Kenya katika chuo kikuu cha Nairobi walitoa wataalamu wa uhandisi.
Hivyo, Owago, alisema mbali ya kuwa chuo hicho kinafundisha uhandisi tena uhandisi wa ujenzi (architect), lakini majengo ya chuo hicho yanajengwa na kampuni kutoka China. Watu walicheka lakini nilihuzunika badala ya kucheka kutokana na dhihaka hiyo.
Wasomi wetu wanafanya nini, serikali za nchi zinazoendelea zinawasaidia vipi wasomi wetu ili wazitumie vizuri elimu zao kwa manufaa ya umma?
Kwa sasa Tanzania ina vyuo vikuu vingi vya kila namna, kuna vyuo vya uhandisi, ualimu, sheria, udaktari, vyuo vya maendeleo ya jamii na kila namna. Lakini kila siku wahitimu wanahangaika mitaani na bahasha za kaki kutafuta ajira.
Kwa namna gani elimu zetu zitatusaidia kutengeneza watanzania watakaopata mwamko wa kutumia elimu zao kunufaisha umma na si matumbo yao? Kwasababu msomi tunaetumia gharama kubwa kumsomesha kwa fedha za walipa kodi, lakini anaishia kujinufaisha yeye na familia yake kwa kufanya kazi kinyume na ile tuliyosomesha.
Niliwahi kuhudhuria mkutano wa waandishi wa habari wakati ( ) wa Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB). alipozungumza kuhusu matatizo wanayoyapata kwa wanafunzi kushindwa kurudisha mikopo kwa wakati.
Bodi hiyo inadai zaidi ya Sh trilioni moja, hazijalipwa na wanafunzi waliohitimu. Moja ya matatizo yanayosababisha kuchelewa kulipwa kwa mikopo hiyo ni wahitimu kukosa ajira.
Mifumo ya elimu nchini itaendelea kutengeneza wasaka ajira mpaka lini? Ipo haja kuangalia upya aina ya wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza, yaani mitihani ya darasa la saba isaidie kujua mwanafunzi gani anataka kuwa nani.
Turudishe mifumo ya zamani ambapo shule ziligaiwa kutokana na sekta, mathalani tuwe na shule za sekondari zinazoandaa madaktari tu mpaka watakapoingia vyuoni. Vilevile kuwe na shule za sekondari zinazoandaa wahasibu, watafati na taaluma nyingine zenye manufaa kwa watanzania.
Hii itasaidia kuondoa uvivu wa kufikiri, kijana wa kitanzania anataka kuwa nani, kwasababu nimeshashuhudia mwanafunzi anamaliza kidato cha sita yaani ameshakaa darasani kwa miaka 13, lakini hajui anataka kuwa nani.
Anahangaika na fomu ya kujiunga na chuo kikuu kuuliza wakubwa wake, achukue kozi gani. Ni kichekesho hata kuona mwanafunzi wa ‘diploma’ hajui masomo yake ya shahada atafanya kozi gani. Tunaanza kupoteza umakini kabla hatujaingia kwenye soko la ajira, unadhani nani atamuajiri mtu katika kampuni yake ambae hajitambui?
Hafidh Kido
Kijitonyama, Alimaua
Dar es Salaam, Tanzania
17 April, 2014 

No comments:

Post a Comment