Tuesday, August 12, 2014

Shahada bila kujituma sawa na umasikini
Na Mtemi Zombwe

Posted  Jumanne,Agosti12  2014  saa 14:40 PM

“Tanzania, nchi yenye mali nyingi, watu wengi wa Ulaya wanaililia sana... Misitu na wanyama, samaki na madini, ardhi yenye rutuba, mabonde na mito, bahari, gesi na maji ya kutosha.”
Hiyo ni sehemu ya wimbo wa kuitukuza nchi yetu tuliyokuwa tukiuimba shuleni enzi za Hayati Mwalimu Julius Nyerere
Ni wimbo uliotutia hamasa wanafunzi kujenga uzalendo na kufahamu thamani na mali ya nchi yetu. Bahati mbaya sana siku hizi watoto hawaimbi tena nyimbo hizi.
Leo mjadala wangu utajikita kwenye maudhui ya wimbo huu.
Miaka ya hivi karibuni mtazamo wa wanajamii wengi umekuwa siyo kufanya kazi wala kutumia rasilimali zetu kujiendeleza.
Kwa sasa kila mmoja anataka kusoma ili apate shahada. Na wenye shahada wanataka kusoma zaidi ili wapate uzamili na uzamivu(PhD). Huo ndiyo mtazamo wa wengi.
Hata watawala wa nchi hii nao wamedumbukia kwenye mtazamo huo huo. Sasa vyuo vikuu kila mahali vinatoa shahada. Elimu yetu sasa hivi ni shahada. Hata kama hujui chochote ilimradi uwe na shahada! Wengi wamepata shahada. Maelfu ya wahitimu wa vyuo vikuu wanamwagika mitaani kila mwaka. Wengine wanaitwa hadi madaktari au maprofesa.
Hata hivyo, kwa kutumia shahada tulizonazo tunapata majibu ya matatizo yetu? Je, baada ya kupata shahada tunaweza sasa kuzitumia rasilimali zetu kuiendeleza nchi yetu?
Tunaweza sasa kuunda vitu anuai? Tunaweza kuzalisha mahitaji yetu wenyewe? Je, tunaweza kuboresha huduma za jamii wenyewe? Tunaweza kuzalisha uchumi wa familia na jamii yetu?
Ukweli ni kwamba bado. Shahada zinaongezeka na umaskini unaongezeka katika jamii. Shahada zinaongezeka na huduma za jamii zinadhoofika kweli kweli. Shahada zinaongezeka watu mbumbumbu nao wanaongezeka maradufu.
Rasilimali zetu zinanufaisha wageni, sisi bado tunabaki walalamikaji kwenye vyombo vya habari na makongamano. Tatizo ni nini na tufanye nini?
Moja, weka shahada pembeni, jitahidi kufikiri na kubuni mambo mapya yatakayokusaidia kupata majibu ya changamoto zinazokukabili au kuikabili jamii.
Tofauti ya binadamu na wanyama wengine ni ule utashi na uwezo mpana wa kufikiri tuliojaliwa na Mungu. Kwa bahati mbaya binadamu wengi hatuutumii uwezo huo kujiletea maendeleo.
Wenzetu wachache walioendelea, mbinu yao ya kwanza ilikuwa ni kuitumia zawadi hii ya ‘kufikiri’ kuibua mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto za maisha.
Pili, kuthubutu kujituma na kufanya kazi kwa makini na kuwekeza. Baada ya kufikiri na kubuni, sasa ni kufanya kazi kwa makini na kuwa na nia thabiti ya kuleta mabadiliko katika familia na jamii. Bila kuthubutu utalala na njaa na shahada yako.
Kumbuka shahada haiwezi kulima, haiwezi kuvua samaki, haiwezi kubuni mradi, haiwezi kukufyatulia matofali. Ni utashi na kujituma kwako ndiko kunaweza kufanya hivyo.
Mungu ametuumba na vipaji vingi, ambayo vikitumika sawa sawa tunaweza kufanikiwa. Mathalan, kama una shahada mbili na una kipaji cha kucheza mpira, usipocheza, huwezi kupata pesa kutokana na shahada zako.
Hata kama una shahada saba, ukijifungia chumbani, unga, mchele haviwezi kuja eti kwa sababu wewe ni msomi. Usomi siyo tiketi ya mafanikio. Tiketi ya mafanikio ni kuthubutu, kujituma, kufanya kazi kwa bidii na kuwekeza.
Digrii inakusaidia kuziona fursa, lakini uthubutu unakusaidia kuzitumia fursa. Ndiyo maana wazee wetu vijijini hawajui kusoma wala kuandika lakini wana chakula cha kutosha, mifugo ya kutosha, nyenzo za kufanyia kazi na familia zenye afya nzuri na maji ya kumwaga. Wanajituma, wanafikiri, wanathubutu na wanafanya kazi kwa bidii.
Kinachosikitisha ni kwamba: Wengi tukipata digrii tunapenda njia za mkato za kujipatia vipato visivyo halali au kupenda vyeo vya kinyonyaji vya kukaa ofisini kwenye viyoyozi kusaini nyaraka bila kuwa na kazi na kudai masurufu na mishahara mikubwa.
Walioendelea walipenda kufanya kazi na kuwekeza. Walijenga nia za kufanya hivyo bila kuchoka wala kukata tamaa.
Kuna usemi usemao: “Wanaofanikiwa zaidi ni wale wanaoshindwa mara nyingi,” je, utashindwaje kama hujajaribu mara nyingi?
Mungu alitujalia wingi wa rasilimali ardhi yenye rutuba, misitu na wanyama pori. Pia akatupatia madini, mito, bahari, maziwa, wadudu na wanyama wenye manufaa makubwa kwetu. Lakini, bado kuna Watanzania wanaosimama kwa ujasiri na kutamka kuwa “hawana kazi” Watanzania tubadilike!
Kulima shamba kijijini ni kazi; tena ina maana sana kuliko hata kuwa karani mijini. Kuotesha miti ya matunda ni kazi, kuvua samaki baharini ni kazi, kutengeneza maua ni kazi, kuimba ni kazi, kusuka mikeka ni kazi halali kabisa, kufundisha watoto ni kazi.
Wenzetu wa mataifa yaliyoendelea, upepo ni utajiri, sauti ni utajiri, kukimbia kwenye barafu ni utajiri, kushona viatu ni utajiri na kulima ni utajiri mkubwa.
Kila kitu ni sehemu ya kipato. Utandawazi umegeuza kila rasilimali asili kuwa biashara.
Pamoja na wingi wa rasilimali zote tulizo nazo mtu atakaa bila kazi? Ni kasumba mbaya kuelekea kwenye umasikini wa kudumu. Maendeleo siyo shahada! Ni kazi!
Chanzo: Mwananchi-Jumanne.

No comments:

Post a Comment