Wednesday, December 26, 2012

Haya sasa Chelsea wameshavurugwa, wanadai chao..... nafasi ya tatu inamuhusu.


Juan Mata aliifungia Chelsea bao lake la pekee na la ushindi dhidi ya Norwich, na kuiweka alama nne pekee nyuma ya mabingwa watetezi Manchester City, iliyoko katika nafasi ya pili kwa sasa.
Mata alivurumisha kombora kali kutoka umbali kwa mita ishirini na tano ambalo lilimuacha kipa wa Norwich Mark Bunn kinywa wazi.
Hata hivyo vijana hao wa Norwich, walicheza mchezo mzuri na kumfanyisha kazi ya ziada kipa wa chelsea Petr Cech.
Sebastien Bassong nusura asawazishe kwa kichwa lakini mpira ukapaa sentimita chache juu ya goli.
Katika mechi nyingine Everton imeimarisha rekodi yake ya kutoshindwa hadi mechi saba mfululizo pale ilipoifunga Wigan kwa magoli mawili kwa moja.
Everton sasa imepanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 33 baada ya kucheza mechi kumi na tisa.
Leon Osman na Phil Jagielka ndio walioifungia Everton magoli yake naye Arouna Kone aliipa Wigan bao lake la kufutia machozi.
Katika mechi nyingine Fulham imetoka sare ya 1-1 na Southampton, huku QPR ikilazwa 2-1 na West Brom, Reading ikatoka sare ya kutofungana na Swansea sawa na Aston vila na Tottenham.
Chanzo: BBC Swahili

kiongozi wa dini ya kikristo ashambuliwa kwa risasi Zanzibar....


Kwa mujibu wa Breaking News  toka Radio One, Padre anayejulikana kwa jina la Ambrose Mkenda amepigwa Risasi na Watu wasiofahamika kwenye gate la nyumbani kwake wakati akifunguliwa gate aingie nyumbani kwake maeneo Kitomondo Mjini Zanzibar, ambako ndiko makazi yake yalipo akiwa ndani ya gari aliyokuwa akiendesha pekee yake.

Hali yake sio nzuri kwani Risasi aliyopigwa imemdhuru maeneo ya mdomoni.
 

Waliompiga Risasi Padre huyo inasemekana ni watu waliokuwa kwenye pikipiki, ambao walimvamia akisubilia afunguliwe gate kuingia nyumbani kwake.
 
Chanzo: radio one.

Kaburi Idriss Abdul Wakil... Rais wa pili wa Zanzibar....

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, (wa pili kulia) akiwa mbele ya Kaburi la Rais wa zamani wa Zanzibar  Hayati Idris Abdulwakil, wakati alipozuru Kijiji cha Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja juzi. Rais  Wakil alifariki dunia mwaka 2001.

Umeshasoma tamko la maaskofu? Ingia kidojembe......

TANZANIA CHRISTIAN FORUM (TCF) MKUTANO MKUU WA NNE WA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA (TCF)

TAMKO RASMI 
“ATUKUZWE MUNGU JUU MBINGUNI, NA DUNIANI IWE AMANI KWA WATU ALIOWARIDHIA”



Utangulizi
Katika Mkutano Mkuu wa Nne wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, Tanzania Christian Forum – TCF, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano na Mafunzo cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Kurasini jijini Dar es Salaam, tarehe 6 Desemba, 2012; Wajumbe walitafakari kwa undani juu ya kuzorota kwa mahusiano baina ya Dini mbili za Ukristo na Uislamu nchini Tanzania, pamoja na kutathmini juu ya wajibu wa Kanisa na Utume wake wa Kinabii kwa taifa letu.

Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) linajumuisha taasisi kuu za Umoja wa Makanisa nchini kama ifuatavyo;-
Jumuiya ya Kikristo Tanzania - CCT
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania - TEC
Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania - PCT
Kanisa la Waadventisti Wasabato – SDA (observers)

Tafakari
Tafakari yetu ilianza kwa kujiuliza yafuatayo:

1. Ni mwenendo gani uliotusibu hivi karibuni kusababisha kukutana kwetu hapa?
 
Vikundi vya kihalifu vikiongozwa chini ya mwavuli wa waamini wa Kiislamu vimekuwa vikishambulia kwa ukali na kikatili sana imani, mali, majengo na makanisa ya Wakristo kwa jeuri na kujiamini.

2. Kwa mwenendo huo ni kitu gani kilicho hatarini?
 
Vitendo na mienendo yote ya namna hiyo inahujumu sana Amani, Mapatano na Uelewano kati ya watu wote nchini mwetu. Tunaelewa kwamba ni waamini wachache tu wenye kutenda maovu hayo, lakini mienendo ya kikatili ya namna hii huchochea shari miongoni mwa walengwa wa ukatili husika na kutaka kulipiza kisasi hata kusababisha uvunjifu wa amani.

3. Ni athari gani kwa nchi, katika muda ujao, iwapo mienendo hiyo haitadhibitiwa na kukomeshwa kabisa?
 

Katika nyakati zetu hizi, tunashuhudia fadhaa na migogoro mingi ya kijamii. Kuna hasira kubwa ya chinichini inayotokana na kasoro nyingi za kiutendaji katika mihimili mikuu ya uongozi na utando mkubwa wa ufukara wa kutupwa kwa wananchi wengi usio na matumaini ya kumalizika hivi karibuni. Hatari ya hali hii ni dhahiri kwamba makundi nyemelezi (kisiasa, kiuchumi na kidini), kwa kutumia vikundi halifu vilivyo katika hali ya ufukara na migogoro, yatavielekeza kimapambano na kiharakati kutetea kijeuri ajenda hasimu za wale walio madarakani au washindani wao kwa maslahi ya wanyemelezi. Hali tunayoelezea sio ya kufikirika kwani ndiyo inayotokea huko nchini Nigeria, Kenya na nchi za Afrika ya Kaskazini hivi sasa. Tanzania haina kinga ya kipekee kuiepusha kukumbwa na maovu ya namna hiyo bila utaratibu na vyombo thabiti kuhimili mienendo hasi kama hii. Kutokana na matukio na kauli zinazotolewa na watu mbalimbali hapa nchini, inawezekana tayari wanyemelezi wako kazini wakiongoza vikundi kusukuma ajenda za kutekeleza maslahi yao.

4. Masuala yanayotakiwa kufafanuliwa na kudhibitiwa na Dola mapema ili yasiendelee kupotoshwa:

  • Hali ya mahusiano kuzorota pamoja na kashfa dhidi ya Kanisa.

Huu ni wakati wa kukubali kwamba misingi ya Haki, Amani na Upendo katika Taifa letu imetikiswa kwa kiwango kikubwa. Uchochezi, kashfa, matusi na uchokozi wa wazi na makusudi unaofanywa na baadhi ya waamini wa dini ya Kiislamu, ukiendeshwa na kuenezwa kupitia vyombo vyao vya habari vya kidini (redio na magazeti) mihadhara, kanda za video, CD, DVD, vipeperushi, makongamano, machapisho mbalimbali na kauli za wazi za viongozi wa siasa na hata viongozi wa dini husika (ushahidi wa mambo yote haya tunao) pasipo Serikali kuchukua hatua yeyote huku bali imekuwa ikibakia kimya tu. Ukimya huu unatoa taswira ya Serikali kuunga mkono chokochoko hizi. Jambo hili linavyoendelea kuachwa hivi hivi linaashiria hatari kubwa ya kimahusiano siku zijazo.

  • Hadhi ya Baba wa Taifa kuhifadhiwa.

Huyu ni kiongozi aliyetoa maisha yake kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu akitetea Watanzania wote bila ubaguzi wowote, akiimarisha umoja wa Kitaifa, amani na upendo kwa watu wote. Kashfa, kejeli na habari za uongo dhidi yake ni kukipotosha kizazi hiki na hata vizazi vijavyo kwa kuondoa moja ya alama muhimu ambazo kiongozi huyo alisimamia kwa ajili ya umoja wa kitaifa.

  • “Memorandum of Understanding” (M.o.U) ya mwaka 1992, kwa ajili ya huduma za kijamii zitolewazo na Makanisa kwa Watanzania wote, ikiwa ni pamoja na huduma za hospitali, vituo vya afya na zahanati na shule mbalimbali zinazoendeshwa na Makanisa nchini kote. Ni vema ikaeleweka wazi kwamba makubaliano hayo (M.o.U) yalikuwa ni kati ya Makanisa ya Tanzania na Makanisa ya nchini Ujerumani ambapo Serikali ya Tanzania ilihusishwa tu, kwa vile raia wake ndio wangenufaika na misaada hiyo ambayo nchi ya Ujerumani ingeitoa kupitia Makanisa hayo. Kanisa limeendelea kujishughulisha na huduma hizi kwa jamii hata kabla ya uhuru na baada ya uhuru pasipo ubaguzi. Ikibidi ni vema kuondoa hali hii, ya Kanisa kuendelea kutukanwa, chuki na kukashifiwa viongozi wake kutokana na huduma hizi kwa jamii yote. Jukwaa la Wakristo Tanzania tunaitaka Serikali itoe tamko la ufafanuzi juu ya M.o.U hiyo, maana yake, makusudi yake na manufaa yake kwa Watanzania wote.


  • Hujuma ya kuchomwa Makanisa na mali za Kanisa, ni tukio la uvamizi na uchokozi wa wazi, ulioyakuta makanisa yetu na waamini wake wakiwa hawana habari na bila maandalizi yoyote. Ni muhimu kuanzia sasa, Wakristo wote wakae macho na wawe waangalifu zaidi.


  • Dhana ya kuwa Tanzania inaendeshwa kwa mfumo Kristo ni potofu na potevu.

Maneno hayo ni ushahidi wa uwepo wa ajenda za waamini wenye imani kali na waliojiandaa kwa mapambano maovu kutetea dhana potovu kinzani na misingi ya demokrasia na haki za binadamu kama ilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa na kuridhiwa na Serikali yetu. Jukwaa la Wakristo nchini tunakanusha wazi wazi na kueleza bayana kuwa, nchi hii haiongozwi kwa mfumo Kristo!. Kwa watu walio makini hakuna kificho kuwa viongozi wote waandamizi wa ngazi ya juu Serikalini awamu ya sasa, asilimia 90 ni Waislamu (Rais wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu, Makamu wa Rais, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi). Kwa mantiki hiyo haiingii akilini kueleza watu kuwa nchi hii inaendeshwa kwa mfumo Kristo! Kwa upande wa Zanzibar asilimia 100 ya viongozi ngazi za juu Serikalini ni Waislamu, na sio kweli kwamba Zanzibar hakuna Wakristo wenye sifa za kuongoza. Kisha, hata uwakilishi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, theluthi mbili ya wajumbe wake ni Waislamu. Tunayo mifano mingine mingi iliyo wazi, na hii ni baadhi tu. Watanzania wanapaswa kuelewa wazi kuwa, nchi hii inaongozwa kwa misingi ya Utawala wa Kisheria na sio vinginevyo.

  • Matumizi hasi ya Vyombo vya Habari vya Kidini:

Vyombo vya habari vya kidini vinatumiwa na viongozi wa dini ya Kiislam kuukashifu Ukristo na kuwachochea Waislamu hadharani kupitia vyombo hivyo wakiwataka wawaue Maaskofu na Wachungaji, iwe kwa siri au hadharani. Japo Serikali imesikia kashfa na uchochezi huo hatarishi, imendelea kukaa kimya, na kuwaacha wachochezi hao wakiendelea kuhatarisha amani bila kuwadhibiti. Jambo hili linatia mashaka makubwa juu ya umakini wa Dola kuhusu usalama wa wananchi nchini mwao. Imani kali za namna hii huchochea vitendo viovu vya uasi na hujuma sio tu dhidi ya waamini na viongozi wa dini fulani, bali hata na kwa Serikali na viongozi waliopo madarakani, endapo waamini wa dini fulani katika taifa kama Tanzania lililo na waamini wa dini nyingi tofauti, hawataheshimu na kutendeana kiungwana baina yao na wale wasio wa dini na mapokeo yao. Hali hii inapelekea kujiuliza kama je,huu ni wakati mwafaka kwa kila raia au kiongozi wa dini kujilinda yeye mwenyewe na waamini wake dhidi ya wenye imani kali?

  • Matukio yanayosababisha hasira na kutenda maovu:

Tumejionea matukio kadhaa ambayo kwayo vikundi vya watu wenye hasira vilisababisha hujuma na uharibifu mkubwa wa mali za watu wengine. Hivyo ni viashiria tosha vya uchovu na unyonge mkubwa katika jamii yetu, ambamo jambo dogo tu na hata la kupuuzwa, likitendwa na afikiriwaye kuwa hasimu wa watu fulani, wahalifu hujipatia fursa ya kuonesha hasira yao kwa vitendo vya hujuma na shari, wakiharibu hata kuteketeza mali na nyenzo za maisha ya jamii. Suala hili lataka uchambuzi yakinifu na wa kiroho ili kupata majibu na maelezo sahihi na wala sio kwa kutumia nguvu za ziada za kijeshi au kwa majibu mepesi ya kisiasa. Hili ni suala lihusulo tunu na maadili ya jamii yote ya Watanzania katika ujumla wao. Kila mmoja wetu ni mhusika na sote tukitakiwa kuwajibikiana katika ujenzi wa amani iletayo mapatano na uelewano kati yetu.

Mapendekezo:
Kutokana na muono wetu huo tunapendekeza yafuatayo:

  • Tabia na mienendo ya kukashifiana ikomeshwe kabisa na badala yake tujengeane heshima/staha tukizingatia utu wa kila mmoja katika utofauti wetu.
  • Tumwendee Mungu wetu na kumwomba atuongoze sote kufuata utashi wake tukitafuta huruma yake iliyo sheheni upendo wake mkuu, ili atujalie umoja wa kuishi pamoja kwa amani nchini mwetu.
  • Tunaitaka Serikali yetu na vyombo vyake vya usalama, sheria na amani kutenda mara moja na bila kuchelewa, katika nyakati ambazo vikundi halifu kisiasa au kidini vinapoanza uchochezi ili kupambanisha wanajamii. Tabia ya kuachia uchochezi wa kidini kuendelea pasipo hatua mathubuti kuchukuliwa na Dola ni udhaifu mkubwa wa uongozi na uwajibikaji. Ikithibitika kwamba uharibifu uliofanywa ulitokana na kikundi mahususi chini ya uongozi wa dini au chama cha kisiasa au asasi isiyo ya kiserikali, basi taasisi husika iwajibishwe na kulipa fidia kwa uharibifu uliofanywa.
  • Lianzishwe Baraza mahsusi lililo huru lisiloegemea chama chochote cha kisiasa wala dini yoyote na litamkwe na kuwezeshwa kikatiba likiwa na dhumuni kuu la kuilinda na kuiongoza Serikali kuto fungamana na dini yoyote na kuhakikisha kwamba dira na dhana ya utu katika mfumo wa uchumi wenye kujali maslahi ya wote havipotoshwi. Baraza hilo liwe na uwezo wa kuvichunguza vyombo vya sheria na usalama itokeapo matatizo makubwa yaashiriayo uvunjifu wa haki na kuteteresha usalama wa nchi.
  • Na sisi viongozi wa dini za Kikristo, Kiislam, Kihindu na nyinginezo tuwajibike katika kufundisha, na katika majiundo ya waamini wetu, hasa vijana, ili kuwajengea uelewa na utashi wa kuvumiliana kwa upendo. Katika kushuhudia na kuadhimisha imani na ibada zetu sote tutambue , tulinde na kukuza maadili, tunu na desturi za imani za watu wengine wanazo ziheshimu na kuzitukuza. Vikundi vya imani kali na pambanishi kwa kutumia kashfa potoshaji sharti vidhibitiwe kwa weledi mkubwa wa viongozi wa dini husika wakisaidiana na usalama wa taifa. Stahamala [kustahimiliana] ni fadhila inayopaswa kufundishwa na kupenyezwa katika mifumo ya uongozi na maisha ya jamii na ihifadhiwe kwa kufuatiliwa kwa karibu sana.


Hitimisho: 
Kwa sasa Kanisa liko katika vita vya Kiroho, hivyo ni vyema Waamini wote wakakumbuka kuwa, katika mapambano kama hayo Mungu mwenyewe, Mwenye enzi yote ndiye mlinzi wa watu wake na Kanisa lake.
JIBU LITAPATIKANA TU, KWA NJIA YA SALA, KUFUNGA NA MAOMBI!

Hivyo siku ya Jumanne tarehe 25 Desemba 2012, inatangazwa rasmi nchini kote kuwa siku ya sala na maombi kwa Wakristo wote na Makanisa yote nchini, pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuomba kwa imani, amani katika nchi yetu, na kumkabidhi Mungu ashughulikie mipango yoyote iliyopo, ya wazi na ya kisirisiri ya kutaka kuondoa amani ya taifa hili na kuyashambulia Makanisa nchini Tanzania ishindwe na kuangukapamoja na wale wote walio nyuma ya mipango hiyo.

1. Askofu Bruno Ngonyani (TEC) - Mwenyekiti 
2. Askofu Dkt. Israel Mwakyolile (CCT) - Mjumbe (Mwenyekiti Mwenza) 
3. Askofu Daniel Aweti (PCT) - Mjumbe (Mwenyekiti Mwenza) 
4. Askofu Oscar Mnung’a (CCT) - Mjumbe
5. Askofu Elisa Buberwa (CCT) - Mjumbe
6. Askofu Stephen Mang’ana (CCT) - Mjumbe
7. Askofu Dkt. Peter Kitula (CCT) - Mjumbe
8. Askofu Alinikisa Felick Cheyo (CCT) - Mjumbe
9. Askofu Christopher Ndege (CCT) - Mjumbe
10. Askofu Michael Hafidh (CCT) - Mjumbe
11. Askofu Charles Salala (CCT) - Mjumbe
12. Askofu Dismus Mofulu (CCT) - Mjumbe
13. Mchg. Conrad Nguvumali (CCT) - Mjumbe
14. Mchg. Ernest Sumisumi (CCT) - Mjumbe
15. Mchg. William Kopwe (CCT) - Mjumbe
16. Askofu Thaddaeus Ruwa’ichi (TEC) - Mjumbe
17. Askofu Paul Ruzoka (TEC) - Mjumbe
18. Askofu Norbert Mtega (TEC) - Mjumbe
19. Askofu Severine Niwemugizi (TEC) - Mjumbe
20. Askofu Michael Msonganzila (TEC) - Mjumbe
21. Askofu Castorl Msemwa (TEC) - Mjumbe
22. Askofu Eusebius Nzigilwa (TEC) - Mjumbe
23. Askofu Renatus Nkwande (TEC) - Mjumbe
24. Askofu Bruno Ngonyani (TEC) - Mjumbe
25. Fr. Antony Makunde (TEC) - Mjumbe
26. Fr. Sieggried Rusimbya (TEC) - Mjumbe
27. Fr. Ubaldus Kidavuri (TEC) - Mjumbe
28. Askofu Dkt. Paul Shemsanga (PCT) - Mjumbe
29. Askofu Ability Samas Emmanuel (PCT) - Mjumbe
30. Askofu Nkumbu Nazareth Mwalyego (PCT) - Mjumbe
31. Askofu Batholomew Sheggah (PCT) - Mjumbe
32. Askofu Dkt. Mgullu Kilimba (PCT) - Mjumbe
33. Askofu Renatus Tondogosso (PCT) - Mjumbe
34. Askofu Emmanuel Mhina (PCT) - Mjumbe
35. Askofu O.S. Sissy (PCT) - Mjumbe
36. Askofu Jackson Kabuga (PCT) - Mjumbe

Kikosi cha Coastal Union B ni kikosi bora vijana chini ya miaka 20 Tanzania.




Na Hafidh Kido

Michuano ya Uhai Cup iliyokuwa ikishirikisha vijana chini ya miaka 20 kwa timu zinazoshiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara imekamilika rasmi jumapili tarehe 23, Desemba wiki iliyopita kwa Azam FC kutawazwa mabingwa baada ya kuifunga Coastal Union kwa penalt 3-1 baada ya dakika 120 kuisha kwa sare ya 2-2.

Hakika Rais wa shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF Leodger Tenga anastahili pongezi kwa kuanzisha utaratibu wa kuweka sheria inazozibana timu zinazoshiriki ligi kuu kuwa na timu ndogo za vijana wa chini ya miaka 20. Utaratibu huu lengo lake ni kuibua vipaji vya vijana ambao awali walikuwa wakiishia kucheza timu za shule na kubaki mitaani bila kuonekana katika dunia ya michezo.

Kanali Iddi Kipingu aliekuwa mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Makongo ndie aliekuwa wa kwanza kusaidia vijana kwa kuwachukua kutoka katika michuano ya shule za sekondari na msingi maarufu UMISETA na UMITASHUMTA aliwaingiza katika shule yake halafu anawasomesha bure huku akiwakuza vipaji vyao.

Utaratibu wake huu ulisaidia kuibua vipaji vya wachezaji waliokuja kusumbua sana katika soka la Tanzania, miongoni mwao ni kipa namba moja wa Taifa Stars Juma Kaseja, wachezaji wengine hatari kama Bonifas Pawasa, Nico Nyagawa, Renatus Njohole na Haruna Moshi ‘Boban’. 

Lakini kwa sasa ni lazima kwa timu yoyote ya ligi kuu kuwa na timu ya vijana, kama timu itakwenda kinyume na utaratibu huu inaweza hata kuondolewa kwenye michuano; zamani timu kubwa tu kama Simba na Yanga ndizo zilizokuwa na timu B ambapo walizitumia kuvuna wachezaji wapya kwa matumizi ya baadae ingawa haikuwa lazima kufanya hivyo.

Coastal Union B ina miaka mitatu tangu ianzishwe, nimekuwa nikifuatilia maendeleo yao nimegundua ni timu yenye vijana wenye vipaji vya hali ya juu ingawa hawana kambi rasmi ‘Academy’ kama wanavyofanya Azam FC, Simba SC na Yanga ambazo ndizo timu zinazofanya vizuri katika ligi kuu ya bara.

Kudhihirisha hayo siku ya fainali iliyowakutanisha Coastal Union kutoka Tanga na Azam FC ya jijini Dar es Salaam, meneja wa Azam FC Said Salim Bakhresa ambae pia yupo katika kamati ya maandalizi ya michuano hiyo, alipopata nafasi ya kusema chochote hakusita kukimwagia sifa kikosi cha Coastl Union chini ya miaka 20 kuwa ni kikosi bora katika michuano hiyo.

“Niwashukuru sana sana tena sana viongozi wa Coastal Union kwa kuweza kuwalea vijana hawa mpaka kuweza kucheza soka katika kiwango cha juu kama hiki, hakika sikutegemea kama wangeweza kucheza namna hii. Walistahili kushinda mchezo huu lakini bahati haikuwa yao ila nikiri tu Coastal Union chini ya miaka 20 ni timu nzuri ya vijana niliyowahi kushuhudia hapa nchini,” Bakhresa.

Si hao tu hata Kanal mstaaf Iddi Kipingu na Leodger Tenga kwa vipindi tofauti waliimwagia sifa Coastal Union kwa kuweza kuwaandaa vijana wao na kuweza kutoa burudani ya hali ya juu.

Katika michuano hiyo Coastal Union hawakupoteza mchezo hata mmoja katika michezo sita waliyocheza ambapo minne katika makundi miwili ni ya robo na nusu fainali. Katika michezo yote hiyo walionyesha soka la hali ya juu hasa katika robo fainali walipokutana na Ruvu Shooting uwanja wa Chamanzi, mpaka wanakwenda mapumziko Coastal walikuwa nyuma kwa magoli mawili.

Lakini waliporejea kwa kipindi cha lala salama vijana wa Coastal Union walifanikiwa kurudisha magoli yote mawili na kuingia hatua ya penalt ambapo walifanikiwa kusonga mbele baada ya kushinda penalt 4-3. katika hatua ya nusu fainali walikutana na Simba SC hiyo ndiyo mechi iliyokuwa ikiwasumbua kichwa, maana Simba walikuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo na waliaminika kucheza soka la kuvutia.

Lakini hali ilikuwa tofauti na vijana wa Simba walikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa vijana wa Coastal Union hivyo kuvuliwa ubingwa rasmi na kuiwezesha Coastal Union kutinga fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza.

Azam ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuingia fainali baada ya kuitoa Mtibwa Sugar kwa mikwaju ya penalt 3-2. Ambapo matokeo ya dakika 90 za kawaida yalikuwa ni 1-1.

Katika fainali iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu hasa ikizingatiwa Azam FC wanasifika kwa soka lao la kuvutia ingawa mwaka huu waliingia dosari ya kuzomewa na mashabiki wakituhumiwa kununua waamuzi lakini bado inabaki kuwa Azam ina wachezaji wenye vipaji na wanalelewa kisoka huko katika kambi ya Chamanzi.

Katika kipindi cha kwanza vijana wa Azam FC walionyesha soka hali ya juu kiasi kuwafanya viongozi wa TFF na vyama vingine vya michezo kuwa kimya na kutoamini kilichokuwa kikitokea baada ya kusikia kutoka kwa watu kuhusu kiwango cha hali ya juu cha vijana wa Coastal Union ambao mpaka kipindi cha kwanza kinaisha walikuwa nyuma kwa mabao mawili sifuri.

Hata hivyo katika kipindi cha pili Coastal Union walirudi kwa kasi na kucheza soka la hali ya juu lililoamsha kelele na kuwafanya viongozi wa soka kushindwa kukaa vitini kutokana na kiwango kilichoonyeshwa uwanjani na Coastal Union.

Mpaka dakika 90 zinaisha mabao yalikuwa 2-2, zikaongezwa dakika 30 lakini hali haikubadilika hivyo kikaja kipindi cha mikwaju ya penalt na ndipo Azam FC walipotawazwa kuwa mabingwa baada ya golikipa wao kuokoa mikwaju mitatu kutoka kwa vijana wa Coastal na kushinda kwa penalt 3-1.

Mbali ya kombe bingwa wa michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji ya Uhai alipata kitita cha Tsh Milioni 1.5 wakati mshindi wa pili alipata kifuta jasho cha Tsh Milioni moja.

Kitu ambacho kinanifanya niendelee kuamini mpaka sasa kuwa Coastal Union walikuwa na kikosi bora timu yao ndiyo iliyotoa golikipa bora Mansour A. Mansour, kama hiyo haitoshi kocha wa Coastal Union Bakari Shime ndie aliekuwa kocha bora wa michuano hiyo inayofanyika kila mwaka.

Aidha Ruvu Shooting imeibuka timu yenye nidhamu, Ramadhan Mkipalamoto wa Simba ameibuka mfungaji bora kwa kufunga mabao 6 na mchezaji bora ametokea Azam FC ambae ni Joseph Kimwaga, na mwamuzi bora amekuwa ni Issck Mwalile..

Ushauri uliotolewa na Rais wa TFF kwa viongozi wa Coastal Union ni kuhakikisha wanaitunza hazina hiyo ya vipaji ambavyo kwa miaka ya baadae wanaweza kuiletea sifa Tanzania na Afrika kwa ujumla katika usakataji kabumbu.

Mafanikio ya timu hii tangu iundwe miaka mitatu iliyopita ni kushiriki mashindano manne ya vijana, mashindano ya vilabu vya Afrika mashariki na kati kwa vijana chini ya miaka 20 yaani Rolling Stone walishiriki mara mbili, ambapo mara ya kwanza waliposhiriki mwaka juzi waliishia hatua ya robo fainali mjini Arusha wakatolewa na wekundu wa msimbazi Simba.

Mashindano ya mwaka huu ya Rolling Stone yaliyofanyika mjini Bujumbura Burundi vijana wa coastal Union walipata mafanikio makubwa hata kuweza kuingia fainali wakafungwa na timu kutoka (Congo DRC), hivyo kushika nafasi ya pili.

Kombe la Uhai wameshiriki mara mbili, mara ya kwanza kushiriki walitolewa katika hatua ya makundi, baadae wakajipanga upya na mwaka huu wakaingiza tena timu kujaribu bahati. Ambao walijaaliwa kushuhudia michuano ya Uhai mwaka huu watathibitisha maneno yangu kuwa vijana walionyesha soka la hali ya juu hivyo kustahili kuingia fainali, ingawa bahati haikuwa yao.

Si vibaya maana lengo la michuano hii ya vijana si kuwa washindi kwa wakati wote, bali ni kuhakikisha soka la vijana linakuwa kwa kasi na kuihakikishia nchi wachezaji wenye uwezo na uzoefu wa kucheza soka mbele ya mashabiki wa nchi yoyote.

Si Coastal Union tu, bali timu zote zinazoshiriki ligi kuu wanatakiwa kuwalea vizuri vijana wao ili kuhakikisha maleno ya viongozi wa soka nchini yanatimia. Vijana ndiwo watakaokuja kulikomboa soka la Tanzania.
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
+255752 593894/ +255713 593894
26/12/2012

Acheni midomodomo Shaaban Kado ni mali ya Coastal Union kwa sasa....

Mwenyekiti wa Coastal Union ya Tanga Hemed Hilal 'Aurora' kushoto na Makamu Mwenyekiti Steven Mnguto kulia wakiwa wamekamilisha kazi ya kumsainisha Mlinda mlango mpya wa timu hiyo Shaaban Kado.

Kwa wiki kadhaa kulikuwa na mvutano baina ya vilabu vitatu hivi Yanga, Mtibwa na Coastal juu ya usajili wa Kado kwani Mtibwa walipewa Kado kwa mkopo kutoka Yanga lakini wanalalamika kuna kiasi cha fedha hakijaingia kwao kwa kuuzwa Kado.

Lakini leo mwenyekiti wa Coastal alizungumza katika kipindi cha Sports Extra kinachorushwa na Clouds FM kwa njia ya simu na kuweka wazi kuwa wameshamalizana na Yanga na sasa Kado ni mchezaji halali wa coastal....

Monday, December 24, 2012

Jana ofisini tulikula keki, ilikuwa siku ya kuzaliwa Mayage S. Mayage alie katika dawati la uhariri....

 Hapa Mayage akizungumza mawili matatu wakati wa kutoa neno la shukurani kwa wafanyakazi wenzie wa kampuni ya Raia Mwema inayochapisha gazeti la kila wiki Raia Mwema.


                                               Ilikuwa ni furaha tuputupu ofisini siku ya jana....

                                     Hapa Mayage akimlisha keki mhariri mkuu Godfrey Dilunga....

                                      Hapa Mayage akimlisha keki meneja masoko John Daniel.

Hakyanani Raia Mwema noma, yaani Mayage anakunywa soda? Mzee wa vitu vikali huyu jamani.


Kwa taarifa tu nina historia kidogo na ndugu Mayage, aliwahi kunifundisha kazi wakati nikiwa kwa mazoezi New Habari mwishoni mwa mwaka 2005, katika gazeti la Mtanzania. Baadae nilipokomaa komaa nikawa naandika makala katika gazeti la Rai nguvu ya hoja, pia akawa ndie anaehariri makala zangu hapohapo New Habari, ila nilipokuwa The African tukawa tunaonana tu ofisini.

Sasa tumekutana tena katika maisha mapya ofisi za Raia Mwema, bado ni mhariri wangu.... Inapendeza sana.... Mungu ampe umri mrefu na afya tele ndugu Mayage mzaliwa wa Kigoma........ Ni mwandishi wa habari nguli kwelikweli..

HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
kidojembe@gmail.com