Thursday, June 28, 2012

Wabunge wakiukana ubunge wao nami nitaukana utanzania wangu



Na Hafidh kido

Siku zinazidi kusonga bunge la bajeti linakaribia kuisha, ni kikao ambacho watu tuliowapa dhamana kutuwakilisha kwa serikali wanajadili mustakabali wetu kiuchumi.

Lakini kuna jambo moja ambalo mpaka sasa ufumbuzi wake una utata, suala la posho za vikao.

Siku spika wa bunge mama Anne Makinda, alizungumza na wapiga kura wake wa Njombe kusini, mjini Iringa kuhusu suala la wabunge kutaka kuachia ubunge kutokana na umaskini, ilinidhihirikia kuwa mama yule anafanya kila namna kuiweka pembeni hoja ya wabunge vijana juu ya ubadhirifu wa pesa za umma kwa kulundikiana mafungu yasiyo na tija.

Swali moja lingetosha kumuumbua mama Makinda, je katika kikao gani nusu ya wabunge ambao ni takriban wabunge 150 katika idadi ya wabunge zaidi ya 300 walipata kumwelezea kadhia hiyo ya kuandamwa na ufukara kutokana na wao kuchagua kuwa wabunge?

Sawa tuseme alizungumza maoni ya jumla baada ya kupata malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa vijana wake, lakini kwa namna alivyokuwa akiongea katika luninga siku ile ni wazi yeye alivaa joho la uwakilishi wa ufukara unaowaandama wabunge. Hata kufikia kusema kwa miaka yote aliyokuwa mbunge hajafanikiwa kujenga hata nyumba yake mwenyewe, anajidai kumuiga Nyerere.

Hakuonekana kusikitishwa na kauli hizo bali alitaka kuonekana shujaa kwa wabunge walafi wasiokuwa na shukurani wala huruma kwa wananchi maskini wasiojua watakula nini wala watapata wapi nauli ya kufika kibaruani ili wakamenyeke kwa ajili ya mlo wa siku moja ‘kesho ina Mungu.’

Spika Makinda kwa madaha kabisa aliwaambia wananchi wa jimbo lake ambao wengi ni maskini kuwa hivi sasa nusu ya wabunge wa bunge la Tanzania wanataka kuacha ubunge kutokana na kulipwa malipo madogo.

Hakuishia hapo bali aliendelea kusema kwa miaka ijayo wabunge wenye taaluma zao hawatagombea tena ubunge ikiwa malipo yataendelea kuwa hivi kwasababu ubunge ni eneo la umaskini wa kutupwa kabisa.

Angalia kituko hiki, mama huyo mwenye heshima zake anaongea maneno hayo mbele ya wananchi ambao nusu yake hawana ajira, na wenye ajira wanalipwa mishahara isiyozidi laki nne kwa mwezi bila ya marupurupu ya chakula, usafiri wala nyumba. Halafu anawatetea wabunge ambao wanalipwa mishahara ya shilingi milioni mbili na nusu kwa mwezi, pesa ya mafuta ya gari, wanalipwa posho ya shilingi 80,000/= kwa kikao, wakiwa Dodoma wanalipwa posho ya kujikimu shilingi 70,000/= kwa siku.

Kwa mwaka tuseme vikao vyote vya bajeti viwe ni miezi mitano, yaani tukiviunganisha kwa pamoja. Na vikao vingine vya kawaida vikiunganishwa vyote viwe ni miezi miwili, maana yake kwa mwaka wanakutana kwa miezi saba mfululizo (tukiunganisha) ambapo katika kipindi hicho cha miezi saba kwa siku mbunge akienda Dodoma akihudhuria kikao au asihudhurie ana shilingi 80,000/= kibindoni ya kujikimu, akihudhuria analipwa shilingi 70,000/= ya kikao maana yake anapata shilingi 350,000/= kwa siku tano za vikao tu, posho za kujikimu zinalipwa wiki nzima ambazo ni shilingi 560,000/=, ukijumlisha malipo ya wiki tu ni shilingi 910,000/= Kwa mwezi ni zaidi ya shilingi milioni tatu na laki sita mara miezi saba ni zaidi ya milioni ishirini na tano.

Kumbuka hiyo ni posho ya vikao tu sijaingiza posho ya mafuta, kadhalika sijaingiza mfuko wa jimbo, kadhalika sijaingiza wale wabunge ambao wapo katika kamati za bunge ambao nao wana vikao vyao vya kikamati, posho za safari na mambo mengine pale inapohitajika, kadhalika sijaingiza mishahara ambayo kwa mwaka ni milioni thalathini. Halafu unatuambia ubunge ni dimbwi la ufukara, tukuelewe vipi?

Fikiria mtanzania ambae analipwa laki na nusu kwa mwezi hakuna posho wala safari zitakazomfanya awe na kipato kingine. Anafanya kazi kuanzia asubuhi na mapema mpaka jioni giza linapoingia. Mtu huyu ukiunganisha mshahara wake wa laki na nusu kwa mwaka ni milioni moja na laki nane, pesa ambayo mbunge anaipata kwa wiki mbili tu.

Sijakataa mbunge kuacha shughuli ambayo anadhani itamtia umaskini, sasa hawa ambao tayari ni maskini je wafanye nini?

Ndipo nikasema ikiwa wabunge watakana dhamana tulizowapa wakatutetee ili kwa pamoja tuondokane katika dimbwi la ufukara matokeo yake wanataka kuwa matajiri peke yao, basi na sisi kwakuwa tayari tu maskini itabidi tuukane utanzania wetu ili tukimbilie ulaya kama wakimbizi wa kisomali, Kinyarwanda ama warundi ili tupokewe tupewa hifadhi katika mataifa tajiri nasi tuwe na nafuu ya maisha kama ambavyo watanzania wengi huishi hivyo nchini uingereza, ubelgiji, na nchi nyingi za bara la Amerika na Australia. Wenyewe wanaita kujilipua.

Swali moja kwa mama Makinda, hivi hao wabunge anaosema wana taaluma zao ni kitu gani kilichowafanya waache kulitumikia taifa lao kulingana na taaluma walizonazo kama uanasheria, uinjinia, udaktari, ualimu ama uhasibu na badala yake wakakimbilia bungeni ambako hakuna maana yoyote?

Hakuna kitu kibaya katika maisha ya msomi kama kushindwa kuchagua, tamaa ni maradhi mabaya sana katika taifa changa linalohitaji uzalendo na kujitolea kwingi kwa faida ya wote.

Najua nitaonekana kichaa ama sijui ninachozungumza, mara nyingine maelezo ya wabunge yanaweza kuwa na mantiki kwa namna moja ama nyingine. Kitendo cha kuwajaza mapesa wabunge ndicho kinachowapa kiburi na kutaka zaidi, siku zote anaepata kingi haridhiki lakini anaepata kidogo hujifunza kuweka ili kimfae baadae.

Kwa mfano kipindi cha awamu ya kwanza ubunge ulikuwa ni kazi ya hiyari, wala watu hawakutumia mapesa mingi kupata nafasi ya ubunge, tofauti na sasa ni biashara na ndiyo maana baada ya wabunge kuona biashara inapunguza mvuto wanadai nyongeza ya kingi; wapo wazee ambao walikuwa wabunge na mawaziri katika serikali ya awamu ya kwanza sijui serikali ina mpango nao gani, lakini wanaishi maisha ya chini kabisa.

Hii inaonyesha wazi walikuwa wakiwatumikia watanzania kwa moyo wote na si kutaka kujilimbikizia mali na kusahau kilichowapeleka bungeni. Tazama watu wanazusha hoja binafsi kwa kununuliwa. Tajiri mmoja tu anaweza kumnunua mbunge na kumwambia peleka hoja hii ikajadiliwe, ikipita tu nakuandalia tumilioni kadhaa. Vitu hivi vipo tusikatae.

Maneno ya wazee waasisi wa nchi hii hata siku moja hayawezi kuanguka, walisema kiongozi akiingia kwa rushwa hata siku moja hatoweza kuongoza kwa ufanisi kwani itabidi aanze kuwaridhisha wale waliompatia fedha kuingia madarakani.

Ubunge ni biashara na ndiyo maana wanaanza kuona hasara, fikiria mtu anakwenda kukopa mamilioni ya fedha, nyingine anakwenda kuomba kwa wafanyabiashara wakubwa ambao malipo yao ni kufuata kila wanachokitaka pindi ukishika madaraka.
Na ndiyo maana baadhi ya ‘wabunge maslahi’ wanaanza kuona hali ni ngumu, miaka mitano inakwisha hajarudisha hata nusu ya alichopoteza, na bado hajamaliza madeni huku wale watu waliomfadhili wanataka kulipwa fadhila kwa mambo ambayo kwa nafasi yake ya ubunge hawezi kuyatimiza, hapo ndipo anapojuta na kuona ubunge ni mzigo.

Naamini mtu ambae ameingia bungeni kwa njia safi na halali hata siku moja hawezi kuwa na majuto, kwani kwa hali za watanzania malipo wanayoyapata wabunge ni makubwa sana hakuna mfanyakazi yeyote anaeweza kuyapata hata awe mkurugenzi.

Tafadhali rejea mchanganuo wa pesa wanazopata wabunge wetu halafu linganisha na maisha ama pesa unazopata kwa mwezi. Hata msomaji akiwa ni mkurugenzi wa shirika lolote ima la umma ama la binafsi hawezi kufikia pesa anazopata mbunge.
Halafu leo wanakwenda kutuambia kiasi wanachopata kinawatia umaskini.
Yaani sijapata kusikia upumbavu namna hii tangu nimezaliwa, hivi hawa wabunge wetu wanatuonaje sisi watanzania. Nauliza kwa nia njema tu wala si kwa kebehi, leo hii kila mtu anatamani kuishi maisha anayoishi mbunge halafu wanakuja kutuambia ubunge unawatia ufukara wanajua kweli fukara wa kitanzania anapata shilingi ngapi kwa siku?


Naishia hapa nisije kutukana bure.

Naomba kuwasilisha.
      


No comments:

Post a Comment