HOTUBA YA MHESHIMIWA DR. JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUAGANA NA BUNGE NA KULIVUNJA
BUNGE LA KUMI LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, UKUMBI WA BUNGE, DODOMA TAREHE
9 JULAI, 2015
Mheshimiwa Spika;
Tunayo kila sababu ya
kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kuishuhudia
siku hii adhimu katika historia ya Bunge letu na nchi yetu. Hatimaye siku ya kuvunja Bunge la Kumi
imewadia ili kuwezesha hatua husika za mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015
ziweze kutekelezwa.
Nakushukuru sana
Mheshimiwa Spika kwa kunipatia nafasi hii ya kulihutubia Bunge lako tukufu ili
niweze kutimiza wajibu wangu huo wa msingi Kikatiba. Lakini, shukrani zangu kubwa ni kwa uongozi
wako mahiri na shupavu. Umeliongoza
Bunge vizuri. Najua haikuwa kazi rahisi.
Penye wengi pana mengi. Lakini kwa uhodari mkubwa umeweza kulifikisha jahazi
bandarini salama salmini. Hakika wewe ni
nahodha makini na jemedari hodari, uliyethibitisha uhodari na umakini wako
katika uwanja wa medani. Wewe ndiwe
mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huu wa juu kabisa katika mhimili huu wa kutunga
sheria na umeidhihirishia dunia kuwa wanawake wakipewa nafasi wanaweza.
Mheshimiwa Spika;
Niruhusu pia nitoe
shukrani na pongezi zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge kwa kazi kubwa na
nzuri mliyoifanya. Mmetimiza ipasavyo wajibu wao wa Kikatiba wa Kutunga Sheria
na kusimamia Serikali. Nawashukuru kwa ushirikiano wenu na msaada wenu. Ni ukweli ulio wazi kuwa bila ya ninyi
Wabunge wetu na Bunge hili, tusingeweza kupata mafaniko na maendeleo
tuliyoyapata. Mmejijengea, nyinyi wenyewe na Bunge letu heshima kubwa mbele ya
wananchi. Mmeitendea haki demokrasia ya
Tanzania na kuliletea heshima kubwa Bunge letu nchini, kikanda na
kimataifa.
Mheshimiwa Spika;
Tarehe 30 Desemba
2005 nilipozindua Bunge la Tisa nilielezea mtazamo wangu kuhusu nchi yetu na
kutaja majukumu ya msingi na vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Nne. Nilisema tutatekeleza wajibu wetu na
vipaumbele hivyo kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya. Tarehe 16 Julai, 2010
wakati wa kuvunja Bunge hilo nilielezea mafanikio tuliyopata na changamoto
zilizotukabili katika kipindi hicho. Tarehe 28 Novemba, 2010 wakati wa kuzindua
Bunge hili la Kumi niliainisha vipaumbele vya Serikali ya Chama cha Mapinduzi
katika kipindi changu cha pili cha uongozi wa nchi yetu na kuahidi kuvitekeleza
kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi. Kama ilivyo ada, leo tunafikia mwisho
wa uhai wa Bunge la Kumi, naomba kutumia fursa hii kutoa mrejesho wa
utekelezaji wa majukumu ya Serikali na yale mambo ambayo tuliahidi na kupanga
kufanya.
Umoja,
Amani na Usalama
Mheshimiwa
Spika;
Niliahidi kuwa katika
kipindi cha uongozi wangu nitafanya kila niwezalo kuhakikisha kuwa Tanzania
inaendelea kuwa nchi moja na watu wake wanaendelea kuwa wamoja, wanaopendana na
kushirikiana licha ya tofauti zao za rangi, dini, makabila, mahali watokako, na
ufuasi wa vyama vya siasa. Pia, kwamba nchi yetu itaendelea kuwa yenye amani, usalama
na utulivu.
Leo tunapoagana,
ninyi na mimi, ni mashuhuda kuwa Tanzania na Watanzania tumebakia kuwa
wamoja. Hata hivyo, katika kipindi hiki
kumekuwepo na matukio ya hapa na pale madogo na makubwa, yaliyotishia umoja wa nchi
yetu na watu wake. Yapo mambo yaliyopandikizwa kuleta chuki baina ya Tanzania
Bara na Zanzibar, baina ya Wakristo na Waislamu na baina ya maeneo fulani ya
nchi na wengine.
Bahati nzuri, msimamo
thabiti wa viongozi wakuu wa Serikali zetu mbili wakisaidiwa na viongozi
wengine pamoja na ushirikiano na viongozi wa dini na wa jamii na uelewa wa
wananchi, vimeliwezesha taifa letu kushinda changamoto hizo na matishio yote
hayo. Changamoto hizi zimethibitisha
ubora wa mazungumzo. Ni kweli kabisa
kwamba wanaozungumza hawagombani na wanaozungumza humaliza tofauti zao bila
kugombana.
Mheshimiwa Spika;
Niruhusuni, nitumie
nafasi hii kuwashukuru kwa mara nyingine viongozi wakuu wenzangu, Makamu wa
Rais, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Waziri Mkuu, Makamu wa Kwanza wa
Rais Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, viongozi wa dini, viongozi wa
jamii na wananchi wote kwa ushindi tulioupata katika kudumisha umoja wetu. Hata hivyo, tahadhari kubwa lazima iendelee
kuchukuliwa kwani watu wenye nia mbaya kwa nchi yetu au na umoja wetu hawajaisha
na hawajafurahi kwamba hawajafaulu. Huenda wakajaribu tena. Tunachotakiwa
kufanya ni kuendelea kushikamana ili hata wakijaribu tena washindwe.
Muungano
Wetu Umeimarika Zaidi
Mheshimiwa
Spika;
Nafurahi kwamba
namaliza kipindi changu cha uongozi tukiwa tumeweza kudumisha na kuuimarisha Muungano
wetu adhimu na adimu Barani Afrika. Mtakumbuka
kuwa katika hotuba yangu ya kufungua Bunge la Tisa nilisisitiza umuhimu wa
viongozi wa pande zetu mbili kukutana mara kwa mara kuzungumzia ustawi wa
Muungano wetu. Nafurahi kwamba jambo
hili limefanyika chini ya uenyekiti wa Makamu wa Rais, akisaidiwa na Waziri
Mkuu kwa upande wa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar, Waziri Kiongozi
katika awamu yangu ya kwanza na Makamu
wa Pili wa Rais katika awamu hii.
Mafanikio yaliyopatikana ni makubwa. Masuala mbalimbali ya zamani na
mapya yamezungumzwa, yameshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Kwa mfano, hadi mwaka
2005 zilikuwa zimebakia kero 13 za
Muungano zilizoainishwa na Tume ya Shelukindo, hivi sasa zimebaki kero nne. Tayari
ufumbuzi wa kero moja unakamilishwa kiutawala na tatu zimeshughulikiwa kwa
ukamilifu katika Katiba Inayopendekezwa. Kama kura ya maoni ingekuwa imefanyika
na Katiba hiyo kupitishwa kungekuwa hakuna kiporo cha kero za Tume ya Shelukindo. Lakini kwa vile kura ya maoni haijafanyika
ndiyo maana tunaendelea kuzitaja. Hata hivyo, Serikali zetu mbili zimezungumza
na kukubaliana tutafute njia ya kumaliza suala la rasilimali ya mafuta na
gesi. Ndiyo maana katika Muswada wa
Petroli hoja ya Zanzibar kuwa na mamlaka kamili ya kusimamia uchimbaji wa mafuta
na kumiliki mapato yake ilijumuishwa. Natoa shukrani nyingi kwa Bunge lako
tukufu kwa kupitisha Muswada huo. Moja ya kero kubwa katika Muungano
tumeimaliza.
Mpasuko
wa Kisiasa Zanzibar
Mheshimiwa Spika;
Mtakumbuka kuwa
nilizungumzia kusononeshwa kwangu na mpasuko wa kisiasa uliokuwepo Zanzibar
wakati ule na kuelezea utayari wangu wa kusaidia kuuondoa. Kama mjuavyo
mazungumzo yalifanyika ndani ya CCM na CUF na baina ya vyama hivyo na muafaka
ukapatikana. Serikali ya Umoja wa Kitaifa ikaundwa na mpasuko wa kisiasa ukawa
umepatiwa tiba. Matokeo ya yote hayo ni
kuwa mazingira ya kisiasa na kijamii yamekuwa bora zaidi siku hizi kuliko ilivyokuwa
kabla ya hapo.
Ni matumaini yangu
kuwa ndugu zetu wa Zanzibar watayadumisha mafanikio haya ili waendelee kuishi
kwa amani, upendo na udugu. Natambua kuwepo kwa changamoto za hapa na pale
katika uendeshaji wa Serikali hiyo.
Jambo linalonipa faraja ni kuwa matatizo yenyewe hayahusu muundo wa
Serikali bali yanaletwa na watu kupishana kauli au kutofautiana katika uendeshaji
wa baadhi ya mambo. Mimi naamini hayo ni mambo yanayoweza kumalizwa kwa wadau
kukaa kitako na kuzungumza kama ilivyokuwa kabla ya muafaka.
Amani
na Usalama
Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu iko salama,
mipaka iko salama kwa sababu Jeshi la Ulinzi
la Wananchi wa Tanzania limeendelea kutimiza ipasavyo jukumu lake la kulinda
uhuru na mipaka ya nchi yetu. Katika kipindi hiki tumewekeza sana katika
kuliimarisha Jeshi letu kwa vifaa na zana za kisasa za kivita na mafunzo.
Tumeimarisha Kamandi za Nchi Kavu, Anga na Majini. Utayari kivita wa jeshi letu
ni mzuri tena wa hali ya juu. Weledi na
nidhamu ya Wanajeshi wetu ni ya hali ya juu. Tumeboresha maslahi na makazi ya
wanajeshi kwa kujenga nyumba mpya za kuishi. Utekelezaji wa mpango wa
kuwajengea nyumba 10,000 unaendelea
vizuri. Hadi hivi sasa nyumba 6,064 zinaendelea
kujengwa nchi nzima na kati yake nyumba 3,096
zimekamilika. Namaliza kipindi changu cha kuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi na Usalama kwa kujiamini kwamba “Tupo vizuri”. Pamoja na hayo kazi ya utekelezaji wa Mpango
wa Miaka 15 wa kuimarisha JWTZ lazima iendelezwe ili kulifikisha Jeshi letu
pale tulipopakusudia.
Mheshimiwa
Spika;
Katika miaka 10 hii
tumefanya jitihada kubwa ya kupambana na uhalifu ili kulinda usalama wa maisha
na mali za watu waishio Tanzania.
Mtakumbuka kuwa mwaka 2005 na mwanzoni mwa 2006 kulikuwa na matukio
mengi ya ujambazi. Niliahidi wakati wa
kampeni na katika hotuba yangu Bungeni kwamba hatutawaacha majambazi waendelee
kutamba. Hali ile imedhibitiwa. Ingawaje matukio ya ujambazi hayajaisha, lakini
hayako kama ilivyokuwa wakati ule.
Hali kadhalika, matukio
ya uhalifu wa kuwania mali yamepungua kutoka 53,268 mwaka 2005 hadi 43,808
mwaka 2014. Natoa pongezi nyingi kwa Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa na nzuri
waliyoifanya na wanayoendelea kufanya. Jambo ambalo bado hatujafanikiwa vya
kutosha ni ajali za barabarani. Lazima tuendelee kuzitafutia muarobaini wake. Niruhusuni
niwatambue na kuwashukuru Inspekta Jenerali (mstaafu) Omari Mahita, Inspekta
Jenerali (mstaafu) Said Mwema na Inspekta Jenerali Ernest Mangu aliyepo sasa kwa
uongozi wao mzuri.
Mafanikio haya ni
matokeo ya uwekezaji wa Serikali katika utakelezaji wa mpango wa maboresho ya
Jeshi la Polisi uliobuniwa wakati wa uongozi wa Ndugu Saidi Mwema, IGP mstaafu.
Jeshi la Polisi linaendelea kuwezeshwa kwa zana, vifaa na mafunzo. Taratibu zimekamilika za kulipatia Jeshi hilo
magari ya kutosha ili kuongeza ufanisi.
Pia, tumeendelea
kuboresha maslahi na mazingira ya kuishi Maafisa na Askari. Kwa ajili hiyo tumekarabati baadhi ya nyumba
zilizopo, tumejenga nyumba kadhaa mpya za ghorofa, za kawaida na mabweni. Mipango imekamilika ya kuwezesha ujenzi wa
nyumba 10,000 ambazo zitapunguza kwa
kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa nyumba za kuishi katika Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Spika;
Jeshi letu la Magereza
nalo limeendelea kutekeleza vizuri majukumu yake ya kulinda wafungwa na
kurekebisha tabia zao. Aidha, huduma za malazi, mavazi, chakula na usafiri kwa
wafungwa zimeendelea kuboreshwa. Changamoto kubwa ni msongamano wa wafungwa
Magerezani. Naamini mipango ya kujenga magereza mapya na kupanua yaliyopo
ikitekelezwa tatizo litaisha. Aidha, mpango
wa maboresho ya Jeshi la Magereza ukikamilika na kutekelezwa, utaboresha
mazingira ya kufanyia kazi na kuishi
maafisa na askari, hivyo kupandisha morali wao na kuongeza ufanisi.
Jeshi
la Kujenga Taifa
Mheshimiwa Spika;
Ahadi yangu ya kuanzisha
upya utaratibu wa kuchukua vijana wa mujibu wa Sheria katika Jeshi la Kujenga Taifa
imetimia. Mpaka hivi sasa vijana 38,200
wamekwisha hitimu mafunzo hayo wakiwemo Waheshimiwa Wabunge. Nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge
walioshiriki kwa kuongoza kwa mfano. Imesaidia sana utaratibu huo kuanza upya
bila vipingamizi. Ni matumaini yangu
kuwa Wizara ya Fedha, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa watakaa pamoja
kujadili namna ya kutafuta ufumbuzi kwa changamoto zilizopo. Naamini zinaweza
kumalizwa, vijana wetu wakashiriki mafunzo bila matatizo yoyote.
Utawala
Bora
Mheshimiwa
Spika;
Katika kipindi cha
miaka kumi hii tumetekeleza dhamira yetu ya kujenga na kuimarisha utawala bora kwa
sera, sheria, mifumo, taasisi na kwa rasilimali watu. Tumefanya hivyo katika
maeneo yote muhimu yakiwemo yale yahusuyo haki za binadamu, demokrasia,
mapambano dhidi ya rushwa, maadili ya viongozi, ukusanyaji wa mapato na nidhamu
ya matumizi ya fedha za umma na mgawano wa madaraka hati ya mihimili.
Bunge
la Jamhuri ya Muungano
Mheshimiwa Spika;
Serikali imetimiza
ipasavyo wajibu wake kwa mhimili mkuu wa dola wa Kutunga Sheria. Tulianzisha Mfuko
wa Bunge na kuongeza fedha katika bajeti ya Bunge toka shilingi bilioni 30.58 mwaka
2005/06 hadi shilingi bilioni 173.76 mwaka 2015/16. Pia tumeanzisha Mfuko
wa Jimbo ili kuwawezesheni Wabunge kuchangia katika kutatua changamoto za
maendeleo zinazowakabili wananchi wa majimbo yao. Bunge letu limetekeleza
ipasavyo majukumu yake kupitia Kamati zake za kudumu na pale ilipolazimu Kamati
teule zilizoundwa.
Katika kipindi hiki
miswada 163 imepitishwa, maswali ya
msingi 7,544 na ya nyongeza 22,632 yameulizwa na kujibiwa. Kamati teule 2 ziliundwa.
Haya ni mafanikio makubwa kwa Bunge letu.
Bunge hili limefanya kazi kubwa na kazi ya kutukuka. Michango na ushauri wake umekuwa chachu ya
baadhi ya hatua na mabadiliko ya kisera, kisheria na kiutendaji yaliyofanywa na
Serikali. Kwa kweli mnastahili pongezi nyingi.
Huwezi kutaja mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne bila kutambua
mchango wa Bunge hili.
Mchakato
wa Katiba
Mheshimiwa
Spika;
Kama sote tujuavyo, kupitia
Sheria iliyotungwa na Bunge hili, mwaka 2013 tulianzisha mchakato wa Mabadiliko
ya Katiba kwa lengo la kuipatia nchi yetu Katiba mpya iliyo bora zaidi kuliko
iliyopo sasa. Nafurahi kwamba mchakato huo ulituwezesha kupata Katiba
Inayopendekezwa ambayo imekidhi matarajio hayo. Narudia kutoa pongezi za dhati
kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Bunge Maalum la Katiba kwa kazi kubwa na
nzuri waliyofanya. Hatua iliyobaki ni Kura ya Maoni ambapo sote tunasubiri
maelekezo ya Tume ya Uchaguzi. Mimi naamini iwapo itapitishwa, Katiba
Inayopendekezwa itaimarisha zaidi taifa letu.
Vyama
vya Siasa
Mheshimiwa
Spika;
Katika kipindi hiki
tumeshuhudia vyama vya siasa vikiendelea kuimarika na kujijenga nchini. Idadi
ya vyama vya siasa imeongezeka kutoka 18
hadi 24. Vyama vya siasa vimefanya shughuli zake kwa
uhuru. Viongozi na wanachama wao wamefanya mikutano mingi na hata maandamano
kote nchini. Baraza la Vyama vya Siasa na TCD vimekuwa vyombo muhimu
vilivyofanya kazi nzuri ya kujenga ushirikiano miongoni mwa vyama vya siasa. Yamekuwa
majukwaa muhimu ya mashauriano baina ya vyama vya siasa kwa masuala
mbalimbali. Matatizo na changamoto
nyingi zimeweza kupatiwa ufumbuzi. Ni
matumaini yangu kuwa vyombo hivi viwili vitaendelezwa na kuimarishwa miaka
ijayo.
Huu ni mwaka wa
Uchaguzi, na vyama vya siasa ndiyo wahusika wakuu. Ni matumaini yangu kuwa vyama
vya siasa vitaheshimu na kuzingatia maadili ya uchaguzi. Hii itasaidia kuwepo kwa utulivu na amani
katika mchakato wa uchaguzi.
Uchaguzi
Mkuu
Mheshimiwa
Spika;
Habari
kubwa hapa nchini sasa ni uchaguzi mkuu.
Tayari Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) na ile ya Zanzibar (ZEC) zimekwisha
tangaza tarehe 25 Oktoba, 2015 kuwa ni siku ya kufanyika uchaguzi mkuu. Maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vizuri.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na zoezi la uandikishaji wa wapiga kura
kwa mfumo mpya wa teknolojia ya Biometric
Voters Register (BVR). Hadi sasa zoezi la uandikishaji limekamilika katika
mikoa 13 na linaendelea katika mikoa
11 na katika mkoa wa Dar es Salaam
na Zanzibar uandikishaji unategemea kuanza mwezi huu. Kwa taarifa za Tume ya Uchaguzi,
tayari wamekwisha andikisha hadi sasa wapiga kura milioni 11 kati ya lengo la kuandikisha wapiga kura kati ya milioni 21 hadi 23.
Sisi katika Serikali tutaendelea
kutimiza wajibu wetu wa kuiwezesha Tume kutimiza wajibu wake. Napenda
kuwahakikishia kuwa kila Mtanzania mwenye haki ya kupiga kura atapata fursa ya
kuandikishwa. Shime tuhimize watu
wajitokeze kujiandikisha ili wasikose haki yao hiyo.
Uhuru
wa Habari
Mheshimiwa
Spika;
Mtakubaliana nami
kuwa katika kipindi hiki uhuru wa habari na uhuru wa watu kutoa maoni yao
umepanuka sana. Tanzania kuna magazeti ya kila siku 16 na kati ya hayo ya Serikali ni 2 (Daily News, Habari Leo). Pia magazeti ya kila wiki yapo 62.
Aidha, kuna vituo vya redio 115
na vya televisheni 29. Serikali haifanyi uhakiki wa habari kabla ya
kuchapishwa au kuandikwa. Tumeamua hivyo
kwa imani yangu kwamba ustawi wa demokrasia hutegemea sana uhuru wa vyombo vya
habari. Pili, kwa vile tunatambua manufaa ya vyombo vya habari kuelimisha jamii,
kupambana na maovu na kuhimiza uwajibikaji.
Pamoja na hayo, hatukusita
wala kuchelea kuchukua hatua pale uhuru huo ulipotumiwa vibaya na kutishia
kuvuruga amani, umoja na usalama wa jamii au taifa. Au, pale ambapo Sheria za nchi zimekiukwa. Huo
ni wajibu wetu wa kikatiba ambao mimi na wenzangu tuliapa kuutimiza.
Mheshimiwa Spika;
Katika kuongeza uwazi
na mawasiliano na wananchi mwaka 2007 tulianzisha tovuti ya wananchi. Tovuti
hiyo imeshapokea hoja 117,243 na kati
ya hizo zilizohusu Serikali zilikuwa 78,258
na zote zimeshughulikiwa.
Katika kuboresha mfumo
wa mawasiliano, Tanzania imeshahama kutoka mfumo wa analogia na kuingia kwenye
mfumo wa digitali. Hii ni hatua kubwa
muhimu kwa maendeleo ya tasnia ya habari nchini. Jambo ambalo nasikitika kuwa
hatukuweza kulikamilisha ni utungaji wa Sheria ya Haki ya Upatikanaji wa Habari
na Sheria ya Vyombo vya Habari. Miswada imekamilika na kusomwa mara ya kwanza hapa
Bungeni lakini mchakato wake haukuweza kufika mwisho. Tunawaachia wenzetu wajao
washughulike nayo katika Bunge la 11.
Vita
dhidi ya Rushwa
Mheshimiwa
Spika;
Vita dhidi ya rushwa
ni eneo jingine ambalo tulilivalia njuga katika Awamu ya Nne. Tumepata
mafanikio ya kutia moyo katika mapambano dhidi ya rushwa ingawaje kazi bado ni
kubwa. Tumefanya mambo matatu. Kwanza, tumetunga Sheria Na. 11 ya mwaka 2007 ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa ambayo imeongeza nguvu ya mapambano dhidi ya uovu
huu. Idadi ya makosa ya rushwa iliongezwa kutoka 4 mpaka 24 na wigo wa
wakosaji pia, kwa kuhusisha watu katika sekta binafsi. Mifumo ya upelelezi na
uendeshaji mashitaka nayo imeimarishwa.
Tumeunda chombo kipya
TAKUKURU badala ya TAKURU ambacho kimepewa majukumu ya kuzuia na kupambana na rushwa
badala ya kuzuia peke yake. TAKUKURU imepewa mamlaka zaidi katika kuongoza mapambano
haya. Taasisi imeendelea kuimarishwa kwa kuipatia zana na vifaa vya kufanyia
kazi pamoja na rasilimali watu na mahitaji mengine. Tumeiwezesha TAKUKURU
kufungua ofisi katika Mikoa na Wilaya zote.
Mheshimiwa Spika;
Maboresho haya
yamewezesha idadi ya kesi za tuhuma za rushwa zinazofikishwa mahakamani kuongezeka
kutoka kesi 50 mwaka 2005 hadi 1,900 mwaka 2014. Jumla ya shilingi bilioni 87.8 ziliokolewa. Watumishi
wa Serikali 97 wameachishwa kazi kwa
tuhuma za rushwa na matumizi mabaya ya ofisi zao baada ya ushahidi wa kijinai
kukosekana. Kwa upande wa kupambana na rushwa kwenye shughuli za uchaguzi,
tumetunga Sheria ya Kudhibiti Gharama za Uchaguzi Na. 6 ya mwaka 2010 ili kutoa
majibu ya kilio cha siku nyingi dhidi ya watu wanaotumia fedha kununua kura.
Mapato na Matumizi ya Fedha na Mali za Serikali
Mheshimiwa Spika;
Nilieleza katika hotuba yangu ya
Kuzindua Bunge la Tisa tarehe 30 Desemba, 2005 kuwa tutatoa kipaumbele cha juu
kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali na nidhamu ya matumizi ya Serikali. Leo miaka kumi baadae ninaona fahari tumepata
mafanikio makubwa. Mapato ya Serikali yameongezeka kutoka shilingi bilioni 177.1 mwaka 2005 kwa mwezi hadi takriban shilingi bilioni 850. Hii imewezesha bajeti ya Serikali kukua kutoka
trilioni 4.13 mwaka 2005/2006 hadi trilioni 22.49 mwaka 2015/2016. Isitoshe
imetuwezesha kupunguza misaada na mikopo ya washirika wa maendeleo kutoka asilimia 42 ya Bajeti ya Serikali mwaka
2005 hadi asilimia 15 mwaka 2014/2015 na tumejipa lengo la kushusha zaidi
hadi asilimia 8 mwaka huu wa fedha
wa 2015/2016.
Mheshimiwa
Spika;
Mafanikio haya yametokana hasa na kazi kubwa tuliyoifanya ya kuimarisha
Mamlaka ya Mapato ambao wanastahili pongezi zetu nyingi. Bado naamini tunaweza
kufanya vizuri zaidi ya hivi, kama tukiongeza udhibiti kwa mianya ya kupoteza
mapato na kuimarisha zaidi TRA na mamlaka nyingine za ukusanyaji mapato ya
Serikali. Bado ukusanyaji wa mapato yasiyokuwa ya kodi katika Halmashauri za
Wilaya na Miji na katika Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala wa Serikali
uko chini ya lengo. Huku kuendelee
kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Spika;
Kwa
upande wa nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za Serikali tulielekeza nguvu
zetu katika kuimarisha utaratibu wa manunuzi Serikalini na ukaguzi wa hesabu za
Serikali. Kwa upande wa ununuzi wa
bidhaa na huduma, tumeendelea kuimarisha Sheria na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma
ili iweze kuhakikisha kuwa kuna usimamizi thabiti wa sheria hiyo na kanuni zake.
Kama mjuavyo sehemu, kubwa ya fedha za Serikali hutumiwa katika ununuzi wa
bidhaa na huduma, hivyo kuwepo usimamizi mzuri ni jambo jema. Ukikosekana, wizi
na rushwa hutawala.
Mheshimiwa
Spika;
Kwa upande wa ukaguzi wa hesabu za Serikali, tumechukua hatua za
makusudi za kuimarisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Tumetunga Sheria mpya inayoipa nguvu na uhuru zaidi Ofisi hiyo. Aidha, tumewaongezea
bajeti, vitendea kazi na rasilimali watu.
Ofisi 8 za Mikoa zimejengwa
na 2 zinaendelea kujengwa.
Nafurahi kwamba maagizo yangu kwa viongozi na watendaji katika Serikali
Kuu na Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali kupewa uzito linazingatiwa. Taarifa hizo sasa zinasomwa,
zinajadiliwa na hatua kuchukuliwa kwa kasoro zilizoonekana. Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali imefanya kazi nzuri.
Wezi na wabadhirifu wanaobainika kuchukuliwa hatua za kisheria mara
makosa yanapogundulika. Kitaifa taarifa
hiyo hujadiliwa Bungeni kwa muda wa kutosha.
Mheshimiwa
Spika;
Niliamua pia kuanzisha Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali na
kuwaweka Wakaguzi wa Ndani wote wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa chini ya
Mamlaka yake na kuwajibika kwake. Ofisi hii imesaidia kuhakikisha sheria na
kanuni za matumizi ya fedha na mali ya umma zinaheshimiwa. Pia, katika
ufuatiliaji na utekelezaji wa mapendekezo ya CAG. Uimarishaji wa ukaguzi wa
ndani na ule wa CAG umesaidia kuboresha hesabu za Serikali kuwa
nzuri zaidi siku hizi. Hati safi zimeongezeka na hati chafu zinazidi kupungua
Serikalini. Kwa mfano katika Halmashauri za Wilaya na Miji, hati safi
zimeongezeka kutoka 56 mwaka 2006
hadi 150 mwaka 2014. Hati zenye
mashaka ni 13 na hakuna Hati
isiyoridhisha. Kazi ya kuimarisha
ukaguzi na nidhamu ya matumizi lazima iendelezwe.
Maadili
ya Viongozi wa Umma
Mheshimiwa
Spika;
Katika miaka 10 hii tumeimarisha mfumo wa kusimamia maadili
ya viongozi. Tumefanya hivyo kwa kutambua kuwa maadili mema ni sifa ya msingi
ya kiongozi na huiletea heshima Serikali. Tumeendeleza Kamati ya Maadili na
kuunda Baraza la Maadili kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya
1995. Tumepanua wigo na kwamba sasa mali za viongozi na familia zao hutolewa
taarifa na kiongozi katika Tamko la Mali la kila mwaka. Hii inasaidia kuondoa uwezekano wa kiongozi kuficha
mali kwa mgongo wa mwenza wake au mtoto.
Mheshimiwa Spika;
Kamati ya Maadili sasa
si tu inapokea fomu na kuzihifadhi, bali inafanya ukaguzi wa mali za viongozi
na kuzifuatilia. Kikwazo chao ni kupata rasilimali fedha. Hili litazamwe zaidi.
Pale inapoonekana kuna makosa ya kimaadili wahusika hufikishwa kwenye Baraza la
Maadili. Sote tumeshuhudia kazi nzuri iliyofanywa na Baraza hilo wakati wa
sakata la Escrow. Bado kazi ya
kuimarisha Kamati ya Maadili kwa rasilimali fedha, vitendea kazi, majengo ya
ofisi na rasilimali watu haina budi kuendelezwa.
Muhimili
wa Mahakama
Mheshimiwa
Spika;
Katika
kipindi cha miaka 10 hii tumefanya
jitihada kubwa za kuimarisha mhimili wa Mahakama. Miongoni mwa mambo mengine, tumefanya
mambo muhimu kwa madhumuni ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa jukumu
lake la msingi la utoaji haki.
Kwanza,
tumetenganisha shughuli za kutoa haki na za utawala. Tumeunda Ofisi ya Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya kushughulikia mambo ya fedha na utawala. Hivyo basi, Wasajili wa Mahakama wanabaki na
jukumu la kutoa haki. Mpaka sasa mabadiliko haya yamekuwa ya manufaa makubwa
kwa Mahakama kwani yameboresha utekelezaji wa majukumu katika Mahakama. Pili, tumeanzisha Mfuko wa Mahakama
ambao unaipa Mahakama uhuru katika kuendesha shughuli zake. Sambamba na hilo tumeongeza bajeti ya
Mahakama kutoka shilingi bilioni 36.6 mwaka
2006/07 hadi shilingi bilioni 87.6 mwaka
2014/15. Jambo linalohitaji kuboreshwa ni Hazina kutoa fedha kwa wakati ili
shughuli zifanyike kama ilivyopangwa.
Mheshimiwa Spika;
Jambo
la tatu, ni kwamba tumeongeza idadi
ya Majaji wa Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu Wakazi na Mahakimu wa
Mahakama za Mwanzo. Lengo letu ni
kuongeza nguvukazi ya kusikiliza na kuamua mashauri. Kwa upande wa Mahakimu wa
Mahakama za Mwanzo wameanza kuteuliwa watu wenye Shahada ya Sheria. Hivi sasa
itawawezesha watu wenye mashauri katika Mahakama hizo kupata utetezi wa Mawakili.
Kati ya mwaka 2005 na 2015 tumeongeza Majaji wa Rufani kutoka 8 mwaka 2005 hadi 16, na Majaji wa Mahakama Kuu kutoka 37 hadi 81 katika
kipindi hicho. Hali kadhalika, tumeongeza idadi ya Majaji wanawake. Katika
Mahakama ya Rufani wapo 5 na katika
Mahakama Kuu wapo 32 na kufanya
jumla yao kuwa 37. Hivi sasa tunao
jumla ya Mahakimu Wakazi 1,266
katika ngazi zote za Mahakama. Kati ya hao 534
sawa na asilimia 35 ni wanawake. Idadi
ya Majaji na Mahakimu wanawake hivi sasa ni kubwa kuliko wakati wowote
uliopita.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana
na mipango mizuri iliyowekwa na Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman Mahakama zimepiga
hatua kubwa katika kupunguza mlundikano wa kesi Mahakamani. Majaji wamejiwekea malengo
kwa kila Jaji asikilize na kuamua mashauri yasiyopungua 220 kwa mwaka na kila Hakimu Mkazi mashauri 250 na wale wa Mahakama ya Mwanzo mashauri 260 kwa mwaka. Kwa sababu hiyo, kuanzia Julai, 2014 hadi kufikia
mwezi Machi mwaka 2015 yalifunguliwa mashauri 177,586 na Mahakama ilisikiliza na kuamua mashauri 179,962. Maana yake ni kuwa
zimesikilizwa zote na nyingine zilizobakia miaka ya nyuma. Bila shaka kwa kasi
hii sasa mrundikano wa kesi utabakia kuwa historia katika kipindi kifupi
kijacho. Nawapongeza sana Majaji na
Mahakimu kwa kazi nzuri waifanyayo.
Kwa
upande wa ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu, wamekamilisha ujenzi wa jengo la
Mahakama Kuu za Divisheni ya Kazi pamoja na majengo ya Mahakama Kuu Mikoa ya
Shinyanga na Kagera. Aidha, majengo
mawili ya Mahakama za Wilaya na 12
ya Mahakama za Mwanzo nayo yamekamilika. Hivi sasa, ujenzi unaendelea wa
majengo ya Mahakama Kuu 9 za mikoa
iliyosalia, Mahakama za Wilaya 9 na
za mwanzo 25.
Maboresho
ya Mfumo wa Utoaji Haki
Mheshimiwa
Spika;
Jambo
lingine ambalo tumefanya katika nia ya kuongeza uwajibikaji, ufanisi, na
kupunguza malalamiko ya wananchi na ucheleweshaji wa mashauri ni kutenganisha
kazi ya upelelezi wa makosa ya jinai na uendeshaji wa mashtaka hayo Mahakamani.
Polisi waliokuwa wanafanya yote sasa watashughulikia upelelezi na ofisi ya Mkurugenzi
wa Mashtaka ndiyo inayoendesha mashauri. Tayari Ofisi za Mkurugenzi wa Mashtaka
zimekwishafunguliwa katika kila Mkoa na sasa tunaenda wilayani. Aidha, tumeboresha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali kwa rasilimali watu, vitendea kazi na fedha ili kuongeza ufanisi
katika utendaji wa ofisi hiyo muhimu sana.
Kuna haja ya kuendelea kuongezea rasilimali fedha na vitendea kazi ili
ufanisi uongezeke zaidi.
Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
Mheshimiwa
Spika;
Katika kipindi hiki, tumeimarisha
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kuiwezesha kwa nyenzo, rasilimali
fedha na watu. Tume sasa inafanya kazi katika eneo lote la Jamhuri ya Muungano.
Aidha, kutokana na utumiaji wa mfumo wa elektroniki malalamiko ya wananchi
mengi zaidi yanafikishwa kwenye Tume na mengi yanapatiwa ufumbuzi. Kwa mfano, idadi ya malalamiko yaliyowasilishwa Tume yameongezeka kutoka 9,455 mwaka 2006 hadi 25,921
mwaka 2014 na uwezo wa Tume kushughulikia malalamiko kwa mwaka umeongezeka
kutoka malalamiko 3,021 mwaka 2005
hadi malalamiko 18,501 mwaka 2014.
Utendaji
Serikalini
Maeneo
ya Utawala
Mheshimiwa
Spika;
Kwa nia ya kusogeza
huduma, mwaka 2010 tulianzisha mikoa mipya 4
ya Geita, Simiyu, Njombe na Katavi na wilaya mpya 19. Pia, tulianzisha Halmashauri
45, kata 1,432, vijiji 1,949,
Mitaa 1,379 na vitongoji 8,777. Nimeamua kuanzisha mkoa mpya wa
Songwe kutoka mkoa wa Mbeya na Wilaya sita
kama ifuatavyo: Tanganyika mkoani Katavi, Kigamboni na Ubungo mkoani Dar es
Salaam, Songwe mkoani Mbeya, Kibiti mkoani Pwani na Malinyi mkoani Morogoro. Najua
tulikuwa na maombi mengi lakini kwa sasa tufanye haya.
Maslahi
ya Wafanyakazi
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya
Nne imelipa umuhimu wa juu suala la kuboresha maslahi ya watumishi wa Serikali.
Karibu kila mwaka tumekuwa tunaongeza kima cha chini cha mshahara. Kwa sababu
hiyo, kima cha chini cha mshahara kimeongezeka kutoka shilingi 65,000 mwaka 2005 hadi shilingi 265,000 mwaka wa jana. Mwaka huu tumefikia shilingi 300,000. Najua bado hakikidhi
mahitaji lakini ukilinganisha na tulikokuwa kipindi hiki tumeongeza sana
mishahara ya wafanyakazi. Vile vile, tumeendelea kupunguza kodi ya mapato kwa mfululizo
kutoka asilimia 18 mwaka 2005 hadi asilimia 11 mwaka huu. Dhamira yetu ni
kutaka kutoa nafuu zaidi kwa wafanyakazi.
Vile vile, tumewapandisha vyeo watumishi 233,876 na kulipa malimbikizo ya watumishi 422,348 ya kiasi cha shilingi
bilioni 384.8.
Mheshimiwa Spika;
Tumetekeleza sera ya
ugatuaji wa madaraka kwa wilaya jambo ambalo limelazimu kuongeza rasilimali fedha
na watu kwa Halmashauri za Wilaya na Miji. Kwa ajili hiyo ruzuku kwa
Halmashauri zetu imeongezeka kutoka shilingi
bilioni 780 mwaka 2005/2006 hadi shillingi
trilioni 4.69 mwaka 2015/2016. Aidha, tumeimarisha utumishi katika Halmashauri
kwa kuajiri watumishi wengi wa kada mbalimbali.
Usawa
wa kijinsia
Mheshimiwa
Spika;
Mwaka 2005 niliahidi wakati
wa kampeni na wakati wa kuzindua Bunge la Tisa, kuwa tutaongeza ushiriki wa wanawake
katika shughuli na nyanja mbalimbali za maisha ya watu wa nchi yetu ikiwemo nafasi
za maamuzi. Ninyi na mimi ni mashahidi kwamba tumetimiza ahadi hiyo. Idadi ya Wabunge wanawake imeongezeka kutoka 62 mwaka 2005 hadi 127. Hivi sasa hamsini kwa hamsini ni rasmi katika Katiba
Inayopendekezwa. Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu na Bunge letu tumepata
Spika mwanamke Mheshimiwa Anne Semamba Makinda.
Wanawake wameongezeka
katika ngazi zote kuu za uamuzi. Kwa mfano, tunao Mawaziri wanawake 10, Naibu Mawaziri wanawake 5,
Majaji wanawake 37 na Wakuu wa
Wilaya wanawake wako 53. Kwa upande wa Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu
Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi Watendaji n.k. pia wameongezeka. Katika
elimu nako tuna usawa wa kijinsia kwa upande wa idadi ya wanafunzi wa kike na
wa kiume katika shule za msingi na sekondari.
Katika vyuo vya elimu ya juu, idadi ya wanafunzi wa kike imeongezeka kwa
kasi kutoka 10,039 mwaka 2005 hadi 78,800 mwaka 2014.
Hali ya Uchumi
Mheshimiwa Spika;
Wakati ninaingia madarakani mwaka 2005 niliwaahidi Watanzania wenzangu
kuwa tutafanya kila tuwezalo kujenga uchumi ulio imara na shirikishi. Hususan,
nilisema nitaendeleza sera za mageuzi ya kiuchumi na kuweka misingi madhubuti
ya kukuza uchumi, kuongeza ajira, kuongeza Pato la Taifa na kupunguza umaskini.
Katika miaka kumi iliyopita tumeendelea kusimamia kwa kiwango kizuri sera za
uchumi jumla na sera za uchumi katika ngazi ya chini zinazogusa wananchi wa
kawaida.
Jitihada zetu hizo zimezaa matunda ya kutia moyo. Katika kipindi hiki, Pato
la Taifa lilikua kwa wastani wa takriban asilimia 7. Nchi yetu ni miongoni
mwa mataifa 10 ya Afrika na 20 duniani ambayo uchumi wake unakua
kwa kasi kubwa. Pato ghafi la Taifa limeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka shilingi trilioni 14.1 mwaka 2005 hadi
kufikia trilioni 79.4 mwaka 2014. Hivyo
basi, pato la wastani la Mtanzania nalo limeongezeka kutoka shilingi 441,030 mwaka 2005 hadi shilingi 1,724,416 mwaka 2014.
Mheshimiwa
Spika;
Mauzo
yetu ya nje yameongezeka kutoka Dola za
Marekani bilioni 1.67 mwaka 2005 hadi Dola
za Marekani bilioni 8.76 mwaka 2014[A1] na kutunisha akiba yetu ya fedha za kigeni na
kutuwezesha kuagiza bidhaa na mahitaji ya nchi kutoka nje kwa kipindi cha miezi
4.1 kama tulivyopanga. Mfumuko wa bei ni asilimia
6.1.
Mheshimiwa
Spika;
Kama mjuavyo, mwaka 2000 nchi yetu ilijiwekea Dira
ya Taifa ya Maendeleo ya hadi mwaka 2025. Mwaka 2010 tulitengeneza Mpango wa
Muda Mrefu (Long Term Perspective Plan) wa (2010 – 2025) wa kuongoza
utekelezaji wa Dira kwa miaka 15 iliyobaki. Tuligawa utekelezaji wake katika
Mipango mitatu ya Maendeleo ya Miaka Mitano kila mmoja. Tuko katika hatua za
mwisho za utekelezaji wa Mpango wa Kwanza, (2011/12 – 2015/16) na kuandaa
mpango wa pili (2016/17 – 2021/22).
Mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa
Mheshimiwa Spika;
Kwa
madhumuni ya kuboresha utendaji wa Serikali nilianzisha Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN). Huu ni mfumo mpya wa
kupanga, kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa malengo na shughuli za Serikali
kwa nia ya kuhakikisha kuwa kilichokusudiwa kinafanyika, tena kwa wakati. Tuliamua
kuanza na sekta sita za Elimu, Nishati,
Kilimo, Uchukuzi, Maji na Mapato ya Serikali. Baadae sekta ya afya na uboreshaji
mazingira ya uwekezaji ziliongezwa.
Katika kipindi hiki
kifupi Mpango umethibitisha kuwa wenye manufaa. Mambo katika sekta zilizojumuishwa
katika BRN yameanza kwenda vizuri. Changamoto
yetu kubwa imekuwa ni upatikanaji wa fedha zinazohitajika kwa wakati kutoka
Hazina. Kama changamoto hiyo isingekuwepo mambo yangekuwa mazuri zaidi.
Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara na Uwekezaji
Mheshimiwa Spika;
Kwa kutambua umuhimu wa uwekezaji katika
kukuza uchumi, kuzalisha ajira, kuongeza mapato na kupunguza umaskini, Serikali
yetu imekuwa inachukua hatua thabiti za kutengeneza mazingira mazuri ya
kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje kuchagua Tanzania kuwa nchi inayofaa kuwekeza.
Mwaka 2010 tumetengeneza Sera na kutunga
Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private
Partnership—PPP). Lengo letu ni kuweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi kuvutika
kushirikiana na Serikali katika shughuli za kiuchumi na maendeleo. Faida kubwa ya utaratibu huu ni kuipunguzia Serikali
mzigo wa kuwekeza katika baadhi ya shughuli ambazo sekta binafsi inaweza kubeba
sehemu ya gharama. Hii siyo tu inaongeza
kasi ya maendeleo, bali kuiwezesha Serikali kuokoa fedha ambazo inaweza
kuzitumia kwa shughuli nyingine.
Juhudi zetu za kuboresha mazingira ya
uwekezaji zinaendelea kuzaa matunda mema. Kati ya 2005 na 2014, Kituo chetu cha
Uwekezaji (TIC) kimesajili miradi 7,159 yenye
thamani ya Dola za Marekani bilioni 154.274.
Kati ya miradi hiyo asilimia 49.38
ni ya wawekezaji wa ndani, asilimia
23.41 ni wawekezaji wa kutoka nje na asilimia
27.18 ni miradi ya ubia baina ya Watanzania na wawekezaji wa kigeni. Ajira 16,000 zilipatikana. Ukuaji huu wa
uwekezaji umeongeza mapato ya Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa ya uwekezaji iliyotolewa na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Viwanda na Biashara Duniani (UNCTAD) ya mwaka 2015, Tanzania
inaongoza Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji. Ilipata Dola za Marekani bilioni 2.142 sawa na asilimia 31.5 ya uwekezaji wote katika Jumuiya yetu.
Sekta za Uzalishaji
Sekta ya Kilimo
Mheshimiwa Spika;
Kuendeleza kilimo ilikuwa ni moja ya mambo tuliyoyapa kipaumbele cha
juu. Shabaha yetu kuu ni kutaka kuongeza tija ili uzalishaji uongezeke,
wakulima wapate mavuno mengi, masoko ya uhakika yawepo na bei iwe nzuri ili
mapato yao yaongezeke na umasikini uwapungukie. Vile vile wao na taifa lijitosheleze
kwa chakula.
Kwa ajili hiyo mwaka 2006 tuliasisi Programu ya miaka 7 ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo
(Agricultural Sector Development Programme—ASDP). Katika Programu hiyo,
matatizo yanayofanya tija na uzalishaji katika kilimo kuwa mdogo yalitambuliwa
na kutengenezewa mpango wa kuyatatua. Serikali pia ilianzisha mikakati, programu
na mipango mingine ya kuongeza msukumo katika kuleta mageuzi ya kilimo.
Miongoni mwa hiyo ni mkakati wa Kilimo Kwanza, Mpango wa Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa
Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo
(TAFSIP), Sera ya Umwagiliaji tuliyoitunga
mwaka 2010 na Programu ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika.
Mheshimiwa
Spika;
Pamoja na hayo, tumeongeza pia bajeti ya sekta ya kilimo kutoka shilingi bilioni 233.3 mwaka 2005/06
hadi shilingi bilioni 1,084.7 mwaka
2014/15. Kuongezwa kwa bajeti kumewezesha fedha za ruzuku ya mbolea na pembejeo
kuongezeka kutoka shilingi bilioni 7.5 mwaka
2005/06 hadi shilingi bilioni 299.3
mwaka 2013/14. Matrekta makubwa na madogo yameongezeka kutoka 7,491 mwaka 2005 hadi 16,412 mwaka 2014. Kwa sababu hiyo matumizi
ya jembe la mkono yamepungua kutoka asilimia
70 hadi asilimia 62. Tumeongeza
maafisa ugani kutoka 3,379 mwaka
2005 hadi 7,974 mwaka 2014.
Vituo vya utafiti wa kilimo tumeviongezea rasilimali fedha, watu na
vitendea kazi. Aidha, tumeanza safari ya kufufua mashamba ya mbegu ya Serikali na
kuhusisha sekta binafsi, Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa katika
kuzalisha mbegu. Aidha, tumeimarisha
Wakala wa Mbegu (Agricultural Seed Agency – ASA) na kuongeza uzalishaji wa
mbegu bora kutoka tani 10,477.17
mwaka 2005 hadi tani 32,340 mwaka
2014.
Mheshimiwa
Spika;
Juhudi za Serikali kuendeleza kilimo zimezaa matunda mazuri. Tija katika
uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula imeongezeka. Kwa upande wa mazao ya
chakula uzalishaji umeongezeka kutoka tani milioni
9.66 mwaka 2005 hadi tani milioni
16.01 mwaka 2014. Ongezeko hili limeliwezesha taifa letu kujitosheleza kwa
chakula kwa asilimia 125 mwaka 2014
ikilinganishwa na asilimia 95 mwaka 2005. Uzalishaji wa mazao ya asili ya biashara
umeongezeka toka tani 427,738 mwaka
2005 hadi tani 569,054 mwaka 2014 na
uzalishaji wa mbegu za mafuta umeongezeka karibu ya mara 4 toka tani 1,389.9 mwaka
2005 hadi tani 5,545.6 mwaka 2014.
Aidha, uzalishaji wa matunda nao umeongezeka toka tani milioni 1.2 mwaka 2005 hadi tani milioni 4.4 mwaka 2014 na maua toka tani 5,862 hadi tani 10,790.
Mheshimiwa
Spika;
Upatikanaji wa masoko ya uhakika na bei nzuri kwa mazao ya wakulima bado
ni changamoto. Pia kuna tatizo la upungufu wa maghala ya kuhifadhi mazao. Jitihada
zinaendelea kupata mkopo au wabia wa kujenga maghala ya kisasa nchi nzima. Programu
ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushiriki ilianzishwa ili kutatua tatizo la
masoko. Aidha, tumeanza maandalizi ya kuanzisha soko la bidhaa (Commodity Market
Exchange) kwa nia hiyo hiyo. Naamini misingi mizuri tuliyoijenga pamoja na kuenea
kwa SACCOS na kuanza kwa Benki ya Kilimo ikiendelezwa itatoa mchango mkubwa
katika kuongeza kasi ya mapinduzi ya kilimo.
Mifugo
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa mifugo, dhamira yetu ilikuwa
kuanza safari ya kuleta mageuzi katika sekta hii. Safari hiyo tumeianza kupitia
Programu ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo. Changamoto zinazochangia maendeleo duni
ya sekta hii zimeainishwa na kutengenezewa mkakati wa utekelezaji. Katika kipindi hiki malambo 1,008, majosho 2,364 na maabara 104 za mifugo zimejengwa. Visima virefu
101 vimechimbwa, malambo 370 na majosho 499 yamekarabatiwa katika kipindi hiki cha miaka 10.
Ukarabati na ujenzi wa majosho umeongeza idadi kutoka 2,177 mwaka 2006 hadi 3,637 mwaka 2015. Tumeongeza Maofisa
Ugani kutoka 2,270 mwaka 2005 hadi 6,041 mwaka 2014. Kuhusu uhamilishaji,
tumeongeza vituo kutoka kituo 1
mwaka 2005 hadi vituo 8 mwaka 2015
na kuwezesha ng’ombe 955,360
kuhamilishwa katika miaka 10 hii.
Mheshimiwa
Spika;
Mazingira mazuri ya uwekezaji kwa
sekta binafsi tuliyoyajenga yamewezesha viwanda vya kusindika nyama, maziwa na
vyakula vya mifugo kuongezeka. Viwanda vya kusindika maziwa vimeongezeka kutoka
22 mwaka 2005 hadi 74 mwaka 2015. Viwanda vya kuzalisha
vyakula vya mifugo vimeongezeka kutoka viwanda 6 mwaka 2005 hadi 80 mwaka
2015 vikiwa na uwezo wa kusindika tani milioni
1.4 za vyakula hivyo kwa mwaka. Aidha viwanda na machinjio ya kisasa 9 vimejengwa katika kipindi hiki.
Usindikaji wa ngozi pia umeongezeka kutoka vipande 790,000 mwaka 2005 hadi vipande milioni 3.78 mwaka 2014. Hivi sasa kwa mfano, uzalishaji wa malisho ya
mifugo (hei) umefikia marobota 957,860
ikilinganishwa na marobota 178,100
mwaka 2005.
Safari yetu ya kuanza kuondoka kwenye uchungaji kwenda kwenye ufugaji
imeanza. Vijiji vingi vimeandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi na hivyo vimetenga
maeneo ya kilimo na ya ufugaji. Tuendelee kuhimiza vijiji vyetu kutekeleza mipango
hiyo ili wafugaji wapate maeneo ya malisho mbali na mazao ya wakulima. Pia, tuhimize
uhamilishaji kama mlango wa kuingilia kwenye kuboresha kosafu za mifugo yetu.
Uvuvi
Mheshimiwa Spika;
Wakati nazindua Bunge la Tisa tarehe
30 Desemba 2005 nilisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nne itatoa kipaumbele kwenye
kuendeleza sekta ya uvuvi. Katika kutekeleza hayo tumefanya yafuatayo. Kwanza, nimeunda Wizara mpya ya Mifugo
na Uvuvi. Pili, tulifuta kodi ya
zana za uvuvi ili kuwawezesha wavuvi kupata zana bora na za kisasa kwa bei
nafuu zaidi. Tatu, tumeimarisha vyuo
vya uvuvi na hivi sasa vina uwezo wa kudahili wanafunzi 1,215 ikilinganishwa na wanafunzi 127 mwaka 2005. Hii imetuwezesha kuongeza wagani wa uvuvi kutoka 103 mwaka 2005 hadi 540 mwaka 2014. Nne, tumeongeza sana juhudi za kupambana na uvuvi haramu ili
kutunza mazingira, mazalia ya samaki na kuzuia kuvuliwa au kuuawa kwa samaki wadogo.
Tumeimarisha maabara ya Taifa ya Samaki pale Nyegezi kwa vifaa vya
kisasa na wataalamu ili iende na wakati. Tano,
tumeongeza msukumo wa kuhimiza ufugaji wa samaki na kuwezesha mashamba ya
samaki kuongezeka kutoka 13, 011
mwaka 2005 hadi 20, 325 mwaka 2014.
Uvuvi haramu unapungua. Mapato ya sekta ya uvuvi yameongezeka kutoka shilingi bilioni 351.6 mwaka 2005 hadi shilingi trilioni 1.8 mwaka 2013. Bado tuna kazi kubwa ya kufanya katika sekta hii ili kuongeza
tija na mapato ya wavuvi na taifa.
Utalii
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa utalii, tumeendelea na
jitihada za kuiendeleza sekta hii muhimu. Tumeongeza kutangaza vivutio vya
utalii vya nchi yetu katika masoko makubwa duniani. Sekta ya utalii imekua kwa wastani
wa asilimia 7.1 na imechangia asilimia 25 ya mapato ya fedha za
kigeni. Idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii 612, 754 mwaka 2005 hadi watalii 1,140,156 mwaka 2014. Idadi ya vitanda katika mahoteli imeongezeka
kutoka 15,828 hadi 21,929. Mapato pia yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 823.05 mwaka
2005 hadi Dola za Marekani bilioni 2
mwaka 2014. Ajira za moja kwa moja zimeongezeka kutoka 32,673 hadi 686,130 na zisizokuwa
za moja kwa moja kutoka 165,883 hadi
1,318,109. Haya ni mafanikio makubwa na ya kujivunia.
Mheshimiwa
Spika;
Katika kipindi hiki tumekabiliana na tukio kubwa la ujangili wa wanyamapori
hasa wa ndovu kutokana na kushamiri kwa biashara ya meno ya ndovu na bei kuwa
kubwa katika nchi za Mashariki ya Mbali. Vuguvugu la ujangili lilifikia kiwango cha
kutishia kumaliza ndovu nchini na dunia nzima. Tukaamua kuchukua hatua za kuidhibiti
hali hiyo. Tumefanya operesheni tatu kukabiliana na tishio hili. Ya kwanza, iliendeshwa na Idara ya
Wanyamapori na Misitu wakishirikiana na TANAPA na Ngorongoro Conservation
Area. Hii hasa ilihusu kupambana na
ujangili katika hifadhi na mapori ya Kaskazini mwa Tanzania. Mafanikio makubwa
yalipatikana.
Mheshimiwa
Spika;
Operesheni ya pili ni ile
iliyohusisha Jeshi la Polisi katika hifadhi na sehemu nyingine za Tanzania.
Operesheni Kipepeo kama ilivyoitwa nayo ilipata mafanikio. Na ya tatu, Operesheni Tokomeza iliyohusisha
vyombo vyote vya ulinzi na usalama. Pamoja na changamoto zake operesheni hizi zimesaidia
sana kupunguza kasi ya ujangili nchini. Matokeo yake katika sensa ya ndovu
iliyofanyika mara ya mwisho, ukiacha Ruaha, hali katika hifadhi na mapori mengine
ina muelekeo mzuri.
Kuundwa kwa Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA) yenye mamlaka makubwa zaidi ya
kusimamia sekta ya wanyamapori nako kutaimarisha uhifadhi na mapambano ya
ujangili. Kwa mipango na program zilizopo Wizarani, naamini mambo yatakuwa
mazuri zaidi muda si mrefu.
Viwanda
Mheshimiwa Spika;
Katika miaka kumi hii, sekta ya viwanda
imeendelea kukua kwa kasi nzuri ya kutia moyo. Viwanda vikubwa, vya kati na vidogo
vimeongezeka kutoka 11, 544 mwaka
2005 hadi viwanda 51,224 mwaka 2015.
Kati ya mwaka 2005 na 2014 na miradi 751
imepewa leseni za kudumu na BRELA ya kuanzisha viwanda. Mchango wa sekta ya viwanda
katika Pato la Taifa umefikia asilimia 7.3
mwaka 2014 kutoka asilimia 6.8 mwaka 2005. Mchango wa viwanda kwenye mauzo ya nje
umeongezeka kutoka asilimia 9.3
mwaka 2005 hadi asilimia 23.3 mwaka
2014.
Tunategemea ukuaji mkubwa wa viwanda katika Mpango wa Pili wa maendeleo
wa miaka 5 kutokana na misingi imara
tuliyoijenga katika Mpango wa Kwanza. Ujenzi wa kiwanda cha chuma kule Liganga na
makaa ya mawe cha Mchuchuma, unatarajiwa kuanza mwaka huu na kiwanda cha kuchakata
gesi pale Lindi unatarajiwa kuanza baada ya taratibu za kuwapatia ardhi
zitakapokamilika. Hivi ni viwanda vya msingi
na mama ambavyo vitachochea kasi ya ukuaji wa viwanda nchini na uchumi kwa
jumla.
Madini
Mheshimiwa Spika;
Sekta ya Madini ndiyo ya pili baada ya
utalii kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni. Kama nilivyoahidi, tulipitia upya
sera, sheria na mikataba ya madini iliyokuwepo na kutengeneza sera na sheria
mpya. Halikadhalika, tulianzisha mazungumzo
na baadhi ya makampuni ambayo hatimaye yalizaa marekebisho ya mikataba yao na
hivyo kuboresha maslahi ya taifa.
Kufuatia marekebisho hayo, makampuni husika ya madini yanalipa kodi ya
mapato. Bila ya hivyo huenda mpaka leo yangekuwa hayajaanza kulipa kodi. Kutumika
kwa Sheria mpya ya Madini, viwango vipya vya mrahaba na kupunguzwa kwa misamaha
ya kodi vimeongeza mapato ya Serikali. Aidha, tuliunda Wakala wa Ukaguzi wa
Madini Tanzania (TMAA) ambao umewezesha kukagua mahesabu ya migodi kuhusu uwekezaji
na mauzo ya madini na kuwawezesha TRA kutoza kodi stahiki kutoka kwa makampuni
hayo.
Mheshimiwa
Spika;
Mabadiliko haya pamoja na kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta hii
yamewezesha mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa kuongezeka kutoka asilimia 2.9 mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 3.5 mwaka 2014. Thamani ya mauzo
ya madini nje ya nchi pia imeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 655.5 mwaka 2005 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 1.794 mwezi Desemba 2014. Mambo yangekuwa mazuri zaidi kama
bei ya dhahabu isingeshuka katika kipindi hiki.
Mheshimiwa
Spika;
Serikali ilifanya uamuzi wa kulifufua
na kuliwezesha Shirika letu la Madini (STAMICO) kuanza tena kazi ya utafutaji
na uchimbaji wa madini kupitia kampuni zake tanzu. STAMICO kwa kupitia kampuni
yake ya STAMIGOLD imeanza kuzalisha dhahabu na kuuza nje. Vilevile, tumejiunga
na Mpango wa Uwazi wa Uvunaji wa Maliasili (EITI) ambao umesaidia sana katika
kuongeza uwazi katika biashara ya madini na kusaidia katika ukusanyaji wa
mapato kutoka kwenye makampuni ya madini.
Katika kipindi hiki, migodi mitatu
mipya ilianzishwa nayo ni Migodi ya dhahabu wa Buzwagi (Shinyanga) na New Luika
(Mbeya) na mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka (Ruvuma). Aidha, miradi mikubwa mingine 8 imeendelezwa na kufikia hatua ya
kuanzisha mgodi ukiwemo Mradi wa Urani wa Mkuju (Ruvuma), Mradi wa Chuma
Liganga na Mradi wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma (Njombe). Pia, ajira rasmi
kwenye migodi mikubwa nchini imeongezeka kutoka waajiriwa 3,517 mwaka 2005 hadi waajiriwa 15,000 mwaka 2014. Hali
kadhalika, makampuni ya madini yameongeza unununzi wa bidhaa na huduma hapa
nchini (local procurement) kutoka Dola
za Marekani milioni 230.41 mwaka 2005 hadi Dola za Marekani milioni 536.56 mwaka 2014.
Mheshimiwa
Spika;
Katika kipindi hiki pia, tumetenga maeneo
8 kwa ajili ya wachimbaji wadogowadogo. Maeneo haya yamewezesha wachimbaji
wadogo kuchimba madini bila bughudha. Aidha, Wizara imenunua mitambo miwili kwa
ajili ya uchorongaji wa miamba kusaidia utafiti wa madini kwa ajili ya
wachimbaji wadogo. Tumeanzisha mfuko wa kuwakopesha wachimbaji wadogo pale
Wizarani ili kutoa fursa kwa wachimbaji wadogo kupata mikopo ya kuendeleza
shughuli zao.
Nishati
Mheshimiwa
Spika;
Wakati naanza kazi ya
uongozi wa nchi yetu, Tanzania ilikuwa inakabiliwa na ukame mkubwa
uliosababisha upungufu mkubwa wa chakula. Pia kulikuwa na upungufu mkubwa wa
umeme kwa sababu ya mabwawa ya kuzalisha umeme kukosa maji ya kutosha. Serikali ililazimika kulisha watu zaidi ya
milioni 3,776,000 na kukodisha
mitambo ya kuzalisha umeme. Kwa siku za usoni tuliamua kuchukua hatua thabiti
ya kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia na vyanzo vingine kama
vile makaa ya mawe, mionzi ya jua na upepo.
Ujenzi umekamilika wa
bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara na Songo Songo litakaloongeza kiasi cha
gesi kuja Dar es Salaam na kuwezesha uzalishaji wa megawati 3000 za umeme. Wakati huo huo kazi ya kujenga vituo vya
kufua umeme inaendelea pale Kinyerezi, Dar es Salaam. Umeme huo utakidhi mahitaji ya umeme sasa na
miaka kadhaa ijayo.
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki tuliunda Wakala wa Umeme
Vijijini (REA) ambao wamefanya kazi kubwa na nzuri ya kusambaza umeme kwa
vijiji 5,336 kati ya vijiji 12,423 nchini. Kazi kubwa iliyofanyika vijijini
inapochanganywa na ile ya mijini imeongeza idadi ya Watanzania wanaopata umeme
kutoka asilimia 10 hadi asilimia 40 mwaka 2015. Uamuzi uliofanywa katika Bajeti ya mwaka huu wa
kukusanya fedha kwa ajili ya umeme vijijini kupitia mafuta ya petroli, utasaidia
sana kuongeza kasi ya kusambaza umeme vijijini.
Gesi
Asilia
Mheshimiwa Spika;
Tumepata mafanikio katika
utafutaji wa mafuta na gesi asilia. Kuanzia mwaka 2010 nchi yetu imepata bahati
ya ugunduzi wa kiasi kikubwa cha gesi bahari kuu. Mpaka sasa zimegundulika futi
za ujazo trilioni 47.08. Ukijumlisha na futi za ujazo trilioni 8
zilizogunduliwa takriban miaka 40 iliyopita kule Songo Songo na Msimbati jumla
ya rasilimali ya gesi asilia nchini ni futi za ujazo trilioni 55.08. Kazi ya utafutaji inaendelea na wataalamu wanasema
kuwa Tanzania inaweza kuwa na akiba ya futi za ujazo trilioni 200. Kiasi cha gesi
kilichogunduliwa mpaka sasa ni kikubwa na kufanya Tanzania kuwa mahala papya pa
kuipatia dunia nishati hii.
Gesi asilia
tuliyonayo ikisimamiwa na kutumiwa vizuri itaiwezesha nchi yetu na watu wake
kupata maendeleo makubwa na kuondokana na umaskini. Ni fursa ya aina yake ya kuipatia Serikali
mapato makubwa na kuiwezesha kutimiza kwa uhakika majukumu yake na mipango
yake. Lakini, ili hayo yaweze kufanyika hapana budi pawepo usimamizi mzuri wa hatua
zote muhimu za mnyororo wa thamani: yaani utafutaji, uchimbaji, usafirishaji,
uuzaji wa gesi asilia na matumizi yake nchini kama nishati na mali ghafi ya
viwanda upande mmoja. Upande mwingine inategemea
sana matumizi mazuri ya mapato yatokanayo na rasilimali hiyo.
Mheshimiwa Spika;
Ni kutokana na kutaka
kuhakikisha kwamba mambo yanakuwa hivyo ndiyo maana tumetunga Sera ya Gesi
Asilia na kuwasilisha katika Bunge hili ile Miswada miwili yaani wa Sheria ya
Petroli na ule wa Matumizi ya Mapato ya Mafuta na Gesi. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa
kuipitisha Miswada hii nami nitaitia saini mara nitakapoletewa.
Usafirishaji
na Uchukuzi
Barabara
Mheshimiwa
Spika;
Serikali ya Awamu ya
Nne, imetoa kipaumbele cha juu kwa uendelezaji wa miundombinu ya usafirishaji
na uchukuzi nchini. Hii ni pamoja na barabara, reli, bandari, usafiri wa majini
na usafiri wa angani. Tumeendeleza kazi
ya kuongeza mtandao wa barabara za lami nchini kwa mafanikio makubwa. Karibu barabara kuu zote nchini na zile
zinazounganisha mikoa zimekamilika kujengwa au kazi ya ujenzi inaendelea. Kwa sababu
hiyo hivi leo kutokea po pote nchini kwenda Dar es salaam unafika siku hiyo hiyo,
tofauti na ilivyokuwa zamani watu walichukua zaidi ya siku moja. Adha ya kupita Kenya na Uganda kwa watu wa
Mikoa ya Ziwa tumeimaliza.
Katika mkakati wetu
wa kupanua mtandao wa barabara za lami nchini, tulitambua barabara za urefu wa kilomita 11,474 za kujengwa kwa kiwango
cha lami. Baadae tuliongeza barabara
nyingine na kufikisha kilomita 17,742
katika mpango huo. Utekelezaji wake upo
katika hatua mbalimbali. Tayari ujenzi
wa kilomita 5,568 kwa upande wa
barabara kuu na kilomita 535 kwa barabara za mijini umekamilika.
Ujenzi wa kilomita 3,873
unaendelea. Upembuzi yakinifu na usanifu
umekamilika kwa barabara za urefu wa kilometa
4,965 kinachosubiriwa ni kupatikana fedha ujenzi uanze. Baadhi ya barabara hizo zimo katika bajeti ya
mwaka huu wa fedha. Barabara za urefu wa kilometa
3,336 zinafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
Mheshimiwa Spika;
Katika
kipindi hiki pia, madaraja madogo 7,200
na makubwa 12 yamejengwa na mengine 16 yapo katika hatua mbalimbali za
ujenzi. Miongoni mwa madaraja makubwa yaliyokamilika
ni daraja la Mto Malagalasi na yanayojengwa ni daraja la Kigamboni na lile la
Mto Kilombero. Madaraja haya yalikuwa
miongoni mwa matano yaliyopangwa kujengwa katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa
Miaka Mitano mara baada ya uhuru. Madaraja mawili yaani la Kirumi lilijengwa mwaka
1985 na la Rufiji mwaka 2003. Kwa upande wa vivuko, tumeongeza vipya 15 na kufikisha idadi ya 28 kote nchini mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika;
Tumeongeza
sana fedha katika mfuko wa barabara kutoka shilingi
bilioni 73.08 mwaka 2005/06 hadi shilingi
bilioni 866.63 mwaka 2015/16. Hii itasaidia katika matengenezo ya barabara
za lami tulizojenga na kujenga nyingine mijini. Hali kadhalika itatumika
kuimarisha barabara za udongo na changarawe wilayani na vijijini ziweze kupitika
wakati wote. Katika kipindi hiki
barabara za changarawe zimeongezeka kutoka kilometa
9,424 hadi kilometa 22,089.
Mheshimiwa Spika;
Katika
miaka kumi hii idadi ya vyombo vya moto yaani magari, bajaji na pikipiki
imeongezeka kutoka 1,696,088 mwaka
2005 hadi 3,313,254 hivi sasa. Ongezeko hili linalotokana na hali ya
kiuchumi ya watu wengi kuwa nzuri limezua tatizo la msongamano wa magari katika
miji mingi nchini. Katika jiji la Dar es
Salaam ambako tatizo ni kubwa zaidi na Serikali imekuwa inachukua hatua
mbalimbali kupunguza ukali wake. Tunapanua ukubwa wa baadhi ya barabara, kujenga
barabara za mzunguko (ring roads) na sasa tunaanza ujenzi wa barabara za juu ya
nyingine (flyovers). Tulianzisha matumizi ya treni katika reli za TAZARA na TRC
kusafirisha abiria. Hivi sasa reli hizo
zinasafirisha abiria milioni 2,804,269 kwa mwaka ambao wangehitaji
daladala 253 kwa siku. Mpango mkubwa wa kuendeleza matumizi ya reli,
Dar es Salaam umeandaliwa na tumeanza kuutafutia fedha.
Usafiri
wa Reli
Mheshimiwa
Spika;
Katika
kipindi hiki tumetumia muda mwingi kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayozikabili
reli zetu za TAZARA na TRC. Kimsingi reli hizo zimekuwa zinakabiliwa na matatizo
ya uchakavu wa miundombinu na uongozi na uendeshaji usioridhisha. Kwa sababu ya
matatizo hayo reli hizi ambazo kila moja inaweza kusafirisha tani milioni 5 kwa mwaka zinasafirisha kati
ya tani 200,000 na 300,000 tu. Hivyo basi, mizigo mingi
husafirishwa kwa barabara na kutishia uhai wa barabara ambazo tumezijenga kwa
gharama kubwa.
Kwa upande wa reli ya
kati, uboreshaji wa reli kati ya Dar es Salaam na Tabora unakaribia kukamilika
na utaendelea mpaka Kigoma na Mwanza. Wakati huo huo mchakato wa ujenzi wa reli
mpya ya upana wa kimataifa (standard gauge) unaendelea. Ujenzi unaweza kuanza
mwaka huu kutegemea kukamilika kwa majadiliano na mabenki yaliyoonyesha utayari
wa kutukopesha pesa za ujenzi.
Mheshimiwa
Spika;
Azma yetu ya kufufua
reli ya TAZARA nayo tumeiwekea mkakati. Sisi na Zambia tumekubaliana
kushirikiana kwa karibu katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili reli
yetu hiyo. Bahati nzuri marafiki zetu wa China nao wamekubali kutusaidia katika
mipango yetu hiyo. Ni matumaini yangu kuwa safari hii tutapata ufumbuzi wa
kudumu kwa matatizo yanayoathiri ufanisi wa reli hii yenye umuhimu wa aina yake
kwa uhai na ustawi wa uchumi wa nchi
zetu na watu wake.
Bandari
Mheshimiwa
Spika;
Tumeboresha na
kuimarisha huduma katika bandari ya Dar es Salaam kwa mafanikio makubwa. Mwaka
2014 bandari yetu ilihudumia tani
milioni 14.4 ukilinganisha na tani milioni 6.7 mwaka 2005. Mwaka huu
inaweza kufikia tani milioni 18.
Siku hizi huduma hutolewa kwa saa 24
na kasi ya kupakua, kupakia na kutoa mizigo imeongezeka sana na wizi umepungua
sana. Hata wale walioacha kuitumia bandari yetu wameanza kurudi.
Mheshimiwa Spika;
Kuanza kutumika kwa
mfumo wa Single Custom’s Territory unaorahisisha
upakuaji na upakiaji mizigo ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kumeongeza
zaidi ufanisi. Tuko katika majadiliano na DRC na Zambia ambao nao wameonyesha
nia ya kuingia katika mfumo huu.
Kuongezeka kwa usafirishaji
wa mizigo inayopita nchini kuna faida kwani sekta ya usafirishaji inachangia
zaidi ya asilimia 15 ya pato la
taifa. Hali kadhalika, ujenzi wa gati za
13 na 14 katika bandari ya Dar
es Salaam unaotegemewa kuanza mwezi huu utawezesha huduma ya makasha kuongezeka
kutoka makasha 600,000 hadi makasha 1,200,000. Mipango ya kuboresha bandari
za Mtwara, Tanga na zile zilizo kwenye Maziwa yetu makuu na ujenzi wa bandari
ya Bagamoyo zitaiwezesha Tanzania kunufaika na fursa ya jiografia yake.
Usafiri
wa Anga
Mheshimiwa
Spika;
Katika kipindi hiki tumefanya
jitihada kubwa ya kuwekeza kwenye ukarabati, upanuzi na ujenzi wa viwanja vya
ndege nchini. Tumekarabati Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere ambao
umeongeza uwezo wa kuhudumia kutoka ndege 7
hadi 30 hivi sasa. Aidha tunajenga jengo
la tatu la abiria kwenye uwanja huo lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni 3.5. Ujenzi huo unategemewa kukamilika mwezi Oktoba
mwaka huu. Kukamilika kwake kutauwezesha
uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuhudumia abiria milioni 6 na ndege nyingi zikiwemo ndege kubwa za kisasa za Airbus
380.
Mheshimiwa Spika;
Vile vile, tumeufanyia
ukarabati na upanuzi Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro ambao ni muhimu sana
kwa sekta ya utalii ya ukanda wa kaskazini. Uwanja mpya wa ndege wa Songwe kule
Mbeya umekamilika na hivi sasa unatumika. Hali kadhalika, tumeviboresha upya
viwanja vya ndege vya Arusha, Mafia, Mpanda, Kigoma, Tabora, Mwanza na Bukoba.
Ujenzi, upanuzi na
ukarabati huu tulioufanya, umechangia sana katika ongezeko kubwa la safari za
ndege na abiria nchini. Safari za ndege kuja nchini zimeongezeka toka safari 78 mwaka 2005 zilizokuwa zinatolewa na kampuni 29 za usafiri wa ndege hadi safari 175 zinazotolewa na kampuni 55 mwaka
2014. Aidha, abiria wanaoondoka na kuwasili katika viwanja vya ndege wameongezeka
kutoka 2,172,519 mwaka 2005 hadi
abiria 4,670,380 mwaka 2013. Siku
hizi Watanzania wanaopanda ndege wanaongezeka kwa kasi kubwa.
Mheshimiwa Spika;
Jambo ambalo hatukuweza
kufanikiwa ni lile la kufufua Shirika letu la Ndege. Tumefanikiwa kulifanya
lisife lakini hatukuweza kulihuisha lirejee hata kwenye ile hali yake ya
zamani. Hata hivyo, fikra na mawazo kuhusu
mkakati wa kulijenga upya shirika hilo yapo. Kwa sasa Menejimenti imepewa jukumu
la kuandaa mpango wa biashara unaoeleweka na unaokopesheka, kisha Serikali itaona
namna ya kulisaidia shirika.
Utabiri
wa Hali ya Hewa
Mheshimiwa
Spika;
Sambamba na hayo,
tumeboresha huduma za utabiri wa hali ya hewa. Mamlaka ya Hali ya Hewa
imepatiwa vifaa vipya ambavyo vimeongeza ufanisi na usahihi wa utabiri unaotolewa.
Mwezi Februari 2014 Mamlaka hiyo ilipata cheti cha utoaji wa huduma bora cha
ISO na hivyo kuufanya taarifa zake kutambuliwa kimataifa.
Mawasiliano
Mheshimiwa Spika;
Tumepiga hatua kubwa
katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Tumejenga Mkongo wa Taifa
wa Mawasiliano wenye urefu wa kilometa
7,560 unaounganisha miji mikuu ya mikoa yote ya Tanzania Bara isipokuwa mkoa
mpya wa Simiyu. Kwa Mikoa ya Unguja na Pemba, ujenzi wake utakamilika mwezi
ujao. Katika Awamu ya Pili, Mkoa wa Simiyu na wilaya zote nchini zitaunganishwa.
Ujenzi wa mkongo huu
umechangia katika kuongeza ubora na kasi ya mawasiliano, na kushusha gharama za
mawasiliano. Kwa mfano, gharama za kupiga simu zimeshuka kutoka shilingi 115 kwa dakika mwaka 2005 hadi shilingi 34.92 mwaka 2014 na gharama za intaneti zimeshuka kutoka wastani wa shilingi 36,000 kwa Gigabyte moja mwaka
2005 hadi wastani wa shilingi 9,000
kwa Gigabyte moja (GB 1) mwaka 2014.
Hii imeshusha pia gharama za biashara kwa
kurahisisha mawasiliano na malipo kati ya mabenki na kwa njia ya mtandao na
simu.
Kwa upande wa laini
za simu, zimeongezeka kutoka laini milioni
2.96 mwaka 2005 hadi milioni 28 mwaka 2014. Watu wanaotumia
intaneti wameongezeka toka milioni 1.6
hadi milioni 9.3 mwaka 2014. Kukua kwa mawasilino ya simu kumewezesha
watumiaji milioni 12.3 kupata huduma
ya fedha kupitia simu za mkononi. Kati
ya Julai 2013 na Aprili 2014 jumla ya miamala milioni 972.6 ilifanyika yenye thamani ya shilingi trilioni 28. Huu ni wastani wa zaidi ya shilingi trilioni 2 kwa mwezi na
kufanya Tanzania kuongoza duniani kwa huduma hii.
Mheshimiwa Spika;
Tulitambua kuwa makampuni
binafsi ya simu hayapendi kuwekeza vijijini ambako biashara si kubwa kama
mijini. Kwa kutambua umuhimu wa huduma ya mawasiliano kwa maendeleo, Serikali
iliamua ibebe mzigo huo. Kwa sababu hiyo tumeanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa
Wote (UCSAF) ambao utawezesha kata na vijiji vyote nchini kufikiwa na huduma za
mawasiliano. Mfuko huo umekwisha wezesha jumla ya kata 52 na vijiji 314 kufikiwa
na huduma hizo. Upelekaji wa huduma za mawasiliano kupitia Mfuko huo
zinaendelea kwa kata nyingine 163
zenye vijiji 922, ambapo wananchi milioni 1.2 watanufaika.
Mheshimiwa Spika;
Tumechukua hatua ya kuhakikisha
kuwa mianya ya kodi inazibwa na kwamba makampuni yanalipa kodi stahiki kwa
kununua na kufunga mtambo wa Kusimamia Mawasiliano ya simu nchini. Mtambo huo
unaowezesha Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kukusanya takwimu halisi za
mawasiliano yanayofanywa. Tangu kuanza kutumika kwa mtambo huo, mwaka jana Serikali
imeweza kukusanya shilingi bilioni 24.6
ambazo vinginevyo zisingepatikana. Aidha, tumekuwa nchi ya kwanza Afrika ya
Mashariki kuhama kutoka mfumo wa analojia kwenda digitali. Karibu tutakamilisha
kwa mikoa yote. Tunazipokea nchi kadhaa zinazokuja kujifunza kwetu juu ya
uendeshaji wa zoezi hili.
Ardhi
na Makazi
Mheshimiwa
Spika;
Maisha bora kwa kila
Mtanzania ni pamoja na kuboresha makazi ya watu. Sote tunafahamu kuwa makazi ni
hitajio la msingi la binadamu. Lengo letu la kuboresha huduma za ardhi, nyumba
na makazi limepata mafanikio makubwa. Tumepeleka huduma za utawala wa ardhi
karibu zaidi na wananchi kwa kuanzisha Kanda nane za kusimamia upangaji,
upimaji na utoaji hatimiliki. Uamuzi huu umepunguza lile tatizo la watu
kuchelewa kupata hati miliki. Toka 2006 hadi sasa jumla ya hati 164,275 zimetolewa, vijiji 10,500 vimepimwa na kati yake vijiji 10,341 vimepatiwa hatimiliki.
Mheshimiwa Spika;
Tumetunga Sheria kwa
ajili ya kuwezesha upatatikanaji wa mikopo ya ujenzi na ununuzi wa nyumba.
Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Mikopo ya Nyumba (Mortage Finance) na Sheria
ya Kutambua Milki ya Sehemu ya jengo haswa kwenye maghorofa (Unit Tittles Act)
ya mwaka 2008. Sheria hizi kwa ujumla wake zimewezesha watu wengi zaidi kupata
mikopo ya kujenga au kukarabati nyumba zao na kuwawezesha watu kupata umiliki
wa sehemu ya jengo.
Mabadiliko hayo pia
yamewezesha sekta ya nyumba kukua kwa kasi kubwa na majengo na nyumba za kisasa
kujengwa katika kipindi cha miaka 10 hii. Dar es Salaam ya leo na ile ya 2005
ni tofauti kabisa. Shirika la Nyumba la Taifa,
Wakala wa Nyumba za Serikali, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nayo imefanya
uwekezaji mkubwa sana katika ujenzi wa nyumba katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa
watumishi wa serikali kuwa na nyumba mwaka 2008 tulianzisha Mfuko wa Mkopo kwa
watumishi wa umma ambao hadi sasa umetoa mikopo ya shilingi bilioni 5.4 kwa watumishi 1,169. Pia, tumeanzisha Kampuni
ya Mikopo ya Nyumba kwa ajili ya watumishi wa umma ambayo tayari imeanza kazi.
Mheshimiwa Spika;
Ninayo furaha kueleza
kuwa makazi ya wananchi pia yameendelea kuwa bora. Takwimu za Sensa ya Watu na
Makazi ya Mwaka 2012, inaonyesha kuwa idadi ya nyumba zilizoezekwa kwa bati zimeongezeka
kutoka asilimia 46 mwaka 2002 hadi asilimia 65 mwaka 2012. Kwa lugha
nyingine nyumba zilizoezekwa makuti na nyasi zimezidi kupungua. Haya ni mafanikio makubwa ya kutia
moyo na hatua muhimu katika kuboresha maisha ya Watanzania.
Utafiti
Mheshimiwa
Spika;
Jambo lingine ambalo
tumeliwekea msingi mzuri ni eneo la utafiti.
Hili ndilo eneo ambalo ilitalivusha taifa letu kwenda
katika maendeleo makubwa zaidi. Niliamua Serikali ichukue hatua za makusudi za
kufufua shughuli za utafiti ambazo zilikuwa zinapita katika kipindi
kigumu. Niliamua kuwa Serikali ianze
safari ya kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya utafiti. Tulianza na shilingi bilioni 10 na kuendelea
kuongeza mwaka hadi mwaka na kufika shilingi
bilioni 60 mwaka 2014, katika kipindi cha kujitahidi kufikia asilimia 1 ya bajeti ya Serikali na
hatimaye asilimia 1 ya pato la Taifa
kwa ajili ya shughuli za utafiti.
Mheshimiwa Spika;
Kwa kutumia kiasi
hiki kidogo kilichopo wanasayansi wetu 344
wamepata ufadhili wa masomo ya shahada ya Uzamili na 173 wa shahada ya Uzamivu.
Miradi 70 ya utafiti
imefadhiliwa, kati ya hiyo 22 ni ya
kilimo. Fedha hizi pia zimewezesha Tume
ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia kuanzisha viatamizi vya teknohama ambavyo
vimewezesha vijana wetu kubuni na kuvumbua teknolojia zenye manufaa kwa
maendeleo ya jamii na taifa. Wamezalisha ajira na kunufaisha watu wengi. Kampuni
ya Max Malipo ni mfano mmojawapo mzuri wa matokeo mazuri ya viatamizi hivi.
Huduma
za Jamii
Elimu
Mheshimiwa
Spika;
Katika
hotuba yangu ya kuzindua Bunge la Tisa mwaka 2005 nilisema kuwa, “Hakuna
Taifa lililopata maendeleo bila kuendeleza elimu. Hivyo kuendeleza elimu nchini
itakuwa agenda muhimu ya Serikali ya Awamu ya Nne”. Tumetimiza ahadi. Katika
kipindi chote cha miaka kumi bajeti ya sekta ya elimu ndiyo iliyokuwa kubwa
kuliko za sekta nyingine zote. Mwaka huu 2015 bajeti
ya elimu imefikia shilingi trilioni 3.4
ikilinganishwa na shilingi bilioni 669.5
za mwaka 2005.
Mafanikio
yaliyopatikana katika sekta ya elimu ndani ya miaka 10 hii ni ya kutia moyo.
Tumeongeza shule za msingi kutoka 14,257
mwaka 2005 hadi 16,538 mwaka 2015 na
wanafunzi wameongezeka kutoka 7,541,208
hadi 8,202,892. Upanuzi huu
umewezesha asilimia 98 ya watoto
wanostahili kupata elimu ya msingi sasa kuandikishwa.
Kwa
kushirikiana na wananchi na sekta binafsi tumeongeza Shule za Sekondari kutoka Shule
1,745 mwaka 2005 hadi Shule 4,753 mwaka 2015. Idadi ya wanafunzi
imeongezeka kutoka 524,325 mwaka
2005 hadi 1,804,056 mwaka 2015.
Katika kipindi hiki pia vyuo vya Ufundi vimeongezeka kutoka 184 mwaka 2005 hadi 744 mwaka 2015 na wanafunzi katika vyuo hivyo wameongezeka kutoka 40,059 hadi 145,511 mwaka 2015. Haya ni mafanikio makubwa sana.
Kwa
nia ya kuongeza ubora wa elimu, tumechukua hatua thabiti za kukabiliana na tatizo
la uhaba wa walimu, vitabu, maabara za sayansi na vifaa vya kujifunzia na
kufundishia. Tumepanua mafunzo ya ualimu wa Cheti, Stashahada na Shahada. Hii imetuwezesha
kuongeza idadi ya walimu wa Shule za Msingi kutoka 135,013 mwaka 2005 hadi 202,752
mwaka 2015, na walimu wa Shule za Sekondari kutoka 18,754 mwaka 2005 hadi 88,908
mwaka 2015. Uhaba wa walimu wa masomo ya sanaa si tatizo tena, tunao wa kutosha.
Tuna upungufu wa walimu 20,141 wa
masomo wa sayansi na hisabati. Ninaamini, hata hivyo, kwa programu za kusomesha
walimu wa sayansi vyuoni zilizopo, katika miaka michache ijayo tatizo hili nalo
tutalipatia ufumbuzi. Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Dodoma, mwaka 2014 kimeanza
kudahili wanafunzi 5,000 wa ualimu
wa masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa maabara
za sayansi, katika shule za sekondari za kata tayari maabara 5,979 zimejengwa na nyingine 4,410 ziko katika hatua mbalimbali za
ukamilishaji. Hivi sasa tunashughulikia upatikanaji na usambazaji wa vifaa kwa matumizi
ya maabara hizo. Kwa upande wa vitabu tumeweza kuboresha upatikanaji wake kwa
mwanafunzi wa Shule za Msingi kutoka uwiano wa 1:5 mwaka 2005 hadi 1:3
mwaka 2015. Katika shule za sekondari uwiano ni 1:2 ukilinganisha na 1:8
mwaka 2005.
Mheshimiwa Spika;
Katika
kipindi hiki pia tumeshuhudia upanuzi mkubwa wa elimu ya juu nchini. Idadi ya
vyuo vikuu imeongezeka kutoka vyuo 26
mwaka 2005 hadi 52 mwaka 2015.
Miongoni mwa vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Dodoma na cha Nelson Mandela cha
Arusha ambavyo vimejengwa na Serikali ya Awamu ya Nne. Tumeanza mchakato wa
kujenga Chuo Kikuu cha Julius Nyerere cha Kilimo kule Butiama. Vyuo hivi ni
fahari ya nchi yetu kwani tumevijenga kwa fedha zetu wenyewe bila msaada kutoka
kwa wafadhili. Ongezeko la vyuo vikuu limefanya idadi ya wanafunzi kuongezeka
kutoka wanafunzi 40,719 mwaka 2005 hadi
218,959 mwaka 2014. Idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo nayo
imeongezeka kutoka wanafunzi 16,345
mwaka 2005 hadi wanafunzi 99,590
mwaka huu.
Afya
Mheshimiwa
Spika;
Tumepata mafanikio ya
kutia moyo kwa upande wa kuboresha na kupanua huduma ya afya nchini. Tuliazimia
kusogeza huduma ya afya karibu na wanapoishi watu kwa kujenga vituo vya kutoa
huduma ya afya vipya na kuimarisha vilivyopo. Kati ya mwaka 2005 na 2014 vituo
vya kutolea huduma za afya 2,175
vimejengwa. Kati yake hospitali 19,
vituo vya afya 168 na zahanati 1,883 zimejengwa.
Tumeimarisha
hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Rufaa za Kanda, Mikoa na Wilaya kwa
kuzipatia vifaa vya tiba na uchunguzi (MRI, CT Scan, X ray, Ultra Sounds, Maabara
n.k). Tumejenga maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ambayo inatumika kama maabara
ya Kimataifa ya Rufaa kwa nchi za SADC. Tumeimarisha maabara za mikoa kwa
majengo na vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa magonjwa. Maabara yetu ya Mbeya
sasa ina uwezo wa kubaini virusi vya Ebola jambo ambalo miezi michache
iliyopita tulikuwa tunapeleka sampuli Nairobi.
Hivi sasa hospitali za wilaya zinaweza kufanya uchunguzi wa mwenendo wa
figo na ini.
Mheshimiwa Spika;
Tumeboresha huduma ya
Afya ya Kinywa katika Hospitali ya Muhimbili kwa kufunga mashine 26 za kisasa za tiba ya meno na maabara
ya kisasa ya kutengeneza meno bandia. Pia tumeimarisha huduma ya afya ya kinywa
kwa kuweka vifaa vya tiba ya meno kwenye Halmashuri 91. Hivi sasa hospitali 136,
vituo vya afya 63 na zahanati 3 zinatoa huduma hiyo nchini.
Tumeanza kupata
mafanikio katika dhamira yetu ya kujenga uwezo wetu wa ndani wa kuchunguza na
kutibu maradhi ya figo, moyo, saratani na mishipa ya fahamu ambayo tumekuwa
tunapeleka wagonjwa wengi nje. Kwa mfano, tangu Taasisi ya Moyo ianze kutoa
huduma pale Muhimbili wagonjwa 71,963
wamepatiwa matibabu wakiwemo 692
waliofanyiwa upasuaji. Watu hao wangepelekwa
nje taifa lingelipa pesa nyingi. Uwezo wetu utaongezeka sana hospitali ya
Mloganzila itakapokamilika.
Mheshimiwa Spika;
Tumebadilisha
utaratibu wa kusambaza dawa kutoka Bohari ya Dawa. Tumeongeza bajeti ya dawa na
vifaa tiba kutoka shilingi bilioni 40.6
mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 147
mwaka 2014. Idadi ya watu wanaonufaika na Mfuko wa Afya ya Jamii na Mfuko wa
Bima ya Afya wameongezeka kutoka asilimia
3 mwaka 2005 hadi asilimia 19
mwaka 2014.
Katika kipindi hiki
tumetoa msukumo mkubwa katika kupambana na maradhi makubwa ya kuambukiza
yanayosababisha vifo vya watu wengi. Tumeendesha kampeni ya kupambana na
malaria nchi nzima kwa kubadilisha dawa ya kutibu malaria na kugawa vyandarua 26,371329 kwa watoto chini ya miaka
mitano, kwa akina mama wajawazito na katika kila kaya. Aidha, tumepulizia dawa
ya kuua mbu ndani ya nyumba katika mikoa ya kanda ya ziwa. Matokeo ya jitihada
hizo ni kupungua kwa maambukizi ya malaria kwa asilimia 51 na vifo kwa asilimia
71. Baada ya kiwanda cha kuzalisha dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu pale
Kibaha kuanza uzalishaji, safari ya kutokomeza malaria hapa nchini ni ya
uhakika.
Mheshimiwa Spika;
Juhudi zetu katika
kupambana na ukimwi zimewezesha kushuka kwa maambukizi ya ukimwi kutoka asilimia 7.7 mwaka 2005 hadi asilimia 5.1
mwaka 2012. Idadi ya watu waliopima virusi vya ukimwi imeongezeka kutoka 365,189 mwaka 2005 hadi 25,468,564 mwaka 2014. Aidha, tumewezesha
vituo 5,244 na asilimia 97 ya vituo vyote vinavyotoa huduma ya uzazi kutoa huduma
ya kuzia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Mheshimiwa Spika;
Kati ya mwaka 2005 na
2014 tumeongeza udahili wa wanafunzi katika vyuo vya afya kutoka 3,025 mwaka 2005 hadi 11,807 mwaka 2014. Katika kipindi hicho
wataalamu wa afya 55,608
wameajiriwa. Aidha, tumeongeza ajira ya kada mbalimbali za afya. Kwa sababu
hiyo idadi ya madaktari imeongezeka kutoka madaktari 1,048 mwaka 2006 hadi madaktari 2,325 mwaka 2014. Halikadhalika, madaktari wasaidizi wameongezeka kutoka
1,223 hadi 1,914, wauguzi kutoka 15,961
hadi 22,942 wataalamu wa Maabara
kutoka 1,277 hadi 2,378 mwaka 2014. Hivi sasa uwiano wa Daktari
kwa wagonjwa ni 1:6,666 ikilinganishwa
na 1:35,714 mwaka 2005. Na, uwiano
wa Muuguzi kwa wagonjwa umeshuka kutoka 1:2,347
mwaka 2005 hadi 1:2,008 mwaka huu.
Mheshimiwa Spika;
Tumeendesha kampeni
ya kuboresha lishe nchini na kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Lishe (2011-2016). Kwa
ajili hiyo mwaka 2013 tulizindua Programu ya Uongezaji wa Virutubishi. Matokeo ya
jitihada zetu hizo yameanza kuonekana. Udumavu umepungua toka asilimia 44 mwaka 2005 hadi asilimia 35 mwaka 2014 na uzito pungufu
toka asilimia 17 hadi asilimia
13.
Kwa jumla juhudi zetu
za kuboresha huduma ya afya zimezaa matunda ya kuridhisha. Wastani wa umri wa kuishi
wa Mtanzania umeongezeka toka miaka 49 mwaka
2005 hadi miaka 62 hivi sasa. Vifo
vya watoto wachanga vimepungua toka vifo 68
kwa kila vizazi hai 1000 hadi vifo 21 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2014. Vifo vya watoto chini ya miaka mitano
vimepungua kutoka vifo 112 kwa kila
vizazi hai 1000 mwaka 2005 hadi vifo
54 kwa kila vizazi hai 1000 mwaka 2014, na vifo vya akinamama
wajawazito vimepungua toka vifo 578
kwa vizazi hai 100,000 hadi vifo 432 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2012. Haya ni mafanikio ya kutia moyo ingawaje bado
tunatakiwa kuendeleza juhudi zaidi mara dufu ili vifo vipungue zaidi na zaidi.
Maji
Mheshimiwa
Spika;
Serikali ya
Awamu ya Nne imefanya juhudi kubwa katika kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji
safi na salama na usafi wa mazingira katika kipindi hiki. Tumekamilisha miradi
ya maji katika miji mikuu ya mikoa 8,
Wilaya 6 na Miji midogo 2. Aidha, miradi katika miji mingine 13 ya mikoa, 27 ya Wilaya na Miji midogo inaendelea kutekelezwa. Utekelezaji wa
miradi hii umewezesha kiwango cha upatikanaji maji mijini kufikia wastani wa asilimia 86 kwa
mwaka 2014 kutoka asilimia
73 mwaka 2005. Na kwa Vijijini imefikia asilimia 67.6 Mwaka 2014 ukilinganisha na asilimia 53 mwaka 2005. Tumevuka
lengo letu la kuwapatia maji asilimia 65
ya wakazi wa vijijini.
Aidha, miradi
inayoendelea kutekelezwa hivi sasa itakapokamilika katika mwaka huu wa fedha upatikanaji
wa maji mijini utafikia asilimia 90
ambalo ndilo lengo la Ilani ya uchaguzi ya CCM. Vijijini inaweza kufikia asilimia 70 ambayo ni juu ya lengo la asilimia 65.
Aidha,
tumeboresha huduma za uondoaji wa maji taka katika miji ya Tanga, Dodoma,
Mwanza, Mbeya, Iringa, Songea, Tabora na Morogoro. Uboreshaji huu wa huduma za
utoaji wa maji taka ni mwanzo mzuri katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na
mipango mizuri ya maji taka mijini.
Uwezeshaji wa Wananchi
Mheshimiwa Spika;
Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ilikuwa
ni moja ya dhima kuu ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Katika kutekeleza
dhamira hii, Serikali imeendeleza kwa mafanikio makubwa mifuko ya kutoa mikopo
kwa vijana, wanawake, wajasiriamali wadogo na kuanzisha fursa nyingine mpya. Watu
wengi wamenufaika na wao wenyewe kuwa chachu ya kuzalisha ajira, kupunguza umasikini
na kuinua hali za maisha ya watu walioguswa na fursa zilizopatikana.
Tumeiwezesha Benki ya Wanawake kuanza na kuendelea kutoa huduma. Kama
mjuavyo niliamua Serikali ichangie mtaji wa mwanzo na inaendelea kuchangia
mtaji huo. Tayari Benki hiyo imeshakopesha watu 125,000 na kati yao wanawake ni asilimia 82. Hali kadhalika, nilifanya uamuzi wa makusudi wa
kuifufua Benki ya Rasilimali (TIB). Dhamira yangu ni kutaka iwepo Benki ya maendeleo
itakayotoa mikopo ya muda mrefu na wa kati kwa wawekezaji wazawa. Hii
itawezesha kuanzisha na kuendesha shughuli za viwanda, madini, utalii na
biashara kwa urahisi.
Tumeiwezesha Benki ya Rasilimali kwa mtaji, rasilimali watu na vitendea
kazi na kuifanya iwe moja ya benki ya kutumainiwa nchini. TIB imeshatoa mikopo
kwa makampuni 365 yenye thamani ya shilingi bilioni 512. Aidha, imetoa
mikopo kwa miradi 201 yenye thamani
ya shilingi bilioni 156 kupitia
dirisha dogo la kilimo. Natoa pongezi maalum kwa viongozi na watumishi wa Benki
ya Rasilimali kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya katika kipindi hiki
kifupi. Naomba waendelee na moyo huo kwa
maslahi ya nchi yetu.
Mheshimiwa
Spika;
Tumetimiza ahadi yetu ya kuimarisha ushirika nchini kama nguzo kuu ya
kuunganisha nguvu za wanyonge kujiletea maendeleo. Katika kipindi hiki, idadi
ya Vyama vya Ushirika vya aina mbalimbali nchini imeongezeka kutoka 5,832 mwaka 2005 hadi 9,604 mwaka 2015.
Kwa upande mwingine, Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS), vimeongezeka
zaidi ya mara tatu kutoka vyama 1,875
mwaka 2005 hadi 5,559 mwaka 2014[A2] . Akiba, hisa na amana za wanachama zimeongezeka kwa
zaidi ya mara tano kutoka Shilingi
bilioni 85.6 mwaka 2005/2016 hadi Shilingi
463 bilioni mwaka 2014 na mikopo kwa wanachama imekua mara 13
toka shilingi bilioni 65.7 hadi shilingi bilioni 893 mwaka huu. Kwa
hakika haya ni mafanikio makubwa ya kujivunia. Watu wengi wamewezeshwa
kupunguza umasikini wao na wengine kuondoka katika lindi la umasikini.
Sanaa
na Michezo
Mheshimiwa
Spika;
Niliahidi kusaidia
kukuza michezo na sanaa nchini. Kwa upande wa michezo niliahidi kuwa Serikali
italipia makocha. Nilitimiza ahadi yangu
kwa michezo ya soka, netiboli na ngumi. Kwa upande wa riadha tuliwapeleka
wanariadha wetu China, Ethiopia na New Zealand kwa maandalizi ya mashindano ya
kimataifa. Timu yetu ya taifa ya soka haijafanya vizuri sana. Kwa upande wa
soka tulianza kupata matumaini lakini baadae yakafifia. Timu yetu ya taifa ya
soka haijafanya vizuri sana pamoja na kubadili makocha. Hata vilabu vyetu pia
havifanyi vizuri. Kwa kweli lazima Watanzania tukae chini na kujiuliza kwa nini
hatufanyi vizuri na tufanye nini tufanikiwe.
Mheshimiwa Spika;
Nilifanya
uamuzi wa kurejesha michezo mashuleni pamoja na mashindano ya michezo kwa shule
za msingi na sekondari (UMISHUMTA na UMISETA). Nia yetu ni kutaka vipaji
vya michezo vya vijana viibuliwe wakiwa bado wadogo na kuendelezwa. Uamuzi huu
umerejesha uhai na matumaini kwamba siku za usoni tutaona matunda yake.
Kwa dhamira hiyo hiyo,
kwa kushirikiana na Kampuni ya Symbion Power na Klabu ya Soka ya Sunderland
kituo cha kuandaa wanamichezo wadogo kinajengwa pale Kidongo Chekundu, Dar es
Salaam. Kituo hiki kinatarajiwa kuwa tayari ifikapo mwezi Septemba, 2015. Kikitumiwa vizuri huenda ikawa ndiyo mwanzo
wa safari ya uhakika ya kuendeleza soka hapa nchini. Tukifanikiwa Kidongo
Chekundu, vituo vingine kama hivyo vinaweza kuanzishwa sehemu nyingine nchini na
wadau mbalimbali.
Mheshimiwa Spika;
Tumepata mafanikio ya
kuridhisha kwa upande wa sanaa za filamu na muziki. Vijana wetu wa tasnia hizi
wamekuwa wanafanya vizuri kiasi kwamba leo hii Bongo Flavor na Bongo Movie
zimevuka mipaka ya Tanzania. Zinaitangaza sanaa ya Tanzania, lugha ya Kiswahili
pamoja na nchi yetu. Vijana hawa wameitoa kimasomaso Tanzania na kutufutia
unyonge tunaopata kwenye michezo. Tasnia hizi zimeajiri vijana wengi, wanalipa
kodi na wanasaidia sana katika kuhamasisha na kufikisha ujumbe kwa mambo muhimu
katika jamii.
Mheshimiwa Spika;
Kwa
nia ya kutaka kuendeleza ujuzi, mbinu na maarifa kwa wasanii wetu mwaka wa jana
niligharimia timu ya watu wazoefu wa fani za muziki na filamu kutoka Marekani
kuja nchini kutoa mafunzo ya muda mfupi. Ninafanya mipango waje tena kwani mafunzo ya
mara kwa mara yatawaimarisha wasanii wetu.
Kwa wasanii wa muziki
niliwatimizia maombi yao ya kutaka kuwa na mastering
studio. Kwa wote nimefanya jitihada
kubwa ya kutafuta majawabu kwa tatizo sugu la kupata malipo ya haki kwa kazi
wazifanyazo. Tumetunga Kanuni ambazo zimewezesha
kazi za wasanii kutambuliwa na kulindwa. Halikadhalika, tumeweza kuanza
utaratibu mpya wa kusambaza kazi za wasanii ambapo wao wenyewe wana sauti nazo.
Nitajitahidi katika kipindi kifupi kilichobaki niyasukume kwa kasi masuala yaliyosalia
ili niwaache wasanii wetu mahali pazuri.
Nataka wapate malipo ya haki kwa vipaji vyao na jasho lao ili wainue
hali zao za maisha.
Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa
Spika;
Wakati nalihutubia
Bunge la Tisa tarehe 30 Desemba 2005 niliahidi kwamba Serikali
itafanya kila iwezalo kuhakikisha Tanzania inakuwa na uhusiano mzuri na mataifa
mengine duniani, na mashirika ya kimataifa na kikanda.
Leo, miaka 10 baadae napenda kuwahakikishia kuwa ahadi yetu tumeitekeleza, tena
vizuri kuliko tulivyotegemea. Tanzania ni rafiki wa kila nchi na kila shirika
la kanda na kimataifa. Hadhi yetu katika uso wa kimataifa imepanda sana. Tunaheshimiwa,
tunasikilizwa, tunathaminiwa na kuaminiwa na mataifa makubwa na madogo.
Katika kipindi hiki
tumetembelewa na wageni wengi mashuhuri kutoka mabara yote. Tumeweka historia
kwa kutembelewa mfululizo na Marais wawili wa Marekani yaani Rais George W. Bush
mwaka 2008 na Rais Barack Obama mwaka
2013, na Marais wawili wa China Rais Hu
Jintao mwaka 2009 na Rais Xi Jinping mwaka 2013. Pia tulitembelewa na Wafalme,
Marais, Mawaziri Wakuu na Mawaziri kutoka nchi za Mabara yote duniani. Aidha,
tumetembelewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais wa Umoja wa Ulaya, Rais
wa Benki ya Dunia n.k.
Tumeshirikishwa
katika shughuli nyingi na mikutano mingi. Nimepata fursa ya kushiriki katika
mikutano mbalimbali ya kimataifa pamoja na miwili ya G8 kuwakilisha Afrika.
Nimewahi kushiriki na kupewa dhamana ya uongozi katika kamati na Tume kadhaa za
Afrika na dunia. Nimewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (2008), Mwenyekiti
wa Kamati ya Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi, Mjumbe wa
Danish Africa Commission, Mwenyekiti
wa ALMA. Hivi karibuni nimeteuliwa kuwa Mwenyekiti
wa Tume ya Umoja wa Mataifa Kupendekeza Namna Bora kwa Dunia Kushughulikia
Majanga ya Afya.
Mheshimiwa Spika;
Katika kipindi hiki tumefungua
Balozi mpya 5 katika nchi za Oman, Malaysia,
Brazil, Uholanzi na Comoro. Hii inafikisha
idadi ya Balozi zetu kuwa 35. Pamoja
na ufinyu wa bajeti jitihada zimekuwa zinafanyika kuboresha huduma kwa Balozi
zetu na wanadiplomasia wetu. Tumejenga jengo la Ubalozi New Delhi na kununua
majengo ya ofisi ya kitega uchumi Washington DC, New York na Ufaransa. Tumeanzisha Kurugenzi ya Diaspora katika
Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ili kuwashirikisha
Watanzania waishio ughaibuni katika maendeleo ya nchi yetu.
Ushirikiano
wa Kanda
Mheshimiwa Spika;
Tanzania imeendelea
kuwa mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC, Umoja wa Afrika
na Umoja wa Mataifa. Tumepiga hatua kubwa katika kuimarisha na kuendeleza
utengamano wa Afrika Mashariki. Katika miaka 10 hii tumefanikiwa kukamilisha utekelezaji wa Umoja wa Forodha
tarehe 1 Januari, 2010 na tarehe 1 Julai, 2010 tulianza utekelezaji wa Soko la
Pamoja ambao unaendelea hivi sasa. Tumetia saini Itifaki ya Umoja wa Sarafu
Novemba 2013 ambayo utekelezaji wake unaendelea vizuri. Matunda ya utekelezaji
wa utengamano kiuchumi yameanza kuonekana. Kwa mfano, mauzo yetu katika soko la
Afrika Mashariki yameongezeka kutoka bidhaa zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 161 mwaka 2005 hadi bidhaa za Dola za Marekani bilioni 1.2 mwaka 2014. Uwekezaji
nchini Tanzania kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki
umeongezeka toka miradi 35 yenye
thamani ya Dola za Marekani milioni 39.5
hadi miradi 244 yenye thamani ya Dola za Marekani milion 676.5. Haya
yote ni mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu Umoja wa
Maendeleo wa Nchi za Kusini Mwa Afrika (SADC). Tumeendelea kushiriki kwa ukamilifu
katika shughuli za umoja huo. Tumeshiriki kwenye kutafuta suluhisho la Visiwa
vya Comoro, Madagascar, Zimbabwe na DRC.
Salamu
za Kuaga
Mheshimiwa
Spika;
Tulipanga
kufanya mengi na tumefanikiwa mengi, lakini hatukuweza kuyamaliza yote kwa
sababu ya changamoto mbalimbali na kubwa zaidi ni uhaba wa rasilimali fedha na
wakati mwingine rasilimali watu na vitendea kazi. Hata hivyo tumeweza kutekeleza zaidi ya asilimia 88 ya ahadi zetu zilizomo kwenye
Ilani za Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na mipango ya Serikali.
Siku
moja nikiwa Marekani mwandishi mmoja wa habari aliniuliza, je, utakapomaliza
uongozi wako utapenda Watanzania wakukumbuke kwa lipi? Nikamjibu, nitapenda
Watanzania waseme, “Rais Kikwete
alitukuta kuleee! na sasa anatuacha hapa palipo juu”. Mimi na ninyi ni
mashahidi kuwa tulipo leo ni bora zaidi ya kule tulipokuwa jana.
Changamoto
za nchi haziishi kila siku zinaibuka mpya. Kila ukimaliza moja inazaa
changamoto nyingine. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa baba wa taifa ambaye naye
hakumaliza changamoto zote, ndivyo ilivyokuwa kwa Mzee Mwinyi na hivyo ndivyo
alivyoniachia Rais Mkapa. Nami namwachia anayekuja, naye afanye yake na
yatakayobakia atamwachia atakayemfuatia. Jambo linalonipa faraja ni kuwa nami
nimetoa mchango wangu kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Shukrani
Mheshimiwa
Spika;
Nitakuwa
mchoyo wa fadhila nisipokushukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Ghalib
Bilal kwa msaada wako, ushauri wako na ushirikiano wa karibu ulionipatia katika
kipindi hiki cha miaka 5. Nakutakia kila
la heri katika maisha yako baada ya mimi na wewe kumaliza kipindi chetu cha
uongozi. Namshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, ambaye pia alikuwa Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika kipindi changu cha kwanza. Nakushukuru
kwa ushirikiano wako mkubwa, msaada wako na ushauri wako wa hekima na busara
ambao umewezesha mafanikio tuliyoyapata katika kujenga nchi yetu na katika
kuimarisha muungano wetu.
Kwa namna ya pekee
namshukuru Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda, Waziri Mkuu na Kiongozi wa shughuli
za Serikali Bungeni kwa kazi nzuri na ya kutukuka uliyoifanya katika kipindi
cha miaka 8. Umepita katika misukosuko mingi, na wakati
mwingine umebebeshwa lawama isiyokuwa yako. Daima umeonyesha ukomavu, uimara na
kutotetereka. Napenda pia kumtambua
Mheshimiwa Edward Lowassa ambaye katika kipindi kifupi alichokuwa Waziri Mkuu
alifanya kazi kubwa na nzuri.
Nawashukuru
pia Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi, Makatibu Wakuu, Wakuu wa
Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Watendaji na watumishi wote wa Serikali
Kuu na Serikali za Mitaa kwa mchango wao katika kufanikisha majukumu ya Awamu
ya Nne. Mmenisaidia sana. Kwa kweli mafanikio haya tunayozungumza leo yameletwa
na juhudi zenu.
Nawashukuru
viongozi wa dini, asasi za kiraia na vyombo vya habari kwa kuniunga mkono mimi
na Serikali yangu na kwa mchango wenu muhimu.
Nawaomba muendelee kuilea amani ya nchi yetu na watu wake.
Nakishukuru
Chama changu, Chama cha Mapinduzi kwa kuniamini, kuniunga mkono na kunisaidia
kwa karibu, katika miaka yote hii kumi. Wakati wote CCM imekuwa pamoja nami na Serikali.
Kimetoa uongozi wa nchi na kuisimamia Serikali kutekeleza Ilani.
Mwisho
lakini sio mwisho wa umuhimu, naishukuru sana familia yangu. Namshukuru mke
wangu Bi. Salma Kikwete kwa mchango wake mkubwa ulionipa utulivu wa kutekeleza
majukumu yangu. Upo msemo kwamba, “kwa kila mwanaume mwenye mafanikio, yuko
mwanamke”, nawaambia ni kweli.
Shukrani zangu, pia, kwa wanangu na wajukuu zangu kwa kunivumilia pale
walipomkosa baba yao na babu yao. Karibuni
mambo yatakuwa tofauti mtaniona mara kwa mara kiasi kuwa huenda mkanichoka.
Hitimisho
Mheshimiwa Spika;
Ninapoagana
na Bunge letu natambua kuwa baadhi ya Wabunge mnarudi kutetea viti vyenu
nawatakia kila la kheri. Nimewahi kuwa Mbunge, hivyo naelewa hofu na mashaka mliyonayo. Mwenyezi Mungu awape utulivu na subira. Nawatakia mapumziko mema kwa wale ambao mmeamua
kustaafu. Wale wanaogombea Urais waliomo humu nawatakia kila la kheri, na
nawashukuru kwa kuonyesha nia ya kunipokea mzigo huu mzito. Nawatakiwa heri katika matamanio yenu.
Kwa ndugu zangu
Watanzania wenzangu, nawashukuruni kwa kuniamini na kunichagua mara mbili kuwa
kiongozi wa nchi yetu. Nawashukuru kwa
kuniunga mkono wakati wote wa uongozi wangu. Mmenipa heshima kubwa ambayo
sitakaa nisahau maishani mwangu. Ninamaliza kipindi changu cha uongozi nikiwa nawapenda
sana na nitaendelea kuwapenda mpaka siku Mwenyezi Mungu atakaponiita. Nitawa-miss kama mtumishi na kiongozi wenu mkuu
lakini tutakutana kwa urahisi zaidi nikiwa raia. Baada ya hotuba yangu ndefu, sasa
natangaza kuwa Bunge la 10 limevunjwa rasmi, lakini linabakia kuwa hai mpaka
tarehe itakayotangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali kwa mujibu wa Katiba.
Mungu
ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.
Asanteni
kwa kunisikiliza!
[A1]Ni
kwa mujibu wa economic survey, angalizo: takwimu zimewekwa kwenye dola milioni
na sio dola bilioni
[A2]Source
Baraza la Uwezeshaji
No comments:
Post a Comment