Wednesday, February 6, 2013

Nigeria imetinga fainali ya AFCON kwa mara ya saba leo usiku baada ya kuilaza Mali 4-1 nchini afrika kusini.


Timu ya Nigeria imefanikiwa kufuzu kuingia fainali katika michuano ya soka mataifa Afrika baada ya kuichabanga timu ya Mali mabao 4-1 nchini Afrika Kusini usiku huu.

Nigeria inaingia katika fainali za michuano hiyo kwa mara ya saba tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo mwaka 1957 nchini Sudan.

Katika mara sita walizofanikiwa kutinga fainali timu ya Nigeria imetwaa kikombe cha Afrika mara tatu na kushindwa mara tatu.

Itakumbukwa Nigeria walichukua kikombe hicho mwaka 1980 katika uwanja wa nyumbani Lagos kwa kuichapa Algeria mabao 3-0 katika fainali iliyotawaliwa na mchezaji wa Nigeri Segun Odegbami kufunga mabao yote matatu, na kuwa washindi wa kombe hilo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake.

Mwaka 1994 Nigeria ilitinga fainali na Zambia waliokuwa na msiba wa kupoteza takriban kikosi kizima katika ajali ya ndege nchini Gabon miezi michache kabla ya kushiriki michuano hiyo. Lakini Nigeria haikuwaonea huruma baada ya kuwatundika goli 2-1 katika fainali ambapo magoli yote mawili ya Nigeria yaliingizwa kimiani na Emmanuel Amunike aliekuwa akiwika sana kwa miaka hiyo.

Mara ya tatu Nigeria kutwaa kombe hilo linaloheshimika Afrika ni mwaka 2000, ambapo waliichapa Cameroon kwa mikwaju ya penalt 4-3 baada ya suluhu ya 2-2 katika dakika za kawaida na nyongeza.

Katika mwaka 1984 Nigeria walipokonywa tonge mdomoni na  Cameroon kwa kuchapwa mabao 3-1 kwenye fainali iliyokuwa na mvuto kwani kwa kipindi hicho timu zote zilikuwa na wachezaji waliokuwa wakiwika barani Ulaya.

Vichwa vigumu Nigeria walizidi kujaribu bahati yao kwa kutinga fainali mwaka 1988 wakakutana na wabishi Cameroon ambapo ndoto za Nigeria zilizimwa na mcheaji wa Cameroon Emmanuel Kunde aliefunga penalt pekee hivyo Nigeria kulala 1-0 mjini Casablanca.


Kwa kudhihirisha Nigeria walikuwa wazuri kwa miaka hiyo mnamo mwaka 1990 walitinga fainali lakini walitoka uwanjani vichwa chini baada ya kuaibishwa na Algeria kwa mabao 5-1.

Haya sasa mwaka huu Nigeria wataingia fainali na nani? Burkina Faso ama Ghana… tusubiri.

HAFIDH KIDO
0713593894
Dar es Salaam, Tanzania


No comments:

Post a Comment