Saturday, June 30, 2012

Mpambanaji Ananilea Nkya atoa msimamo wake juu ya mgomo wa madaktari


Katika nchi  yeyote duniani serikali ndiyo  yenye  jukumu la kuweka mazingira mazuri katika hospitali za umma na kuhakikisha kuwa madaktari na wafanyakazi  wa afya  wanafanya kazi yao ya kutibu wagonjwa  kwa  furaha .

Hii  ni kwa sababu serikali  iliyowekwa  madarakani na wananchi moja ya kazi ya   kodi inayokusanya kutoka kwa wananchi   ni  kuhakikisha kuwa  hospitali, vituo vya afya na zahanati za umma ziko katika mazingira mazuri na zinatoa huduma nzuri kwa wananchi.

Mazingira mazuri hospitalini ni pamoja na  kuwepo kwa vitanda vya kutosha kwa  wagonjwa,  madawa ya kutosha na ya viwango bora, vifaa kwa ajili ya kupima na kubaini magonjwa na vifaa  na vyumba maalum vya kusaidia watu  wanaofanyiwa upasuaji  wasipoteze maisha.

Lakini hali ya hosipitali zetu za umma ni hairidhishi.   Kwa mfano hospitali ya taifa ya   Rufaa Muhimbili ni hospitali  madaktari wanalalamika kuwa hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinawafanya madaktari  kushindwa kutimiza wajibu wao wa  kuokoa maisha ya wagonjwa.

Kwa mfano  hospitali hiyo ina   mashine  ya MRI  ya kupima na kutambua ugonjwa  mbali mbali  kwenye mwili ikiwa ni pamoja na kwenye   ubongo, uti wa mgongo na kifua.

Lakini  cha kushangaza mashine hiyo  iliyonunuliwa kwa  shilingi zisizopungua Bilioni mbili miaka michache iliyopita,  inapungukiwa  kifaa cha bei ndogo  tu cha    kuwezesha  watoto kupimwa.

Hivyo watoto wenye matatizo yanayohitaji kupimwa kwa mashine hiyo  wanalazimika kupelekwa India au Afrika ya Kusini kwa wale wenye uwezo  wa kujigharamia  vinginevyo kwa maskini walio wengi  huishia  watoto wenye matatizo makubwa yanayoitaji utambuzi wa mashine hiyo, huishia kufa. 

Aidha  madaktari wanalalamika   jinsi wanavyoshindwa kuokoa maisha ya watoto   wanaozaliwa na tatizo la koromeo  la chakula kuungana na koromeo la hewa. Mabingwa wa upasuaji  wa watoto katika hospitali hiyo  wanasema kwa upande wao wanajitahidi kuwafanyia  watoto hao upasuaji, lakini watoto hao huishia  hufariki dunia  kutokana na hospitali hiyo ya Rufaa kukosa  vifaa maalum vya kuhudumia watoto hao na vyumba maalumu vya kuwaweka  baada ya kufanyiwa operasheni. 

“Kinauma sana  na kinakatisha tamaa sana kuona kwamba mtoto anafanyiwa   upasuaji vizuri lakini anapoteza maisha siku chache baadaye kutokana na kukosekana kwa vifaa na mazingira ya kumwezesha  kupona baada ya upasuaji”, anasema  Dakta Catherine Mungo’ngo, Bingwa wa upasuaji wa watoto Hospitali ya Rufaa ya Taifa.

Kwa mujibu wa bingwa huyo kwa mwaka huu pekee watoto watatu  waliozaliwa na tatizo la la koromeo  la chakula kuungana na koromeo la hewa ambao  walifanyiwa upasuaji  Muhimbili,    baadaye  walikufa hospitalini hapo kutokana na kukosekana kwa vifaa vya kuwasaidia kupumulia na chumba maalumu  cha kuwafanyia uangalizi baada ya upasuaji.

Aidha anasema watoto  kati ya 6 hadi 8 wanaohitaji kufanyiwa upasuaji kwa siku, upasuaji huo huahirishwa kutokana na ukosefu wa vifaa , dawa na chumba maalum cha kuwatunzia baada ya upasuaji.

Ni mtu gani mwenye akili timamu  ambaye atafurahia  kuona kazi anayoifanya  haitoi  matunda yanayotarajiwa.?  Ni Daktari gani  atakayeendelea kufurajhia kazi yake wakati lengo lake la kuokoa maisha ya watu  linakwamishwa  na  mambo yanayowezekana  kurekebishwa?

 Daktari furaha yake ni kutibu mgonjwa na kuona anapona. Lakini Daktari katika hospitali za  serikali  atafanyaje kazi yake kuepusha vifo  visivyo vya lazima kama hana vifaa vya kufanyia kazi ?  

Nionavyo mimi,  serikali yetu inapaswa kutafakari tena kwa utulivu na busara kubwa  na kuweka mikakati ya kupata suluhisho la kudumu la mgogoro  wake na madaktari.

Vinginevyo hata kama wataagizwa  madaktari kutoka Ulaya, na wa hapa nchini kufukuzwa kazi au hata kama viongozi wao ‘watashughulikiwa’,  tatizo la  mazingira ya kazi  hospitalini ambalo ni moja  ya  mambo ya msingi   linalosababisha mgomo wa madaktari   litakuwa halijashughulikiwa  na litaendelea kujirudia  hata kama litapoozwa   kwa mbinu yoyote ile.

 Na ikumbukwe watakaoendelea kuumia zaidi hapa ni wananchi wengi  ambao maisha yao yanategemea uwajibikaji wa serikali yao.
Nijuavyo mimi, serikali  ya wananchi, madaktari wakiwa ni sehemu ya wananchi, husikiliza kero za wananchi na kuzishughulikia badala ya kutumia mabavu na vitisho.  Mungu ibariki Tanzania.
 
Ananilea Nkya
Executive Director
Tanzania Media Women's Association (TAMWA)
P. O. Box 8981, Sinza-Mori
Dar es Salaam, TANZANIA
Tel: +255-22 2772681 Fax +255 22 2772681 E-
mail:ananilea_nkya@yahoo.com
Cellphone:+255-754-464-368


No comments:

Post a Comment