Na Hafidh Kido
Abdulrahman Mohammed babu
aliekuwa kiongozi wa chama cha kisiasa cha UMMA Party kabla ya mapinduzi ya Zanzibar wakati akizungumzia vuguvugu la mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 katika kitabu chake cha ‘Husuda ya
Marekani dhidi ya mapinduzi ya Zanzibar .
Siku 100 za kuundwa kwa Tanzania ’
alisema usiku wa tarehe 11 Januari, mwaka 1964 katika hali ngumu ya maisha
vijana wa mitaani watoto wa makabwela wasio na kazi waliamua kuingia mitaani na
kufanya vurugu kupinga uongozi wa kisultani.
Katika kitabu hicho Babu
alielezea ushiriki wa mapinduzi kwa vijana wa Unguja ambao hawakufurahishwa na
utawala wa kiarabu kuendelea kushikilia uchumi wa visiwa hivyo mbali ya kupata
uhuru mwaka 1963.
Miezi michache iliyopita
tumeshuhudia viongozi wa chama cha kiislam cha muamsho walivyofanya vurugu katika
visiwa hivyo kwa madai ya kuitaka Zanzibar
ijitenge na Tanzania
bara ili kuepuka baadhi ya mambo waliyoyaita ukiukwaji wa maadili ya Mzanzibari
na hali mbaya ya maisha inayosababishwa na kunyonywa katika mgawo usio halali
katika keki ya taifa.
Lakini cha kushangaza siku
chache baada ya vurugu zile zilizosababisha hasara kubwa kwa wamiliki wa sehemu
za starehe, makanisa na watu kutoka Tanzania bara watu wasiojulikana walitoa
waraka wa kupinga vurugu zile na kuziita ni za wapemba wasio na uchungu na
visiwa hivyo kwani wanataka muungano uvunjike ili uongozi wa kisultani urudi
Zanzibar.
Waraka huo uliotolewa na watu
waliojiita waunguja umewashutumu watu wanaotoka kisiwa cha Pemba kuwa si
wenyeji wa ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na ni wamakonde kutoka sehemu za Pemba nchini Msumbiji, na ndiyo maana kipindi cha
mapinduzi hawakuwa upande wa wanamapinduzi badala yake waliunga mkono utawala wa
Sultan Jamshid.
Sehemu ya waraka huo inasema
“Watu wa Unguja tunatoa ujumbe makhsusi kwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania
Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, sisi watu wa
Unguja tumechoka kuishi na Wapemba katika kisiwa chetu cha Unguja, kwani ni
watu wasio na fadhila ya aina yoyote, hivyo tunakuomba Mh. Rais wa jamhuri
fanya mazungumzo na Mh. Rais wa Zanzibar na ifikie hatua maalim Seif Sharif
Hamadi apewe kisiwa chake cha Pemba na akatawale wapemba wenziwe.”
Taarifa hiyo ya kurasa moja
iliendelea kueleza “Hapo siku za nyuma wapemba walidai kisiwa chao na nyinyi
viongozi mkang’ang’ania kuwa hatuwezi kuvunja umoja sasa mnawaona hao tayari
wameanzisha chama cha kisiasa cha ‘Muamsho’ kwa kisingizio cha dini.”
Utaona kuna hali ya
kuchanganya mada hapa na haijulikani kuwa hii hoja ya kutaka muungano uvunjwe
ina baraka za visiwa vyote viwili vya Unguja na Pemba
ama la. Na ikiwa hoja hii inatoka kwa watu kutoka kisiwa kimoja tu cha Pemba inamaana zile tetesi za kutaka kumrudisha Sultani Jamshid
ambae kwa sasa anaishi uhamishoni nchini Uingereza zina ukweli ndani yake.
Waraka huu unaodaiwa kutolewa
na watu toka kisiwa cha Unguja kwa sababu haukutiwa saini na mtu yeyote
inawezekana ni njia za serikali kuu kupoteza lengo la watu wa visiwani kupinga
muungano ama inawezekana ni kweli hakuna maelewano na muafaka wa visiwa viwili
hivi katika kupinga muungano.
Binafsi nilibahatika kukaa
Unguja kwa miezi miwili nikifanya mazoezi ya habari TVZ mwaka 2007,
nilichojifunza ni kuwa kuna mpasuko mkubwa baina ya watu wenye asili ya Unguja
na Pemba . Hakuna mahusiano mazuri kama watu wengi wanavyodhani.
Waunguja wanajinasibu na
hekima, utu na busara ya kutafakari mambo. Wapemba wanaonekana daima ni
wapinzani na watu wenye chembechembe za uarabu kadhalika ni watu wenye hasira
za haraka na huchukua maamuzi bila ya kutafakari. Hii ni tafsiri yangu baada ya
kukaa Unguja kwa miezi hiyo michache, sijawahi kufika kisiwa cha Pemba lakini waliofika wananiambia kuna athari kubwa ya
watu wenye asili ya uarabu kuliko waafrika.
Na ndiyo maana hata Rais wa
kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ndugu Abeid Amani Karume inadaiwa alikuwa hana
mapenzi na watu kutoka kisiwa cha Pemba .
Alifikia kusema mpemba hatoshika uongozi wa juu katika visiwa vya Zanzibar , cheo cha mwisho
kwa mpemba ni mwalimu mkuu wa shule.
Lakini cha ajabu mara hii
viongozi wawili wa juu kabisa wanatoka kisiwa cha Pemba .
Rais na Makamu wa kwanza wa Rais wote ni wapemba. Nadhani watu kutoka Pemba walitegemea makubwa kwa matokeo hayo lakini kinyume
chake hakuna lolote lililobadilika zaidi ya wapemba kuendelea kukandamizwa.
Kudhihirisha chuki dhidi ya
mapinduzi watu wenye asili ya kisiwa cha Pemba
kwa muda mrefu wamekuwa wakipinga kitendo cha watu wa Unguja kupindua serikali
ya Sultan Jamshid Bin Abdullah al-Said, chini ya waziri mkuu Mohammed Shamte.
Mwandishi wa kitabu cha
‘Ukweli ni huu kuusuta uwongo’ Amani Thani Fairooz, alichokiandika akiwa
uhamishoni katika falme za kiarabu mwaka 1995; anaandika “Matunda makubwa
waliyopata wananchi wa visiwani Unguja na Pemba
kutokana na hayo yenyekuitwa ‘mapinduzi’, ni shida za kimaisha katika kila
upande. Vyakula havinunuliki, nguo hazikamatiki mradi wananchi wamo katika
kuhiliki kwa maisha yalivyo magumu . Vijana wamekuwa wazee kwa shida,” uk .
15.
Fairooz anaendele kuandika
katika kitabu hicho kuhusu mapinduzi; “Mafisadi wachache kwa ajili ya maslahi
ya nafsi zao hawakutahayari kuchanganyika na wageni waliokuwepo ndani ya nchi
na walioletwa kutoka nchi jirani kwa makusudio khasa ya kuivamia Zanzibar na kuiondoa
Serikali ya wananchi. Wananchi mafisadi hao walikubali kuongozwa na wageni,
John Okello aliyetoka kwao Uganda ,
Injinia aliyetoka kwao Kenya
na Mfaranyaki aliyetoka kwao Tanganyika ,
kuivamia nchi yao
katika usiku wa manane wa kuamkia taarikh 12 Januari 1964.
“Wananchi, mafisadi kwa sababu
ya maslahi ya nafsi zao hawakuhisi uchungu kuipoteza nchi yao , wala kuzipoteza roho za wazee wao, za
ndugu zao na za marafiki zao….. ukatili, ushenzi na unyama uliofanywa katika
visiwa hivi vilivyokuwa na ustaarabu wa kupigiwa mfano, hauwezi hata kuhadithika.”
Ukitazama maneno yaliyo
katika kitabu cha Abdulrahman Babu miongoni mwa waasisi wa mapinduzi na mwenye
asili ya Unguja, ukipambanisha na maneno yaliyo katika kitabu cha Amani Fairooz
mwenye asili ya Pemba na mpinga mapinduzi
utaona ni namna gani visiwa hivi viwili vilivyo na mitafaruku ya kikanda tangu
zamani.
Kilichotokea kipindi cha
utawala wa Kisultani ni watu wenye asili ya kiarabu, kihindi na kizungu kupewa
kipaumbele katika masuala ya kimaendeleo lakini waafrika ama ‘Magozi’ kama walivyokuwa wakiitwa na watu wenye asili ya kiarabu
walikuwa wakidharauliwa na kutengwa.
Wakwezi na wakulima lilikuwa
ni jina la watu toka Unguja ambao ndiwo walionekana kuwa na uchungu sana kwa hali duni za
kimaisha. Wakati wa vuguvugu visiwani humo watawala wa kiingereza walikuwa
mbioni kuachia madaraka kwa wazalendo baada ya kufanya hivyo kwa nchi jirani za
Afrika ya mashariki. lakini utaratibu uliotakiwa kutumika ilikuwa ni kupiga
kura.
Kulikuwa na pande mbili
zilizokuwa zikivutana kwa karibu vyama viwili vilivyoungana vya ZPPP (Zanzibar and Pemba People’s Party) na ZNP (Zanzibar
Nationalist Party) maarufu kama Hizbul-Wattan,
dhidi ya chama cha ASP (Afro Shirazi Party) chama kilichokuwa na watu wengi
kutoka Unguja.
Muungano wa ZPPP/ZNP
ulifanikiwa kushinda uchaguzi wa mwaka 1961, June kwa kupata viti 13 dhidi ya
ASP waliopata viti 10. Ndipo ZPPP/ZNP walipounda serikali ya madaraka. Lakini
tatizo likawa ni mgawanyiko wa wananchi juu ya nani akabidhiwe uhuru kutoka kwa
waingereza.
Baada ya mvutano wa kuunda
katiba ya Zanzibar ili wakabidhiwe uhuru wao, Machi na April 1962
huko Lancaster House, London
baina ya upinzani na serikali ya madaraka lakini mazungumzo hayakufikia mwisho
yakavunjika.
ASP ambao walikuwa ni upande
wa upinzani walisusia mazungumzo yoyote ya kutangazwa tarehe ya uhuru mpaka
ufanyike uchaguzi mwengine kwani kwa maelezo yao hawakuridhishwa na matokeo ya uchaguzi
uliowaweka madarakani ZPPP/ZNP.
Baada ya mazungumzo ya muda
mrefu vyama vyote vilikubaliana uchaguzi urudiwe, ndipo mwaka 1963, Julai
ukaitishwa uchaguzi mwingine na muungano wa ZPPP/ZNP wakashinda tena viti 18
dhidi ya ASP iliyopata viti 13.
Serikali ya Uingereza ikawaita kwa mara
nyingine wapinzani na viongozi wa serikali ya Zanzibar kuenda Uingereza kuzungumzia tarehe
ya uhuru, mambo yalikwenda vizuri na ASP walikubali shingo upande muungano wa
ZPPP/ZNP kupewa uhuru. Ndipo ikapangwa
10 December, 1963 kuwa tarehe
ya uhuru wa Zanzibar
chini ya waziri mkuu Mohammed Shamte na kiongozi wa nchi Sultani Jamshid
al-Said.
Kilichowafanya watu toka
Unguja kupinga uhuru huo ilikuwa ni kile kitendo cha Zanzibar kuendelea kutawaliwa na waarabu.
Yaani walikuwa wakifuata mfumo wa kiingereza Sultan angekuwa mkuu wa nchi ambae
atakuwa wa maisha akiendeleza ukoo wa kisultani, lakini Waziri mkuu atakuwa
akichaguliwa kila baada ya muda fulani uliopangwa katika katiba ya Zanzibar . Kihalisi huo
haukuwa uhuru bali kiini macho tu.
Ndipo ASP baada ya mwezi
mmoja tu tangu Zanzibar
kupata uhuru walifanya mapinduzi na kuungoa utawala wa kisultani nchini humo.
Sasa ninaposikia mtu kutoka Zanzibar
anapinga mapinduzi nakuwa simuelewi.
Hivyo naiasa serikali ya Tanzania
chini ya Rais Kikwete, kuacha kudharau hizi vurugu za vikundi vya waislam kwani
kirahisi tu vinaweza kuchota fikra za wazanzibari wote maana hata kipindi cha
mapinduzi walioanza chokochoko ni vijana wa mitaani tu baadae kina Karume
wakaingilia kati baada ya kuona mambo yamenoga. Huwezi kujua hata ndani ya
Serikali ya mapinduzi Zanzibar
kuna viongozi wakubwa wanataka muungano uvunjwe wanasubiri gari ikolee kasi ili
wadandie.
Naomba kuwasilisha
lor '
c ;
No comments:
Post a Comment