Monday, February 25, 2013

Soma nafasi ya tatu ya makala ya mwanajeshi aliemuua Osama Bin Laden.



MAREKANI inaamini kuwa vita vya kukabiliana na ugaidi vimepata mafanikio baada ya kuuawa kwa kiongozi wa kundi la Al-Qaeda, Osama bin Laden aliyeuawa Mosi, 2011 nchini Pakistan.
Hivi karibuni askari aliyefyatua risasi na kumuua kiongozi huyo alifanya mahojiano na mwandishi mmoja wa habari kuelezea namna operesheni hiyo ilivyofanikiwa.
Katika mfululizo wa simulizi hiyo leo mwandishi George Njogopa anapitia sehemu ya mwisho ambayo inamulika upande wa maisha yake binafsi.
Kulikuwa na furaha na shangwe kila kona ya Marekani na duniani kote. Mhalifu wa kimataifa alikuwa ameondoshwa kwenye uso wa dunia.
Askari aliyefyatua risasi na kumaliza uhai wa Osama alikuwa tayari amerejea nyumbani.
Rais Barack Obama aliingia kwenye rekodi mpya kwa kuwa kiongozi aliyefanikisha kuangusha ngome muhimu ya mtandao wa Al-Qaeda.
Baadhi ya askari wa Marekani waliopiga kambi katika mji wa Jalalabad nchini Pakistan waliambatana na askari mlenga shabaha kurejea nyumbani.
Askari huyo anasema kuwa, “Tulivyomaliza operesheni yetu tukarejea nyumbani kuendelea na majukumu mengine. Nakumbuka nilivyoondoka Jalalabad nilirejea moja kwa moja kwenye kituo cha vikosi vya majini na kuendelea na shughuli nilizopangiwa.”
Askari huyu ambaye ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho kumwona Osama wakati akiwa hai kabla hajammiminia risasi mbili za usoni amesema sasa anaishi maisha ya upweke tofauti na miaka ya nyuma.
Anasema kuwa wakati akiwa katika operesheni nchini Pakistan mkewe pamoja na watoto wake waliishi maisha ya mahangaiko na  wakati mwingine walilazimika kuhama mji mmoja hadi mwingine wakihofia pengine wangevamiwa na makundi yenye uhusiano na vikundi vya kigaidi.
“Wakati nikiwa Jalalabad niliwaambia watoto wangu kutosema chochote kwa marafiki zao kuhusiana na kazi yangu hasa baada ya kujulikana kuwa mimi ndiye niliyemuua Osama.
Nakumbuka wakati fulani mke wangu aliwafuata maofisa wa CIA akitaka kubadilisha jina na apelekwe katika mji mwingine kwa hofu kuwa pengine angevamiwa na watu wasiojulikana.
Hata hivyo jaribio lake hilo halikufaulu na baadaye akaamua kuondoka na kwenda kuishi katika mji mwingine akiwa na watoto.  Askari huyo anasema kuwa muda mwingi aliotumia jeshini ulimfanya apoteze upendo wa karibu na familia yake jambo lililosababisha kuvunjika kwa ndoa yake.
Wakati akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi mmoja wa habari, mke wa askari huyo alieleza sababu za kuachana na mumewe ambaye alikuwa ameishi naye kwa zaidi miaka 10.
“Sikupenda kuendelea kuishi maisha ya hofu… halafu isitoshe muda mwingi nilikuwa mpweke na mwenzangu mara zote alikuwa kwenye safari za mbali.
“Hata hivyo, siwezi kusema simpendi hapana, bado tunawasiliana na jambo kubwa ni hawa watoto wetu tungependa kuona wanaendelea kupata uangalizi wa karibu kutoka pande zote mbili. Nimefurahi kuona sasa niko peke yangu lakini bado tunawasiliana kwa karibu na mwenzangu,” alisema mama huyo.
Mama huyo ambaye hata hivyo hakutaka  jina lake kuchapishwa hadharani, hivi sasa anaishi Milwaukee ambako anajishughulisha na  kazi za hapa na pale kwa ajili ya kuendesha maisha yake.
Akizungumzia maisha yake baada ya kurejea toka kwenye operesheni nchini Pakistan, askari huyo anasema kuwa, aliendelea kuishi maisha ya furaha na amani huku akipata pongezi toka kwa ndugu na marafiki zake kutokana na kitendo  cha kishujaa cha kuondosha maisha ya Osama.
Lakini hata hivyo bado anakumbuka jinsi operesheni ya kusambaratisha ngome ya Osama ilivyoendeshwa.
“Unajua mie ndiye niliyekuwa wa mtu wa mwisho kumwona Osama wakati akiwa bado hai. Baada ya hapo askari wote waliokuja baada yangu walikuta mwili umelala sakafuni ndiyo maana walipiga risasi za ovyo ovyo tu.
“Nakwambia ile operesheni ilifanikiwa kwa mazingira ya ajabu sana, kwani wakati tunakwenda kuvamia nyumba yake tulikuwa bado tuna mashaka mengi kama kweli hesabu zetu zilikuwa sahihi au la.
“Wakati fulani nakumbuka tukiwa bado angani lakini tumekaribia eneo la tukio tuliulizana je, tulipue kwa bomu ama twende kwa kutumia uvamizi wa ardhini.Tulishauriana kwa muda kidogo lakini baadaye tukafikia uamuzi wa pamoja kwenda kwa kutumia mashambulizi ya ardhini kwani tulikuwa tayari tumejifua vya kutosha.
“Nakumbuka pia wakati  tunatoka Washington kuelekea Pakistan tulikuwa tumegawanywa kwa makundi. Kuna wale waliokuwa kitengo cha CIA, makomandoo, walenga shabaha na wengine katika idara za kawaida. Pia nakumbuka tulikuwa tumeambatana na mbwa wawili ambao walitusaidia kwa kiwango kikubwa wakati tulipoendesha upekuzi katika nyumba ya Osama baada ya kufanikiwa kumzingira na kumuua.
Akirejelea kwenye maisha yake baada ya kurejea nyumbani askari huyo anasema kuwa aliendelea kulitumikia jeshi hilo kwa miaka mingine 12 na baadaye ilipofika mwaka 2011 alistaafu na kurejea kwenye maisha ya uraiani.
“ Nimelitumikia jeshi kwa miaka mingi lakini ilipofika mwaka 2012 nikaamua kustaafu na kurejea kwenye maisha ya uraiani. Maisha ya jeshi kwa kweli yalikuwa na mikikimikiki mingi sana, lakini hata hivyo namshukuru Mungu niliingia salama na nimetoka salama pia.”
Anasema kuwa jambo linaloendelea kusalia kichwani mwake ni kuwa mazingira yaliyomsukuma kuingia jeshini ndiyo hayohayo yaliyomponza wakati akiwa jeshini.
Pamoja na ufahari mkubwa alionao wa kuondosha uhai wa aliyekuwa adui mkubwa wa Marekani, Osama bin Laden lakini anasema kuwa alijikuta akitengana na mkeo kutokana kile alichokieleza kuwa uhusiano wa mbali uliosababishwa na asili ya kazi yake.
Kwa upande mwingine anasema kuwa, “Jambo jingine linaloendelea kunivunja moyo ni kupuuzwa na Serikali. Unajua wakati mwingine hizi kazi hazina shukrani kabisa. Hebu fikiria mie ndiye niliyekuwa mstari wa mbele na kufanikisha kumuua yule gaidi nambari moja, lakini sijawahi kupewa nishani yoyote ama barua ya shukrani… nadhani hilo ndilo ninaloniumiza sana moyo.”
Anasema kuwa pamoja na kwamba sheria na taratibu za uajiri zinazuia kutoa hadharani baadhi ya taarifa zinazohusu utendaji wa jeshi lakini hata hivyo amedhamiria kutunga kitabu kitachoelezea jumla ya mambo ili dunia ipate kujua .
“Nafahamu kuna baadhi ya taarifa ni classified (maalumu) hazipaswi kutolewa hadharani mpaka itakapoamuliwa ifanywe hivyo, lakini mimi na rafiki yangu tupo kwenye mpango wa kuandika kitabu ambacho nadhani kitatoa picha nzima itakayoelezea uzoefu wangu jeshini na kwa kiasi operesheni ya kusambaratisha ngome ya Osama,” alieleza.
Chanzo: Mwananchi, gazeti.

No comments:

Post a Comment