Kada wa Chadema Arnold Swai akipokea kipigo kutoka kwa makada wa chama cha mapinduzi mjini Dodoma jana baada ya kuvamia sherehe za chama hicho na kujaribu kuweka bendera ya chama chake cha chadema kwa jeuri tu.
SHEREHE za miaka 36 za kuzaliwa kwa CCM jana ziliingia dosari,
baada ya kuibuka vurugu kubwa kati ya wafuasi wa chama hicho na Chadema mkoani Dodoma wakati wakigombea
eneo na mti wa kutundika bendera za vyama vyao.
Vurugu hizo zilizotulizwa na Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU),
zilitokea jana mchana katika uwanja huo uliopo karibu na Baa ya Mwanga, baada
ya CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwepo uwanjani hapo, ili waweke bendera
zao kwa ajili ya mkutano ambao ulikuwa sehemu ya maadhimisho hayo.
Vurugu zilizuka baada ya wafuasi wa Chadema kuwataka wenzao wa
CCM waendelee na mkutano katika eneo hilo
kwa sharti la kurejeshwa kwa bendera iliyong’olewa. Wafuasi wa vyama hivyo
wakiwamo wabunge wa CCM walionekana wakivutana kunyang’anyana mti wa bendera.
“Baada ya CCM kugoma, Chadema walijaribu kurudisha bendera hiyo
kwa nguvu, jambo ambalo lilifanya wafuasi wa CCM waanze kuokota mawe na
kuwarushia wapinzani wao hao, huku Chadema nao walianza kujibu mapigo,” alisema
mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo .
Baadhi ya wabunge wa CCM walioshiriki katika vurugu hizo na
majimbo yao kwenye mabano ni Ismail Aden Rage (Tabora Mjini), Nyambari
Nyangwine (Tarime), Seleman Jafo (Kisarawe), Said Mtanda (Mchinga) na Mary
Chatanda (Viti Maalumu).
Baadhi ya wafuasi wa CCM walionekana wakibeba mawe na kuwapiga
wenzao wa Chadema na kusababisha tafrani kubwa katika eneo hilo la mkutano.
Katibu wa Chadema Wilaya ya Dodoma Mjini, Jellah Mambo alisema
kuwa tukio hilo
limetokana na wafuasi wa CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwa ikipepea eneo
la Mwanga Baa kulikofanyika sherehe za chama chao (CCM).
“Kwanza wamechukua bendera
yetu. Halafu tumeshangazwa na CCM kuruhusiwa kufanya maadhimisho yao wakati kuna agizo la
Mkuu wa Mkoa na polisi kukataza mikusanyiko ya kisiasa wakati wa Bunge.
“Kwa nini sisi (Chadema) tuzuiwe mikutano yetu wakati wenzetu
wanafanya? Huku si kutenda haki....Tulikuwa na mikutano ya kuimarisha chama
katika kata kuanzia Ijumaa, Jumamosi na Jumapili, lakini tumezuiwa na
tukaheshimu mamlaka,” alisema katibu huyo.
Pia tulikuwa tufanye mkutano na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma , lakini tukazuiwa
na tuliheshimu amri hiyo, alisema.
Mambo alisema katika vurugu hizo wafuasi wawili wa Chadema; Idd
Kizota na Anord Swai waliumizwa na kushonwa nyuzi saba usoni.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma , Ezekiel Mpuya alisema hana taarifa za
majeruhi hao.
“Ni vigumu kujua, unless (isipokuwa) wafike hospitalini
wakisindikizwa na kundi la wafuasi wenzao waliokuwa kwenye sare. Kama walikuja
kama wagonjwa wengine sio rahisi sana
kwangu kujua,” alisema Dk Mpuya.
Kumi mbaroni
Vurugu hizo zilizosababisha watu wawili kuumizwa vibaya,
zililazimisha Jeshi la Polisi kuwatia mbaroni watu kumi wanaosadikiwa kuwa
wafuasi wa Chadema
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma ,
David Misime alikiri kutokea vurugu hizo, lakini akasema bado anafanyia kazi
suala hilo .
Kamanda Misime alikiri Serikali mkoani Dodoma kuzuia mikutano ya kisiasa wakati wa
Bunge, lakini akasema kwa CCM ni tofauti kwa kuwa hizo ni sherehe zao za
kuzaliwa kwa chama.
“Ninasoma hapa magazeti yenu, mmeandika wenyewe maadhimisho ya
miaka 36. Sasa hawa wanaadhimisha hiyo miaka 36 na siyo mkutano wa
kisiasa...Tulichokataza ni maandamano, misafara ya pikipiki na kufanya mikutano
ya siasa,” alisema Misime.
Akihutubia katika mkutano huo baada ya hali kutulia mgeni rasmi,
Mbunge wa Jimbo la Tarime, Nyangwine aliwakandia wapinzani na kusema kuwa
wanachokifanya ni kuendeleza vurugu nchini na hawana sera ya maendeleo.
“Hivi jamani, hii leo hawa jamaa watasema nini? Kama suala la
barabara, leo hii unaweza kutoka Mtwara hadi Mwanza kwa baiskeli, kama maji,
michakato inafanyika, kama umeme ndiyo
usiseme, hivi wanataka nini?
“Hawa jamaa wamezoea kufanya vurugu...Si mmeona wenyewe hapa,
hawana lolote zaidi ya kufikiria vuru, wananchi msikubali kuhadaiwa,”alisema.
No comments:
Post a Comment