Kidojembe hapa nikiwa na mkuu wa Wilaya ya Handeni Muhingo Rweyemamu mwishoni mwa mwaka jana nilipokwenda kujionea hali halisi ya tatizo la ndoa za utotoni Wilayani humo na kuipa nguvu kampeni ya niache nisome iliyoanzishwa na ndugu Muhingo.
MSICHANA wa jamii ya wafugaji wa Wamang’ati anayesoma kidato cha
pili Sekondari ya Tongani, Kata ya Mkaramo, wilayani Pangani, Mkoa wa Tanga,
ametoroka kwao na kukimbilia kwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, kuomba msaada
kukwepa kufungishwa ndoa kwa nguvu.
Agnes Mhina (14), ambaye ni mkazi wa Mbugani Kijiji cha Mkaramo,
alilazimika kukimbia kwao kwenda kulala porini, baada ya kulazimishwa kuacha
shule ili aolewe.
Akizungumza eneo la ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Handeni jana,
Mhina alisema tukio hilo
lilitokea Ijumaa kijijini hapo.
Alisema aliamua kuchukua uamuzi huo mgumu na wa kushangaza,
baada ya kuona akifikisha suala hilo
serikalini wilayani ambayo amesikia ina mradi wa kukomboa wasichana, atasaidiwa
ili amalize masomo yake.
“Naishi kwa babu yangu, alitaka kuniozesha mwanaume ambaye wala
sijawahi kumuona, lakini nadhani naye ni Mang’ati. Alitaka niache shule ili
niolewe, nikamkatalia kwa vile nataka nisome, alivyoona vile alitaka kunipiga,”
alisema Mhina na kuongeza:
“Nilivyoona anataka kunipiga nikakimbilia porini kujificha tangu
saa 5:00 asubuhi hadi saa 10:00 usiku, nikapanda gari ya kwenda Mkata,
nilipofika huko nikapata gari nyingine iliyonifikisha kwa Mkuu wa Wilaya. Lengo
langu ni kuomba msaada serikali inisaidie nisome au ikibidi niweze kufika kwa ndugu
zangu Dodoma
ili nisome.”
Binti huyo ambaye ni mmoja kati ya watoto wanne wa familia yao , ndiye pekee msomi.
Alisema babu yake alihamia katika eneo hilo
tangu mwaka 2006, akitokea mkoani Dodoma ,
akiwa na mifugo yake kwa nia ya kutafuta malisho.
“Sijui mwenyewe alitaka kupewa mahari kiasi gani, maana kuna
aina mbili ya mahari katika kabila letu. Kuna ng’ombe watatu na debe tatu za
asali, nyingine ni ng’ombe saba, labda alitaka apate mali ,” alisema Juma na kuongeza:
“Pia, huku nimesikia serikali inawasaidia wasichana ili wasome
kwa kuvunja ndoa za wanafunzi.”
Akizungumzia tukio hilo ,
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu alisema anaona faraja kubwa na
mafanikio makubwa kwa Mradi wa ‘Niache Nisome’.
Mradi huo ulianzishwa kumkomboa mtoto wa kike katika mimba na
ndoa za utotoni wilayani hapa.
“Huyu mtoto amenishangaza sana ,
ameonyesha ujasiri wa ajabu kwenda kulala porini ni jambo la ujasiri wa hali ya
juu. Pia, nimeshangaa kwa mabinti sasa kutambua kwamba Serikali yao inawajali katika elimu kwa kuwatetea ili wafikie
malengo yao ,”
alisema Rweyemamu.
Chanzo: Mwananchi.
No comments:
Post a Comment