Tuesday, August 12, 2014

Mkuu wa polisi auawa nchini Libya





MKUU wa Jeshi la Polisi nchini Libya, ameuwawa na watu wasiojulikana katika Mji Mkuu wa nchi hiyo Tripoli, imearifiwa.
Kanali Muhammad Suwaysi alipigwa risasi, alipokuwa anaondoka kwenye mkutano katika eneo la Tajoura, mashariki mwa Tripoli.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya mambo ya Ndani ya Nchi hiyo, baada ya kuuwawa Kanali Suwaysi, wenzake wawili walitekwa nyara na hawajulikani walipo mpaka sasa.
Libya imekumbwa na vurugu zinazosemekana kusababishwa na wapiganaji wa kiisilamu, ambao walisababisha harakati za kumuondoa mamlakani Muammar Gaddafi mwaka 2011.
Maelfu ya watu wamelazimika kutoroka Tripoli.
Zaidi ya miaka mitatu baada ya kuondolewa mamlakani kwa Gadaffi, jeshi la polisi nchini Libya linasemekana kuwa dhaifu,
ikilinganishwa na wapiganaji wanaodhibiti sehemu kubwa za nchi hiyo.

Wapiganaji wa kiisilamu ambao wamekuwa wakizua vurugu nchini Libya
Afisa huyo aliuawa wakati alipokuwa anatoka katika mkutano na maafisa wa mtaa wa Tajoura.
Maafisa wengine wawili waliokuwa naye, walitii masharti ya washambuliaji na kuondoka kwenye gari lao huku wakitekwa nyara.
Mamia ya watu wamefariki katika miezi ya Julai na Agosti katika kile kinachoonekana kuwa kukithiri kwa vurugu.
Chanzo: BBC Swahili

No comments:

Post a Comment