William Zelothe Stepehen ni Mtanzania
wa Kwanza Mmaasai aliyepewa ithibati ya
kuiongoza ndege aina ya Airbus A319 punde tu baada ya kupokea mafunzo ya
urubani yaliyodhaminiwa na shirika la ndege la fastjet. Alipata mafunzo hayo
nchini Uingereza kwa muda wa takriban miezi miwili na amerudi nchini Tanzania hivi
karibuni. William alikulia Olosipe jijini Arusha ambapo ni nyumbani kwa wazazi
wake.
William anafananisha
anavyojihisi anapoiongoza ndege ya Airbus A319, na wakati akiwa katika nyumba
nzuri ya kifahari na ya kisasa; anaielezea ndege ya Airbus A319 kama ndege iliyo imara na ambayo imewekewa mifumo mingi
ya usalama. Kwa maneno yake mwenyewe, anasema “Ndege ya Airbus inakulinda kweli
kweli, kama unaifahamu vyema”
William amewahi kusomea
usimamizi wa wanyama pori ; alipata mafunzo ya
urubani kwa mara ya kwanza kule Florida
Aviation Academy
nchini Marekani mwaka 2006 ambapo alipata leseni yake ya usafirishaji kwa
ndege. Ingawa ana umri mdogo, ana uzoefu wa masaa 3,053 ya kuongoza ndege.
Kumwajiri rubani huyu
mtanzania mwenye miaka 28, ni mojawapo ya jitihada za fastjet za kuhakikisha
kuwa kampuni hiyo inaajiri watendaji wazawa waliobobea katika fani hiyo hapa
nchini. Mikakati yao ya kuajiri pia ni mojawapo
ya wajibu wao mpana wa kuwekeza nchini Tanzania . Kwa kila rubani
aliyepokea mafunzo, fastjet imetumia gharama inayokadiriwa shilingi 49,546,400
hela za kitanzania ambayo ni sawa na 31,027 dola za kimarekani.
fastjet ni shirika jipya
la ndege la nauli nafuu Afrika ambalo lilipata umiliki wa FLY540 na kwa mantiki
hiyo likazindua kampuni ya kwanza ya usafiri wa ndege ambalo linazingatia
bajeti. Fastjet, ambayo inaungwa mkono na mwanzilishi wa Lonrho na easyGroup Bwana
Stelios Haji Ioannou, imetambulisha nauli za kiwango cha chini hadi kiasi cha
Tsh32,000 bila kujumlisha kodi ili kuwawezesha mamilioni ya watu
ambao walikuwa wameshindwa kusafiri kwa ndege, kuweza kusafiria ndege kwa mara
ya kwanza na kuendelea kutumia ndege mara kwa mara. Tangu kuzinduliwa kwake
mwezi Novemba 2012, shirika hili la fastjet limewasafirisha zaidi ya watu
70,000 na asilimia 99.7 ya safari za ndege zikisafiri katika muda uliopangwa.
No comments:
Post a Comment