Friday, February 22, 2013

Angalia habari picha ziara ya Rais Mwai Kibaki nchini Tanzania.

 Rais Mwai Kibaki wa Kenya akiwa na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete wakati wa uzinduzi wa barabara ya Mwai Kibaki ambayo awali ilikuwa ikiitwa Old Bagamoyo jana asubuhi jijini Dar es Salaam.

 
Rais wa Kenya, Mwai Kibaki (kushoto) akimsalimia Mkuu wa Jeshi la Magareza nchini, Kamishna Jenerali John Minja kabla ya kuingia ndani ya Kiwanda cha Magereza Ukonga, jijini Dar es Salaam. Wa pili kutoka kushoto ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, anayefuata ni Naibu Waziri wa wizara hiyo, Pereira Ame Silima.

 

 
Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna Jeneral John Minja (kushoto) akimkabidhi zawadi maalum ya kiti Rais Mwai Kibaki wa Kenya.

 

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete na mgeni wake Rais Mwai Kibaki wa Kenya aliyehitimisha ziara yake ya nchini Februari 21, 2013 ziara yake ya Kiserikali nchini, wakisiliza taarifa ya pamoja ikisomwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe Bernard Membe katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam


Rais Jakaya Mrisho Kikwete na mgeni wake Rais Mwai Kibaki wa Kenya alipohitimisha ziara yake ya Kiserikali nchini wakisimama kupokea heshima wakati nyimbo za taifa zikipigwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam jana.

RAIS Mwai Kibaki wa Kenya, amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutambua kuwa zinakabiliwa na changamoto za kuwaletea wananchi wake maendeleo na zinapaswa kuweka mikakati ya dhati kukabiliana na hali hiyo ikiwemo uimarishwaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Alisema matumizi ya Kiswahili yataziwezesha nchi wanachama kuwa na agenda ya pamoja, hatua ambayo itasaidia kusukuma mbele shughuli za ukuzaji uchumi na kuharakisha maendeleo.
Rais Kibaki ambaye alikuwa akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam kama sehemu ya kuwaaga wananchi wa Tanzania kabla ya nchi yake kufanya Uchaguzi Mkuu mwanzoni mwa mwezi ujao, alisema Kiswahili kinaendelea kukua duniani kote.

Aliwasihi Watanzania kukienzi Kiswahili na nawaomba wazunguke nchi za Afrika kusaidia pale wanapokwama.

Alisema kuwa lugha ya Kiswahili licha ya kuzungumzwa kwa ufasaha katika nchi za Afrika Mashariki, pia imekaribishwa kama lugha rasmi katika nchi za Rwanda na Burundi ambazo zilijiunga katika Jumuiya ya Afrika Mashariki katika miaka ya hivi karibuni.

Alieleza kuwa, amepata taarifa lugha hii pia inazungumzwa pia katika maeneo ya mbali ikiwemo nchini Afrika Kusini ambapo baadhi ya viongozi waliopambana na ubaguzi wa rangi walitumia muda mwingi nchini Tanzania kupanga mikakati ya kukabiliana na siasa za ubaguzi wa rangi.
Awali Rais huyo alifungua rasmi barabara ambayo ilikuwa ikijulikana kama Old Bagamaoyo ambayo sasa imepewa jina lake.

“Naishukuru Tanzania kwa kuifanya barabara hii kama ‘Mwai Kibaki Road’, nimepokea kwa furaha uamuzi huu. Watanzania nasi kule kwetu tutaandaa utaratibu ili tuweke majina mazuri ya nchi hii”.

Kuhusu uchaguzi wa Kenya uliopangwa kufanyika Machi 4, mwaka huu, Rais Mwai Kibaki na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete walitoa wito kwa mataifa ya Magharibi kutoingilia uchaguzi huo wakieleza kuwa wananchi wa Kenya ndiyo wenye uamuzi wa mwisho kuhusu taifa lao.

No comments:

Post a Comment