Rais Kikwete akipongezana na waziri mkuu mpya wa Ethiopia ambae ndie mwenyeji wa mkutano huo ndugu Hailemariam Desalegn baada ya utiliaji saini mpango huo kwenye jumba la umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia jana Feb 24, 2013. Anaeshuhudia furaha hiyo katikati ni mwenyekiti wa kamisheni ya umoja wa mataifa Dk Nkosazana Clarice Dlamini-Zuma.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo Februari 24, 2013 ameungana na Wakuu
wenzake wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kutia saini Mpango
wa Umoja wa Mataifa wa Amani, Usalama na Ushirikiano katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Mhe. Rais Kikwete alisema mara baada ya
utiwaji saini wa Mpango huo kwamba: “Hii ni siku kubwa na ya kihistoria kwa watu wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jirani zake na Ukanda wote wa Maziwa Makuu.
Ni siku ya kukumbukwa kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC),
Afrika, Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na Jumuiya yote ya Kimataifa. “Watu
wa Kongo wameteseka kwa muda mrefu sana .
Wanastahili kupumua sasa. Wanastahili kuishi maisha
bora; maisha ambayo usalama wao
umehakikishiwa na kuthibitishwa; maisha ambayo yatawafanya waendeshe maisha yao kwa kufanya mambo ya maana zaidi katika
kuboresha maisha yao
ya kila siku.
“Saini tulizotia kwa Mpango huo leo ni
kielelezo cha dhati na ahadi ya utekelezwaji wa yale yanayotarajiwa
na watu wa Kongo na Ukanda wa Maziwa Makuu kwa ajili ya Amani, Usalama na
Ushirikiano.
“Kwa niaba ya Serikali na Watu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania naahidi kwamba sisi tutatekeleza kwa dhati yale yote
yanayotarajiwa kwa upande wetu”, alisema.
Mpango huo umetiwa saini na viongozi
kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jamhuri ya Uganda , Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Angola , Jamhuri ya Burundi ,
Jamhuri ya Kongo (Brazaville), Jamhuri ya Zambia ,
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
pamoja na Jamhuri ya Afrika Kusini.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Ban
Ki-moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa, Dkt. Nkosazana
Dlamini-Zuma, pamoja na wenyeviti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
(SADC) na Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) wametia saini Mpango huo kama mashahidi na wadhamini.
Mpango huo una nia ya kuchangia juhudi
ambazo zimefanywa na ICGLR na SADC katika kutafuta amani Mashariki ya Kongo na
ukanda wote wa Maziwa Makuu kwa ujumla.
Mpango huo pia umetilia maanani
mapendekezo muhimu yaliyokubalika baada ya mashauriano kati ya wakuu wa nchi za
ICGLR na SADCna Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Mapendekezo ya mpango huo ni pamoja na
kuboresha sekta ya Ulinzi na usalama, hususan jeshi la polisi, Kuimarisha
mamlaka ya nchi hasa mashariki ya Kongo; na kuendeleza ajenda kuhusu maelewano,
kuvumiliana na kudumisha demokrasia nchini humo.
Vile vile, nchi za Kanda zimetakiwa
kutoingilia mambo ya ndani ya nchi jirani, kututoa msaada wowote wa vikundi vya
waasi, kuheshimu utawala na maeneo ya nchi jirani na kuimarisha mahusiano ya
Kanda.
Hali kadhalika, Jumuiya ya Kimataifa
imetakiwa kuisaidia DRC na Kanda yote ya Maziwa Makuu kwa ujumla katika
utekelezaji wa miradi muhimu pamoja na mkataba wa Amani, Usalama na Maendeleo
katika Ukanda wa Maziwa Makuu.
Aidha, Mpango huo unapendekeza kuwepo kwa
chombo cha usimamizi (Oversight Mechanism) ambacho kitaundwa na viongozi wote wa
nchi 11 pamoja na Umoja wa Mataifa, SADC na ICGLR.
Imetolewa na:
Muhidin Issa Michuzi,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
24 Februari, 2013
No comments:
Post a Comment