Na Hafidh Kido
DHANA ni kitu kibaya kabisa kwa dunia ya sasa ambayo imejaa taaluma na utitiri wa wataalamu wa fani mbalimbali.
Huonekana ni jambo lililozoeleka kwa wanaadamu kudhania mambo tu na kukubali kupelekwa kibubusa; tunaridhika haraka kwa uchovu wa kufikiri.
Tumekuwa wavivu wa kuamua, hakika hainiridhishi hata kidogo. Jambo dogo linapodharauliwa linaweza kugeuka gharika ya matukio mabaya usiyoweza kutarajia katika maisha. Si vema kudharau kitu pale unapoona kitakudhuru.
Husemwa tone hujaza kiganja na kufanya bwawa la maji, na chembe ya mchanga hufanya tofali pakatokea nyumba; ndivyo hivyo hivyo ujinga mmoja huzaa matatizo katika jamii pakatokea mabahauu.
Tukirudi katika mada yetu, dhana imefanywa kitabu cha kukaririwa na kila mja mvivu. Si ajabu kumkuta kijana wako hakwenda shule, unapomuuliza anakujibu ‘nadhani leo shule hakuna kitu cha maana, hivyo nimeamua kubaki nyumbani na nitakweda kesho Mungu akipenda.’ Ni jibu la kipuuzi kabisa.
Kwanini udhani, kwanini huna majibu ya moja kwa moja yasiyoambatana na dhana? Ni hatari sana kauli ya kudhani ikachukuliwa kama dharura ama sababu ya kukimbia ukweli, bali bila kujua tunageuka mbuni kwa kuficha vichwa vyetu mchangani ili tusimuone adui ama kuomba hatari ituepuke. Tunajidanganya.
Dhana, neno hili linaweza kutumika katika mwanzo wa sentesi yenye shaka, sentesi ya mtu anaeuliza ama kuhitaji ufafanuzi wa jambo kadha, hiyo imewafikiwa na watu wa lugha. Lakini dhana inapotumika katika sentensi sahihi na yenye kuonyesha ushupavu wa muongeaji, hapo ndipo shaka inapoanzia.
Mfano: mtu anaweza kusema ‘nadhani tunahitaji mwalimu wa kutuelekeza somo hili.’ Hiyo imekaa vizuri, neno dhana hapo limetumika kama kiulizo. Lakini mtu anaposema ‘nadhani mvua itanyesha, hivyo leo sitokwenda shambani kulima.’ Hiyo ni dhana ya kipuuzi kabisa na yenye kurudisha nyuma maendeleo.
Kwanini udhani kitu ambacho huna uhakika nacho? Na nimegundua mara nyingi wavivu ndiwo wepesi sana wa kudhani vitu vya ajabu ajabu kama ajali, mvua na mambo ya kumzuia au kumkatisha tamaa mtu kufanya jambo la maendeleo.
‘Nadhani kesho sitokuja, hivyo kazi yetu itaendelea keshokutwa,’ tazama wavivu wanavyojua kukwepa kazi. Kwanini hutoi sababu kamili ya kutokuja kwako na badala yake utumbukize neno ‘nadhani’ kama sababu ya msingi?
Tukumbuke tunaishi katika dunia ya kiminyano cha maisha, si vema kuchelewesha kazi kwa uvivu tu, punguza kudhani bali fanya utafiti upate sababu njema ya kutokamilisha jambo.
Mtu anaweza kuwa hana ufahamu na jambo kadha, badala ya kuuliza wanaojua ama kufaya matafiti juu ya suala hilo, matokeo yake hukwambia anadhani jambo hilo hufanyika kadha au halipo kwa maana halijui. ‘Nadhani hili haliwezekani, kwa maana hiki kimekaa hivi na hakipaswi kuwa hivi.’ Epuka sana kauli hizo za dhana.
Mitandao ya intaneti, magazeti, vitabu na kila namna ya taaluma katika redio na luninga; bado tu tunaamua kuishi katika dhana? Tubadilike japo kidogo, tujitahidi kubadili matamshi yetu na kuipa dhana muda mdogo wa matumizi katika matamshi ya siku nzima.
Unaonaje kuzungumza na wanafunzi au wafanyakazi wenzio huku ukitumia kauli za kujiamini, kutoa maelekezo na ufafanuzi kwa kila jambo linaloonekana kikwazo katika masomo au kazi? Hakika ni jambo la kuvutia sana kujiamini.
HAFIDH KIDO
Kijitonyama, Dar es Salaam Tanzania
23 Novemba, 2013
Umalizapo kusoma makala haya nataka ule yamini ya kutotumia neno ‘nadhani’ kwa siku nzima tangu kusoma makala haya. Baada ya hapo tazama nafsi yako ina furaha ama kuna majuto kwa kukosa kulitumia tamko hilo dhalili
No comments:
Post a Comment