Tuesday, December 2, 2014

Aliyewakosoa Sasha na Malia ajiuzulu


WASHINGTON, Marekani
 
Mfanyakazi katika chama cha Republican nchini Marekani amejiuzulu baada ya kukosolewa kwa kuwatuhumu wanawe Rais wa Marekani Barack Obama , Sasha na Malia kwa kuwaambia kuwa wamekosa ustaarabu.
Elizabeth Lauten, afisaa mkuu wa mawasiliano wa mwanasiasa mkuu wa chama hicho, Stephen Fincher, alijiuzulu Jumatatu.
Bi Lauten, aliwakosoa watoto wa Obama Sasha na Malia kwenye ukurasa wake wa Facebook baada ya watoto hao kuonekana wakiwa wamevalia sketi fupi kwenye hafla ya jioni.
 
 
Baadaye Lauten alifuta maandiko yake ambayo baadaye aliyataja ya kuumiza moyo na kuudhi.
Bi Lauten pia alikuwa amewakosoa Sasha na Malia kwa kusema walionekana wasio na furaha walipokuwa wamesimama na baba yao katika hafla ya maankuli katika Ikulu ya White House.
Wakati watu wengi walihisi kwamba Sasha na Malia hawakua na furaha kuwa na baba yao katika hafla ile na hata kulizungumzia swala hilo kwenye mitandao ya kijamii,Bi Lauten aliamua kujitoa kimasomaso na kuwakosoa wasichana hao kupitia kwa Facebook.
 
 
Mwanamke huyo akiomba msamaha, alisema baada ya kufanya maombi na hata kuzungumza na wazazi wake na kisha kusoma maandiko yake kuwahusu Sasha na Malia, alihisi kweli aliwakera wasichana hao.
"ningependa kuomba radhi kwa wote niliowaudhi kwa matamshi yangu, na nina ahidi kujifunza na kubadilisha mwenendo wangu, '' alisema Lauten.
Chanzo: BBC Swahili.

Al Shabaab waua 36 Mandera,Kenya


NAIROBI, Kenya
Kundi la wanamgambo nchini Somalia Al Shabaab limekiri kuwaua watu 36 katika shambulio lililotokea kwenye machimbo ya kokoto karibu na mji wa Mandera kaskazini mwa Kenya.
Katika taarifa iliyotolewa kwenye mtandao wa kundi hilo, wanamgambo hao wamesisitiza kuwa ndio waliowaua wakenya hao kwa sababu ya majeshi ya Kenya kuendelea kuwa nchini Somalia.
Taarifa za mauaji hayo zilitolewa kwa mara ya kwanza na Shirika la Msalaba Mwekundu.
Inaarifiwa kuwa wafanyakazi hao walipigwa risasi wakiwa katika mahema ya. Walioshuhudia shambulizi walisema kwamba wapiganaji hao waliwatenga waisilamu na wakristo huku wakiwachinja baadhi, na kuwapiga risasi wlaiosalia.
Wakazi wa eneo hilo wamesema waathirika wote wa tukio hilo ni watu wasio Waislam ambao walikuwa wakifanya kazi katika machimbo hayo yaliyopo Kormey kilomita 15 kutoka mji wa Mandera Kaskazini mwa Kenya.
Tukio hili linafuatia tukio la wiki moja iliyopita ambapo watu wapatao 28 waliuawa katika shambulio la basi la abiria huko Mandera.
 
Kundi la wapiganaji wa Kiislam la Al Shabab wamekiri kuhusika na mauaji hayo.
Mkuu wa Polisi eneo hilo, amesema bado wanafuatilia tukio hilo.
Katika tukio lingine, mtu mmoja ameripotiwa kuuawa nchini Kenya kufuatia mlipuko katika klabu moja ya usiku katika mji wa Wajir kaskazini mwa Kenya.
 
Kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi wa Wajir, Frederick Sishia, shambulio hilo limefanyika saa mbili usiku na kuua mtu mmoja na watu wengine wanne wamejeruhiwa.
Washambuliaji hao walitumia magruneti na silaha nyingine za kijeshi kufanya shambulio hilo.
Wiki iliyopita watu wengi waliuawa eneo la Mandera kaskazini mwa Kenya.
Kenya imejikuta ikilengwa na mashambulio ya kigaidi tangu majeshi yake yapelekwe nchini Somalia kukabiliana na wapiganaji wa Al Shabab. Mbali na miji ya kaskazini mwa Kenya kushambuliwa kila mara, miji mikubwa nchini humo ya Nairobi na Mombasa imekuwa ikilengwa na mashambulio ya kigaidi.
Chanzo: BBC Swahili

Jela miaka 50 kwa kuwaharibu watoto Kenya






NAIROBI, Kenya
Mahakama nchini Kenya imemhukumu kifungo cha miaka 50 jela raia mmarekani kwa kutengeza na kusambaza picha chafu za video za watoto wakifanya vitendo vya ngono.
Terry Ray Krieger alikiri makosa yake mbele ya mahakama mwezi jana. Pia alipatikana na kosa la kuwadhalilisha watoto wadogo huku akinasa vitendo hivyo kwa kanda ya video.
Alikamatwa na maafisa wa usalama Kenya baada ya kupata taarifa kutoka kwa shirika la kimataifa la polisi kwamba alikuwa anasambaza video hizo zilizokuwa zinaonyesha watoto wakifanyiwa vitendo vichafu kwenye mtandao.
Krieger amewahi kushtakiwa kwa makosa sawa na hayo na kufungwa jela nchini Marekani miaka 20 iliyopita.
Polisi wa Kenya walipokea taarifda kutoka kwa polisi nchini Marekanmi wakiwaamiwa kuwa kuna raia mmarekani nchini Kenya anayetengeza na kusambaza video chafu za watoto wadogo wakihishwa na vitendo vya ngono.
Aliomba mahakama kumuonea huruma kutokana na maradhi anayougua ya mifupa lakini mahakama ilisema kuwa maradhi yake sio haiwezi kuwa sababu ya kutowajibishwa kwa makosa yake.
Chanzo: BBC Swahili

Friday, September 5, 2014

China yaishawishi A.Kusini kumzuia Dalai Lama



                                                   Dalai Lama
 
Kiongozi wa kiroho wa Tibet, Dalai Lama, amesitisha ziara yake nchini Afrika Kusini ambako alitarajiwa kukutana na washindi wenzake wa tuzo ya Nobel,mjini Cape Town mwezi ujao.
Kiongozi huyo ambaye yuko uhamishoni, alisitisha ombi lake la Viza kuingia Afrika Kusini baada ya maafisa wake kusema kuwa huenda akanyimwa viza hiyo.
Serikali ya Afrika Kusini imekanusha madai ya kumnyima Dalai Lama Visa kutokana na shinikizo kutoka kwa China ambaye ni mshirika wake mkubwa wa kiuchumi.
China inamuona Dalai Lama ambaye hutetea haki za watu wa Tibet kama kiongozi hatari anayetaka kusambaratisha nchi hiyo.
Miaka miwili iliyopita mahakama ilisema kuwa Afrika Kusini ilikiuka sheria kwa kuchelewa bila sababu kumpa Dalai Lama Viza kuingia nchini humo.
kuchelewa huko kulimaanisha kwamba Dalai Lama asingeweza kuhudhuria sherehe za kuadhimisha miaka 80 ya rafiki yake mkubwa askofu mstaafu Desmond Tutu mjini Cape Town.
CHANZO: BBC SWAHILI

Ajali Mbaya Musoma.....



                                         Miili ya marehemu ikisubiri kutambuliwa.



                                                  Mabasi yaliyogongana leo
Basi la Jumanne lililokuwa linatoka Sirari kwenda Mwanza limegongana uso kwa uso na basi la Mwanza coach lililokuwa linatoka Mwanza kwenda Musoma. Ajali imetokea katika eneo la daraja la sabasaba, Musoma. 

Mpaka sasa inadaiwa zaidi ya watu 40 wamepoteza maisha huku wengine wameumia vibaya.
endelea kufuatilia zaidi... 

Ajali hiyo imehusisha basi la Mwanza coach lenye namba za usajili T 736 AWJ lililokuwa likitokea Musoma kwenda Mwanza na basi la J4 lenye namba za usajili  T 677 CYC likitokea Mwanza kwenda Sirari na gari dogo aina ya Land Cruiser ambayo namba zake  hazikuweza kufahamika mara moja kugongana uso kwa uso majira ya saa 5 asabuhi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kwa niaba ya Mganga Mkuu,Dakatari wa hospitali hiyo Martini Khani alisema kuna idadi kubwa ya maiti zilizopokelewa pamoja na majeruhi na idadi kamili ya vifo na majeruhi itfahamika baadaye.
Wakizungumzia tukio hilo mashuhuda wa ajali hiyo walisema mabasi hayo ambayo yote yalikuwa kwenye mwendo kasi yalikutana kwenye daraja dogo katika eneo hilo huku pia gari dogo aina ya Land Cruiser lililokuwa likitokea Musoma likitaka kulipita basi la Mwanza Coach hali iliyosababisha  kutokea kwa ajali hiyo.

ICC yaahirisha kesi ya Rais Kenyatta



                         Uhuru Kenyatta

Kiongozi wa mashitaka katika mahakama ya kimataifa ya ICC, Fatou Bensouda, ameiomba mahakama hiyo kuahirisha kesi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kwa muda usiojulikana.
Hii ni baada ya malalamiko kutoka kwake kuwa Kenya imekataa kushirikiana na mahakama hiyo katika kuikabidhi ushahidi unaohitajika kuendesha kesi kwa hiyo ina maana kuwa hana ushahidi wa kutosha dhidi ya Kenyatta.
Serikali ya Kenya ilitakiwa kuikabidhi mahakama taarifa za kifedha za Rais Kenyatta pamoja na maelezo kuhusu mali yote anayomiliki.
Katika uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo Fatou Bensouda amesema kuwa hana ushahidi wa kutosha kumfungulia mashitaka Rais Kenyatta ambaye anadaiwa kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya mwaka 2007.
Zaidi ya watu 1,000 walifariki katika ghasia hizo. Bensouda amenukuliwa akisema kuwa halitakuwa jambo la busara kufutulia mbali kesi hiyo hasa ikizingatiwa kuwa Kenya haitaki kutoa ushahidi unaohitajika na mahakama hiyo.
Badala yake aliomba mahakama kuiahirisha kesi hiyo hadi pale Kenya itakapokubali kutoa ushahidi unaohitajika.
Kesi dhidi ya Kenyatta ilipaswa kuanza mapema mwezi Oktoba.
CHANZO: BBC SWAHILI