Friday, December 20, 2013

Soma taarifa ya bunge iliyosababisha kung'olewa mawaziri wanne.


ISOME HAPA: taarifa ya kamati ya kudumu ya Bunge ya ardhi, maliasili na mazingira kuhusu tathmini ya matatizo yaliyotokana na oparesheni tokomeza
# 0
2435 Views
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, wakati Bunge likijadili hoja ya kuahirisha shughuli za Bunge ili kujadili jambo muhimu la dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 47 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2013, iliyowasilishwa na Mhe. Said Nkumba, Mbunge wa Sikonge kuhusu Mgogoro kati ya Wafugaji na Wakulima, Hifadhi na Uwekezaji, Mheshimiwa Spika alitoa Uamuzi ‘Speakers Ruling’  kuwa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ishughulikie kazi ya kutathmini na kuangalia jinsi Mpango wa Kupambana na Majangili  ulivyopangwa na kutekelezwa na Serikali kupitia ‘Operesheni Tokomeza’.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Taarifa Rasmi za Bunge za tarehe 1 Novemba 2013, wakati Bunge likihitimisha Hoja ya Kuairisha Shughuli za Bunge, Mhe. Spika alitoa uamuzi ufuatao:-
…Kamati ile ya kawaida ya Maliasili itaendelea na kazi yake ya kufanya tathmini ya kuangalia jinsi mpango ule wa Kupambana na Majangili ulivyopangwa na ndani yake itashughulikia kama kulikuwa na uzembe ama kuna watu wanahusika katika kuondoa maisha ya watu kwa sababu za uzembe …
1.1 Kuundwa kwa Kamati Ndogo ya Uchunguzi
Mheshimiwa Spika, kufuatia uamuzi ulioutoa tarehe 01 Novemba, 2013 Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ilikutana Dodoma tarehe 9 Novemba, 2013 kwa lengo la kujadili utaratibu wa kutekeleza jukumu hilo. 
Katika kikao hicho Kamati iliazimia kuunda Kamati Ndogo kwa mujibu wa Kanuni ya 117(18), ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Tole la 2013 ili iweze kushughulikia suala hilo kikamilifu.

1.2 Hadidu za Rejea, Wajumbe wa Kamati na muda wa kazi
Mheshimiwa Spika, Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyoundwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwa agizo lako la tarehe 01 Novemba, 2013, ilipewa Hadidu za Rejea Nne (4) zifuatazo:-
1) Kutathmini na kuangalia jinsi Mipango ya Kupambana  na Majangili ilivyopangwa;
2) Kuangalia kasoro zilizojitokeza katika kutekeleza mpango  huo;
3) Kutathmini iwapo kulikuwa na uzembe katika kutekeleza  Operesheni Tokomeza ambao ulisababisha watu wasio na hatia kupoteza maisha na mali zao; na
4) Kuchunguza migogoro ya Ardhi inayohusu Wakulima, Wafugaji na Wawekezaji kwenye maeneo yanayozunguka hifadhi.
Mheshimiwa Spika, Kamati hii ya uchunguzi iliundwa na Wajumbe Tisa (9) kama ifuatavyo:-
i. Mhe. James Daudi Lembeli, Mb.
ii. Mhe. Abdulkarim Esmail Shah, Mb.
iii. Mhe. Susan Limbweni Kiwanga, Mb.
iv. Mhe. Kaika Sanin’go Telele, Mb.
v. Mhe. Dk. Henry Daffa Shekifu, Mb.
vi. Mhe. Amina Andrew Clement, Mb.
vii. Mhe. Haji Khatibu Kai, Mb.
viii. Mhe. Muhammad Amour Chomboh, Mb.
ix. Mhe. Dk. Mary Mwanjelwa
Mheshimiwa Spika, Sekretarieti iliyohudumia Kamati Ndogo ya Uchunguzi iliundwa na Wajumbe wafuatao:-
i. Ndg. Theonest K. Ruhilabake
ii. Ndg. Gerald S. Magili
iii. Ndg. Chacha T. Nyakega
iv. Ndg. Stanslaus W.Kagisa
Mheshimiwa Spika, Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilitakiwa kutekeleza majukumu yake na kuwasilisha ripoti katika Mkutano wa Kumi na Nne (14) wa Bunge.  Hivyo basi, baada ya uteuzi huo, Wajumbe wa Kamati Ndogo walipanga kuanza kazi tarehe 25 Novemba, 2013 na kuikamilisha ifikapo tarehe 15 Desemba, 2013.
1.3 Njia zilizotumika katika kukamilisha kazi
Mheshimiwa Spika, Kamati Ndogo ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilitekeleza majukumu yake kwa kuongozwa na Hadidu za Rejea ilizopewa kwa kufanya rejea na kuzingatia yafuatayo:-
a) Kusoma na kuchambua nyaraka zilizoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuandaa na kutekeleza Operesheni Tokomeza nchini. Nyaraka hizo ni hizi zifuatazo:-
i. Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza (Concept Paper)
ii. Tathmini ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
iii. Sheria ya Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge (Na.3) 1988
iv. Sheria ya Wanyamapori (Na. 5) 2009
v. Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la mwaka 2013
b) Kufanya mahojiano na watu mbalimbali:-
i. Waziri wa Maliasili na Utalii
ii. Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii
iii. Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori
iv. Mkurugenzi Msaidizi Kikosi wa Dhidi ya Ujangili
v. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
vi. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)
vii. Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
viii. Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Hifadhi za Misitu (TFS)
ix. Mahojiano na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge
c) Kuzuru maeneo yaliyoanishwa katika Taarifa ya Wizara kuhusiana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na yale yenye migogoro kati ya Wakulima au Wafugaji na Wawekezaji katika maeneo ya hifadhi kwa lengo la kuhakiki (verify) masuala yaliyoainishwa kupitia uchambuzi uliofanywa na Kamati.
2.0 KUPOKEA NA KUCHAMBUA NYARAKA MBALIMBALI ZILIZOHUSU OPERESHENI TOKOMEZA
Mheshimiwa Spika, Hadidu Rejea ya kwanza iliitaka Kamati Ndogo ya Ardhi, Malisili na Mazingira, kufanya tathmini na kuangalia jinsi mipango ya kupambana na majangili ilivyopangwa. Ili kukamilisha jukumu hilo, Kamati ilifanya yafuatayo:-
a) Kupitia na kuchambaua Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza (Concept Paper) ulioandaliwa na Wizara
b) Kupitia na kuchambua Tathmini ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
2.1 Uchambuzi kuhusu Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, katika kuchambua Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza kwa lengo la kupata uelewa zaidi wa namna operesheni hiyo ilivyopangwa na kutekelezwa, Kamati ilibaini kuwa, mpango huo uliandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na ulikuwa na mambo yafuatayo:-
i. Ukubwa wa tatizo la ujangili
ii. Aina za ujangili na sababu za ukuaji wake
iii. Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ujangili
iv. Malengo ya Operesheni Tokomeza
v. Njia zilizotumika kutekeleza operesheni
vi. Maeneo ya operesheni na gharama za utekelezaji
vii. Tamko la Serikali kusitisha Operesheni Tokomeza
2.1.1 Ukubwa wa tatizo la ujangili
Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwa, tatizo la ujangili ni kubwa na limekuwa likisababisha idadi ya Tembo iendelee kupungua nchini. Takwimu zinaonesha kuwa, idadi ya Tembo imepungua kutoka 350,000 (miaka ya 1970) hadi kufikia 55,000 (mwaka 1989). Juhudi za kukabiliana na hali hiyo kupitia Operesheni zilizowahi kutekelezwa huko nyuma zilisaidia kuongeza idadi ya Tembo hadi 141,000 (mwaka 2006) ingawa ilishuka tena hadi kufikia 110,000 (mwaka 2009).
2.1.2  Aina za ujangili na sababu za ukuaji wake
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Serikali, vitendo vya ujangili vinavyofanyika nchini vimegawanyika katika makundi mawili yafuatayo:-
i. Ujangili wa Kujikimu (subsistance poaching)
Aina hii ya ujangili inahusisha watu wenye kipato kidogo na hulenga zaidi katika kujipatia kitoweo na fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji mengine. Ujangili wa aina hii huathiri zaidi wanyama wanaoliwa na si Tembo.
ii. Ujangili wa Biashara (commercial poaching)
Aina hii ya ujangili inahusisha zaidi watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha na hulenga kupata nyara zenye thamani kubwa. Wanyama wanaoathiriwa zaidi na aina hii ya ujangili ni pamoja na Tembo, Faru, Simba na Chui.
Mheshimiwa Spika, taarifa ilibainisha kuwa, kuongezeka kwa masoko haramu katika nchi za Asia na Mashariki ya Kati ambayo yanatoa bei kubwa ya nyara hizo, imekuwa ni chachu ya kuimarika kwa mitandao inayojihusisha na ujangili (ndani na nje ya nchi) na hivyo kusababisha ongezeko kubwa la vitendo vya ujangili.
2.1.3  Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ujangili
Mheshimiwa Spika, Mpango Kazi waKupambana na Ujangili ulilenga kujikita katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na ujangili wa wanyamapori na misitu. Mpango huo ulioelezewa kuwa niwa muda mrefu na kusimamiwa na kikosi kazi cha Taifa (national task force),umeanisha maeneo yafuatayo kuwa ndiyo yaliyoathirika zaidi:-
i. Pori la Akiba Selous
ii. Hifadhi ya Taifa Serengeti, Pori la Akiba Maswa na Pori Tengefu la Loliondo.
iii. Hifadhi ya Taifa Katavi na Mapori ya Akiba Rukwa na Lukwati.
iv. Hifadhi ya Taifa Mikumi
v. Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi za Taifa Tarangire na Ziwa Manyara.
vi. Mapori ya Akiba Burigi, Biharamuro, Ibanda na Rumanyika.
vii. Mapori ya Akiba Moyowosi, Kimisi, Ugalla na Hifadhi ya Misitu Luganzo.
2.1.4 Malengo ya Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, Operesheni Tokomeza ambayo ilizinduliwa rasmi tarehe 04 Oktoba, 2013 ilikuwa na malengo yafuatayo:-
i. Kuzuia vitendo vya ujangili ndani na nje ya Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na Misitu ya Hifadhi na kufanya operesheni maeneo yote yaliyoathiriwa na ujangili.
ii. Kuwatambua mapema majangili na kujua nyendo zao ndani na nje ya maeneo ya hifadhi.
iii. Kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wafanyabiashara haramu wa nyara za Serikali na mazao ya misitu.
iv. Kuvunja mitandao ya wafadhili, wanunuzi wadogo na wakubwa pamoja na mawakala wa biashara haramu ya nyara za Serikali na mazao ya misitu.
v. Kufuatilia na kukamata mali za majangili zilizotokana na biashara haramu ya nyara za Serikali na mazao ya misitu.
2.1.5 Njia zilizotumika kutekeleza Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwa, Mpango Kazi wa Serikali kuhusiana na Operesheni Tokomeza, uliainisha kuwa operesheni hiyo itaendeshwa kwa kutekeleza mambo yafuatayo:-
i. Kufanya uchambuzi wa kina wa watuhumiwa wa mtandao wa ujangili wa nyara za Serikali na wavunaji na wasafirishaji haramu wa mazao ya misitu.
ii. Kuwakamata watuhumiwa wote waliobainishwa kwenye taarifa za kiintelijensia.
iii. Kupiga picha na kuchora ramani ya eneo la tukio kwa kila mtuhumiwa (sketch map).
iv. Kuhoji na kuandika maelezo ya watuhumiwa wa ujangili wa nyara za Serikali na wavunaji na wasafirishaji haramu wa mazao ya misitu.
v. Kukusanya na kuhifadhi vielelezo vyote vitakavyokamatwa kutoka kwa majangili kwa ajili ya kujenga ushahidi mahakamani.
vi. Kuandika maelezo ya mashahidi na askari wakamataji kwa ajili ya kujenga ushahidi mahakamani.
vii. Kuandaa mashitaka dhidi ya watuhumiwa na kuwapeleka mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
2.1.6 Maeneo ya Operesheni na gharama za utekelezaji
Mheshimiwa Spika, Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza ulianisha kuwepo awamu mbili za utekelezaji ambazoni; Mpango Kazi wa Muda Mfupi na Mpango Kazi wa Muda Mrefu.
Katika Mpango Kazi wa Muda mfupi itafanyika operesheni maalum katika maeneo yote ya ndani na nje ya hifadhi za wanyamapori na misitu nchi nzima. Maeneo hayo yaligawanywa katika kanda 12 za utekelezaji kama ifuatavyo:-
i. Selous, Mikumi, Udzungwa, Lukwika/ Lumesule na Liparamba,
ii. Burigi/Biharamuro, Ibanda/Rumanyika na Rubondo,
iii. Moyowosi, Ugalla na Lugazo,
iv. Serengeti, Loliondo, Maswa, Ikorongo na Kijeshi,
v. Kilimanjaro, Arusha, Mkomazi/Umba, Simanjiro na Longido,
vi. Tarangile, Manyara, Karatu/Ngorongoro, Swagaswaga na Mkungunero,
vii. Rungwa, Ruaha, Mpanda – Kipengele,
viii. Rukwa, Lukwati, Katavi, Lwafi, Piti na Wembere,
ix. Mahale na Gombe,
x. Saadani na kwenye maeneo yenye misitu ya mikoko,
xi. Pori Tengefu la Handeni, Kilindi na Mkinga na
xii. Msitu wa Kazimzumbwi, Kisarawe, Rufiji na Mkuranga
,
Mheshimiwa Spika, ilianishwa kuwa, awamu ya kwanza ya Mpango Kazi wa muda mfupi ingegharimu jumla ya Tshs. 3,968,168,667/= ambazo zingechangwa na Taasisi za wanyamapori (WD, TANAPA, NCAA na TFS) kwa kila moja jumla ya Tshs. 992,042,167/=
2.1.7  Tamko la Serikali kusitisha Operesheni
Mheshimiwa Spika, kufuatia michango na malalamiko ya Waheshimiwa Wabunge wakati wakichangia hoja iliyotolewa na Mhe. Said Nkumba Mbunge wa Sikonge, pamoja na maagizo ya Bunge kutaka Serikaliitoe maelezo kuhusu hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge, Serikali ilitoa Tamko la kusitisha Operesheni Tokomeza tarehe 01 Novemba, 2013.
2.2 Uchambuzi wa Taarifa ya awali ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika, taarifa hii ya awali kuhusiana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ilikuwa na mambo yafuatayo:-
i. Washiriki wa operesheni
ii. Awamu za operesheni
iii. Mafanikio ya operesheni
iv. Idadi ya watuhumiwa na kesi zilizofunguliwa
v. Changamoto za operesheni
2.2.1 Washiriki wa Operesheni
Mheshimiwa Spika
, Operesheni Tokomeza ilihusisha jumla ya washiriki 2,371 kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa mgawanyo ufuatao:-
i. Wanajeshi (885) kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania,
ii. Askari (480) kutoka Jeshi la Polisi,
iii. Askari (440) kutoka Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU)
iv. Askari Wanyamapori (383) kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)
v. Askari (99) kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS)
vi. Askari Wanyamapori (51) kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
vii. Waendesha Mashitaka (23)  na
viii. Mahakimu (100
2.2.2 Awamu za Operesheni
Mheshimiwa Spika
, Operesheni Tokomeza ilipangwa kutekelezwa katika awamu Nne (4) kama ifuatavyo:-
i. Awamu ya kwanza ambayo ililenga kusaka Silaha za Kivita na Meno ya Tembo kutoka miongoni mwa wanaojihusisha na vitendo vya ujangili.
ii. Awamu ya pili ambayo ililenga kusaka silaha zisizomilikiwa kihalali na zile zinazomilikiwa kihalali lakini zinasadikiwa kutumika kwenye vitendo vya ujangili.
iii. Awamu ya tatu, ambayo ililenga kutafuta yalipo Maghala ya Nyara, kusaka Wafadhili na Wanunuzi wa nyara hizo na kuwabaini watu wanaowakingia kifua wahusika wa vitendo vya ujangili.
iv. Awamu ya nne, ambayo ililenga kukamata Nyara nyingine mbali na Meno ya Tembo na kuhakikisha watu walio katika makundi  yafuatayo wanakamatwa:-
- Wawindaji haramu,
- Wavunaji haramu wa mazao ya misitu,
- Watu wanaolisha Mifugo ndani ya hifadhi, na
- Watu waliojenga ndani ya maeneo ya hifadhi
2.2.3 Mafanikio ya Operesheni Tokomeza
a) Idadi ya watuhumiwa na kesi zilizofunguliwa
Mheshimiwa Spika, tangu kuanza kutekelezwa kwaOperesheni Tokomeza (tarehe 04 Oktoba, 2013 hadi ilipositishwa (tarehe 01 Novemba, 2013) jumla ya kesi 687 zilifunguliwa zikiwahusisha watuhumiwa 1,030 katika maeneo yote kama ifuatavyo:-
i. Kanda ya Kwanza kesi 105 zikiwahusisha watuhumiwa 105
ii. Kanda ya Pili kesi 370 ambazo zilihusisha watuhumiwa 375
iii. Kanda ya Tatu kesi 165 zilizohusisha watuhumiwa 498
iv. Kanda ya Nne kesi 47 zilizohusisha watuhumiwa 52
Mheshimiwa Spika, hadi wakati Operesheni Tokomeza inasitishwa tarehe 01 Novemba, 2013 kati ya Kesi 687 zilizokuwa zimefunguliwa ni 132 tu ndiyo zilikuwa zimetolewa maamuzi na 555 bado zilikuwa katika hatua ya kusikilizwa.  (Tazama Kiambatisho Na. 1)
i. Kukamatwa kwa meno ya Tembo 211 yenye uzito wa kilo 522, meno ya Ngiri 11, Mikia ya wanyama mbalimbali 36, Ngozi za wanyama mbalimbali 21, Pembe za Swala 46, Mitego ya wanyama 134, ng’ombe 7,621 Baiskeli 58, Pikipiki 8 na Magari 9.
ii. Kupungua kwa kasi ya mauaji ya Tembo kutoka wastani wa Tembo wawili (2) kwa siku hadi tembo wawili tu katika kipindi chote cha operesheni (siku 29).
iii. Hadi kufikia tarehe 11 Novemba, 2013 jumla ya Bunduki za Kijeshi 18 zilikamatwa, Bunduki za kiraia 1579, Risasi 1964, Mbao vipande 27,913, Mkaa Magunia 1242, Magogo 858 na Misumeno 60. Vyote hivyo vilikamatwa katika Kanda ya Nne.
2.2.4 Changamoto za Operesheni Tokomeza
a) Vifo vilivyotokea wakati wa Operesheni
Mheshimiwa Spika,Taarifa ya Serikaliiliainisha vifo kamachangamoto kubwa iliyojitokeza wakati wautekelezaji wa Operesheni Tokomeza kutokana na watumishi 6 na watuhumiwa 13 kupoteza maisha. (Tazama Kiambatisho Na. 2)
b) Hujuma dhidi ya Operesheni
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Serikali ilifafanua kuwa,utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ulikumbwa na vitendo vya hujuma kutoka kwa baadhi ya makundi ya jamii kama ifuatavyo:-
i. Mamluki miongoni wa washiriki wa Operesheni. Mfano; kukamatwa kwa Askari Polisi na Askari Wanyamapori wakisindikiza gari lenye Meno ya Tembo, na gari la Serikalikutumika kusafirisha Meno ya Tembo.
ii. Vyombo vya Habari kutumika kuvuruga operesheni kwakueneza propaganda zilizolenga kushawishi wananchi kupinga operesheni hiyo.
iii. Baadhi ya wamiliki wa silaha kutuhumiwa kutoa silaha zao ili zitumike kwa ajili ya vitendo vya ujangili.
C) Tuhuma dhidi ya Operesheni
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Serikai ilifafanua kuwa,ingawa lengo la operesheni lilikuwa ni kupambana na vitendo vya ujangili dhidi ya raslimali za Taifa, utekelezaji wake ulikumbwa na tuhuma kadhaa zikiwemo zifuatazo:-
i. Mateso dhidi ya watuhumiwa yaliyosababisha maumivu, kupata ulemavu wa kudumu na hata wengine kupoteza maisha (Mfano; Marehemu Emiliana Gasper Maro wa Gallapo – Babati).
ii. Matumizi mabaya ya Silaha (Mfano; Mzee wa miaka 70 kuuawa kwa kupigwa risasi 3).
iii. Nyumba za wananchi kuchomwa moto (Mfano; Kijiji cha Kabage Wilaya ya Mpanda – Katavi).
iv. Mifugo kuuawa kikatili kwa kuchomwa moto na kupigwa risasi (Mfano; Ng’ombe 60 kuuawa kwakupigwa risasi).
v. Kukosekana kwa mwongozo wa utoaji wa taarifa jambo lililosababisha viongozi husika wa Serikali kutopewa taarifa muhimu za utekelezaji wa Operesheni. (Mfano; Waziri wa Maliasili  naUtalii, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri wa Ulinzi na Wakuu wa Mikoa na Wilaya).
vi. Askari waliotuhumiwa kukiuka taratibu kukataa kutoa ushirikiano wa kutosha pale walipohitajika kufanya hivyo.
vii. Kutoshirikishwa kwa viongozi wa Mamlaka za Utawala katika ngazi za Mikoa na Wilaya.
3.0 MAHOJIANO BAINA YA KAMATI NA WIZARA PAMOJA NA WABUNGE
Mheshimiwa Spika, Kamati ilifanya mahojiano na makundi yafuatayo:-
i. Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake
ii. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
iii. Waheshimiwa Wabunge
3.1 Mahojiano baina ya Kamati na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake
Mheshimiwa Spika
, ili kuhakikisha wajumbe wa Kamati wanapata uelewa wa kutosha kuhusiana na Operesheni Tokomeza, Kamati liagiza uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ukiongozwa na Waziri, kufika mbele ya Kamati ili kueleza namna Operesheni Tokomeza ilivyoandaliwa na kutekelezwa hadi ilipositishwa kupitia tamko la Serikali lililotolewa Bungeni tarehe 01 Novemba, 2013.
Mheshimiwa Spika, Kamati ilikutana na Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na timu yake kwa siku tatu, tarehe 28- 29 Novemba, na tarehe 01 Desemba, 2013. Katika vikao hivyo, Waziri aliieleza Kamati juu ya Mpango Kazi wa Operesheni Tokomeza, raslimali (watu na fedha) pamoja na tathmini iliyofanyika kwa kipindi ambacho Operesheni Tokomeza ilitekelezwa.
Mheshimiwa Spika, katika mahojiano na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Khamis Kagasheki, Mb na watendaji wake Kamati ilifahamishwa yafuatayo:-
i. Kwamba Operesheni Tokomeza ilikuwa ya kijeshi kama alivyonukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard) akisema: “…Operesheni ilikuwa ya kijeshi. Ilikuwa ya kijeshi kwa sababu ilitekelezwa kwa amri ya jeshi Namba 0001/13 iliyotolewa tarehe 28 Septemba, 2013 na kusainiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi…”
ii. Kwamba, kinadharia inaonekana kwamba, Waziri wa Maliasili na Utalii ndiye alikuwa Msemaji Mkuu, lakini kiuhalisia hakuwa msemaji mkuu wa Operesheni Tokomeza kama alivyonukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge akisema; “…kinadharia inaweza ikasemekana kwamba mimi ndiye msemaji mkuu, lakini mimi sikuwa msemaji mkuu wa Operesheni Tokomeza …”
iii. Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ulisimamiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
iv. Taarifa za mwenendo wa operesheni zilikuwa zinapelekwa moja kwa moja kwa Mkuu wa Majeshi na kwamba, hazikumfikia Waziri wa Maliasili na Utalii.
v. Operesheni Tokomeza iliingiliwa na Wanasiasa.
vi. Pamoja na Mpango kazi huo kuandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa namna ambayo haieleweki Waziri hakuuona wala kuidhinisha rasimu ya mwisho ya Mpango huo. Hiyo ilidhihirika mbele ya Kamati kutokana na Waziri kukiri kwamba hakuuona wala kuudhinisha
3.1.1 Tathmini ya Kamati kuhusu majibu ya Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na watendaji wa Wizara
Mheshimiwa Spika
,kwa kutumia tathmini ya awali ya nyaraka zilizowasilishwa pamoja na mahojiano na Waziri ilionekana kwamba, Operesheni Tokomeza iliandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini yake na kushirikisha vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Mheshimiwa Spika, licha Mpango wa Operesheni Tokomeza kuandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, hata hivyo utekelezaji wake ulisimamiwa na kuongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Hatua ya jeshi kuchukua jukumu la kuongoza Operesheni Tokomeza, lilifanya viongozi wa Wizara kujiengua katika jukumu la kuongoza (ead agency) na badala yake kuacha jukumu hilo kwa Jeshi pekee jambo lililotafsiriwa kwamba, Operesheni Tokomeza ilikuwa ya kijeshi.
Mheshimiwa Spika, kupitia mahojiano ilibainika kwamba, hakukuwa na utaratibu mzuri wa kupashana habari kuhusiana na mwenendo mzima wa Operesheni Tokomeza jambo lililofanya baadhi ya wahusika kutotambua kikamilifu wajibu waokatika Operesheni hiyo.Mfano mzuri ni kwamba, licha ya kuelezwa kwenye Kanuni za Utendaji (Operational Guidelines) za Operesheni Tokomeza kwamba, Waziri wa Maliasili na Utalii ndiye atakuwa Msemaji Mkuu wa Operesheni Tokomeza, bado Mhe. Waziri hakutekeleza jukumu hilo kwani alikwishatoa mapendekezo katika rasimu kwamba Msemaji Mkuu awe ni Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Aidha, Kamati ilibaini kuwa baadhi ya Watendaji wa juu wa Wizara walidaiwa kukwamisha utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Maliasili na Utalii kutokana na kuingilia mawasiliano aliyokuwa anayafanya na baadhi ya Watumishi. Mfano ni majibizano kwa njia ya barua pepe kati ya Waziri na Katibu Mkuu, Waziri na Mkurugenzi wa Wanyamapori na pia Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Wanyamapori. Kwa mujibu wa majibizano hayo Waziri anaonekana kushangazwa na hatua ya Katibu Mkuu kuhoji hatua ya yeye kumuita mmoja wa mtumishi wa Wizara ofisini kwake. (Kiambatisho Na. 3)
Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa mfumo mzuri wa kupashana habari kwa pande husika kuhusu mwenendo mzima wa Operesheni Tokomeza, kulionekana kuathiri utaratibu mzima wa viongozi husika akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, kupata taarifa zinazotakiwa kwa wakati. Hali hiyo ilichangia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kukumbwa na athari ambazo zingeweza kuepukika iwapo kungekuwa na mfumo mzuri wa mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, kupitia mahojiano pia Kamati ilibaini uwepo wa hujuma kutoka kwa viongozi wa kisiasa na Serikali ambao kwa namna moja au nyingine walionekana kuhusishwa na Operesheni Tokomeza ama wao binafsi au ndugu zao.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa hujuma ambazo Kamati ilizibaini kupitia mahojiano naWaziri wa Maliasili na Utalii na Watendaji wake ni pamoja na:-
i. Baadhi ya watuhumiwa wenye mahusiano na viongozi wa kisiasa kutumia majina ya viongozi hao kuingilia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
ii. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kutuhumiwa kujihusisha navitendo vya ujangili na biashara haramu ya nyara za Serikali.
iii. Baadhi ya Mawaziri kutoa kauli zenye kuingilia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. (Mfano: kutoa maelekezo kwa wahusika wa Operesheni Tokomeza kwamba wasiguse viongozi wa kisiasa wa ngazi zote).
iv. Baadhi ya viongozi wavyombo vya Ulinzi na Usalama kushiriki kudhoofisha utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kwa kusindikiza au kusaidia watuhumiwa wa ujangili kutoroka. (Mfano; viongozi wa Polisi wa Wilaya na Mikoa)
Mheshimiwa Spika, kubainika kwa hujuma hizo ni ishara tosha kwamba hata ndani ya Serikali yenyewe hakukuwa na dhamira ya dhati kwa baadhi ya kwa viongozi na watendaji katika kuhakikisha vita dhidi ya vitendo vya kijangili inapiganwa kikamilifu.
Hali hiyo ilisababisha utekelezaji wa operesheni kukumbwa na athari nyingi kama vile; wananchi kupoteza maisha, mifugo kuuawa kwa kuchomwa moto, njaa, kiu au kupigwa risasi), upotevu wa mali, nyumba kuchomwa moto na vitendo vya ukatili dhidi ya wananchi ambavyo vilikiuka haki za kibinadamu. Hali hiyo imesababisha utekelezaji wazoezi la Operesheni Tokomeza kutafsiriwa kwamba ulilenga wananchi wasio na hatia na kuacha wahusika wa ujangili.
3.2 Mahojiano baina ya Kamati na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mheshimiwa Spika
, mnamo tarehe 30 Novemba, 2013 Kamati ilikutana na kufanya mahojiano na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kubaini namna ilivyoshiriki katika Operesheni Tokomeza.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Dk. Emmanuel Nchimbi, Mb alieleza kuwa, operesheni hii ilikuwa na lengo la kutimiza azma (Commitment) ya Serikali iliyoitoa Bungeni kwamba, inakusudia kufanya Operesheni ya kupambana na majangili.
Wizara yake ilishiriki kwa kutoa Askari Polisi 504 pamoja na baadhi ya vyombo vya usafiri na kwamba vyombo vya Ulinzi na Usalama vya nchi vilikuwa vikikutana mara kwa mara kwa lengo la kuandaa mkakati wa namna ya kushirikiana katika kutekeleza mpango huo wa vita dhidi ya ujangili.
Mheshimiwa Spika,Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alikiri kuwa, licha ya lengo la operesheni kuwa zuri, kulijitokeza changamoto kadhaa zilizotokana na baadhi ya washiriki wa operesheni kwenda kinyume na malengo yaliyokusudiwa kama vile; ukatili dhidi ya mifugo na vitendo vya unyanyasaji wa wananchi kwa kuwatesa kiasi cha kuwasababishia ulemavu wa kudumu au vifo. 
Pia Mheshimiwa Waziri alikiri kwamba, kutokuwepo mfumo mzuri wa mawasiliano na Operesheni kuongozwa na jeshi, iliashiria kwamba taarifa za operesheni zilikuwa zinakwenda kwa Mkuu wa Majeshi – CDF moja kwa moja na hivyo kufanya pande zingine zinazohusika zisijue kinachoendelea.
3.2.1    Tathmini ya Kamati kuhusu majibu ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na watendaji wake
Mheshimiwa Spika, Kamati ilibaini kuwepo kwamawasiliano hafifu kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara nyingine zilizoshiriki katika operesheni hii.Pia,kukosekana kwa mfumo mzuri wa mawasiliano, kuliikosesha Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo iliandaa na kugharamia Operesheni Tokomeza,fursa ambazo zingeiwezesha kufanya tathmini kuhusu utekelezaji wa Operesheni hii.
Aidha, Kamati ilibaini kwamba, hatua ya kutoshirikisha Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya ililenga kutovujisha siri dhidi ya watuhumiwa wa ujangili. Hatua hiyo ilisababisha usumbufu mkubwa kwa viongozi wa mamlaka za utawala za Wilaya na Mikoa kutokana na kulaumiwa na wananchi kwa kushindwa kuwasaidia pale walipokumbwa na matatizo.
3.3     Mahojiano baina ya Kamati na Waheshimiwa Wabunge
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala hili liliibukia Bungeni baadaya  wawakilishi wa wananchi kupaza sauti kuhusu athari zilizowakumba wapiga kura wao, Kamati iliona ni busara kuhoji baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja hii. Wabunge hao walitoa taarifa muhimu kuhusu vitendo vilivyofanyika katika maeneo yao wakati wa operesheni.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge walieleza kusikitishwa na namna ambavyo Operesheni Tokomeza ilikiuka malengo yaliyokusudiwa na badala yake ikanyanyasa wafugaji kwa kuangamiza mifugo yao na kuwaharibia mali zao kama vile; kuchoma moto nyumba, kupora fedha na vitu vingine. Mbunge mmoja alinukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge akisema:-
“…badala ya Operesheni Tokomeza kusaka majangili, ikageuka kuwa Operesheni Tokomeza Ufugaji…”
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge waliieleza Kamati kuwa, siyo jambo la kawaida kwa watu wanaoagizwa kufanya jambo fulani kwenda kinyume na maagizo.
Wakashauri kuwa, wahusika wote waliotenda kinyume namaagizo wachukuliwe hatua stahiki ili kuepusha vitendo vya aina hiyo visijirudie katika operesheni zitakazofuata. Pia Waheshimiwa Wabunge walishauri kasoro zilizojitokeza zirekebishwe na operesheni iweze kuendelea ili kutowapa mwanya majangili kujipanga upya.
3.3.1 Tathmini ya Kamati kuhusu majibu ya Waheshimiwa Wabunge
Mheshimiwa Spika, kimsingi Waheshimiwa Wabunge wanaunga mkono Operesheni Tokomeza ambayo ililenga kukomesha vitendo vya kijangili na kunusuru raslimali za nchi hasa wanyamapori na misitu. Hata hivyo, walieleza kusikitishwa na vitendo vilivyojitokeza wakati wa utekelezaji wa operesheni na walisema haviwezi kuvumilika.
Mheshimiwa Spika, baada ya kupata taarifa mbalimbali kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge, mahojiano na viongozi na watendaji wa Wizara na kuzingatia taarifa zilizowasilishwa na Serikali, Kamati iliazimia kuzuru baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na Operesheni Tokomeza ili kufanya uhakiki.
4.0      KAMATI KUZURU MAENEO YALIYOATHIRIKA KWA AJILI YA KUHAKIKI (VERIFICATION/OUTREACH)
Mheshimwa Spika, kutokana na wingi wa maeneo pamoja na ufinyu wa muda, Kamati ilijigawa katika makundi matatu ili yaweze kutembelea baadhi ya maeneo yaliyoainishwa katika Taarifa ya Serikali ili kufanya tathmini (verification) kwa utaratibu ufuatao:-
4.1 Kundi la kwanza lilielekea Kanda ‘C’iliyohusisha maeneo yaliyoathiriwa na Operesheni Tokomeza katika Mikoa ya Shinyanga, Kagera, Tabora,   Kigoma, Rukwa, Katavi na Singida.
Mheshimiwa Spika, kundi hili liliundwa na Wajumbe wafuatao:-
Mheshimiwa James Daudi Lembeli, Mb, Mheshimiwa Haji Khatibu Kai, Mb na Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mb.
4.2 Kundi la pili lilielekea Kanda ‘B’iliyohusisha maeneo yaliyoathiriwa na Operesheni Tokomeza katika Mikoa ya Simiyu, Mara, Arusha na Manyara.
Mheshimiwa Spika,kundi hili liliundwa na wajumbe wafuatao,  Mheshimiwa Abdulkarim E. Shah, Mb, Mheshimiwa Henry Daffa Shekifu, Mb na Mheshimiwa Amina Andrew Clement, Mb.
4.3 Kundi la tatu lilielekea Kanda ‘D’iliyohusisha maeneo yaliyoathiriwa na Operesheni Tokomeza katika Mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa, Ruvuma na Mtwara.
Mheshimiwa Spika, kundi hili liliundwa na wajumbe wafuatao; Mheshimiwa Kaika Saning’o Telele, Mb, Mheshimiwa Muhammad Amour Chomboh, Mb na Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, ambaye hata hivyo hakushiriki kutokana na dharura.
Mheshimiwa Spika,kama ilivyoainishwa hapo juu lengo la Kamati kutawanyika Mikoani lilikuwa kutathmini athari zilizotokana na Operesheni Tokomeza ambayo iliendeshwa nchini kuanzia tarehe 04 Oktoba, 2013 hadi tarehe 01 Novemba, 2013.
Mheshimiwa Spika, ili kutimiza jukumu hilo kikamilifu, Kamati iliongozwa na taarifa zifuatazo;
i. Mpango Kazi wa Operesheni Maalum ya kupambana na Ujangili nchini,
ii. Taarifa ya Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza iliyotolewa na Serikali.
iii. Michango ya Waheshimiwa Wabunge kama ilivyonukuliwa katika Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard).
iv. Madai yaliyotolewa na Wabunge kuhusiana na athari zilizotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
v. Maelezo yaliyotolewa na Mashahidi ambao walihojiwa na Kamati.
vi. Vielelezo vilivyowasilishwa na Mashahidi waliofika mbele ya Kamati.
5.0  MAKUNDI YA KAMATI YALIVYOTEKELEZA MAJUKUMU YAKE
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu hili, Kamati ilikutanana makundi yafuatayo:-
i. Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya
ii. Waheshimiwa Madiwani
iii. Waathirika wa Operesheni Tokomeza
5.1 Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya
Mheshimiwa Spika
, Kamati ilikukutana na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya na kupokea taarifa iliyohusu hali ya Ulinzi na Usalama hususan wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
Mheshimiwa Spika, kwa sehemu kubwa taarifa za Ulinzi na Usalama za Wilaya zilisaidia kuanisha maeneo na matukio yaliyojiri wakati wa Operesheni Tokomeza na athari zilizojitokeza. Wajumbe wa Kamati walitumia uchambuzi wa taarifa hizo kupata uelewa zaidi kuhusiana na utekelezaji wa Operesheni hiyo kabla ya kukutana na wananchi walioathirika ili kupata maelezo zaidi.
5.2 Waheshimiwa Madiwani
Mheshimiwa Spika
,katika baadhi ya Wilaya, Kamati ilikutana nabaadhi ya Madiwani wakiwa ni wawakilishi wa wananchi katika ngazi ya halmashauri ili kupata maelezo zaidi kuhusu utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kabla ya kukutanana waathirika wa Operesheni.
5.3  Waathirika wa Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika
, Kamati ilikutana nabaadhi ya wananchi walioathirika na Operesheni Tokomeza na kupokea maelezo na malalamiko yao kuhusu namna walivyoathiriwa na uekelezaji wa Operesheni.
Mheshimiwa Spika, wapo baadhi ya waathirika walitoa ushahidi/vielelezo vya maandishi na picha ili kuthibitisha yale waliyokuwa wakiyaeleza mbele ya Kamati. Wengine walikwenda mbali kiasi cha kuonesha majerahana makovu waliyoyapata katika miili yao kutokana na mateso waliyopata kwenye kambi maalum za mahojiano zilizoandaliwa na waendeshaji wa Operesheni Tokomeza.
5.4  Kuzuru maeneo yaliyoathirika zaidi na Operesheni
Mheshimiwa Spika
, Kamati ilipata fursa ya kutembelea baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na athari za operesheni Tokomeza kwa lengo la kushuhudia mabaki ya vielelezo ili kujiridhisha iwapo tuhuma za athari zilizotolewa kuhusu maeneo hayo zilikuwa zakweli.
6.0  YALIYOBAINIKA KATIKA ZIARA ZA KAMATI
6.1 Vikao na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa/Wilaya
Mheshimiwa Spika, katika vikaona Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa/ WilayaKamati ilibaini kuwa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza haukushirikisha viongozi wa maeneo hayo ya utawala. 
Kulikuwa na manung’uniko kwamba licha ya Wakuu wa Wilaya na Mikoa kuwa wawakilishi wa Rais, waliachwa kando na Operesheni kuendeshwa katika maeneo wanayosimamia hadi malalamiko ya wananchi waliokamatwa yalipowafumbua macho kwamba walikuwa wanateswa na kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na watekelezaji wa Operesheni. Aidha, 
Kamati ilielezwa kwamba utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ulisababisha hofu miongoni mwa wananchi na viongozi na kusababisha baadhi yao kukimbia makazi. Mfano; Mkuu wa Wilaya ya Ulanga alikiri kujihifadhi kwenye Hoteli moja nje ya Wilaya yake ambako alikutana na baadhi wananchi wake waliokimbia adha za Operesheni Tokomeza.
Viongozi hao walieleza kwamba, kimsingi hawapingi Operesheni Tokomeza Majangili kwaniililenga kunusuru raslimali za nchi hasa wanyamaporina misitu visitoweke kutokana nakushamiri kwa vitendo vya ujangili. Hata hivyo, walieleza kuwa hatua ya kutowashirikisha imelifanya zoezi hilo kuwa na kasoro nyingi pamoja na udhalilishaji hata kwa viongozi waliochaguliwa na wananchi.
6.2 Vikao vya Kamati na Waathirika wa Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika,
Kamati ilifanya mikutano mbalimbali katika baadhi ya maeneo ilikofanyika Operesheni Tokomezakwa lengo la kuwasilikiliza waathirika na kubaini mambo yafuatayo:-
Watuhumiwa kupekuliwa, kudhalilishwa na baadhi kutojulikana walipo
i. Mheshimiwa Spika, badhi ya wananchi wakiwemo viongozi, Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji na Watumishi wa Serikali walikamatwa na kudhalilishwa mbele ya wananchi wanaowaongoza. Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa walikuwa hawajulikani walipo hadi Kamati ilipozuru maeneo hayo. Mfano; Vijana watatu wa Kijiji cha Osteti, Kata ya Chapakazi, Wilayani Kiteto, walituhumiwa kujihusisha na biashara ya Meno ya Tembo. Vijana hao ni Nyafuka Ng’onja, Ng’onja Kipana na Mswaya Karani.
ii. Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa walidai kudhalilishwa mbele ya wanafamilia kwa kupewa adhabu wakiwa uchi na wanawake kushikwa sehemu za siri bila ridhaa yao. Mfano; ndugu Ali Nyenge (38) wa Kata ya Iputi, Wilaya ya Ulanga alidai kuvuliwa nguo, kumwagiwa maji yaliyochanganywa na chumvi na kuchapwa viboko huku mwanae wa kiume (11) akishuhudia. 
Pia alidai kulazimishwa kuchora picha ya Chatu kwa kutumia wembe kwenye paja lake. Vilevile, Bi. Neema Moses wa Babati alidai kuvuliwa nguo na kulazimishwa afanye mapenzi na wakwe zake na pia kuingizwa chupa sehemu zake za siri.
Aidha, baadhi ya akina mama walidai kubakwa na kulawitiwa. Mfano; katika Kata ya Iputi, Wilaya ya Ulanga, mwanamke mmoja alidai kubakwa na Askari wawili (2) wa Operesheni Tokomeza Ujangili mida ya usiku. Vilevile, mama mmoja mkazi wa Kata ya Matongo Wilayani Bariadi, alibakwa na askari watatu (3) wa Operesheni Tokomeza Ujangili huku akiwa ameshikiwa mtutu wa bunduki
iii. Watuhumiwa waliokamatwa walifanyiwa upekuzi bila kuhusisha viongozi wa Serikali za maeneo husika na kutokuwepo kwa mashahidi na hati za upekuzi. 
Mfano; Ndg. Abdallah Pata na Bi. Flora Mwarabu wa Kata ya Iputi Wilayani Ulanga na Ndg. Elias Cosmas Kibuga wa Gallapo Babati, walipekuliwa bila kufuata utaratibu.
Ukatili na Udhalilishaji katika Kambi za Mahojiano
iv. Mheshimiwa Spika, baadhi ya watuhumiwa waliopelekwa katika kambi za mahojiano walidai kuteswa kwa adhabu zinazokiuka haki za binadamu. Mfano; Diwani wa Kata ya Sakasaka wilaya ya Meatu Ndg. Peter Samwel, alidai kuadhibiwa akiwa mtupu kwa kupewa adhabu za kijeshi kama kuning’inizwa kichwa chini miguu juu, kupigwa kwa vyuma na kulazimishwa kufanya mapenzi na mti.
 
Mheshimiwa Spika, kutokana naukatili uliopitiliza, baadhi ya kambi za mahojiano zilipewa majina kama vile Guantanamo (Ruaha), Goligota (Ngorongoro), Duma na Andajega (Serengeti).
Upotevu wa mali za watuhumiwa na faini zisizoeleweka
v. Mheshimiwa Spika
, ilidaiwa kuwa wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, baadhi ya watuhumiwa walipoteza mifugo, mali na fedha zao. Mfano; katika Wilaya ya Ulanga Kata ya Iputi mwananchi mmoja alidai kuporwa sanduku la VICOBA lenye shilingi laki saba na nusu (750,000/=) pamoja na simu ya mkononi na Askari wa Operesheni Tokomeza waliovamia nyumbani kwake. Vilevile Ndugu Musa Masanja wa Sakasaka Wilaya ya Meatu, alidai kuporwa shilingi laki tatu 300,000/= pamoja na simu 2 za mkononi na Askari Askari wa Operesheni.
Mheshimiwa Spika,Pia ilidaiwa kuwa mifugo ya watuhumiwa ilikamatwa na kuingizwa ndani ya maeneo ya hifadhi na kufa kwa kupigwa risasi au kukosa maji na malisho kutokana na kuzuiliwa kwa muda mrefu. 
Baadhi ya mifugo ilitozwa faini bila stakabadhi au stakabadhi kuonesha viwango vidogo ikilinganishwa na fedha halisi iliyolipwa. Mfano:Ndugu Sosoma Shimula mwenye Ng’ombe 1700 Wilayani Kasulu alidai kwamba alitakiwa kulipa faini ya shilingi Milioni thelathini (30,000,000/=, alipowasihi alipunguziwa hadi Milioni kumi na mbili (12,000,000/=) hata hivyo aliweza kulipa Milioni kumi (10,000,000/=). 
Alionesha Kamati stakabadhi inayoonesha kuwa amelipa faini ya shilingi milioni moja tu (1,000,000/=). Stakabadhi hiyo ilijazwa sehemu ya tarakimu, lakini hakuna kilichoandikwa katika sehemu ya kiasi cha fedha kwa maneno. (Tazama Kiambatisho Na. 4)
Watuhumiwa kuteswa na kuumizwa
vi. Mheshimiwa Spika
, baadhi ya watuhumiwa walidai kupigwa na kuumizwa na askari wa Operesheni na wengine kupata ulemavu wa kudumu. Mfano; katika Wilaya ya Itilima,Kijiji cha Mbogo Ndg Sita Rumala alidai kupigwa na kuvunjwa mkono alionesha wajumbe mkono uliokuwa umefungwa bandeji ngumu (P.O.P).
Aidha, Diwani Peter Samwel Ndekija wa Kata ya Sakasaka, Wilaya ya Meatu, alidai kupigwa na kuumizwa vibaya mgongoni na alionesha kwa wajumbe wa Kamati makovu aliyoyapata. Vilevile,ilielezwa kuwa Ndugu Munanka Machumbe (24) ambaye ni bubu alipigwa risasi 3 zilizomjeruhi mapajani na kuharibu sehemu za siri wakati akijaribu kuwahoji Askari wa Operesheni kwa ishara sababu za kumtesa baba yake.
Aidha, katika tuko lingine Shekhe Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ali Mohamed (70) aishiye kijiji cha Iputi, alidai kurushwa kichura na kutandikwa bakora na Askari wa Operesheni Tokomeza. Pia,Ndg.  Nyasongo Magoro Serengeti wa Kata ya Majimoto wilaya ya Mulele alidhalilishwa mbele ya wananchi wake.  (Tazama Kiambatisho Na. 5)
Mifugo kuingizwa hifadhini na watuhumiwa kubambikwa kesi
vii. Mheshimiwa Spika
,wakati wa Operesheni, mifugo mingi ilikuwa hifadhinilakini hata ile iliyokuwa nje ya hifadhi iliingizwa na askari wa hifadhi na wafugaji kutakiwa walipe faini ya shilingi Milioni tatu (3,000,000/=) hadi Sita (6,000,000/=) kwa idadi ya ng’ombe 30 hadi ng’ombe 100 na aliyeshindwa kulipa faini mifugo yake iliuawa au kupigwa mnada na mfugaji kufilisiwa. 
Walioshindwa kulipa faini mifugo ilipigwa mnada na wafugaji hawakuruhusiwa kununua wala kukaribia eneo la mnada, na katika mnada mifugo iliuzwa kwa bei ya chini kuliko faini iliyotozwa Mfano; shilingi elfu sitini (60,000/ =) kwa kila ng’ombe.
Watuhumiwa kubambikwa kesi
viii.Ilidaiwa kwamba, baadhi ya watuhumiwa walidai kubambikwa makosa ambayo hawahusiki nayo kama vile kumiliki silaha kinyume na sheria, kukutwa na bangi au nyara za Serikalimfano; Bw. Elias Cosmas Kibuga wa Gallapo Babati alidai kubambikiwa kesi ya kumiliki bunduki kukutwa na mkia wa twiga kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Spika, pia Bibi Zuhura Ali wa Kilombero alidai kuteswa huku akilazimishwa kutoa silaha ambayo hakuwa nayo. Aidha, Bw. Melkzedeck Abraham Sarakikya wa Itigi alidai kuteswa akilazimishwa atoe silaha.
Mateso na vifo kwa Watuhumiwa
ix. Mheshimiwa Spika
, baadhi ya wananchiwalidai kuwa ndugu zao waliteswa kikatili kwa muda mrefu na bila kupatiwa huduma za lazima kama chakula, maji na matibabu (siku 1 -2) hadi mauti yalipowafika. Kwa mfano Ndg. Kipara Issa wa Wilaya ya Kaliua na ndugu Emiliana Gasper Maro wa Gallapo, Wilaya ya Babati. 
Aidha, wananchi hao walidaikuwa mahojiano kwa watuhumiwa yaliambatana na mateso makali kwa muda mrefu kiasi cha kusababisha vifo. (Tazama Kiambatisho Na. 6).
Vilevile, watuhumiwa wengine waliodaiwa kupoteza maisha wakati wa Operesheni Tokomeza ni Ndg. Wegesa Kirigiti wa Kijiji cha Remagwe na Ndg. Peter Masea wa Kijiji cha Mrito (Tarime), Ndg. Mohamed Buto (Masasi) na Gervas Nzoya (Kasulu).
Mheshimiwa Spika, pamoja na uthibitisho wa picha zilizotolewa na wananchi kuhusu kuteswa hadi kufa kwa Bi Emiliana Gasper Maro, Serikali kupitia Mkurugenzi wa Wanyamapori ilitoa Taarifa kwa Umma ikipinga Taarifa iliyorushwa na kituo cha luninga cha ITV tarehe 19 Oktoba 2013 kuhusu mauaji ya kutisha yaliyofanywa na Askari wa kupambana na ujangili. 
Taarifa hiyo ya Serikali inapinga kuwa Askari wa Operesheni Tokomeza hawausiki na kifo cha mtajwa. Taarifa hiyo imeonekana kukosa umakini kutokana na kujichanganya juu ya watu inaowazungumzia. Taarifa hiyo inazungumzia majina mawili tofauti (Evelyn Gasper na Mariana Gaspar Mallo wa eneo la Olongadiola) wakati muathirika halisi ni Bi. Emilliana Gasper Maro wa Kijiji cha Orngadida, Gallapo.  (Tazama kiambatisho Na.7)
Ukatili dhidi ya Wanyama
x. Mheshimiwa Spika
, kuhusu vitendo vya ukatili kwa wanyama ilidaiwa kwamba ng’ombe walipigwa risasi, na ndama walikufa kwa kukosa maziwa kutokana na mama zao kukamatwa na kuzuiwa kwenye mazizi yaliyopo maeneo ya hifadhi kwa muda mrefu. (Tazama Kiambatisho Na. 8)
Rushwa kwenye Mapori ya Akiba
xi. Mheshimiwa Spika
, Wananchi walidai kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwa watumishi wanaosimamia mapori ya akiba ya Maswa, Kigosi Moyowosi, Burigi, Kimisi na Mkungunero kwa kutaja majina ya baadhi ya watumishi wanaowatuhumu. Mfano; Ndg. Kileo mtumishiwa pori la Maswa, alidaiwa kuwa na tabia ya kutoza wananchi faini bila stakabadhi au kutoa stakabadhi kinyume na faini iliyotolewa au kutoa stakabadhi bandia. 
Aidha, katika pori la Kigosi-moyowosi, watumishi wafuatao walidaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa; Ndg. Msocha, Alfred, Kobelo na Odhiambo.
Aidha, ilidaiwa kuwa katika mapori ya Kigosi Moyowosi na Kimisi zaidi ya wafugaji 100 wenye ng’ombe wanaokadiriwa kuwa 50,000 wanalipia kuchungia ng’ombe wao kwenye mapori hayo ya hifadhi tangu mwaka 2000 kwa malipo maalum na hata Operesheni Tokomeza haikuwagusa. 
Aidha, ilidaiwa kuwa Ndg. Msocha (Meneja wa Pori la Akiba la Kigosi Muyowosi), alituhumiwa na baadhi ya wananchi kuwa amekuwa akiwakodisha wafugaji hao kwa vipindi vya miezi mitatu, na wafugaji huruhusiwa kulipa tena muda unapoisha. Aidha, Mfugaji ambaye hulipa kiasi kidogo hulazimishwa kulipa huku akipigwa namifugo yake kuuawa kwa kupigwa risasi.
Ilielezwa kuwa, Wafugaji na Askari Wanyamapori huwasiliana kwa simu ilil kutekeleza makubaliano ya malipo kwa malisho yao. Nambaza simu zinazodaiwa kuwa za Askari Wanyamapori zimeorodheshwa. (Tazama Kiambatisho Na. 9)
Mahusiano kati ya wananchi na Askari wa mapori ya Akiba
xii. Mheshimiwa Spika
, wananchi wanaoishi kwenye Mapori ya Akiba yanayo wazunguka walidai kuwa katika mahusiano mabaya na Askari wa mapori hayo. Mfano;wananchi wa kijiji cha Kimotorok, Wilaya ya Simanjiro na Askari wa pori la akiba la Mkungunero kiasi cha kufikia hatua ya kutishiana maisha. Vitendo hivyo pia vipo kwa jamii zinazopakana na mapori ya Gurumeti.
Mahakama na Magereza kuzidiwa uwezo
xiii.Mheshimiwa Spika,
kutokana na Operesheni Tokomeza ilidaiwa kuwa vyombo Mahakama na Magereza katika maeneo husika vilizidiwa uwezo kutokana na wingi wa kesi na idadi ya Mahabusu. Mfano; Gereza la Wilaya ya Bunda lenye uwezo wa kuchukua jumla ya wafungwa na mahabusu 217 lililazimika kuchukua hadi watu 411. 
Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa wanalazimika kusafiri umbali mrefu kuhudhuria kesi zao. Mfano; katika wilaya ya Serengeti baadhi ya watuhumiwa walifunguliwa kesi Wilaya za Tarime, Bunda na Bariadi.
Watumishi wa Umma kuhusishwa na Ujangili
xiv.Mheshimiwa Spika
, ilidaiwa kuwa baadhi ya Watumishi wa Serikali na vyombo vya dola (Polisi) wanajihusisha na ujangili. Mfano ni Dereva wa OCD, Wilaya ya Ngorongoro aliyetuhumiwa kujihusisha na ujangili wa Meno ya Tembo.
Askari huyo alihojiwa na viongozi wa Operesheni Tokomeza katika kituo chake cha kazi. Vilevile, Ndg. Mohamed Ismail, Afisa Wanyamapori (W) Meatu anatuhumiwa kukutwa na nyara za Serikali. Aidha,Askari Polisi wawili (2 )Cpl. Isaack na PC Sixbert wa Mugumu Wilayani Serengeti walikamatwa wakiwa na meno ya Tembo.
Mheshimiwa Spika, pia ilidaiwa kuwa baadhi ya Maofisa wa Serikali wamekuwa wakitumia magari ya Umma ama kusafirisha au kusindikiza watoroshaji wa nyara za Serikali. Mfano nigari la Serikali lililokamatwa likifaulisha meno ya Tembo kutoka kwenye gari jingine huko Mkuranga kwa lengo la kuyasafirisha kwenda Dar es Salaam. 
Sambamba na hilo baadhi viongozi wa jeshi la Polisi wametuhumiwa kusaidia watuhumiwa wa vitendo vya kijangili kutoroka na kuepuka mkono wa sheria.
Migogoro kuhusu mipaka ya Maeneo ya Hifadhi
xv. Mheshimiwa Spika
, wananchi walidai kuwa baadhi ya Mapori ya Akiba naHifadhi yamekuwa yakipanua mipaka yake bila kushirikisha wananchi wa maeneo yanayowazunguka. Mfano; wananchi wa Wilaya ya Bunda wanaopakana na Pori la Akiba la Gurumeti.
Pia, wananchi wa vijiji vya Kegonga na Masanga, katika Kata ya Nyanungu, Wilayani Tarime wako katika mgogoro wa mpaka na TANAPA wakidai kuwa bonde la Nyanungu limemezwa na eneo la Hifadhi kutokana na TANAPA kuongeza mipaka yake bila kushirikisha wananchi wa maeneo hayo. 
Aidha, katika Wilaya ya Ulanga kuna mgogoro katika kata za Iputi na Lupiro dhidiHifadhi ya Selous.
Idara za Wanyamapori katika Halmashauri kukosa vitendea kazi
xvi.Mheshimiwa Spika
, kutokana na silaha za Idara ya Wanyamapori katika baadhi ya Halmashauri kuchukuliwa wakati wa Operesheni Tokomeza kwa ajili ya uchunguzi, wananchi wamedai kupata shida kutokana na wanyama hasa Tembokuvamia mashamba na kuharibu mazao pamoja na kujeruhi au kuua watu na mifugo.
Wanasiasa kushawishi wananchi kuishi kwenye maeneo ya Hifadhi
xvii. Mheshimiwa Spika
, wakati wa kutekeleza Operesheni Tokomeza ilidaiwa kuwa nyumba na maboma ndani ya mapori ya akiba zilichomwa moto. Mfano; Wilaya ya Sumbawanga kijiji cha Msila Kata ya Mfinga na kijiji cha Kabage Wilaya ya Mpanda. Hata hivyo baadhi ya wananchi wameanza kurejeakatika baadhi ya maeneo ya hifadhi kutokana na ushawishi wa wanasiasa.
Mfano; katika Pori la Hifadhi ya Jamii Ubende Wilaya ya Mpanda walichangishwa shilingi laki moja (100,000/ =) kwakila kaya kwa ajili ya kupatiwa huduma za kisheria iwapo mamlaka husika zitajaribu kuwaondoa ndani ya hifadhi.
Aidha, Kamati ilipata taarifa kuwa, baadhi ya viongozi wa Vyama vya Siasa wamekuwa wakigawa kadi za vyama vyao kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya hifadhi na kwa ahadi kwamba, vyama walivyojiunga nga navyo vitawatetea wasiondoke katika maeneo hayo.
Tatizo la Vibali vya Wakulima wa Muda
xviii. Mheshimiwa Spika
, Kamati ilielezwa lipo tatizo la raia wa nchi jirani kuingia nchini na kupewa vibali vyakuendesha shughuli za kilimo(Peasant Permit)kwa muda, ambavyo hutolewa bilakubandika picha ya mhusika/mwombaji hasa maeneo ya Karagwe. 
Raia hao wanadaiwa kutumia nakala za vibali hivyo kuingiza nchini wahamiaji haramu ambao baadhi yao huingiza makundi makubwa ya mifugo hasa ng’ombe na wengine kutumia mwanya huo kuingiza silaha na kujihusisha na vitendo vya ujangili katika baadhi ya mapori ya akiba. Mfano; Pori la Akiba la Ibanda Rumanyika.
Vilevile kuna tatizo la majangili kutumia vivuli va wafugaji kuingia kwenye hifadhi huku wakiwa wameficha silaha, na hivyo kuwepo mazingira ya kushindwa kutofautisha kati ya majangili na wafugaji hususan katika maeneo ya hifadhi ya Ruaha.
xix.Mheshimiwa Spika, kuna mgogoro katika eneo la Ushoroba (Buffer Zone) katika Kata za Lupiro, Mbugana Iputi Wilaya ya Ulanga, maeneo ambayo jamii imejenga miundombinu kwa miaka mingi ikiwa ni pamoja na shule, nyumba, mashamba, misikiti na makanisa huku Serikali ikiwa kimya kwa muda mrefu.Hata hivyo, wakati wa Operesheni Tokomeza wananchi hao walilazimishwa kuhama bila kuelekezwa waende wapi.
Michango ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu Operesheni
xx. Mheshimiwa Spika,
Kamati ilibaini kuwa baadhi ya michango iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wakichangia Hoja ya Mhe. Saidi Nkumba haikuwa imefanyiwa utafiti wa kutosha kwani baadhi ya madai waliyoyatoa hayakuwa na uhusiano na Oparesheni Tokomeza. 
Kwa mfano;ni kweli kwamba ng’ombe 51 walitumbukia katika mto Rubana Wilayani Bunda na kufa, hata hivyo tukio hilo lilitokea mwezi April, 2013 ikiwa ni miezi 6 kabla ya Operesheni.
Aidha, ni kweli kuwa Wakazi wa Vijiji vya Kabage Wilayani Mpanda na Luchima Wilayani Mulele walihamishwa kutoka katika maeneo ya hifadhi na nyumba zao kuchomwa moto katika utaratibu uliofanywa na Halmashauri hizo mwezi Septemba, 2013 kwa lengo la kuwapeleka kwenye maeneo rasmi ya makazi.
7.0 MAONI NA USHAURI WA KAMATI KUHUSU TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA OPERESHENI TOKOMEZA
Mheshimiwa Spika,
baada ya Kamati kuchambua nyaraka husika kuhusiana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza, kuwahoji viongozi mbalimbali wa Wizara na Waheshimiwa Wabunge, pamoja na kufanya ziara mikoani kwa lengo la kuhakiki yaliyojiri kutokana na Operesheni Tokomeza, Kamati inapenda kutoa maoni na ushauri ufuatao:-
i. Kwa kuwa, lengo la Operesheni Tokomeza lilikuwa kunusuru raslimali za nchi hususani Wanyamapori na hasa Tembo na Misitu, na kwa kuwa Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wameiunga mkono mbali na matatizo ya kiutendaji yaliyojitokeza, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali irekebishe haraka kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ili kuendeleza na kukamilisha awamu zote za operesheni kama zilivyo kwenye mpango na kunusuru raslimali za Taifa hasa wanyamapori na misitu ambayo inatishiwa kutoweka kutokana na vitendo vya ujangili.
ii. Kwa kuwa,Kamati imejiridhisha kwamba matatizo na upungufu uliojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza yamechangiwa na maandalizi mabaya ya Mpango kazi ambao Waziri Mwenye dhamana hakuidhinisha, na kwa kuwa, imedhihirika kuwepo hali ya sintofahamu (kwa mujibu wa hansard) iliyosababishwa na watendaji wakuu wa Wizara kwa makusudi kuamua kutomshirikisha kikamilifu Waziri katika hatua za mwisho za maandalizi ya Mpango kazi, hivyo basi Bunge linaazimia kwamba, Serikali iwachukulie hatua stahiki za kinidhamu Wasaidizi Wakuu wote wa Waziri walioshiriki katika Mpango kazi huo.
iii. Kwa kuwa, Kamati imebaini kwamba pale Jeshi la Wananchi (JWTZ) linaposhirikishwa katika Operesheni ufanisi mkubwa hupatikana, na kwa kuwa, bado iko haja ya kuendeleza Operesheni Tokomeza kwa maslahi ya Taifa, na kwa kuwa ushahidi wa mazingira ‘circumstantial evidence’ unaonesha kuwa Jeshi lilichukua uongozi wa operesheni baada ya kugundua kuwa washiriki kutoka Vikosi vingine (Polisi, TANAPA, TSF na NCAA) kwa kushirikiana na wafugaji wenye ushawishi wa kifedha pamoja na wanasiasa, walihujumu operesheni hiyo kwa kutoa taarifa kwenye mtandao mkubwa wa kijangili ambao umejengeka kuanzia Wizarani hadi kwenye maeneo ya Hifadhi na kusaidia ‘majangili papa’ wasikamatwe, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba:- 
- Serikali kuchukua hatua za makusudi kuuvunja mtandao huo na pia;
- Kuandaa operesheni nyingine ambayo itapangwa na kutekelezwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Idara ya Usalama wa Taifa.
iv. Kwa kuwa, kumekuwepo na operesheni kadhaa kabla ya Operesheni Tokomeza ambazo zililenga kupambana na ujangili, na kwa kuwa, Operesheni Tokomeza imeshindwa kupata mafanikio yaliyotarajiwa, na kwa kuwa, ushahidi wa mazingira unaonesha wazi kwamba, Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) kimeshindwa kutimiza wajibu wake, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali iimarishe kikosi hicho kwa kukifanyia tathmini na kukiunda upya ikiwa ni pamoja na kukiwezesha kwa rasilimali (Watu, fedha, magari, silaha za kisasa na vifaa vya mawasiliano kama redio na simu).
Serikali iunde chombo ambacho kitakuwa na jukumu la kusimamia na kutathmini utendaji kazi wa KDU.  Iwapo utaratibu huo utazingatiwa ni wazi vitendo vya ujangili vitadhibitiwa bila kutumia operesheni kubwa kama Uhai na Tokomeza.
v. Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwepo kwa vitendo vya utesaji na ukatili wa hali ya juu, ukiukwaji wa haki za binadamu na uzembe miongoni mwa Askari wa Operesheni Tokomeza (ushahidi wa wahusika upo), hali ambayo imesababisha baadhi ya Wananchi kupoteza maisha, kupata ulemavu wa kudumu pamoja na kupoteza mali zao. Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba:-
- Serikali Iwabaini wote waliohusika na vitendo vya kinyama, mateso na udhalilishaji dhidi ya watuhumiwa, iwachukulie hatua stahiki na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa agizo hili katika Mkutano ujao wa Bunge.
-  Ifanye tathmini ya kina kwa kupitia Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili kujua athari za Operesheni hii na kutafuta njia ya kutoa kifuta machozi kwa waathirika, ili kurejesha imani ya Wananchi kwa Serikali yao.
vi. Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa Operesheni Tokomeza ilikuwa haikutengewa fedha katika Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 na kwa kuwa kiasi cha fedha Tshs. 3,968,168,667/= kilichopatikana kutoka Idara na Mashirika Tanzu ya Wizara haikutosheleza mahitaji ya fedha ya Operesheni Tokomeza kutokana na ukubwa wa eneo la Operesheni, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali itenge Bajeti Maalum ya kutosheleza mahitaji ya Operesheni Tokomeza.
Serikali kutenga Bajeti kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uhifadhi katika maeneo ya Hifadhi ikiwa ni pamoja na kuweka raslimali watu ya kutosha na miundombinu mingine muhimu.
vii. Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa Taarifa kwa Umma iliyotolewa kwa Vyombo vya Habari na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori tarehe 23 Oktoba 2013, haikuwa sahihi na pia ililenga kuudanganya Umma kwa kuficha mazingira na sababu za kifo cha Bi Emilliana Gasper Maro, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali ichukue hatua za kumwajibisha Mkurugenzi wa Idara ya Wanyapori kwa kuudanganya umma kwa kujaribu kuficha ukweli.
viii.Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa kumekuwapo mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya Maafisa Wanyamapori, Maafisa Misitu katika mapori ya akiba, Misitu ya Serikali na katika baadhi ya Hifadhi za Taifa wa kupokea rushwa, kutesa wananchi, kuwabambika kesi na kujihusisha na ujangili,na kwa kuwa Kamati inayo majina na vielelezo vya wahusika, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali ifanye tathmini nchi nzima kwa lengo la kutambua kiwango cha vitendo vya rushwa miongoni mwa watumishi hao, na kuwachukulia hatua stahiki za kinidhamu wale watakaobainika kuhusika ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
ix. Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa baadhi ya viongozi wa kisiasa na Serikali waliingilia utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kwa manufaa yao binafsi, kwa mfano, agizo la kuwataka wahusika wa Operesheni Tokomeza kutowagusa Viongozi wa Kisiasa wa ngazi zote, kauli ambayo ilitafsiriwa kuathiri utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kwa kubagua Watanzania katika makundi ya Viongozi na Wananchi wa kawaida, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali ihakikishe kuna uwajibikaji wa pamoja pale inapoamua kutekeleza jambo la Kitaifa kama Operesheni Tokomeza.
x. Kwa kuwa, Kamati imethibitisha kuwa, baadhi ya wanasiasa wamekuwa wanawadanganya wananchi waliothibitika kufanya shughuli za uchumi kwenye maeneo ya hifadhi, na kuwaahidi kuwatetea pindi Serikali inapochukua hatua za kuwaondoa katika sehemu hizo, ikiwa ni pamoja na kuwapa kadi za vyama vyao vya siasa, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, serikali ihakikishe kwamba, wananchi hawaendeshi shughuli za kiuchumi kwenye maeneo ya hifadhi na kuwaonya wanasiasa waache kuwalaghai wananchi kwa maslahi yao binafsi.
xi. Kwa kuwa, Kamati imebaini kwamba katika baadhi ya  maeneo ya mipakani mfano Karagwe, Idara ya Uhamiaji hutoa vibali kwa raia wa nchi  jirani vya kuishi na kulima hapa nchini, vibali ambavyo havina udhibiti wala tija kwa nchi, na kusababisha migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji lakini pia uharibifu wa mazingira kwa kuingiza mifugo hifadhini, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali isitishe mara moja zoezi la kutoa vibali hivyo, kufuta vilivyopo na kuwataka raia hao wa kigeni wenye vibali  kuondoka Nchini mara moja.
xii.Kwa kuwa, Kamati imebaini kwamba zaidi ya asilimia 25 ya eneo la  Nchi ni hifadhi, namipaka ya maeneo mengi yaliyohifadhiwa haijaainishwa, na kwa kuwa Serikali haina uwezo wa (raslimali watu na fedha) wa kusimamia na kulinda mipaka ya maeneo haya kikamilifu, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali kufanya yafuatayo:-
• Kuridhia Idara ya Wanyamapori na Wakala wa Huduma ya Misitu kuajiri idadi ya watumishi wanaotakiwa kama Serikali bado inaendelea kuyahifadhi maeno hayo.
• Kuainisha mipaka ya mapori yote ya akiba, hifadhi za taifa na Misitu ya Serikali kwa alama maalumu na za kudumu ili kuepusha Wananchi kuingia katika maeneo hayo kwa kutojua mipaka.
• Kuyaachia mapori ya Serikali ambayo yamekosa sifa, ili yatumike kwa kilimo na ufugaji kwa kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi.
xiii.Kwa kuwa,yapo maeneo ya mapori na Hifadhi ambayo yana migogoro ya muda mrefu ambapo wananchi wameishi katika maeneo hayo kwa muda mrefu, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali irekebishe mipaka husika au iwahamishie Wananchi hao  kwenye maeneo mengine yenye miundombinu. Serikali iwaagize Mawaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maliasili na Utalii na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kutembelea maeneo yote yenye migogoro nchini na kuitafutia ufumbuzi ili wananchi waweze kuelewa hatma yao katika maeneo hayo kwani wamekuwa katika hali ya sintofahamu kwa muda mrefu.
xiv.Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwepo kwa migogoro baina ya Wananchi, Wawekezaji na hifadhi katika maeneo ya Meatu, Tarime, Bunda na ile ya Loliondo na Kimotorok ambayo inashughulikiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali ihakikishe inamaliza (kama ilivyoahidi) migogoro iliyopo Loliondo na Kimotorok na maeneo mengine mapema iwezekanavyo.
Kurekebisha haraka kasoro zote za kisheria zilizokiukwa kwa makusudi na Idara ya Wanyamapori kiasi cha kusababisha mgogoro baina ya Halmashauri ya Wilaya ya Meatu na mwekezaji katika Pori la Hifadhi ya Jamii la Makao pamoja na kuwawajibisha Watendaji wa Idara ya Wanyamapori waliosababisha mgogoro huo.
xv.Kwa kuwa, Kamati imebaini kwamba, migogoro wanayokumbana nayo wafugaji kutokana na kuingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na kero nyingine ni kutokana na kukosekana kwa miundombinu sahihi na endelevu kwa ajili ya ustawi wa mifugo, na kwa kuwa, Mheshimiwa Rais aliunda Wizara mahsusi kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Mifugo nchini akitambua umuhimu wa Sekta hii kwa uchumi wa Taifa, na kwa kuwa, Tanzania ni ya pili kwa wingi wa mifugo Barani Afrika, ni wazi kwamba adha wanazokumbana nazo wafugaji ni matokeo ya kutokuwepo sera na mipango madhubuti ya muda mfupi na mrefu. 
Hivyo basi, Bunge linaishauri Serikali kumtaka Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, kujipima na kuona iwapo bado anastahili kuendelea kuhodhi wadhifa alionao.
xvi.Kwa kuwa, Kamati imebaini kuwa baadhi ya madai yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge Bungeni wakati wakichangia Hoja ya Mhe. Saidi Nkumba ilikuwa ni ya kweli; na kwa kuwa yaliyoelezwa katika madai hayo hayana uhusiano na Operesheni Tokomeza kwani yalitokea kabla ya Operesheni hiyo; hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Waheshimiwa Wabunge kuwa makini zaidi na kufanya utafiti kwa lengo la kuhakikisha michango yao inakuwa sahihi na inalenga hoja mahsusi iliyo mbele ya Bunge.
8.0  HITIMISHO
Mheshimiwa Spika
, jukumu uliloikabidhi Kamati hii lilikuwa zito na lilihitaji umakini mkubwa na muda wa kutosha katika kulitekeleza. Kutokana na ufinyu wa muda na mazingira magumu wakati wa kutekeleza jukumu hilo, Kamati inakiri kwamba haikuweza kutembelea maeneo yote yaliyoathirika na zipo lawama kutoka kwa baadhi ya wananchi kwamba, Kamati haikuweza kupita katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, Kamati inapenda kuwahakikishia wananchi wote kuwa, kupitia taarifa mbalimbali za viongozi na wawakilisihi wa waathirika mbele ya Kamati, malalamiko yao yamezingatiwa na kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Spika, kama tulivyoeleza katika maelezo yetu ya utangulizi, Kamati inaamini na kote tulikopita wananchi wanakiri kuwa, lengo na azma ya Serikali kuanzisha Operesheni Tokomeza Ujangili lilikuwa jema kwani lililenga kunusuru maliasili zetu kwa ajili ya maendeleo endelevu na heshima ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaamini maelezo yote yaliyotolewa na wananchi pamoja na viongozi wao yalikuwa na dhamira njema. Aidha, mapendekezo yaliyotolewa na Kamati yanalenga kuisaidia Serikali kuchukua hatua za makusudi na haraka kurekebisha kasoro zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, ili kuepuka kutokea kwa vitendo vinavyoashiria ukiukwaji wa misingi ya haki za binadamu na Utawala Bora nchini.
Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru wewe binafsi kwa dhati kutokana na kuiamini Kamati yangu na kuikabidhi jukumu hili zito. Hii ni ishara tosha kwamba una imani na Wabunge wako na kwamba wanaweza kufanya kazi kwa niaba yako.
Mheshimiwa Spika, pia nitoe shukrani za dhati kwa Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Didimu Kashilillah, kwa kuiwezesha Kamati hii kufanya kazi yake vizuri na kuikamilisha kwa wakati. Aidha, kwa namna ya pekee napenda kuwashukuru makatibu walioihudumia Kamati hii wakiongozwa na Ndugu Theonest K. Ruhilabake ambao ni Ndugu Gerald Magili, Ndugu Chacha Nyakega na Ndugu Stanslaus Kagisa. 
Aidha, ninapenda kuwashukuru viongozi wa Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji ambao walionyesha ushirikiano mkubwa Kamati ilipotembelea maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, mwisho lakini si kwa umuhimu Kamati inawashukuru watumishi wafuatao; Ndugu Silva Chindandi, Ndugu Ndigwako Mwaigaga, Ndugu Victoria Mizengo, Ndugu Germina Magohe na watumishi wengine ambao kwa namna moja au nyingine walishiriki katika kuihudumia Kamati hii hadi inakamilisha taarifa hii.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
James Daud Lembeli, Mb
MWENYEKITI KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA MAZINGIRA

.

No comments:

Post a Comment