MWENYEKITI wa Jumuiya ya
Madaktari aliyetekwa nyara na kuumizwa vibaya usiku wa kumkia juzi, kisha
kutupwa Msitu wa Pande, Dk Steven Ulimboka amesema atazungumza kwa kina yote
yaliyomsibu baadaye na kuomba sasa aachwe auguze maumivu makali yanayomkabili.
Dk Ulimboka aliokotwa na
wasamaria wema juzi asubuhi katika Msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam, baada ya kutekwa nyara na watu waliokuwa na silaha akiwa katika Viwanja
vya Klabu ya Leaders, Kinondoni.
Jana, Dk Ulimboka ambaye
amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili huku hali yake ikiwa haijatengemaa vyema,
alitoa kauli akisema ingawa ana maumivu makali anaendelea vizuri ikilinganishwa
na siku ya kwanza.
Dk Ulimboka alitoa kauli
hiyo baada ya kutakiwa aeleze mkasa huo uliomfika wa kukamatwa, kuteswa na
kutupwa msituni.
Hata hivyo, hadi sasa
wingu zito la nani alimteka na watekaji walitaka kujua nini kutoka kwa kiongozi
huyo wa madaktari, bado limetanda.
Siri nzito
Akisimulia mkasa huo
kupitia Kituo cha Redio cha Clouds FM, Dk Ulimboka alisema, akiwa katika klabu
hiyo ya Leaders alipigiwa simu na rafiki yake ambaye alikuwa atokee Tandika na
baada ya kumsubiri ndipo alipofika kwenye klabu hiyo, lakini, alianza kujisikia
vibaya tofauti na siku nyingine na kuongeza; "Yaani sikuwa na amani."
Alisema, "Mara,
katikati ya maongezi tukaona mtu anaongea na simu. Ghafla tukiwa tunasema
tuagane, wakaja watu kama watano hivi na
bunduki, wakasema wewe na yule bwana mko free (huru), tunakuchukua wewe (Dk
Ulimboka)," alieleza na kuongeza:
"Sijakaa sawa,
nikaona nimeshaburutwa nikaanguka kwenye lami, wakaniinua na kuniingiza kwenye
gari nyeusi, lakini halikuwa na namba."
Hata hivyo, jana Dk
Ulimboka hakuonana na mwandishi wa habari hii, badala yake alirekodiwa, na
Mwananchi kupata sauti yake akijibu swali kuhusu hali yake na tukio hilo , baada ya uongozi wa
Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) kuzuia watu kumwona.
Daktari huyo wa magonjwa
ya binadamu, amelazwa katika chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu
(ICU).
"Kidogo najisikia
nafuu ikilinganishwa na nilivyokuja ingawaje, bado nina maumivu makali. Kwa
hivyo, ingependeza niendelee na mapumziko na mtu yeyote anayetaka kuniona
pengine hilo
jambo lisifanyike sasa. Hivi sasa ni vizuri nipumzike," ilisikika sauti
hiyo ya Dk Ulimboka.
Lakini, uchunguzi wa
gazeti hili umebaini kuwa wodini alikolazwa Dk Ulimboka, kuna ulinzi mkali wa
madaktari na hairuhusiwi watu kumwona kiholela siyo tu kwa sababu za kutaka
aachwe apumzike, bali pia kutowaamini watu ovyo.
Madaktari wanaolinda
eneo hilo walisikika jana wakisema, “Huyu
tunamlinda wenyewe na haiwezekani mtu asiyefahamika kuingia humu ndani, na hilo tutahakikisha sisi
wenyewe,”alisikika akisema mmoja wa madaktari hao.
Kiongozi jopo la
madaktari
Katika hatua nyingine,
kiongozi wa jopo la madaktari wanaomuhudumia Dk Ulimboka, Profesa Joseph
Kahamba aliwaambia waandishi wa habari kuwa Dk Ulimboka ana majeraha mwili
mzima.
“Ingawa kwa sasa
anaendelea vizuri, Dk Ulimboka ameumia sana ,
kwani mwili wake mzima una majeraha kutokana na kupigwa na watekaji
hao,”alisema Profesa Kahamba na kuongeza:
“Aliumia
mbavuni,kifuani, miguuni, mikononi ambako aling’olewa baadhi ya kucha za vidole
na kichwani na kinywani, ambako aling’olewa meno mawili,”alisema.
Alifafanua kwamba,
kutokana na maumivu hayo ya kichwa, Dk Ulimboka alipata tatizo la mtikisiko wa
ubongo, lakini akasisitiza kuwa madaktari bingwa wanaendelea na harakati za
kuokoa maisha yake.
Uongozi wa Moi watoa
neno
Uongozi wa Taasisi ya
Mifupa (Moi) umeeleza kuwa hali yake inaendelea vizuri ingawa bado amelazwa
katika chumba cha wagonjwa mahututi cha taasisi hiyo.
Msemaji wa Moi, Almas
Jumaa aliwaambia waandishi wa habari kuwa licha ya hali yake kuendelea vizuri,
lakini haingewezekana kwa waandishi wa habari kuingia ndani ya chumba
alikolazwa na kumwona Dk Ulimboka.
“Mgonjwa anaendelea
vizuri ukilinganisha na jana (juzi), anaongea, anawatambua watu wanaokwenda
kumwona, lakini utaratibu wa kwenda kumwona kwa ninyi imeshindikana kwa sababu
yupo (ICU) ni chumba chenye utaratibu wake,”alisema Jumaa.
Jumaa aliongeza kwamba
ili mtu aweze kuingia wodini analazimika kuvaa vazi maalumu na mavazi yaliyopo,
yasingetosha, lakini pia wapo watu wanaoendelea kumpatia huduma ya matibabu.
chanzo cha habari: mjengwa.blogspot.com
No comments:
Post a Comment