Ndugu Wanahabari,
Nimelazimika nizungumze nanyi
kuhusu tukio la kuuwawa kwa Padre Evaristi Mushi wa Kanisa Katoliki Zanzibar
lililotokea leo asubuhi tarehe 17 Februari, 2013 eneo la Mtoni mkoa wa Mjini
Magharibi, ambapo watu wasiofahamika walimpiga risasi Padre huyo alipokuwa
anaenda kusalisha ibada katika kanisa la Betras. Baada ya tukio hilo kutokea
alikimbizwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja, ambapo baadae alifariki dunia.
Tukio hili ni baya na la kusikitisha.
2 Kufuatia kutokea kwa
tukio hilo na kujirudiarudia kwa vitendo vya kuwashambulia na kuwadhuru
viongozi wa dini na uchomaji wa nyumba za ibada, Jeshi la Polisi kwa
kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama tumeanza uchunguzi wa kina
wa kuwatafuta wanaohusika na matukio hayo.
3Hivyo, nimetuma timu ya
wataalam waliobobea kwenye masuala ya upelelezi na oparesheni kutoka Makao
Makuu ya Polisi, kwenda kushirikiana na timu ya wataalam iliyoko Zanzibar . Hadi sasa watu
watatu wananshikiliwa kwa mahojiano.
Jeshi la Polisi
limeimarisha doria maeneo yote hapa nchini na tunafuatilia mienendo na
kuakamata watu wote wanaochochea, kufadhili, kuhamasisha na kushiriki katika
vitendo vya uhalifu, vurugu na fujo.
Tukiwa katika kipindi
hiki, nawaomba wananchi wote hapa nchini kuwa watulivu wakati suala hili
linaposhughulikiwa kuhakikisha kwamba wahalifu hao wanakamatwa na sheria
inachukua mkondo wake.
Naomba nitumie fursa hii
pia, kuwasiliana na wananchi wenzangu wenye taarifa zitakazosaidia wahalifu hao
kukamatwa kutupa ushirikiano kupitia namba zetu maalum za simu zifuatazo
0754785557 au 0782417247 na namba za makamanda wa mikoa na vikosi, ili
kuhakikisha kwamba amani, usalama na utulivu vinadumishwa hapa nchini.
Nawashukuru
wananchi wote ambao wamekuwa wakitupa ushirikiano.
No comments:
Post a Comment