Na Hafidh kido
Mwalimu wangu wa somo la “issues in mass communication”
Mohammed Matovu, aliwahi kutuuliza darasani ni nani adui mkubwa wa vyombo vha
habari, ni serikali ama mashirika ya matangazo (Advertising companies). Kila
mmoja alikuwa na jibu lake, lakini jibu langu lilikuwa ni mashirika ya
matangazo ndie adui mkubwa wa vyombo vya habari, na mwalimu wangu akanipongeza
kwa jibu zuri.
Sitofafanua jibu langu kwani leo sijakusudia kuogelea katika
bahari hiyo ambayo wajuzi wa taaluma hii wanajua namna kina chake kilivyo
kirefu.
Nina miezi kadhaa tangu nimalize shahada yangu ya mawasiliano
ya umma nchini Kampala , Uganda . Bado nina zile chembechembe
za kiuanafunzi, napenda sana
kulumbana na hasa nikiona kitu ambacho kinagusa taaluma yangu ya
uandishi.
Miezi kama mitatu iliyopita nilisoma katika gazeti kuhusu taarifa za
kushughulikiwa wahariri wawili wa shirika la utangazaji Zanzibar, Zanzibar
Broadcasting Cooperation (ZBC), kwa kosa la kumbagua Rais Shein kwa kumwandika
kwa uchache kuliko inavyotoa taarifa zinazomuhusu makamu wa kwanza wa Rais Seif
Sharrif Hamad.
Wahariri hao wawili Juma Mohammed Salum na Ramadhan Ali
walihamishwa kutoka ZBC makao makuu ambayo zamani ikitambulika kama Televisheni ya Zanzibar (TVZ) iliyopo Karume House,
karibu na Hospitali ya mnazi mmoja Unguja. Na kuhamishiwa idara ya habari
(MAELEZO) ya Zanzibar ,
ambayo ni ofisi ya chini ukilinganisha na ZBC.
Huku ni kukosa uzalendo na kupungukiwa akili, mtu ambae
alikuwa anahariri habari za shirika la utangazaji katika nchi (Zanzibar ), leo hii
unampeleka eneo ambalo atakuwa anasimamia upokeaji na usambazaji wa taarifa za
habari, tena zisizohaririwa, kwasababu tu anatuhumiwa kuhujumu matukio ya
kihabari ya Rais. Maana kazi ya kuhariri inahitaji uwezo wa hali ya juu, na
ninaamini mpaka wizara inawateua ni wazi uwezo wao ni wa hali ya juu.
Alipoulizwa na waandishi wa habari mjini Zanzibar katibu
mkuu wa wizara ya habari, utamaduni, utalii na michezo ya serikali ya Umoja wa
kitaifa Zanzibar Ali Saleh Mwinyikai, kuhusiana na sakata hilo alisema kosa
kubwa la wahariri hao Juma Mohammed Salum (mhariri mkuu) na msaidizi wake
Ramadhan Ali, ni kuvuruga ama kutofuata maelekezo ya namna ya kuripoti habari
za viongozi.
Yaani kitendo cha kuandika sana habari za makamu wa pili wa Rais
Zanzibar na kuandika kwa uchache matukio ya Rais Dk Ali Mohammed Shein, ndilo
kosa hasa lililowafanya wahariri hawa kufukuzwa katika nafasi zao na kuwekwa
watu wengine wanaojua kumpamba Rais.
Taarifa hizo si tu zinanifanya nianze kubadili fikra na
kuanza kuamini kuwa adui mkubwa wa vyombo vya habari ni serikali iliyo
madarakani, lakini zinamdhalilisha Rais Shein kwa kumuweka katika kundi la watu
wanaopenda kuonekana katika vyombo vya habari hata akiwa analisha kuku wake wa
kufuga pale Ikulu. Kwani wahariri hawa wamepewa karipio kali na serikali ya
mapinduzi Zanzibar kwa kosa la kutomuandika sana muheshimiwa, na
badala yake kumuandika msaidizi wake ambae ni mpinzani asiefaa kuonekana kwenye
luninga.
Katika taaluma ya habari suala hilo tunaliita ‘conflict of interest or
ethical dilema’ yaani ni kugongana kwa maslai ama kuweka rehani maadili ya
kitaaluma.
Haiyumkiniki kumfundisha
mtu kazi usiyoiweza. Kwasababu sitaki kuamini kinachozungumzwa, kwani mwandishi
yeyote wa habari hupenda vitu viwili katika vingi.
Maana ya kusema hayo ni kuwa, mpaka Rais anakosa kuonekana
katika vyombo vya habari ni kuwa hatengenezi tukio ama wazungu wanaita (he does
not make news). Seif kwa kuwa alipambana kuipata nafasi hiyo kwa miaka mingi ni
wazi wananchi wa Zanzibar na dunia wanataka
kuona utekelezaji wake kama miongoni mwa
viongozi wa juu katika nchi ambayo ilimtesa na kumnyanyasa mpaka kufikia hapo.
Hii inanikumbusha tukio la mwaka jana pale mkurugenzi wa Tanzania Broadcasting Cooperation (TBC) ndugu
Tido Mhando, alipokutwa na masaibu kama hayo ya kutimuliwa katika nafasi yake
kwasababu tu wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, alikuwa akitoa sana taarifa zinazohusu
mikutano ya CHADEMA kuliko CCM.
Inatia kinyaa sana
kuona serikali yetu inafanya vitu vya hovyo kwa watu wenye uwezo wa kipekee
katika taaluma mbalimbali kwa kutaka kuwaridhisha wanasiasa.
Naamini kwa uwezo wake wa hali ya juu katika taaluma ya
habari Tido Mhando, asingeweza kuwapa ‘coverage’ kubwa CHADEMA na kuwaacha CCM,
ikiwa CCM ‘wana-make news’ ni wazi chama hicho kikongwe hakikuwa na sera yoyote
mpya katika uchaguzi ule. Kitu ambacho kiliwafanya waonekane kwa uchache sana katika chombo hicho
cha taifa.
Sote tunakumbuka mwanzoni mwa mwaka 2006 mara baada ya Rais
Kikwete kuingia madarakani kila chombo cha habari wakati wa jioni lazima kianze
na habari inayomuhusu Rais. Hata kama habari hiyo haikuwa na maana yoyote ni
lazima itawekwa ya kwanza.
Mpaka ikafika mahali watu wakawa wanakejeli vyombo vya
habari kila ifkapo saa mbili usiku wakati wa taarifa ya habari ya siku nzima.
Habari ikianza tu utasikia watu wakikejeli ‘Rais kikwete….’ Yaani ni lazima
mtangaji atataja jina la Rais Kikwete ndipo aendelee na habari nyingine.
Lakini baada ya Tido Mhando kukabidhiwa TBC kitu cha kwanza
kufanya ni kuliondoa shirika hilo
katika uangalizi wa Serikali yaani liwe shirika linaloingia katika upinzani wa
kibiashara. Kwani hapo awali lilikuwa likipata ruzuku ya asilimia mia moja
kutoka serikalini hivyo kukifanya kituo hicho kuwa tegemezi na kufuata kila
ambacho serikali inataka.
Baada ya hapo tukashuhudia TBC ikianza kuja juu, vifaa vya
kazi vya kisasa vikaingia, watangazaji wa shirika hilo wakaanza kuneemeka, aina ya habari za
awali za kutukuza tu bila kufanya uchunguzi wa kina zikaanza kufutika na mwanga
kuonekana na watu kurudisha imani.
Hakuna mtu ambae hajaridhishwa na kazi nzuri iliyofanywa na
Tido Mhando wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Kila mtu
alitamani ifike saa mbili aangalie TBC kuona nini kinaendelea, taswira halisi
ya nchi yetu ilionekana na wapinzani walipata pa kuzungumzia.
Kiuhalisia TBC ilikuwa sahihi kufanya hivyo kwani shirika hilo la habari lilikuwa likijitegemea, na hata kama
lingekuwa halijitegemei lakini chombo hicho kipo chini ya serikali hivyo kuacha
kuandika mambo ya CCM sidhani kama ni kosa la
kumfanya mtu kutimuliwa kazi. Kwani wakati wa kampeni CCM haikuwa na serikali,
vyama vyote vilikuwa chini ya serikali.
Hivyo kitendo cha kumfukuza Mhando, kimeidhalilisha serikali
na chama tawala cha CCM kwa kuonekana wanapenda kuonyeshwa kwenye vyombo vya
habari hata kama hawana cha kuiambia jamii.
Mwanahabari habembelezwi wala kuombwa kuonyesha tukio, bali yeye mwenyewe
atafanya kila juhudi kuweza kulipata tukio hilo ili kulitumia katika chombo chake.
Kitu ambacho kinanitia kinyaa kuhusu suala la Serikali ya
Zanzibar na kuwatimua wahariri kwasababu tu hawampi ‘coverage’ kubwa Rais
Shein, ni kuwa hata huyo ambae anapewa ‘coverage’ ni kiongozi wa serikali kuna
ubaya gani?
Inawezekana hili agizo hata halitoki ikulu ya Zanzibar lakini kuna
baadhi ya watu hupenda kujikombakomba kwa viongozi wa juu ili waonekane
wanafanya kazi. Hakuna anaejua labda Rais mambo yamemtinga na hushiriki sana shughuli za nje ya
nchi, shughuli zinazohusu kuzindua miradi, kutembelea wananchi na kutatua
baadhi ya kero za kimaendeleo mambo hayo amemuachia makamu wake wa kwanza ambae
ni Seif.
Sasa Seif Sharrif akionekana kwenye luninga vijana wa kisasa
tunaita ‘akiuza sura’ sana
kuliko bosi wake kuna ubaya gani?
Nadhani hili linapasa kuangaliwa kwa jicho la samaki, yaani
liangaliwe kwa pande zote kitaaluma na kiutendaji. Yaani wanahabari wachunguze
hili na kutoa tamko, kadhalika watendaji wa serikali nao walichunguze na
kulitolea tamko hii ni aibu kwa wizara ya habari kubembeleza habari.
Waandishi tusiwe mabubu katika mambo yanayowahusu wenzetu,
kudhalilishwa kwa wahariri Zanzibar
kunaigusa taaluma hii kila pembe ya nchi. Hivyo hatuna budi kuzungumza na
wanahabari wa Zanzibar
ili kufanya uchunguzi wa kilichotokea.
Naamini heshima yetu itarudi, naomba kuwasilisha
No comments:
Post a Comment