Mganda aliyeua JWTZ
arudishwa kwao
KAMPALA, Uganda
KIONGOZI wa kundi la waasi la Allied
Democratic Forces (ADF) kutoka Uganda, Jamil Mukulu (51) amerudishwa kwao na
kupokewa na vyombo vya dola Ijumaa iliyopita
akitokea Tanzania.
Mukulu alirejeshwa Uganda chini ya ulinzi mkali
akapokewa na Jenerali wa Polisi (IGP) Kale Kayihura, mbele ya waandishi wa
habari na kuwahakikishia kuwa haki itatendeka dhidi ya muasi huyo aliyezisumbua
nchi za ukanda huu katika misitu ya Jamhuri ya watu wa Kongo (DRC).
“Maelfu ya familia za Uganda na DRC walipoteza
ndugu zao kutokana na mtu huyu. Serikali ina deni kwao na sasa haki itatendeka,”
alisema Kayihura ambaye kwa zaidi ya miaka 10 ameshiriki kumsaka Mukulu katika misitu
ya Congo.
Aliongeza kuwa anaipongeza Serikali ya
Tanzania kwa kumkamata mtu huyo hatari na kumfungulia mshtaka katika Mahakama
zao kabla Uganda haijaomba arejeshwe ili wamfungulie mashtaka dhidi ya uhaini,
ugaini na mauaji.
ADF chini ya Mukulu wanadaiwa kukishambulia kikosi
cha kulinda amani cha JWTZ huko Congo na kuwaua askari wawili papo hapo.
Jenerali Kayihura alisema, Mahakama ya Tanzania kwa kutambua kuwa Uganda kuna utawala
wa sheria ilikubali ombo ya kurudishwa mshtakiwa huyo.
Baada ya mapigano ya muda mrefu Januari16,
2014, Jeshi la DRC lilianzisha Operesheni Sukola dhidi ya ADF na kuwatimua wanamgambo
wake katika mapori walikokuwa wamejificha.
Aidha, mwanzoni mwa Aprili mwaka jana ngome kuu
ya ADF iliyopo Madina ilisambaratishwa na kundi hilo kugawanyika, lakini kundi lililoongozwa
na Mukulu lilifanikiwa kukimbia usiku wa manane.
Mukulu, ambayelengo lake kuu lilikuwa ni kumwondoa
madarakani Rais Yoweri Museveni na
kumweka kiongozi wa Kiislamu, alitoroka na wapiganaji 30 wakiwamo maofisa wa juu
17 wa ADF pamoja na familia yake.
Hata hivyo historia ya muasi huyo inaeleza alikuwa
Mkatoliki akifahamika kwa jina la David Amos Mazengo, kabla ya kubadili dini na
kuwa Muislamu mwishoni mwa mwaka 1989.
Inaelezwa kuwa kamanda huyo wa ADF alipewa mafunzo
na kundi la kigaidi la Al Qaeda huko Mashariki ya Kati ingawa Umoja wa Mataifa haujathibitisha
iwapo ADF hupata misaada kutoka katika makundi ya kigaidi ya kimataifa.
Mwisho
Ugiriki
yakubaliwa mkopo ukanda wa euro
BRUSSELS, Ubelgiji
VIONGOZI wa mataifa 19 yanayotumia
sarafu ya Euro wamekubaliana kuisaidia Ugiriki kupata mkopo wa tatu ili
ijikwamue na janga la kuporomoka uchumi.
Katika mkutano uliofanyika mjini
Brussels, Ubelgiji jana Mwenyekiti wa Jumuiya ya Ulaya (EU), Donald Tusk
alisemaviongozi wamekubaliana kwa pamoja kuisaidia Ugoriki.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa
Ugiriki, Alexis Tsipras baada ya mvutano mkali alisema taifa lake litapewa
mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Euri bilioni 35.
“Ugiriki haiwezi kuondoka kwenye
ukanda wa Euro tena,” alisema mkuu wa kamisheni hiyo Jean-Claude Juncker
akifuta minong’ono kuwa ikiwa mazungumzo hayatakwenda sawa Ugiriki itaondolewa
kwene mataifa yanayotumia sarafu hiyo.
Tsipras alisema kwa kujiamini, “Kuondoka
kwenye ukanda huu ilikuwa habari ya zamani tunaamini hivyo. Mkataba una
masharti magumu lakini hatuna namna zaidi ya kukubali ili kujiokoa kiuchumi.”
Kwa upande wake kiongozi wa mawaziri
wa fedha katika ukanda huo, Jeroen Dijsselbloem alisema kiasi cha fedha
walichokopeshwa kinajumuisha Euro bil 50 zitakazoimarisha uwekezaji katika mali
za nchi hiyo, ambapo bilioni 25 kati ya hizo itaimarisha huduma za kibenki.
Benki za Ugiriki zimefungwa kwa wiki
mbili sasa ambapo miamala ya fedha katika mashine haitakiwi kuzidi Euro 60 kwa
siku, hali hiyo imetajwa kuwa ngumu kuliko hali yoyote ya anguko la kiuchumi
kuwahi kutokea hata kusababisha biashara nyingi kufungwa.
Hata hivyo uamuzi wa kuidhinisha
mkopo huo si wa mwisho kwani vikao katika mabunge ya nchi wanachama lazima
viamue kuidhinisha na kukubaliana kwa pamoja kuisaidia Ugiriki kwa mara ya tatu
sasa.
“Bado safari ni ndefu ya kuamua juu
ya makubaliano haya mazito,” alisema Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel jana
asubuhi baada ya kutoka katika kikao.
Kwa upande wake Rais Francois
Hollande wa Ufaransa alisema, “Maamuzi haya yamedumisha utu na mshikamano baina
yetu nchi wanachama. Tumeonyesha kuwa Ulaya ina uwezo wa kumaliza matatizo ya
ukanda wa sarafu ya Euro yaliyodumu kwa miaka saba sasa.”
Inaelezwa kuwa viongozi hao wamekaa
katika meza ya mazungumzo mjini Brussels kwa zaidi ya saa 17 usiku mzima
kuhakikisha mwafaka unapatikana kuisaidia Ugiriki iliyokumbwa na mdororo wa
uchumi katika miaka ya hivi karibuni.
Majadiliano hayo yalianza Jumamosi
kwa mkutano wa mawaziri wa fedha. Wakuu wa nchi walikutana Jumapili mchana na
walijadiliana hadi Jumatatu alfajiri.
Mapendekezo yaliyowasilishwa na
Tsipras yalihusisha utekelezaji wa hatua kali za kubana matumizi zikiwemo
makato ya pensheni ya uzeeni, mageuzi ya masoko na ubinafsishaji mali za umma.
Mwisho
Somalia yaipeleka
Kenya Mahakama ya Kimataifa
MOGADISHU, Somalia
SERIKALI ya
Somalia jana imefungua kesi dhidi ya majirani zao Kenya katika Mahakama ya kimataifa
(ICJ) kutokana na mgogoro wa mpaka baina ya nchi hizo.
Kwa mujibu wa taarifa za kuamini kutoka ndani
ya serikali hiyo zinaeleza kuwa Somalia inailamu Kenya kwa kumiliki sehemu ya
bahari iliyo ndani ya mipaka yake kwa njia isiyo halali.
“Mgogoro huu umekuwepo kwa miaka sita sasa,
ni wa muda mrefu lakini mazungumzo ya ndani inaonekana yameshindikana ndio
maana Somalia wameamua kulipeleka mahakamani,” alisema mtoa taarifa huyo
aliyetaka hifadhi ya jina lake.
Somalia inaipeleka Kenya katika mahakama ya
kimataifa huko The Hague Uholanzi kwa madai imekataa usuluhishi nje ya Mahakama.
Mgogoro huo umekuwa mkubwa baada ya kuwepo
fununu za kupatikana utajiri wa mafuta na gesi katika sehemu hiyo ya bahari.
Mwisho
No comments:
Post a Comment