Saturday, December 7, 2013

Sijasikitishwa na kifo cha Madiba.

KILA mtu ameandika kusikitishwa na kifo cha Mzee Madiba, lakini mimi nipo tofauti. Sijasikitishwa hata kidogo na kifo cha Baba wa Afrika. Mandela ni mpambanaji, ni mwanamapinduzi, ana moyo wa chuma, hajakufa, bali ameifariki dunia amekwenda kuanza maisha mapya upande wa pili wa dunia.

Wanamapinduzi hatupeani pole kwa msiba, kwasababu hatuogopi kifo, kifo ni ishara ya ushujaa, ishara ya kukamilisha mapambano. Naam kazi ya Mzee Nelson Mandela, humu duniani imekamilika.

Sasa tuulizane, kazi ikikamilika tunahuzunika ama tunasherehekea? Kwanini tunainamisha vichwa chini.... Hatuna sababu ya kuinamisha vichwa chini, tufurahi Mzee Madiba amekamilisha majukumu yake na amefanikiwa kwa asilimia 100 kubadili nyoyo za watu dhaifu.

Ndiyo maana Mabaniani wanapofiwa na mtu mzee wanafanya sherehe, wanapiga makofi na kufurahi. Sisi Wagunya tukiondokewa na mtu Mzee tunafanya sherehe pia, nakumbuka mwaka 1994 babu yangu Mzee Athumani Al-Amir, alipoaga dunia tulifunga 'Spika' na kuanza kuimba usiku kaka zangu wakavaa nguo zake wakiiga maisha yake, nikamuuliza shangazi yangu Mwanakida Abdallah, kuna harusi? Akanijibu hapana, babu yako alikuwa shujaa.... Tunasherehekea ushujaa wake.

Hata kwetu Tongoni, kijiji kilicho karibu na Wilaya ya Pangani anapokufa mtu Mzee kuna goma kubwa linapigwa na kijiji kizima kinalipuka kwa kelele... hakuna kulia ni furaha.

Hata Mandela alipokuwa gerezani, hakutaka watu wahuzunike, hakutaka kuonewa huruma, shujaa haonewi huruma. Hongera Mandela.


HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment