Thursday, February 7, 2013

Rais Kikwete aahidi vitambulisho kabla ya mwaa 2015

 Mfano wa kitambulisho cha taifa kikionyesha picha ya Rais Kikwete na taarifa zilizokuwemo katika vutambulisho vyote kwa wananchi wa Tanzania.

Rais Kikwete akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa vitambulisho vya Taifa leo asubuhi katika viwanja vya Karemjee jiji Dar es Salaam. Wengine katika picha ni kutoka kusoto Dickson Mwaimu mkurugenzi mkuu wa NIDA, wa pili baada ya Rais ni waziri wa mambo ya ndani Dk Emmanuel Nchimbi na wa mwisho ni mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Said Mecky Saddick.


Na Hafidh kido

Rais Jakaya Kikwete amesema atahakikisha mpaka mwaka 2015 watanzania wote wanapata vitambulisho vya utaifa kwani vitambulisho hivyo vitatumika katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015.

Akizungumza katika uzinduzi wa kutoa vitambulisho hivyo leo katika viwanja vya Karemjeekwa Rais Kikwete alisisitiza zoezi hilo haliwezi kushindikana kwa hali yoyote na atakuwa tayari kutumia kiasi chochote cha pesa kuhakikisha mpaka anaondoka madarakani zoezi hilo liwe limekamilika kwa asilimia 100.

“Hii ni ndoto ya Serikali tangu uhuru, yakaja mapinduzi matukufu na hata muungano, tumekumbana na changamoto nyingi sana ikiwemo fedha na wakati wa kipindi cha mzee Mkapa Serikali ilifikishwa mahakamani lakini hatimae leo tumefanikiwa.

“Kwa kuanzia tutaanza na wakaazi wa Dar es Salaam, Zanzibar na Kilombero, nitahakikisha mpaka mwaka 2015 watanzania wote wamepata vitambulisho hivi maana tunategemea tutavitumia katika uchaguzi ujao. Na pia niwaase viongozi wa serikali za mitaa watoe taarifa sahihi ili kuepuka kuwapa vitambulisho watu wasiosatahiki,” alisema  Kikwete.

Aidha alibainisha kuwa makosa yanayofanyika katika kupata pasi za kusafiria yasitokee katika vitambulisho kwani vitambulisho hivi vitatumika katika shughuli nyingi hivyo wakipewa watu wasiostahiki taifa litakuwa matatani.

Mbali ya hivyo siku ya leo ambayo ndiyo imezindua rasmi zoezi hilo walianza kupewa viongozi wa juu wa Serikali na wawakilishi wa wananchi kutoka Zanzibar, Kilombero na wilaya za Dar es Salaam.

Akizungumza awali waziri wa mambo ya ndani ambae ndie anaesimamia mchakato huo Dk Emmanuel Nchimbi alisema zoezi hili litakapokamilika Serikali itapata nafuu katika shughuli zake za kila siku kwani vitambulisho hivi vitatumika katika masuala ya simu, taarifa za kiusalama, utumishi na mishahara, taasisi za fedha kama benki, udahili wa wanafunzi vyuoni, na shughuli nyingine za kiofisi.

“Zoezi hili litakapokamilika vitambulisho vitatumika katika shughuli nyingi za kiofisi, lakini bado tuna changamoto moja ya fedha kwani tulitakiwa kutumia mashine elfu 5 za kuweka alama za vidole katika vituo vyote nchi nzima, lakini kutokana na kutaka kulikamilisha zoezi hili mapema tunahitajika kuongeza mashine zifikie elfu 12,” alisema Dk Nchimbi.

Katika hatua nyingine mkurugenzi wa vitambulisho vya taifa Dickson Mwaimu amesema kutokana na upungufu wa vifaa na rasilimali watu wameamua kushirikiana na tume ya uchaguzi ili waweze kuendesha zoezi hilo kwa ufanisi na haraka ili kuhakikisha ikifika mwaka wa uchaguzi kila mtanzania awe na kitambulisho cha taifa.

Aidha watanzania wa mwanzo kupata vitambulisho hivyo ni kama wafuatao: Jakaya Kikwete, Salma Kikwete, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Amani Karume, Maalim Seif Sharif Hamad, Kingunge Ngombare Mwiru, Dk Didas Masaburi (meya wa jiji), Fatma Karume (mke wa Rais wa kwanza wa Zanzibar), Meck Sadick (mkuu wa mkoa Dar es Salaam).

Wengine ni Anna Mkapa (mke wa rais wa awamu ya tatu), Dr Salim Mohammed Salim, Joseph Sinde Warioba, Easter Sumaye (mke wa waziri mkuu wa zamani), Prof Ibrahim Lipumba (mwenyekiti CUF), Reginald Mengi, Dr Ramadhan Dau, Erick mkurugenzi (PPF), Avod Menda (mwakilishi Tango), Mkwizu, Absalom Kibanda, Freeman Mbowe (mwenyekiti chadema) na Daniel Lymo.

Wengine waliopewa vitambulisho vyao leo ni mkuu wa majeshi Davis Mwamunyange, IGP Said Mwema, mkuu wa usalama wa taifa Othman Rashid, na msaidizi wake ndugu Zoka, CGP Minja, CGfire Nyambacha, Alex Mwalasusa (askof), Seidf din Jamal (sheikh wa mabohora), Mussa Alhad Salum (sheikh wa mkoa), mwengine ni mwakilishi wa walemavu Lupi Mwaisako na Mbaraka Abdul Wakil.

Hata hivyo wawakilishi kutoka Dar es Salaam, Zanzibar na kilombero walikuwa ni, John Mbega (ilala), Amina Rashid (Temeke), Gaudience Mfute (Temeke), Shaaban Kisano (kinondoni), Moses Msangi (kinondoni), Mohammed Kipaka (Kilombero)Mourice August (kilombero), Ally Said Issa (znz), Ally Ahmada Ally (znz), Juma Khatib Chum (znz), Mohammed Ally Hamad (znz), Fatma Ally Abdallah (znz)

Zoezi la kupata vitambulisho vya utaifa lilianza miaka sita baada ya Tanzania kupata uhuru mwaka 1962, likaendelea mpaka kipindi cha awamu ya tatu lakini kutokana na changamoto kubwa ikiwa ni ukosefu wa fedha na utaalamu zoezi hilo limekuwa gumu mpaka Rais Kikwete alipoamua kuuanzisha tena January 7, 2008.

Vitambulisho vya utaifa vitatolewa kwa watanzania, wageni wanaoishi kwa njia za halali na wakimbizi waliopewa hifandhi katika mipaka ya nchi.

Utaratibu utakaotumika kwa watanzania ni kuwasilisha vyeti vya kuzaliwa na kuweka alama za vidole ili kupata vitambulisho hivyo. Kwa wale ambao hawana nyaraka hizo itabidi wahakikiwe na viongozi wa serikali za mitaa na vijiji kujua uhalali wao katika maeneo wanayotoka.

HAFIDH KIDO
Dar es Salaam, Tanzania
6/02/2013

No comments:

Post a Comment