ISOME HAPA: taarifa ya kamati ya kudumu ya Bunge ya
ardhi, maliasili na mazingira kuhusu tathmini ya matatizo yaliyotokana na
oparesheni tokomeza
2435 Views
1.0
UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika, wakati Bunge likijadili hoja ya
kuahirisha shughuli za Bunge ili kujadili jambo muhimu la dharura kwa mujibu wa
Kanuni ya 47 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2013, iliyowasilishwa na
Mhe. Said Nkumba, Mbunge wa Sikonge kuhusu Mgogoro kati ya Wafugaji na
Wakulima, Hifadhi na Uwekezaji, Mheshimiwa Spika alitoa Uamuzi ‘Speakers
Ruling’ kuwa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ishughulikie
kazi ya kutathmini na kuangalia jinsi Mpango wa Kupambana na Majangili
ulivyopangwa na kutekelezwa na Serikali kupitia ‘Operesheni Tokomeza’.
Kwa
mujibu wa kumbukumbu za Taarifa Rasmi za Bunge za tarehe 1 Novemba 2013, wakati
Bunge likihitimisha Hoja ya Kuairisha Shughuli za Bunge, Mhe. Spika alitoa
uamuzi ufuatao:-
…Kamati
ile ya kawaida ya Maliasili itaendelea na kazi yake ya kufanya tathmini ya
kuangalia jinsi mpango ule wa Kupambana na Majangili ulivyopangwa na ndani yake
itashughulikia kama kulikuwa na uzembe ama kuna watu wanahusika katika kuondoa
maisha ya watu kwa sababu za uzembe …
1.1
Kuundwa kwa Kamati Ndogo ya Uchunguzi
Mheshimiwa Spika, kufuatia uamuzi ulioutoa tarehe 01 Novemba, 2013
Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ilikutana Dodoma tarehe 9 Novemba,
2013 kwa lengo la kujadili utaratibu wa kutekeleza jukumu hilo.
Katika
kikao hicho Kamati iliazimia kuunda Kamati Ndogo kwa mujibu wa Kanuni ya
117(18), ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Tole la 2013 ili iweze kushughulikia
suala hilo kikamilifu.
1.2 Hadidu za Rejea, Wajumbe wa Kamati na muda wa kazi
Mheshimiwa
Spika, Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili
na Mazingira iliyoundwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira kwa agizo lako la tarehe 01 Novemba, 2013, ilipewa Hadidu za Rejea
Nne (4) zifuatazo:-
1)
Kutathmini na kuangalia jinsi Mipango ya Kupambana na Majangili
ilivyopangwa;
2) Kuangalia kasoro zilizojitokeza katika kutekeleza mpango huo;
3) Kutathmini iwapo kulikuwa na uzembe katika kutekeleza Operesheni
Tokomeza ambao ulisababisha watu wasio na hatia kupoteza maisha na mali zao; na
4) Kuchunguza migogoro ya Ardhi inayohusu Wakulima, Wafugaji na Wawekezaji
kwenye maeneo yanayozunguka hifadhi.
Mheshimiwa
Spika, Kamati hii ya uchunguzi iliundwa
na Wajumbe Tisa (9) kama ifuatavyo:-
i. Mhe. James Daudi Lembeli, Mb.
ii. Mhe. Abdulkarim Esmail Shah, Mb.
iii. Mhe. Susan Limbweni Kiwanga, Mb.
iv. Mhe. Kaika Sanin’go Telele, Mb.
v. Mhe. Dk. Henry Daffa Shekifu, Mb.
vi. Mhe. Amina Andrew Clement, Mb.
vii. Mhe. Haji Khatibu Kai, Mb.
viii. Mhe. Muhammad Amour Chomboh, Mb.
ix. Mhe. Dk. Mary Mwanjelwa
Mheshimiwa
Spika, Sekretarieti iliyohudumia Kamati
Ndogo ya Uchunguzi iliundwa na Wajumbe wafuatao:-
i. Ndg. Theonest K. Ruhilabake
ii. Ndg. Gerald S. Magili
iii. Ndg. Chacha T. Nyakega
iv. Ndg. Stanslaus W.Kagisa
Mheshimiwa
Spika, Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira ilitakiwa kutekeleza majukumu yake na kuwasilisha ripoti katika
Mkutano wa Kumi na Nne (14) wa Bunge. Hivyo basi, baada ya uteuzi huo,
Wajumbe wa Kamati Ndogo walipanga kuanza kazi tarehe 25 Novemba, 2013 na
kuikamilisha ifikapo tarehe 15 Desemba, 2013.
1.3
Njia zilizotumika katika kukamilisha kazi
Mheshimiwa
Spika, Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira ilitekeleza majukumu yake kwa kuongozwa na Hadidu za Rejea ilizopewa
kwa kufanya rejea na kuzingatia yafuatayo:-
a)
Kusoma na kuchambua nyaraka zilizoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii
katika kuandaa na kutekeleza Operesheni Tokomeza nchini. Nyaraka hizo ni hizi
zifuatazo:-
i. Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza (Concept Paper)
ii. Tathmini ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
iii. Sheria ya Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge (Na.3) 1988
iv. Sheria ya Wanyamapori (Na. 5) 2009
v. Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la mwaka 2013
b)
Kufanya mahojiano na watu mbalimbali:-
i. Waziri wa Maliasili na Utalii
ii. Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii
iii. Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori
iv. Mkurugenzi Msaidizi Kikosi wa Dhidi ya Ujangili
v. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
vi. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)
vii. Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
viii. Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Hifadhi za Misitu (TFS)
ix. Mahojiano na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge
c)
Kuzuru maeneo yaliyoanishwa katika Taarifa ya Wizara kuhusiana na utekelezaji
wa Operesheni Tokomeza na yale yenye migogoro kati ya Wakulima au Wafugaji na
Wawekezaji katika maeneo ya hifadhi kwa lengo la kuhakiki (verify) masuala
yaliyoainishwa kupitia uchambuzi uliofanywa na Kamati.
2.0
KUPOKEA NA KUCHAMBUA NYARAKA MBALIMBALI ZILIZOHUSU OPERESHENI TOKOMEZA
Mheshimiwa Spika, Hadidu Rejea ya kwanza iliitaka Kamati Ndogo ya Ardhi,
Malisili na Mazingira, kufanya tathmini na kuangalia jinsi mipango ya kupambana
na majangili ilivyopangwa. Ili kukamilisha jukumu hilo, Kamati ilifanya
yafuatayo:-
a)
Kupitia na kuchambaua Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza (Concept Paper)
ulioandaliwa na Wizara
b) Kupitia na kuchambua Tathmini ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
2.1
Uchambuzi kuhusu Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, katika kuchambua Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza kwa lengo
la kupata uelewa zaidi wa namna operesheni hiyo ilivyopangwa na kutekelezwa,
Kamati ilibaini kuwa, mpango huo uliandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii
na ulikuwa na mambo yafuatayo:-
i. Ukubwa wa tatizo la ujangili
ii. Aina za ujangili na sababu za ukuaji wake
iii. Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ujangili
iv. Malengo ya Operesheni Tokomeza
v. Njia zilizotumika kutekeleza operesheni
vi. Maeneo ya operesheni na gharama za utekelezaji
vii. Tamko la Serikali kusitisha Operesheni Tokomeza
2.1.1
Ukubwa wa tatizo la ujangili
Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwa, tatizo la ujangili ni kubwa na
limekuwa likisababisha idadi ya Tembo iendelee kupungua nchini. Takwimu
zinaonesha kuwa, idadi ya Tembo imepungua kutoka 350,000 (miaka ya 1970) hadi
kufikia 55,000 (mwaka 1989). Juhudi za kukabiliana na hali hiyo kupitia
Operesheni zilizowahi kutekelezwa huko nyuma zilisaidia kuongeza idadi
ya Tembo hadi 141,000 (mwaka 2006) ingawa ilishuka tena hadi kufikia
110,000 (mwaka 2009).
2.1.2
Aina za ujangili na sababu za ukuaji wake
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Serikali, vitendo vya
ujangili vinavyofanyika nchini vimegawanyika katika makundi mawili yafuatayo:-
i.
Ujangili wa Kujikimu (subsistance poaching)
Aina hii ya ujangili inahusisha watu wenye kipato kidogo na hulenga zaidi
katika kujipatia kitoweo na fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji mengine.
Ujangili wa aina hii huathiri zaidi wanyama wanaoliwa na si Tembo.
ii.
Ujangili wa Biashara (commercial poaching)
Aina hii ya ujangili inahusisha zaidi watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha na
hulenga kupata nyara zenye thamani kubwa. Wanyama wanaoathiriwa zaidi na aina
hii ya ujangili ni pamoja na Tembo, Faru, Simba na Chui.
Mheshimiwa
Spika, taarifa ilibainisha kuwa,
kuongezeka kwa masoko haramu katika nchi za Asia na Mashariki ya Kati ambayo
yanatoa bei kubwa ya nyara hizo, imekuwa ni chachu ya kuimarika kwa mitandao
inayojihusisha na ujangili (ndani na nje ya nchi) na hivyo kusababisha ongezeko
kubwa la vitendo vya ujangili.
2.1.3
Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ujangili
Mheshimiwa Spika, Mpango Kazi waKupambana na Ujangili ulilenga kujikita
katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ujangili wa wanyamapori na misitu. Mpango
huo ulioelezewa kuwa niwa muda mrefu na kusimamiwa na kikosi kazi cha Taifa
(national task force),umeanisha maeneo yafuatayo kuwa ndiyo yaliyoathirika
zaidi:-
i.
Pori la Akiba Selous
ii. Hifadhi ya Taifa Serengeti, Pori la Akiba Maswa na Pori Tengefu la
Loliondo.
iii. Hifadhi ya Taifa Katavi na Mapori ya Akiba Rukwa na Lukwati.
iv. Hifadhi ya Taifa Mikumi
v. Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi za Taifa Tarangire na Ziwa Manyara.
vi. Mapori ya Akiba Burigi, Biharamuro, Ibanda na Rumanyika.
vii. Mapori ya Akiba Moyowosi, Kimisi, Ugalla na Hifadhi ya Misitu Luganzo.
2.1.4
Malengo ya Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, Operesheni Tokomeza ambayo ilizinduliwa rasmi tarehe
04 Oktoba, 2013 ilikuwa na malengo yafuatayo:-
i. Kuzuia vitendo vya ujangili ndani na nje ya Hifadhi za Taifa, Mapori ya
Akiba, Mapori Tengefu, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na Misitu ya Hifadhi na
kufanya operesheni maeneo yote yaliyoathiriwa na ujangili.
ii. Kuwatambua mapema majangili na kujua nyendo zao ndani na nje ya maeneo ya
hifadhi.
iii. Kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wafanyabiashara haramu
wa nyara za Serikali na mazao ya misitu.
iv. Kuvunja mitandao ya wafadhili, wanunuzi wadogo na wakubwa pamoja na
mawakala wa biashara haramu ya nyara za Serikali na mazao ya misitu.
v. Kufuatilia na kukamata mali za majangili zilizotokana na biashara haramu ya
nyara za Serikali na mazao ya misitu.
2.1.5
Njia zilizotumika kutekeleza Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwa, Mpango Kazi wa Serikali
kuhusiana na Operesheni Tokomeza, uliainisha kuwa operesheni hiyo itaendeshwa
kwa kutekeleza mambo yafuatayo:-
i.
Kufanya uchambuzi wa kina wa watuhumiwa wa mtandao wa ujangili wa nyara za
Serikali na wavunaji na wasafirishaji haramu wa mazao ya misitu.
ii. Kuwakamata watuhumiwa wote waliobainishwa kwenye taarifa za kiintelijensia.
iii. Kupiga picha na kuchora ramani ya eneo la tukio kwa kila mtuhumiwa (sketch
map).
iv. Kuhoji na kuandika maelezo ya watuhumiwa wa ujangili wa nyara za Serikali
na wavunaji na wasafirishaji haramu wa mazao ya misitu.
v. Kukusanya na kuhifadhi vielelezo vyote vitakavyokamatwa kutoka kwa majangili
kwa ajili ya kujenga ushahidi mahakamani.
vi. Kuandika maelezo ya mashahidi na askari wakamataji kwa ajili ya kujenga
ushahidi mahakamani.
vii. Kuandaa mashitaka dhidi ya watuhumiwa na kuwapeleka mahakamani ili sheria
ichukue mkondo wake.
2.1.6
Maeneo ya Operesheni na gharama za utekelezaji
Mheshimiwa Spika, Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza ulianisha kuwepo
awamu mbili za utekelezaji ambazoni; Mpango Kazi wa Muda Mfupi na Mpango Kazi
wa Muda Mrefu.
Katika
Mpango Kazi wa Muda mfupi itafanyika operesheni maalum katika maeneo yote ya
ndani na nje ya hifadhi za wanyamapori na misitu nchi nzima. Maeneo hayo
yaligawanywa katika kanda 12 za utekelezaji kama ifuatavyo:-
i.
Selous, Mikumi, Udzungwa, Lukwika/ Lumesule na Liparamba,
ii. Burigi/Biharamuro, Ibanda/Rumanyika na Rubondo,
iii. Moyowosi, Ugalla na Lugazo,
iv. Serengeti, Loliondo, Maswa, Ikorongo na Kijeshi,
v. Kilimanjaro, Arusha, Mkomazi/Umba, Simanjiro na Longido,
vi. Tarangile, Manyara, Karatu/Ngorongoro, Swagaswaga na Mkungunero,
vii. Rungwa, Ruaha, Mpanda – Kipengele,
viii. Rukwa, Lukwati, Katavi, Lwafi, Piti na Wembere,
ix. Mahale na Gombe,
x. Saadani na kwenye maeneo yenye misitu ya mikoko,
xi. Pori Tengefu la Handeni, Kilindi na Mkinga na
xii. Msitu wa Kazimzumbwi, Kisarawe, Rufiji na Mkuranga
,
Mheshimiwa Spika, ilianishwa kuwa, awamu ya kwanza ya Mpango Kazi wa
muda mfupi ingegharimu jumla ya Tshs. 3,968,168,667/= ambazo zingechangwa na
Taasisi za wanyamapori (WD, TANAPA, NCAA na TFS) kwa kila moja jumla ya Tshs.
992,042,167/=
2.1.7
Tamko la Serikali kusitisha Operesheni
Mheshimiwa Spika, kufuatia michango na malalamiko ya Waheshimiwa Wabunge
wakati wakichangia hoja iliyotolewa na Mhe. Said Nkumba Mbunge wa Sikonge,
pamoja na maagizo ya Bunge kutaka Serikaliitoe maelezo kuhusu hoja zilizotolewa
na Waheshimiwa Wabunge, Serikali ilitoa Tamko la kusitisha Operesheni Tokomeza
tarehe 01 Novemba, 2013.
2.2
Uchambuzi wa Taarifa ya awali ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, taarifa hii ya awali kuhusiana na utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza ilikuwa na mambo yafuatayo:-
i. Washiriki wa operesheni
ii. Awamu za operesheni
iii. Mafanikio ya operesheni
iv. Idadi ya watuhumiwa na kesi zilizofunguliwa
v. Changamoto za operesheni
2.2.1
Washiriki wa Operesheni
Mheshimiwa Spika, Operesheni Tokomeza ilihusisha
jumla ya washiriki 2,371 kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa mgawanyo
ufuatao:-
i. Wanajeshi (885) kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania,
ii. Askari (480) kutoka Jeshi la Polisi,
iii. Askari (440) kutoka Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU)
iv. Askari Wanyamapori (383) kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)
v. Askari (99) kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS)
vi. Askari Wanyamapori (51) kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
vii. Waendesha Mashitaka (23) na
viii. Mahakimu (100
2.2.2
Awamu za Operesheni
Mheshimiwa Spika, Operesheni Tokomeza ilipangwa
kutekelezwa katika awamu Nne (4) kama ifuatavyo:-
i. Awamu ya kwanza ambayo ililenga kusaka Silaha za Kivita na Meno ya Tembo
kutoka miongoni mwa wanaojihusisha na vitendo vya ujangili.
ii. Awamu ya pili ambayo ililenga kusaka silaha zisizomilikiwa kihalali na zile
zinazomilikiwa kihalali lakini zinasadikiwa kutumika kwenye vitendo vya
ujangili.
iii. Awamu ya tatu, ambayo ililenga kutafuta yalipo Maghala ya Nyara, kusaka
Wafadhili na Wanunuzi wa nyara hizo na kuwabaini watu wanaowakingia kifua
wahusika wa vitendo vya ujangili.
iv. Awamu ya nne, ambayo ililenga kukamata Nyara nyingine mbali na Meno ya
Tembo na kuhakikisha watu walio katika makundi yafuatayo
wanakamatwa:-
- Wawindaji haramu,
- Wavunaji haramu wa mazao ya misitu,
- Watu wanaolisha Mifugo ndani ya hifadhi, na
- Watu waliojenga ndani ya maeneo ya hifadhi
2.2.3
Mafanikio ya Operesheni Tokomeza
a) Idadi ya watuhumiwa na kesi zilizofunguliwa
Mheshimiwa
Spika, tangu kuanza kutekelezwa
kwaOperesheni Tokomeza (tarehe 04 Oktoba, 2013 hadi ilipositishwa (tarehe 01
Novemba, 2013) jumla ya kesi 687 zilifunguliwa zikiwahusisha watuhumiwa 1,030
katika maeneo yote kama ifuatavyo:-
i.
Kanda ya Kwanza kesi 105 zikiwahusisha watuhumiwa 105
ii. Kanda ya Pili kesi 370 ambazo zilihusisha watuhumiwa 375
iii. Kanda ya Tatu kesi 165 zilizohusisha watuhumiwa 498
iv. Kanda ya Nne kesi 47 zilizohusisha watuhumiwa 52
Mheshimiwa
Spika, hadi wakati Operesheni Tokomeza
inasitishwa tarehe 01 Novemba, 2013 kati ya Kesi 687 zilizokuwa zimefunguliwa
ni 132 tu ndiyo zilikuwa zimetolewa maamuzi na 555 bado zilikuwa katika hatua
ya kusikilizwa. (Tazama Kiambatisho Na. 1)
i.
Kukamatwa kwa meno ya Tembo 211 yenye uzito wa kilo 522, meno ya Ngiri 11,
Mikia ya wanyama mbalimbali 36, Ngozi za wanyama mbalimbali 21, Pembe za Swala
46, Mitego ya wanyama 134, ng’ombe 7,621 Baiskeli 58, Pikipiki 8 na Magari 9.
ii.
Kupungua kwa kasi ya mauaji ya Tembo kutoka wastani wa Tembo wawili (2) kwa
siku hadi tembo wawili tu katika kipindi chote cha operesheni (siku 29).
iii.
Hadi kufikia tarehe 11 Novemba, 2013 jumla ya Bunduki za Kijeshi 18
zilikamatwa, Bunduki za kiraia 1579, Risasi 1964, Mbao vipande 27,913, Mkaa
Magunia 1242, Magogo 858 na Misumeno 60. Vyote hivyo vilikamatwa katika Kanda
ya Nne.
2.2.4
Changamoto za Operesheni Tokomeza
a) Vifo vilivyotokea wakati wa Operesheni
Mheshimiwa
Spika,Taarifa ya Serikaliiliainisha vifo
kamachangamoto kubwa iliyojitokeza wakati wautekelezaji wa Operesheni Tokomeza
kutokana na watumishi 6 na watuhumiwa 13 kupoteza maisha. (Tazama Kiambatisho
Na. 2)
b)
Hujuma dhidi ya Operesheni
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Serikali ilifafanua kuwa,utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza ulikumbwa na vitendo vya hujuma kutoka kwa baadhi ya
makundi ya jamii kama ifuatavyo:-
i.
Mamluki miongoni wa washiriki wa Operesheni. Mfano; kukamatwa kwa Askari Polisi
na Askari Wanyamapori wakisindikiza gari lenye Meno ya Tembo, na gari la
Serikalikutumika kusafirisha Meno ya Tembo.
ii.
Vyombo vya Habari kutumika kuvuruga operesheni kwakueneza propaganda
zilizolenga kushawishi wananchi kupinga operesheni hiyo.
iii. Baadhi ya wamiliki wa silaha kutuhumiwa kutoa silaha zao ili zitumike kwa
ajili ya vitendo vya ujangili.
C)
Tuhuma dhidi ya Operesheni
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Serikai ilifafanua kuwa,ingawa lengo la
operesheni lilikuwa ni kupambana na vitendo vya ujangili dhidi ya raslimali za
Taifa, utekelezaji wake ulikumbwa na tuhuma kadhaa zikiwemo zifuatazo:-
i.
Mateso dhidi ya watuhumiwa yaliyosababisha maumivu, kupata ulemavu wa kudumu na
hata wengine kupoteza maisha (Mfano; Marehemu Emiliana Gasper Maro wa Gallapo –
Babati).
ii. Matumizi mabaya ya Silaha (Mfano; Mzee wa miaka 70 kuuawa kwa kupigwa
risasi 3).
iii. Nyumba za wananchi kuchomwa moto (Mfano; Kijiji cha Kabage Wilaya ya
Mpanda – Katavi).
iv. Mifugo kuuawa kikatili kwa kuchomwa moto na kupigwa risasi (Mfano; Ng’ombe
60 kuuawa kwakupigwa risasi).
v. Kukosekana kwa mwongozo wa utoaji wa taarifa jambo lililosababisha viongozi
husika wa Serikali kutopewa taarifa muhimu za utekelezaji wa Operesheni.
(Mfano; Waziri wa Maliasili naUtalii, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Waziri wa Ulinzi na Wakuu wa Mikoa na Wilaya).
vi. Askari waliotuhumiwa kukiuka taratibu kukataa kutoa ushirikiano wa kutosha
pale walipohitajika kufanya hivyo.
vii. Kutoshirikishwa kwa viongozi wa Mamlaka za Utawala katika ngazi za Mikoa
na Wilaya.
3.0
MAHOJIANO BAINA YA KAMATI NA WIZARA PAMOJA NA WABUNGE
Mheshimiwa Spika, Kamati ilifanya mahojiano na makundi yafuatayo:-
i. Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake
ii. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
iii. Waheshimiwa Wabunge
3.1
Mahojiano baina ya Kamati na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi
zake
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha wajumbe wa Kamati
wanapata uelewa wa kutosha kuhusiana na Operesheni Tokomeza, Kamati liagiza
uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ukiongozwa na Waziri, kufika mbele ya
Kamati ili kueleza namna Operesheni Tokomeza ilivyoandaliwa na kutekelezwa hadi
ilipositishwa kupitia tamko la Serikali lililotolewa Bungeni tarehe 01 Novemba,
2013.
Mheshimiwa
Spika, Kamati ilikutana na Waziri wa
Maliasili na Utalii pamoja na timu yake kwa siku tatu, tarehe 28- 29 Novemba,
na tarehe 01 Desemba, 2013. Katika vikao hivyo, Waziri aliieleza Kamati juu ya
Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza, raslimali (watu na fedha) pamoja na
tathmini iliyofanyika kwa kipindi ambacho Operesheni Tokomeza ilitekelezwa.
Mheshimiwa
Spika, katika mahojiano na Waziri wa
Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Khamis Kagasheki, Mb na watendaji wake Kamati
ilifahamishwa yafuatayo:-
i.
Kwamba Operesheni Tokomeza ilikuwa ya kijeshi kama alivyonukuliwa katika
Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard) akisema: “…Operesheni ilikuwa ya
kijeshi. Ilikuwa ya kijeshi kwa sababu ilitekelezwa kwa amri ya jeshi Namba
0001/13 iliyotolewa tarehe 28 Septemba, 2013 na kusainiwa na Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi…”
ii. Kwamba, kinadharia inaonekana kwamba, Waziri wa Maliasili na Utalii ndiye
alikuwa Msemaji Mkuu, lakini kiuhalisia hakuwa msemaji mkuu wa Operesheni
Tokomeza kama alivyonukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge akisema;
“…kinadharia inaweza ikasemekana kwamba mimi ndiye msemaji mkuu, lakini mimi
sikuwa msemaji mkuu wa Operesheni Tokomeza …”
iii. Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ulisimamiwa na Jeshi la Wananchi wa
Tanzania.
iv. Taarifa za mwenendo wa operesheni zilikuwa zinapelekwa moja kwa moja kwa
Mkuu wa Majeshi na kwamba, hazikumfikia Waziri wa Maliasili na Utalii.
v. Operesheni Tokomeza iliingiliwa na Wanasiasa.
vi. Pamoja na Mpango kazi huo kuandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa
namna ambayo haieleweki Waziri hakuuona wala kuidhinisha rasimu ya mwisho ya
Mpango huo. Hiyo ilidhihirika mbele ya Kamati kutokana na Waziri kukiri kwamba
hakuuona wala kuudhinisha
3.1.1
Tathmini ya Kamati kuhusu majibu ya Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na watendaji
wa Wizara
Mheshimiwa Spika,kwa kutumia tathmini ya awali ya
nyaraka zilizowasilishwa pamoja na mahojiano na Waziri ilionekana kwamba,
Operesheni Tokomeza iliandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa
kushirikiana na taasisi zilizo chini yake na kushirikisha vyombo vya Ulinzi na
Usalama.
Mheshimiwa
Spika, licha Mpango wa Operesheni
Tokomeza kuandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, hata hivyo utekelezaji
wake ulisimamiwa na kuongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Hatua
ya jeshi kuchukua jukumu la kuongoza Operesheni Tokomeza, lilifanya viongozi wa
Wizara kujiengua katika jukumu la kuongoza (ead agency) na badala yake
kuacha jukumu hilo kwa Jeshi pekee jambo lililotafsiriwa kwamba, Operesheni
Tokomeza ilikuwa ya kijeshi.
Mheshimiwa
Spika, kupitia mahojiano ilibainika
kwamba, hakukuwa na utaratibu mzuri wa kupashana habari kuhusiana na mwenendo
mzima wa Operesheni Tokomeza jambo lililofanya baadhi ya wahusika kutotambua
kikamilifu wajibu waokatika Operesheni hiyo.Mfano mzuri ni kwamba, licha ya
kuelezwa kwenye Kanuni za Utendaji (Operational Guidelines) za
Operesheni Tokomeza kwamba, Waziri wa Maliasili na Utalii ndiye atakuwa Msemaji
Mkuu wa Operesheni Tokomeza, bado Mhe. Waziri hakutekeleza jukumu hilo kwani
alikwishatoa mapendekezo katika rasimu kwamba Msemaji Mkuu awe ni Mkurugenzi wa
Wanyamapori.
Aidha,
Kamati ilibaini kuwa baadhi ya Watendaji wa juu wa Wizara walidaiwa kukwamisha
utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Maliasili na Utalii kutokana na kuingilia
mawasiliano aliyokuwa anayafanya na baadhi ya Watumishi. Mfano ni majibizano
kwa njia ya barua pepe kati ya Waziri na Katibu Mkuu, Waziri na Mkurugenzi wa
Wanyamapori na pia Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Wanyamapori. Kwa mujibu wa
majibizano hayo Waziri anaonekana kushangazwa na hatua ya Katibu Mkuu kuhoji
hatua ya yeye kumuita mmoja wa mtumishi wa Wizara ofisini kwake. (Kiambatisho
Na. 3)
Mheshimiwa
Spika, kukosekana kwa mfumo mzuri wa
kupashana habari kwa pande husika kuhusu mwenendo mzima wa Operesheni Tokomeza,
kulionekana kuathiri utaratibu mzima wa viongozi husika akiwemo Waziri wa
Maliasili na Utalii, kupata taarifa zinazotakiwa kwa wakati. Hali hiyo
ilichangia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kukumbwa na athari ambazo
zingeweza kuepukika iwapo kungekuwa na mfumo mzuri wa mawasiliano.
Mheshimiwa
Spika, kupitia mahojiano pia Kamati
ilibaini uwepo wa hujuma kutoka kwa viongozi wa kisiasa na Serikali ambao kwa
namna moja au nyingine walionekana kuhusishwa na Operesheni Tokomeza ama wao
binafsi au ndugu zao.
Mheshimiwa
Spika, miongoni mwa hujuma ambazo Kamati
ilizibaini kupitia mahojiano naWaziri wa Maliasili na Utalii na Watendaji wake
ni pamoja na:-
i. Baadhi ya watuhumiwa wenye mahusiano na viongozi wa kisiasa kutumia majina
ya viongozi hao kuingilia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
ii. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kutuhumiwa kujihusisha navitendo vya ujangili
na biashara haramu ya nyara za Serikali.
iii. Baadhi ya Mawaziri kutoa kauli zenye kuingilia utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza. (Mfano: kutoa maelekezo kwa wahusika wa Operesheni Tokomeza kwamba
wasiguse viongozi wa kisiasa wa ngazi zote).
iv. Baadhi ya viongozi wavyombo vya Ulinzi na Usalama kushiriki kudhoofisha
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kwa kusindikiza au kusaidia watuhumiwa wa
ujangili kutoroka. (Mfano; viongozi wa Polisi wa Wilaya na Mikoa)
Mheshimiwa
Spika, kubainika kwa hujuma hizo ni
ishara tosha kwamba hata ndani ya Serikali yenyewe hakukuwa na dhamira ya dhati
kwa baadhi ya kwa viongozi na watendaji katika kuhakikisha vita dhidi ya
vitendo vya kijangili inapiganwa kikamilifu.
Hali
hiyo ilisababisha utekelezaji wa operesheni kukumbwa na athari nyingi kama
vile; wananchi kupoteza maisha, mifugo kuuawa kwa kuchomwa moto, njaa, kiu au
kupigwa risasi), upotevu wa mali, nyumba kuchomwa moto na vitendo vya ukatili
dhidi ya wananchi ambavyo vilikiuka haki za kibinadamu. Hali hiyo imesababisha
utekelezaji wazoezi la Operesheni Tokomeza kutafsiriwa kwamba ulilenga wananchi
wasio na hatia na kuacha wahusika wa ujangili.
3.2
Mahojiano baina ya Kamati na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 30 Novemba, 2013
Kamati ilikutana na kufanya mahojiano na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili
kubaini namna ilivyoshiriki katika Operesheni Tokomeza.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Dk. Emmanuel Nchimbi, Mb alieleza kuwa,
operesheni hii ilikuwa na lengo la kutimiza azma (Commitment) ya
Serikali iliyoitoa Bungeni kwamba, inakusudia kufanya Operesheni ya kupambana
na majangili.
Wizara
yake ilishiriki kwa kutoa Askari Polisi 504 pamoja na baadhi ya vyombo vya
usafiri na kwamba vyombo vya Ulinzi na Usalama vya nchi vilikuwa vikikutana
mara kwa mara kwa lengo la kuandaa mkakati wa namna ya kushirikiana katika
kutekeleza mpango huo wa vita dhidi ya ujangili.
Mheshimiwa
Spika,Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
alikiri kuwa, licha ya lengo la operesheni kuwa zuri, kulijitokeza changamoto
kadhaa zilizotokana na baadhi ya washiriki wa operesheni kwenda kinyume na
malengo yaliyokusudiwa kama vile; ukatili dhidi ya mifugo na vitendo vya
unyanyasaji wa wananchi kwa kuwatesa kiasi cha kuwasababishia ulemavu wa kudumu
au vifo.
Pia
Mheshimiwa Waziri alikiri kwamba, kutokuwepo mfumo mzuri wa mawasiliano na
Operesheni kuongozwa na jeshi, iliashiria kwamba taarifa za operesheni zilikuwa
zinakwenda kwa Mkuu wa Majeshi – CDF moja kwa moja na hivyo kufanya pande
zingine zinazohusika zisijue kinachoendelea.
3.2.1
Tathmini ya Kamati kuhusu majibu ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi na watendaji wake
Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwepo kwamawasiliano hafifu kati ya
Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara nyingine zilizoshiriki katika
operesheni hii.Pia,kukosekana kwa mfumo mzuri wa mawasiliano, kuliikosesha
Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo iliandaa na kugharamia Operesheni
Tokomeza,fursa ambazo zingeiwezesha kufanya tathmini kuhusu utekelezaji wa
Operesheni hii.
Aidha,
Kamati ilibaini kwamba, hatua ya kutoshirikisha Kamati za Ulinzi na Usalama za
Wilaya ililenga kutovujisha siri dhidi ya watuhumiwa wa ujangili. Hatua hiyo
ilisababisha usumbufu mkubwa kwa viongozi wa mamlaka za utawala za Wilaya na
Mikoa kutokana na kulaumiwa na wananchi kwa kushindwa kuwasaidia pale
walipokumbwa na matatizo.
3.3
Mahojiano baina ya Kamati na Waheshimiwa Wabunge
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala hili liliibukia Bungeni baadaya wawakilishi
wa wananchi kupaza sauti kuhusu athari zilizowakumba wapiga kura wao, Kamati
iliona ni busara kuhoji baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja hii.
Wabunge hao walitoa taarifa muhimu kuhusu vitendo vilivyofanyika katika maeneo
yao wakati wa operesheni.
Mheshimiwa
Spika, Waheshimiwa Wabunge walieleza
kusikitishwa na namna ambavyo Operesheni Tokomeza ilikiuka malengo
yaliyokusudiwa na badala yake ikanyanyasa wafugaji kwa kuangamiza mifugo yao na
kuwaharibia mali zao kama vile; kuchoma moto nyumba, kupora fedha na vitu
vingine. Mbunge mmoja alinukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge akisema:-
“…badala
ya Operesheni Tokomeza kusaka majangili, ikageuka kuwa Operesheni Tokomeza
Ufugaji…”
Mheshimiwa
Spika, Waheshimiwa Wabunge waliieleza
Kamati kuwa, siyo jambo la kawaida kwa watu wanaoagizwa kufanya jambo fulani
kwenda kinyume na maagizo.
Wakashauri
kuwa, wahusika wote waliotenda kinyume namaagizo wachukuliwe hatua stahiki ili
kuepusha vitendo vya aina hiyo visijirudie katika operesheni zitakazofuata. Pia
Waheshimiwa Wabunge walishauri kasoro zilizojitokeza zirekebishwe na operesheni
iweze kuendelea ili kutowapa mwanya majangili kujipanga upya.
3.3.1
Tathmini ya Kamati kuhusu majibu ya Waheshimiwa Wabunge
Mheshimiwa
Spika, kimsingi Waheshimiwa Wabunge
wanaunga mkono Operesheni Tokomeza ambayo ililenga kukomesha vitendo vya
kijangili na kunusuru raslimali za nchi hasa wanyamapori na misitu. Hata hivyo,
walieleza kusikitishwa na vitendo vilivyojitokeza wakati wa utekelezaji wa
operesheni na walisema haviwezi kuvumilika.
Mheshimiwa
Spika, baada ya kupata taarifa mbalimbali
kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge, mahojiano na viongozi na watendaji wa Wizara na
kuzingatia taarifa zilizowasilishwa na Serikali, Kamati iliazimia kuzuru baadhi
ya maeneo yaliyoathiriwa na Operesheni Tokomeza ili kufanya uhakiki.
4.0
KAMATI KUZURU MAENEO YALIYOATHIRIKA KWA AJILI YA KUHAKIKI
(VERIFICATION/OUTREACH)
Mheshimwa Spika, kutokana na wingi wa maeneo pamoja na ufinyu wa muda, Kamati
ilijigawa katika makundi matatu ili yaweze kutembelea baadhi ya maeneo
yaliyoainishwa katika Taarifa ya Serikali ili kufanya tathmini (verification)
kwa utaratibu ufuatao:-
4.1
Kundi la kwanza lilielekea Kanda ‘C’iliyohusisha maeneo yaliyoathiriwa na
Operesheni Tokomeza katika Mikoa ya Shinyanga, Kagera, Tabora, Kigoma,
Rukwa, Katavi na Singida.
Mheshimiwa
Spika, kundi hili liliundwa na Wajumbe
wafuatao:-
Mheshimiwa James Daudi Lembeli, Mb, Mheshimiwa Haji Khatibu Kai, Mb na
Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mb.
4.2
Kundi la pili lilielekea Kanda ‘B’iliyohusisha maeneo yaliyoathiriwa na
Operesheni Tokomeza katika Mikoa ya Simiyu, Mara, Arusha na Manyara.
Mheshimiwa
Spika,kundi hili liliundwa na wajumbe
wafuatao, Mheshimiwa Abdulkarim E. Shah, Mb, Mheshimiwa Henry Daffa
Shekifu, Mb na Mheshimiwa Amina Andrew Clement, Mb.
4.3
Kundi la tatu lilielekea Kanda ‘D’iliyohusisha maeneo yaliyoathiriwa na
Operesheni Tokomeza katika Mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa, Ruvuma na Mtwara.
Mheshimiwa
Spika, kundi hili liliundwa na wajumbe
wafuatao; Mheshimiwa Kaika Saning’o Telele, Mb, Mheshimiwa Muhammad Amour
Chomboh, Mb na Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, ambaye hata hivyo hakushiriki
kutokana na dharura.
Mheshimiwa
Spika,kama ilivyoainishwa hapo juu lengo
la Kamati kutawanyika Mikoani lilikuwa kutathmini athari zilizotokana na
Operesheni Tokomeza ambayo iliendeshwa nchini kuanzia tarehe 04 Oktoba, 2013
hadi tarehe 01 Novemba, 2013.
Mheshimiwa
Spika, ili kutimiza jukumu hilo
kikamilifu, Kamati iliongozwa na taarifa zifuatazo;
i. Mpango Kazi wa Operesheni Maalum ya kupambana na Ujangili nchini,
ii. Taarifa ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza iliyotolewa na Serikali.
iii. Michango ya Waheshimiwa Wabunge kama ilivyonukuliwa katika Taarifa Rasmi
za Bunge (Hansard).
iv. Madai yaliyotolewa na Wabunge kuhusiana na athari zilizotokana na
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
v. Maelezo yaliyotolewa na Mashahidi ambao walihojiwa na Kamati.
vi. Vielelezo vilivyowasilishwa na Mashahidi waliofika mbele ya Kamati.
5.0
MAKUNDI YA KAMATI YALIVYOTEKELEZA MAJUKUMU YAKE
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu hili, Kamati ilikutanana
makundi yafuatayo:-
i. Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya
ii. Waheshimiwa Madiwani
iii. Waathirika wa Operesheni Tokomeza
5.1
Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya
Mheshimiwa Spika, Kamati ilikukutana na Kamati za
Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya na kupokea taarifa iliyohusu hali ya
Ulinzi na Usalama hususan wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
Mheshimiwa
Spika, kwa sehemu kubwa taarifa za Ulinzi
na Usalama za Wilaya zilisaidia kuanisha maeneo na matukio yaliyojiri wakati wa
Operesheni Tokomeza na athari zilizojitokeza. Wajumbe wa Kamati walitumia
uchambuzi wa taarifa hizo kupata uelewa zaidi kuhusiana na utekelezaji wa
Operesheni hiyo kabla ya kukutana na wananchi walioathirika ili kupata maelezo
zaidi.
5.2
Waheshimiwa Madiwani
Mheshimiwa Spika,katika baadhi ya Wilaya, Kamati
ilikutana nabaadhi ya Madiwani wakiwa ni wawakilishi wa wananchi katika ngazi
ya halmashauri ili kupata maelezo zaidi kuhusu utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza kabla ya kukutanana waathirika wa Operesheni.
5.3
Waathirika wa Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, Kamati ilikutana nabaadhi ya
wananchi walioathirika na Operesheni Tokomeza na kupokea maelezo na malalamiko
yao kuhusu namna walivyoathiriwa na uekelezaji wa Operesheni.
Mheshimiwa
Spika, wapo baadhi ya waathirika walitoa
ushahidi/vielelezo vya maandishi na picha ili kuthibitisha yale waliyokuwa
wakiyaeleza mbele ya Kamati. Wengine walikwenda mbali kiasi cha kuonesha
majerahana makovu waliyoyapata katika miili yao kutokana na mateso waliyopata
kwenye kambi maalum za mahojiano zilizoandaliwa na waendeshaji wa Operesheni
Tokomeza.
5.4
Kuzuru maeneo yaliyoathirika zaidi na Operesheni
Mheshimiwa Spika, Kamati ilipata fursa ya kutembelea
baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na athari za operesheni Tokomeza kwa lengo la
kushuhudia mabaki ya vielelezo ili kujiridhisha iwapo tuhuma za athari
zilizotolewa kuhusu maeneo hayo zilikuwa zakweli.
6.0
YALIYOBAINIKA KATIKA ZIARA ZA KAMATI
6.1 Vikao na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa/Wilaya
Mheshimiwa
Spika, katika vikaona Kamati za Ulinzi na
Usalama za Mikoa/ WilayaKamati ilibaini kuwa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
haukushirikisha viongozi wa maeneo hayo ya utawala.
Kulikuwa
na manung’uniko kwamba licha ya Wakuu wa Wilaya na Mikoa kuwa wawakilishi wa
Rais, waliachwa kando na Operesheni kuendeshwa katika maeneo wanayosimamia hadi
malalamiko ya wananchi waliokamatwa yalipowafumbua macho kwamba walikuwa
wanateswa na kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na watekelezaji wa Operesheni.
Aidha,
Kamati
ilielezwa kwamba utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ulisababisha hofu miongoni
mwa wananchi na viongozi na kusababisha baadhi yao kukimbia makazi. Mfano; Mkuu
wa Wilaya ya Ulanga alikiri kujihifadhi kwenye Hoteli moja nje ya Wilaya yake
ambako alikutana na baadhi wananchi wake waliokimbia adha za Operesheni
Tokomeza.
Viongozi
hao walieleza kwamba, kimsingi hawapingi Operesheni Tokomeza Majangili
kwaniililenga kunusuru raslimali za nchi hasa wanyamaporina misitu visitoweke
kutokana nakushamiri kwa vitendo vya ujangili. Hata hivyo, walieleza kuwa hatua
ya kutowashirikisha imelifanya zoezi hilo kuwa na kasoro nyingi pamoja na
udhalilishaji hata kwa viongozi waliochaguliwa na wananchi.
6.2
Vikao vya Kamati na Waathirika wa Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, Kamati ilifanya mikutano mbalimbali
katika baadhi ya maeneo ilikofanyika Operesheni Tokomezakwa lengo la
kuwasilikiliza waathirika na kubaini mambo yafuatayo:-
Watuhumiwa
kupekuliwa, kudhalilishwa na baadhi kutojulikana walipo
i.
Mheshimiwa Spika, badhi ya wananchi wakiwemo viongozi, Madiwani na Wenyeviti wa
Vijiji na Vitongoji na Watumishi wa Serikali walikamatwa na kudhalilishwa mbele
ya wananchi wanaowaongoza. Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa walikuwa
hawajulikani walipo hadi Kamati ilipozuru maeneo hayo. Mfano; Vijana watatu wa
Kijiji cha Osteti, Kata ya Chapakazi, Wilayani Kiteto, walituhumiwa kujihusisha
na biashara ya Meno ya Tembo. Vijana hao ni Nyafuka Ng’onja, Ng’onja Kipana na
Mswaya Karani.
ii.
Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa walidai kudhalilishwa mbele ya wanafamilia
kwa kupewa adhabu wakiwa uchi na wanawake kushikwa sehemu za siri bila ridhaa
yao. Mfano; ndugu Ali Nyenge (38) wa Kata ya Iputi, Wilaya ya Ulanga alidai
kuvuliwa nguo, kumwagiwa maji yaliyochanganywa na chumvi na kuchapwa viboko
huku mwanae wa kiume (11) akishuhudia.
Pia
alidai kulazimishwa kuchora picha ya Chatu kwa kutumia wembe kwenye paja lake.
Vilevile, Bi. Neema Moses wa Babati alidai kuvuliwa nguo na kulazimishwa afanye
mapenzi na wakwe zake na pia kuingizwa chupa sehemu zake za siri.
Aidha,
baadhi ya akina mama walidai kubakwa na kulawitiwa. Mfano; katika Kata ya
Iputi, Wilaya ya Ulanga, mwanamke mmoja alidai kubakwa na Askari wawili (2) wa
Operesheni Tokomeza Ujangili mida ya usiku. Vilevile, mama mmoja mkazi wa Kata
ya Matongo Wilayani Bariadi, alibakwa na askari watatu (3) wa Operesheni
Tokomeza Ujangili huku akiwa ameshikiwa mtutu wa bunduki
iii. Watuhumiwa waliokamatwa walifanyiwa upekuzi bila kuhusisha viongozi wa
Serikali za maeneo husika na kutokuwepo kwa mashahidi na hati za upekuzi.
Mfano;
Ndg. Abdallah Pata na Bi. Flora Mwarabu wa Kata ya Iputi Wilayani Ulanga na
Ndg. Elias Cosmas Kibuga wa Gallapo Babati, walipekuliwa bila kufuata
utaratibu.
Ukatili
na Udhalilishaji katika Kambi za Mahojiano
iv. Mheshimiwa Spika, baadhi ya watuhumiwa waliopelekwa katika kambi za
mahojiano walidai kuteswa kwa adhabu zinazokiuka haki za binadamu. Mfano;
Diwani wa Kata ya Sakasaka wilaya ya Meatu Ndg. Peter Samwel, alidai kuadhibiwa
akiwa mtupu kwa kupewa adhabu za kijeshi kama kuning’inizwa kichwa chini miguu
juu, kupigwa kwa vyuma na kulazimishwa kufanya mapenzi na mti.
Mheshimiwa
Spika, kutokana naukatili uliopitiliza,
baadhi ya kambi za mahojiano zilipewa majina kama vile Guantanamo (Ruaha),
Goligota (Ngorongoro), Duma na Andajega (Serengeti).
Upotevu
wa mali za watuhumiwa na faini zisizoeleweka
v. Mheshimiwa Spika, ilidaiwa kuwa wakati wa
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, baadhi ya watuhumiwa walipoteza
mifugo, mali na fedha zao. Mfano; katika Wilaya ya Ulanga Kata ya Iputi
mwananchi mmoja alidai kuporwa sanduku la VICOBA lenye shilingi laki saba na
nusu (750,000/=) pamoja na simu ya mkononi na Askari wa Operesheni Tokomeza
waliovamia nyumbani kwake. Vilevile Ndugu Musa Masanja wa Sakasaka Wilaya ya
Meatu, alidai kuporwa shilingi laki tatu 300,000/= pamoja na simu 2 za mkononi
na Askari Askari wa Operesheni.
Mheshimiwa
Spika,Pia ilidaiwa kuwa mifugo ya watuhumiwa
ilikamatwa na kuingizwa ndani ya maeneo ya hifadhi na kufa kwa kupigwa risasi
au kukosa maji na malisho kutokana na kuzuiliwa kwa muda mrefu.
Baadhi
ya mifugo ilitozwa faini bila stakabadhi au stakabadhi kuonesha viwango vidogo
ikilinganishwa na fedha halisi iliyolipwa. Mfano:Ndugu Sosoma Shimula mwenye
Ng’ombe 1700 Wilayani Kasulu alidai kwamba alitakiwa kulipa faini ya shilingi
Milioni thelathini (30,000,000/=, alipowasihi alipunguziwa hadi Milioni kumi na
mbili (12,000,000/=) hata hivyo aliweza kulipa Milioni kumi
(10,000,000/=).
Alionesha
Kamati stakabadhi inayoonesha kuwa amelipa faini ya shilingi milioni moja tu
(1,000,000/=). Stakabadhi hiyo ilijazwa sehemu ya tarakimu, lakini hakuna
kilichoandikwa katika sehemu ya kiasi cha fedha kwa maneno. (Tazama Kiambatisho
Na. 4)
Watuhumiwa
kuteswa na kuumizwa
vi. Mheshimiwa Spika, baadhi ya watuhumiwa walidai
kupigwa na kuumizwa na askari wa Operesheni na wengine kupata ulemavu wa
kudumu. Mfano; katika Wilaya ya Itilima,Kijiji cha Mbogo Ndg Sita Rumala alidai
kupigwa na kuvunjwa mkono alionesha wajumbe mkono uliokuwa umefungwa bandeji
ngumu (P.O.P).
Aidha,
Diwani Peter Samwel Ndekija wa Kata ya Sakasaka, Wilaya ya Meatu, alidai
kupigwa na kuumizwa vibaya mgongoni na alionesha kwa wajumbe wa Kamati makovu
aliyoyapata. Vilevile,ilielezwa kuwa Ndugu Munanka Machumbe (24) ambaye ni bubu
alipigwa risasi 3 zilizomjeruhi mapajani na kuharibu sehemu za siri wakati
akijaribu kuwahoji Askari wa Operesheni kwa ishara sababu za kumtesa baba yake.
Aidha,
katika tuko lingine Shekhe Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ali Mohamed (70) aishiye
kijiji cha Iputi, alidai kurushwa kichura na kutandikwa bakora na Askari wa
Operesheni Tokomeza. Pia,Ndg. Nyasongo Magoro Serengeti wa Kata ya
Majimoto wilaya ya Mulele alidhalilishwa mbele ya wananchi wake. (Tazama
Kiambatisho Na. 5)
Mifugo
kuingizwa hifadhini na watuhumiwa kubambikwa kesi
vii. Mheshimiwa Spika,wakati wa Operesheni, mifugo mingi
ilikuwa hifadhinilakini hata ile iliyokuwa nje ya hifadhi iliingizwa na askari
wa hifadhi na wafugaji kutakiwa walipe faini ya shilingi Milioni tatu
(3,000,000/=) hadi Sita (6,000,000/=) kwa idadi ya ng’ombe 30 hadi ng’ombe 100
na aliyeshindwa kulipa faini mifugo yake iliuawa au kupigwa mnada na mfugaji
kufilisiwa.
Walioshindwa
kulipa faini mifugo ilipigwa mnada na wafugaji hawakuruhusiwa kununua wala
kukaribia eneo la mnada, na katika mnada mifugo iliuzwa kwa bei ya chini kuliko
faini iliyotozwa Mfano; shilingi elfu sitini (60,000/ =) kwa kila ng’ombe.
Watuhumiwa
kubambikwa kesi
viii.Ilidaiwa kwamba, baadhi ya watuhumiwa walidai kubambikwa makosa ambayo
hawahusiki nayo kama vile kumiliki silaha kinyume na sheria, kukutwa na bangi
au nyara za Serikalimfano; Bw. Elias Cosmas Kibuga wa Gallapo Babati alidai
kubambikiwa kesi ya kumiliki bunduki kukutwa na mkia wa twiga kinyume cha
sheria.
Mheshimiwa
Spika, pia Bibi Zuhura Ali wa Kilombero
alidai kuteswa huku akilazimishwa kutoa silaha ambayo hakuwa nayo. Aidha, Bw.
Melkzedeck Abraham Sarakikya wa Itigi alidai kuteswa akilazimishwa atoe silaha.
Mateso
na vifo kwa Watuhumiwa
ix. Mheshimiwa Spika, baadhi ya wananchiwalidai kuwa
ndugu zao waliteswa kikatili kwa muda mrefu na bila kupatiwa huduma za lazima
kama chakula, maji na matibabu (siku 1 -2) hadi mauti yalipowafika. Kwa mfano
Ndg. Kipara Issa wa Wilaya ya Kaliua na ndugu Emiliana Gasper Maro wa Gallapo,
Wilaya ya Babati.
Aidha,
wananchi hao walidaikuwa mahojiano kwa watuhumiwa yaliambatana na mateso makali
kwa muda mrefu kiasi cha kusababisha vifo. (Tazama Kiambatisho Na. 6).
Vilevile,
watuhumiwa wengine waliodaiwa kupoteza maisha wakati wa Operesheni Tokomeza ni
Ndg. Wegesa Kirigiti wa Kijiji cha Remagwe na Ndg. Peter Masea wa Kijiji cha
Mrito (Tarime), Ndg. Mohamed Buto (Masasi) na Gervas Nzoya (Kasulu).
Mheshimiwa
Spika, pamoja na uthibitisho wa picha zilizotolewa na wananchi kuhusu kuteswa
hadi kufa kwa Bi Emiliana Gasper Maro, Serikali kupitia Mkurugenzi wa
Wanyamapori ilitoa Taarifa kwa Umma ikipinga Taarifa iliyorushwa na kituo cha
luninga cha ITV tarehe 19 Oktoba 2013 kuhusu mauaji ya kutisha yaliyofanywa na
Askari wa kupambana na ujangili.
Taarifa
hiyo ya Serikali inapinga kuwa Askari wa Operesheni Tokomeza hawausiki na kifo
cha mtajwa. Taarifa hiyo imeonekana kukosa umakini kutokana na kujichanganya
juu ya watu inaowazungumzia. Taarifa hiyo inazungumzia majina mawili tofauti
(Evelyn Gasper na Mariana Gaspar Mallo wa eneo la Olongadiola) wakati
muathirika halisi ni Bi. Emilliana Gasper Maro wa Kijiji cha Orngadida,
Gallapo. (Tazama kiambatisho Na.7)
Ukatili
dhidi ya Wanyama
x. Mheshimiwa Spika, kuhusu vitendo vya ukatili kwa
wanyama ilidaiwa kwamba ng’ombe walipigwa risasi, na ndama walikufa kwa kukosa
maziwa kutokana na mama zao kukamatwa na kuzuiwa kwenye mazizi yaliyopo maeneo
ya hifadhi kwa muda mrefu. (Tazama Kiambatisho Na. 8)
Rushwa
kwenye Mapori ya Akiba
xi. Mheshimiwa Spika, Wananchi walidai kukithiri kwa
vitendo vya rushwa kwa watumishi wanaosimamia mapori ya akiba ya Maswa, Kigosi
Moyowosi, Burigi, Kimisi na Mkungunero kwa kutaja majina ya baadhi ya watumishi
wanaowatuhumu. Mfano; Ndg. Kileo mtumishiwa pori la Maswa, alidaiwa kuwa na
tabia ya kutoza wananchi faini bila stakabadhi au kutoa stakabadhi kinyume na
faini iliyotolewa au kutoa stakabadhi bandia.
Aidha,
katika pori la Kigosi-moyowosi, watumishi wafuatao walidaiwa kujihusisha na
vitendo vya rushwa; Ndg. Msocha, Alfred, Kobelo na Odhiambo.
Aidha,
ilidaiwa kuwa katika mapori ya Kigosi Moyowosi na Kimisi zaidi ya wafugaji 100
wenye ng’ombe wanaokadiriwa kuwa 50,000 wanalipia kuchungia ng’ombe wao kwenye
mapori hayo ya hifadhi tangu mwaka 2000 kwa malipo maalum na hata Operesheni
Tokomeza haikuwagusa.
Aidha,
ilidaiwa kuwa Ndg. Msocha (Meneja wa Pori la Akiba la Kigosi Muyowosi),
alituhumiwa na baadhi ya wananchi kuwa amekuwa akiwakodisha wafugaji hao kwa
vipindi vya miezi mitatu, na wafugaji huruhusiwa kulipa tena muda unapoisha.
Aidha, Mfugaji ambaye hulipa kiasi kidogo hulazimishwa kulipa huku akipigwa
namifugo yake kuuawa kwa kupigwa risasi.
Ilielezwa
kuwa, Wafugaji na Askari Wanyamapori huwasiliana kwa simu ilil kutekeleza
makubaliano ya malipo kwa malisho yao. Nambaza simu zinazodaiwa kuwa za Askari
Wanyamapori zimeorodheshwa. (Tazama Kiambatisho Na. 9)
Mahusiano
kati ya wananchi na Askari wa mapori ya Akiba
xii. Mheshimiwa Spika, wananchi wanaoishi kwenye Mapori
ya Akiba yanayo wazunguka walidai kuwa katika mahusiano mabaya na Askari wa
mapori hayo. Mfano;wananchi wa kijiji cha Kimotorok, Wilaya ya Simanjiro na
Askari wa pori la akiba la Mkungunero kiasi cha kufikia hatua ya kutishiana
maisha. Vitendo hivyo pia vipo kwa jamii zinazopakana na mapori ya Gurumeti.
Mahakama
na Magereza kuzidiwa uwezo
xiii.Mheshimiwa Spika, kutokana
na Operesheni Tokomeza ilidaiwa kuwa vyombo Mahakama na Magereza katika maeneo
husika vilizidiwa uwezo kutokana na wingi wa kesi na idadi ya Mahabusu. Mfano;
Gereza la Wilaya ya Bunda lenye uwezo wa kuchukua jumla ya wafungwa na mahabusu
217 lililazimika kuchukua hadi watu 411.
Baadhi
ya watuhumiwa waliokamatwa wanalazimika kusafiri umbali mrefu kuhudhuria kesi
zao. Mfano; katika wilaya ya Serengeti baadhi ya watuhumiwa walifunguliwa kesi
Wilaya za Tarime, Bunda na Bariadi.
Watumishi
wa Umma kuhusishwa na Ujangili
xiv.Mheshimiwa Spika, ilidaiwa kuwa baadhi ya Watumishi
wa Serikali na vyombo vya dola (Polisi) wanajihusisha na ujangili. Mfano ni
Dereva wa OCD, Wilaya ya Ngorongoro aliyetuhumiwa kujihusisha na ujangili wa
Meno ya Tembo.
Askari
huyo alihojiwa na viongozi wa Operesheni Tokomeza katika kituo chake cha kazi.
Vilevile, Ndg. Mohamed Ismail, Afisa Wanyamapori (W) Meatu anatuhumiwa kukutwa
na nyara za Serikali. Aidha,Askari Polisi wawili (2 )Cpl. Isaack na PC
Sixbert wa Mugumu Wilayani Serengeti walikamatwa wakiwa na meno ya Tembo.
Mheshimiwa
Spika, pia ilidaiwa kuwa baadhi ya Maofisa
wa Serikali wamekuwa wakitumia magari ya Umma ama kusafirisha au kusindikiza
watoroshaji wa nyara za Serikali. Mfano nigari la Serikali lililokamatwa
likifaulisha meno ya Tembo kutoka kwenye gari jingine huko Mkuranga kwa lengo
la kuyasafirisha kwenda Dar es Salaam.
Sambamba
na hilo baadhi viongozi wa jeshi la Polisi wametuhumiwa kusaidia watuhumiwa wa
vitendo vya kijangili kutoroka na kuepuka mkono wa sheria.
Migogoro
kuhusu mipaka ya Maeneo ya Hifadhi
xv. Mheshimiwa Spika, wananchi walidai kuwa baadhi ya
Mapori ya Akiba naHifadhi yamekuwa yakipanua mipaka yake bila kushirikisha
wananchi wa maeneo yanayowazunguka. Mfano; wananchi wa Wilaya ya Bunda
wanaopakana na Pori la Akiba la Gurumeti.
Pia,
wananchi wa vijiji vya Kegonga na Masanga, katika Kata ya Nyanungu, Wilayani
Tarime wako katika mgogoro wa mpaka na TANAPA wakidai kuwa bonde la Nyanungu
limemezwa na eneo la Hifadhi kutokana na TANAPA kuongeza mipaka yake bila
kushirikisha wananchi wa maeneo hayo.
Aidha,
katika Wilaya ya Ulanga kuna mgogoro katika kata za Iputi na Lupiro
dhidiHifadhi ya Selous.
Idara
za Wanyamapori katika Halmashauri kukosa vitendea kazi
xvi.Mheshimiwa Spika, kutokana na silaha za Idara ya
Wanyamapori katika baadhi ya Halmashauri kuchukuliwa wakati wa Operesheni
Tokomeza kwa ajili ya uchunguzi, wananchi wamedai kupata shida kutokana na
wanyama hasa Tembokuvamia mashamba na kuharibu mazao pamoja na kujeruhi au kuua
watu na mifugo.
Wanasiasa
kushawishi wananchi kuishi kwenye maeneo ya Hifadhi
xvii. Mheshimiwa Spika, wakati
wa kutekeleza Operesheni Tokomeza ilidaiwa kuwa nyumba na maboma ndani ya
mapori ya akiba zilichomwa moto. Mfano; Wilaya ya Sumbawanga kijiji cha Msila
Kata ya Mfinga na kijiji cha Kabage Wilaya ya Mpanda. Hata hivyo baadhi ya
wananchi wameanza kurejeakatika baadhi ya maeneo ya hifadhi kutokana na
ushawishi wa wanasiasa.
Mfano;
katika Pori la Hifadhi ya Jamii Ubende Wilaya ya Mpanda walichangishwa shilingi
laki moja (100,000/ =) kwakila kaya kwa ajili ya kupatiwa huduma za kisheria
iwapo mamlaka husika zitajaribu kuwaondoa ndani ya hifadhi.
Aidha,
Kamati ilipata taarifa kuwa, baadhi ya viongozi wa Vyama vya Siasa wamekuwa
wakigawa kadi za vyama vyao kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya hifadhi na
kwa ahadi kwamba, vyama walivyojiunga nga navyo vitawatetea wasiondoke katika
maeneo hayo.
Tatizo
la Vibali vya Wakulima wa Muda
xviii. Mheshimiwa Spika, Kamati
ilielezwa lipo tatizo la raia wa nchi jirani kuingia nchini na kupewa vibali
vyakuendesha shughuli za kilimo(Peasant Permit)kwa muda, ambavyo hutolewa bilakubandika
picha ya mhusika/mwombaji hasa maeneo ya Karagwe.
Raia
hao wanadaiwa kutumia nakala za vibali hivyo kuingiza nchini wahamiaji haramu
ambao baadhi yao huingiza makundi makubwa ya mifugo hasa ng’ombe na wengine
kutumia mwanya huo kuingiza silaha na kujihusisha na vitendo vya ujangili
katika baadhi ya mapori ya akiba. Mfano; Pori la Akiba la Ibanda Rumanyika.
Vilevile
kuna tatizo la majangili kutumia vivuli va wafugaji kuingia kwenye hifadhi huku
wakiwa wameficha silaha, na hivyo kuwepo mazingira ya kushindwa kutofautisha
kati ya majangili na wafugaji hususan katika maeneo ya hifadhi ya Ruaha.
xix.Mheshimiwa
Spika, kuna mgogoro katika eneo la
Ushoroba (Buffer Zone) katika Kata za Lupiro, Mbugana Iputi Wilaya ya Ulanga,
maeneo ambayo jamii imejenga miundombinu kwa miaka mingi ikiwa ni pamoja na
shule, nyumba, mashamba, misikiti na makanisa huku Serikali ikiwa kimya kwa
muda mrefu.Hata hivyo, wakati wa Operesheni Tokomeza wananchi hao
walilazimishwa kuhama bila kuelekezwa waende wapi.
Michango
ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu Operesheni
xx. Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwa baadhi ya
michango iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wakichangia Hoja ya Mhe.
Saidi Nkumba haikuwa imefanyiwa utafiti wa kutosha kwani baadhi ya madai
waliyoyatoa hayakuwa na uhusiano na Oparesheni Tokomeza.
Kwa
mfano;ni kweli kwamba ng’ombe 51 walitumbukia katika mto Rubana Wilayani Bunda
na kufa, hata hivyo tukio hilo lilitokea mwezi April, 2013 ikiwa ni miezi 6
kabla ya Operesheni.
Aidha,
ni kweli kuwa Wakazi wa Vijiji vya Kabage Wilayani Mpanda na Luchima Wilayani
Mulele walihamishwa kutoka katika maeneo ya hifadhi na nyumba zao kuchomwa moto
katika utaratibu uliofanywa na Halmashauri hizo mwezi Septemba, 2013 kwa lengo
la kuwapeleka kwenye maeneo rasmi ya makazi.
7.0
MAONI NA USHAURI WA KAMATI KUHUSU TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA OPERESHENI
TOKOMEZA
Mheshimiwa Spika, baada ya Kamati kuchambua nyaraka
husika kuhusiana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza, kuwahoji viongozi
mbalimbali wa Wizara na Waheshimiwa Wabunge, pamoja na kufanya ziara mikoani
kwa lengo la kuhakiki yaliyojiri kutokana na Operesheni Tokomeza, Kamati
inapenda kutoa maoni na ushauri ufuatao:-
i.
Kwa kuwa, lengo la Operesheni Tokomeza lilikuwa kunusuru raslimali za nchi
hususani Wanyamapori na hasa Tembo na Misitu, na kwa kuwa Waheshimiwa Wabunge
na Wananchi wameiunga mkono mbali na matatizo ya kiutendaji yaliyojitokeza,
hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali irekebishe haraka kasoro
zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ili kuendeleza na
kukamilisha awamu zote za operesheni kama zilivyo kwenye mpango na kunusuru
raslimali za Taifa hasa wanyamapori na misitu ambayo inatishiwa kutoweka
kutokana na vitendo vya ujangili.
ii.
Kwa kuwa,Kamati imejiridhisha kwamba matatizo na upungufu uliojitokeza katika
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza yamechangiwa na maandalizi mabaya ya Mpango
kazi ambao Waziri Mwenye dhamana hakuidhinisha, na kwa kuwa, imedhihirika
kuwepo hali ya sintofahamu (kwa mujibu wa hansard) iliyosababishwa na
watendaji wakuu wa Wizara kwa makusudi kuamua kutomshirikisha kikamilifu Waziri
katika hatua za mwisho za maandalizi ya Mpango kazi, hivyo basi Bunge
linaazimia kwamba, Serikali iwachukulie hatua stahiki za kinidhamu Wasaidizi
Wakuu wote wa Waziri walioshiriki katika Mpango kazi huo.
iii.
Kwa kuwa, Kamati imebaini kwamba pale Jeshi la Wananchi (JWTZ)
linaposhirikishwa katika Operesheni ufanisi mkubwa hupatikana, na kwa kuwa,
bado iko haja ya kuendeleza Operesheni Tokomeza kwa maslahi ya Taifa, na kwa
kuwa ushahidi wa mazingira ‘circumstantial evidence’ unaonesha kuwa
Jeshi lilichukua uongozi wa operesheni baada ya kugundua kuwa washiriki kutoka
Vikosi vingine (Polisi, TANAPA, TSF na NCAA) kwa kushirikiana na wafugaji wenye
ushawishi wa kifedha pamoja na wanasiasa, walihujumu operesheni hiyo kwa kutoa
taarifa kwenye mtandao mkubwa wa kijangili ambao umejengeka kuanzia Wizarani
hadi kwenye maeneo ya Hifadhi na kusaidia ‘majangili papa’ wasikamatwe, hivyo
basi, Bunge linaazimia kwamba:-
-
Serikali kuchukua hatua za makusudi kuuvunja mtandao huo na pia;
- Kuandaa operesheni nyingine ambayo itapangwa na kutekelezwa na Jeshi la
Wananchi wa Tanzania na Idara ya Usalama wa Taifa.
iv.
Kwa kuwa, kumekuwepo na operesheni kadhaa kabla ya Operesheni Tokomeza ambazo
zililenga kupambana na ujangili, na kwa kuwa, Operesheni Tokomeza imeshindwa
kupata mafanikio yaliyotarajiwa, na kwa kuwa, ushahidi wa mazingira unaonesha
wazi kwamba, Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) kimeshindwa kutimiza wajibu wake,
hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali iimarishe kikosi hicho kwa
kukifanyia tathmini na kukiunda upya ikiwa ni pamoja na kukiwezesha kwa
rasilimali (Watu, fedha, magari, silaha za kisasa na vifaa vya mawasiliano kama
redio na simu).
Serikali
iunde chombo ambacho kitakuwa na jukumu la kusimamia na kutathmini utendaji
kazi wa KDU. Iwapo utaratibu huo utazingatiwa ni wazi vitendo vya
ujangili vitadhibitiwa bila kutumia operesheni kubwa kama Uhai na Tokomeza.
v.
Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwepo kwa vitendo vya utesaji na ukatili wa hali ya
juu, ukiukwaji wa haki za binadamu na uzembe miongoni mwa Askari wa Operesheni
Tokomeza (ushahidi wa wahusika upo), hali ambayo imesababisha baadhi ya
Wananchi kupoteza maisha, kupata ulemavu wa kudumu pamoja na kupoteza mali zao.
Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba:-
-
Serikali Iwabaini wote waliohusika na vitendo vya kinyama, mateso na
udhalilishaji dhidi ya watuhumiwa, iwachukulie hatua stahiki na kuwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa agizo hili katika Mkutano ujao wa Bunge.
-
Ifanye tathmini ya kina kwa kupitia Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili kujua
athari za Operesheni hii na kutafuta njia ya kutoa kifuta machozi kwa
waathirika, ili kurejesha imani ya Wananchi kwa Serikali yao.
vi.
Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa Operesheni Tokomeza ilikuwa haikutengewa fedha
katika Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika mwaka wa fedha wa
2013/2014 na kwa kuwa kiasi cha fedha Tshs. 3,968,168,667/= kilichopatikana
kutoka Idara na Mashirika Tanzu ya Wizara haikutosheleza mahitaji ya fedha ya
Operesheni Tokomeza kutokana na ukubwa wa eneo la Operesheni, hivyo basi, Bunge
linaazimia kwamba, Serikali itenge Bajeti Maalum ya kutosheleza mahitaji ya
Operesheni Tokomeza.
Serikali
kutenga Bajeti kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uhifadhi katika maeneo ya
Hifadhi ikiwa ni pamoja na kuweka raslimali watu ya kutosha na miundombinu
mingine muhimu.
vii.
Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa Taarifa kwa Umma iliyotolewa kwa Vyombo vya
Habari na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori tarehe 23 Oktoba 2013, haikuwa
sahihi na pia ililenga kuudanganya Umma kwa kuficha mazingira na sababu za kifo
cha Bi Emilliana Gasper Maro, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali
ichukue hatua za kumwajibisha Mkurugenzi wa Idara ya Wanyapori kwa kuudanganya
umma kwa kujaribu kuficha ukweli.
viii.Kwa
kuwa, Kamati imebaini kuwa kumekuwapo mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya
Maafisa Wanyamapori, Maafisa Misitu katika mapori ya akiba, Misitu ya Serikali
na katika baadhi ya Hifadhi za Taifa wa kupokea rushwa, kutesa wananchi,
kuwabambika kesi na kujihusisha na ujangili,na kwa kuwa Kamati inayo majina na
vielelezo vya wahusika, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali ifanye
tathmini nchi nzima kwa lengo la kutambua kiwango cha vitendo vya rushwa
miongoni mwa watumishi hao, na kuwachukulia hatua stahiki za kinidhamu wale
watakaobainika kuhusika ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha na kuwafikisha kwenye
vyombo vya sheria.
ix.
Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa baadhi ya viongozi wa kisiasa na Serikali
waliingilia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kwa manufaa yao binafsi, kwa
mfano, agizo la kuwataka wahusika wa Operesheni Tokomeza kutowagusa Viongozi wa
Kisiasa wa ngazi zote, kauli ambayo ilitafsiriwa kuathiri utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza kwa kubagua Watanzania katika makundi ya Viongozi na Wananchi
wa kawaida, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali ihakikishe kuna
uwajibikaji wa pamoja pale inapoamua kutekeleza jambo la Kitaifa kama
Operesheni Tokomeza.
x.
Kwa kuwa, Kamati imethibitisha kuwa, baadhi ya wanasiasa wamekuwa
wanawadanganya wananchi waliothibitika kufanya shughuli za uchumi kwenye maeneo
ya hifadhi, na kuwaahidi kuwatetea pindi Serikali inapochukua hatua za
kuwaondoa katika sehemu hizo, ikiwa ni pamoja na kuwapa kadi za vyama vyao vya
siasa, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, serikali ihakikishe kwamba,
wananchi hawaendeshi shughuli za kiuchumi kwenye maeneo ya hifadhi na kuwaonya
wanasiasa waache kuwalaghai wananchi kwa maslahi yao binafsi.
xi.
Kwa kuwa, Kamati imebaini kwamba katika baadhi ya maeneo ya mipakani
mfano Karagwe, Idara ya Uhamiaji hutoa vibali kwa raia wa nchi jirani vya
kuishi na kulima hapa nchini, vibali ambavyo havina udhibiti wala tija kwa
nchi, na kusababisha migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji
lakini pia uharibifu wa mazingira kwa kuingiza mifugo hifadhini, hivyo basi,
Bunge linaazimia kwamba, Serikali isitishe mara moja zoezi la kutoa vibali
hivyo, kufuta vilivyopo na kuwataka raia hao wa kigeni wenye vibali
kuondoka Nchini mara moja.
xii.Kwa
kuwa, Kamati imebaini kwamba zaidi ya asilimia 25 ya eneo la Nchi ni
hifadhi, namipaka ya maeneo mengi yaliyohifadhiwa haijaainishwa, na kwa kuwa
Serikali haina uwezo wa (raslimali watu na fedha) wa kusimamia na
kulinda mipaka ya maeneo haya kikamilifu, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba,
Serikali kufanya yafuatayo:-
•
Kuridhia Idara ya Wanyamapori na Wakala wa Huduma ya Misitu kuajiri idadi ya
watumishi wanaotakiwa kama Serikali bado inaendelea kuyahifadhi maeno hayo.
• Kuainisha mipaka ya mapori yote ya akiba, hifadhi za taifa na Misitu ya
Serikali kwa alama maalumu na za kudumu ili kuepusha Wananchi kuingia katika
maeneo hayo kwa kutojua mipaka.
• Kuyaachia mapori ya Serikali ambayo yamekosa sifa, ili yatumike kwa kilimo na
ufugaji kwa kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi.
xiii.Kwa
kuwa,yapo maeneo ya mapori na Hifadhi ambayo yana migogoro ya muda mrefu ambapo
wananchi wameishi katika maeneo hayo kwa muda mrefu, hivyo basi, Bunge
linaazimia kwamba, Serikali irekebishe mipaka husika au iwahamishie Wananchi
hao kwenye maeneo mengine yenye miundombinu. Serikali iwaagize Mawaziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maliasili na Utalii na Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa kutembelea maeneo yote yenye migogoro nchini na kuitafutia
ufumbuzi ili wananchi waweze kuelewa hatma yao katika maeneo hayo kwani
wamekuwa katika hali ya sintofahamu kwa muda mrefu.
xiv.Kwa
kuwa, Kamati imebaini kuwepo kwa migogoro baina ya Wananchi, Wawekezaji na
hifadhi katika maeneo ya Meatu, Tarime, Bunda na ile ya Loliondo na Kimotorok
ambayo inashughulikiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, hivyo basi, Bunge linaazimia
kwamba, Serikali ihakikishe inamaliza (kama ilivyoahidi) migogoro iliyopo
Loliondo na Kimotorok na maeneo mengine mapema iwezekanavyo.
Kurekebisha
haraka kasoro zote za kisheria zilizokiukwa kwa makusudi na Idara ya
Wanyamapori kiasi cha kusababisha mgogoro baina ya Halmashauri ya Wilaya ya
Meatu na mwekezaji katika Pori la Hifadhi ya Jamii la Makao pamoja na
kuwawajibisha Watendaji wa Idara ya Wanyamapori waliosababisha mgogoro huo.
xv.Kwa
kuwa, Kamati imebaini kwamba, migogoro wanayokumbana nayo wafugaji kutokana na
kuingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na kero nyingine ni kutokana na
kukosekana kwa miundombinu sahihi na endelevu kwa ajili ya ustawi wa mifugo, na
kwa kuwa, Mheshimiwa Rais aliunda Wizara mahsusi kwa ajili ya kuendeleza Sekta
ya Mifugo nchini akitambua umuhimu wa Sekta hii kwa uchumi wa Taifa, na kwa
kuwa, Tanzania ni ya pili kwa wingi wa mifugo Barani Afrika, ni wazi kwamba
adha wanazokumbana nazo wafugaji ni matokeo ya kutokuwepo sera na mipango
madhubuti ya muda mfupi na mrefu.
Hivyo
basi, Bunge linaishauri Serikali kumtaka Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi, kujipima na kuona iwapo bado anastahili kuendelea kuhodhi wadhifa
alionao.
xvi.Kwa
kuwa, Kamati imebaini kuwa baadhi ya madai yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge
Bungeni wakati wakichangia Hoja ya Mhe. Saidi Nkumba ilikuwa ni ya kweli; na
kwa kuwa yaliyoelezwa katika madai hayo hayana uhusiano na Operesheni Tokomeza
kwani yalitokea kabla ya Operesheni hiyo; hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba,
Waheshimiwa Wabunge kuwa makini zaidi na kufanya utafiti kwa lengo la
kuhakikisha michango yao inakuwa sahihi na inalenga hoja mahsusi iliyo mbele ya
Bunge.
8.0
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, jukumu uliloikabidhi Kamati hii
lilikuwa zito na lilihitaji umakini mkubwa na muda wa kutosha katika
kulitekeleza. Kutokana na ufinyu wa muda na mazingira magumu wakati wa
kutekeleza jukumu hilo, Kamati inakiri kwamba haikuweza kutembelea maeneo yote
yaliyoathirika na zipo lawama kutoka kwa baadhi ya wananchi kwamba, Kamati
haikuweza kupita katika maeneo yao.
Mheshimiwa
Spika, Kamati inapenda kuwahakikishia
wananchi wote kuwa, kupitia taarifa mbalimbali za viongozi na wawakilisihi wa
waathirika mbele ya Kamati, malalamiko yao yamezingatiwa na kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa
Spika, kama tulivyoeleza katika maelezo
yetu ya utangulizi, Kamati inaamini na kote tulikopita wananchi wanakiri kuwa,
lengo na azma ya Serikali kuanzisha Operesheni Tokomeza Ujangili lilikuwa jema
kwani lililenga kunusuru maliasili zetu kwa ajili ya maendeleo endelevu na
heshima ya Taifa letu.
Mheshimiwa
Spika, Kamati inaamini maelezo yote
yaliyotolewa na wananchi pamoja na viongozi wao yalikuwa na dhamira njema.
Aidha, mapendekezo yaliyotolewa na Kamati yanalenga kuisaidia Serikali kuchukua
hatua za makusudi na haraka kurekebisha kasoro zilizojitokeza wakati wa
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, ili kuepuka kutokea kwa vitendo
vinavyoashiria ukiukwaji wa misingi ya haki za binadamu na Utawala Bora nchini.
Mheshimiwa
Spika, napenda kukushukuru wewe binafsi
kwa dhati kutokana na kuiamini Kamati yangu na kuikabidhi jukumu hili zito. Hii
ni ishara tosha kwamba una imani na Wabunge wako na kwamba wanaweza kufanya
kazi kwa niaba yako.
Mheshimiwa
Spika, pia nitoe shukrani za dhati kwa
Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Didimu Kashilillah, kwa kuiwezesha Kamati hii
kufanya kazi yake vizuri na kuikamilisha kwa wakati. Aidha, kwa namna ya pekee
napenda kuwashukuru makatibu walioihudumia Kamati hii wakiongozwa na Ndugu
Theonest K. Ruhilabake ambao ni Ndugu Gerald Magili, Ndugu Chacha Nyakega na
Ndugu Stanslaus Kagisa.
Aidha,
ninapenda kuwashukuru viongozi wa Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji ambao
walionyesha ushirikiano mkubwa Kamati ilipotembelea maeneo yao.
Mheshimiwa
Spika, mwisho lakini si kwa umuhimu
Kamati inawashukuru watumishi wafuatao; Ndugu Silva Chindandi, Ndugu Ndigwako
Mwaigaga, Ndugu Victoria Mizengo, Ndugu Germina Magohe na watumishi wengine
ambao kwa namna moja au nyingine walishiriki katika kuihudumia Kamati hii hadi
inakamilisha taarifa hii.
Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.
James
Daud Lembeli, Mb
MWENYEKITI KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA MAZINGIRA
.