Na Mwandishi Maalum
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amemteua Naibu
Katibu Mkuu anayemaliza muda wake, Dkt, Asha-Rose Migiro kuwa mjumbe wake
maalum katika masuala yaukimwi na ugonjwa wa ukimwi Barani Afrika.
Ban Ki Moon
ametangaza uteuzi huo wakati wa hafla maalum aliyoiandaa mahsusi kwaajili ya
kumuaga Naibu Katibu Mkuu wake ambaye anahitimisha utumishi wa miaka mitano na nusu katika nafasi yake.
Hafla hiyo imefanyika siku ya alhamisi katika viunga
vya Umoja wa Mataifa, na kuhudhuriwa na wageni waalikwa mbalimbali
wakiwamo mabalozi na wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa.
“Ninatangaza
rasmi kwamba ninamteua Dk. Asha- Rose Migiro kuwa mjumbe wangu
maalum katika masuala ya ukimwi na ugonjwa wa Ukimwi Barani Afrika," alisema Ban
Ki Moon huku akishangiliwa kwa nguvu na wageni
waalikwa.
Akiongea kwa hisia, Ban Ki Moon, ameeleza kwamba ingawa Migiro
alikuwa naibu wake, lakini amekuwa mwalimu kwake kwani amejifunza mengi kwa kipindi alichokaa nae na daima ataendelea kuenzi mchango wake mkubwa.
“ Kama ni kuvaa viatu vyake, naweza kusema ningechekesha
sana, kwa ufupi siwezi kuvaa viatu vya Migiro, amekuwa msaada mkubwa sana
kwangu, ameniwakilisha vema kila mahali nilipomtuma hata katika mazingira
magumu na ya hatari, kote ameniwakilisha vema sana, kama mwalimu
wangu, ni kama profesa wangu anastahili alama ya juu sana” akasema Ban Ki
Moon na kushangiliwa.
Akamuelezea Migiro kama kiongozi si tu mwadilifu, lakini
mwanadiplomasia aliyebobea aliyefanya kazi kubwa ngumu na nzito kwa moyo
mkunjufu, uhodari, umakini na uadilifu wa hali ya juu sana.
“ Siyo rahisi kuelezea yale aliyoyafanya nyuma ya pazia, namna
gani alivyochapa kazi kwa nguvu, yapo mengi makubwa ambayo Migiro ameyafanya
na kuyakamilisha kwa uadilifu wa hali ya juu. Migiro ni mwanadiplomasia
aliyebobea lakini ni mtu wa vitendo, vitendo ambavyo lazima utaona matunda
yake” akabainisha Ban Ki Moon.
Akaongeza “Migiro amefanya kazi na viongozi wagumu, akiwamo aliyekuwa Rais wa Libya Muammar Quadaff aliyethubutu hata
kumrushia katiba ya Umoja wa Mataifa amezikuna nyonyo za watu wengi wakiwamo
watu wanyonge na wenye matatizo mbalimbali. Migiro unaondoka, lakini
Umoja wa Mataifa hautasahau mchango wako. Hapa ni nyumbani kwako, na
nitaendelea kuomba msaada wako na ushirikiano wako, bado nitaendelea
kukuhitaji” akasisitiza Ban Ki Moon.
nae Dk Migiro alimshukuru kiongozi huyo wa umoja wa mataifa na kuita uteuzi wake ni wa heshima na suala la UKIMWI lipo moyoni mwake atalitumikia kwa uwezo wake wote.
"Masuala ya ukimwi na ugonjwa wa ukimwi,
ni eneo ambalo limo ndani ya moyo wake na kwamba nashukuru kuona kwamba Katibu
Mkuu ameniamini kwamba naweza kumsaidia, naahidi nitalitekeleza
jukumu hilo
kwa heshima kubwa".
Hafla hiyo pia imehudhuriwa na familia ya Naibu Katibu Mkuu
ikijumuisha mume wake, Profesa Cleophas Migiro, mdogo
wa Naibu Katibu Mkuu, Bi. Amina Mtengeti na mtoto wa mwisho
wa Migiro Chansa Jasmin.
Asha-Rose Migiro
anakuwa mwanamke wa pili kushika wadhifa huo na mwanamke mwafrika wa kwanza. Lakini
pia ni naibu katibu mkuu ambaye amehudumu
katika wadhifa huo kwa miaka mitano na nusu.
No comments:
Post a Comment