Thursday, February 28, 2013

Rwanda yateua Mtanzania, kuwa Waziri wa miundombinu wa nchi hiyo.


RAIS Paul Kagame wa Rwanda amemteua Mtanzania, Profesa Silas Rwakabamba kuwa Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika Jumatatu iliyopita.

Kabla ya uteuzi huo, Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda. Ni mmoja wa mawaziri wanaoingiza sura mpya katika Baraza la Rais Kagame ambalo amelifanyia mabadiliko kwa kuunda wizara nyingine mpya.

Sura nyingine mpya katika Baraza hilo ambalo liliapishwa juzi Ikulu ya Rwanda ni pamoja na Seraphine Mukantabana (Wakimbizi na Menejimenti ya Maafa) na Oda Gasinzigwa (Ofisi ya Waziri Mkuu- Familia na Jinsia).

Akizungumza kwa simu na mwandishi wetu jana, mdogo wa Profesa Rwakabamba, Timothy Rwamushaija anayeishi Dar es Salaam, alisema ndugu yake alizaliwa katika Kijiji cha Bushagara, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Alisema Profesa Rwakabamba alikuwa Mtanzania aliyeamua kuchukua uraia wa Rwanda na wote baba yao ni Mzee Titus Rwamushaija... “Huyu ni kaka yangu wa tumbo moja na kwa kweli tumefurahi sana kwa mafanikio yake sisi kama wanafamilia.”

Naibu Makamu Mkuu - Taaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Profesa Makenya Maboko alisema Profesa Rwakabamba alifanya kazi katika chuo hicho na aliondoka akiwa Mkuu wa Kitivo cha Uhandisi.

“Aliondoka wakati Kagame alipoingia madarakani na alikwenda kuongoza Taasisi ya Teknolojia ya Kigali (KIST) kabla ya kwenda katika Chuo Kikuu cha Kigali,” alisema Profesa Maboko.

Msomi huyo alikwenda Rwanda mwaka 1997, baada ya kuombwa na Rais Kagame ambaye alikwenda UDSM kuwaomba baadhi ya wahadhiri kwenda Kigali kufungua chuo kikuu katika taifa lake baada ya kumalizika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994.

Profesa Rwakabamba alikuwa Mkuu wa kwanza wa KIST na kukifanya kuwa miongoni mwa vyuo bora barani Afrika kwa masuala ya teknolojia jambo lililomfurahisha Rais Kagame.

Baada ya mafanikio hayo, Rais Kagame alimteua kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda, Butare ambako pia alijizolea sifa baada ya kusimamia vyema ujenzi wa mabweni kwa wingi na kiongozi huyo alimtunukia uraia wa nchi hiyo kama zawadi.

Hata hivyo, Profesa Rwakabamba atakuwa amelazimika kuukana uraia wa Tanzania kwa kuwa katiba ya nchi hairuhusu uraia wa nchi mbili.
Profesa Rwakabamba alipata elimu ya msingi huko Muleba na akajiunga na Shule ya Sekondari ya Ihungo.

Baada ya hapo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza na kupata Shahada ya Uhandisi mwaka 1971 na 1975 alipata Shahada ya Uzamivu katika fani hiyohiyo.
Alirejea Tanzania na kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Kitivo cha Uhandisi ambacho kilikuwa kimeanza mwaka huo.
Alipata nafasi mbalimbali katika muda mfupi aliokuwa hapo hadi alipotunukiwa kuwa Profesa mwaka 1981.

Mwaka 1985, Profesa Rwakabamba aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mwanzilishi wa Mafunzo katika Kituo cha Afrika cha Uhandisi Ubunifu na Uzalishaji (ARCEDEM), kinachodhaminiwa na Umoja wa Mataifa (UN) kilichopo Nigeria. Baada ya kazi hiyo, ndipo alipokwenda Kigali.

Tangu 1975, Profesa Rwakabamba amekuwa mjumbe wa bodi mbalimbali kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na kuwa Bodi ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) na pia Kiongozi Mwandamizi wa Muungano wa Vyuo vya Kimataifa (IAUP).
 Chanzo: Mwananchi.

No comments:

Post a Comment