Monday, February 18, 2013

Tayari ndoto yangu ya kutembea Tanzania nzima inaanza kukaribia kutimia.


 Mkoa wa Geita huu, tumeuacha mji wa Geita sasa tunautafuta mji wa Katoro palipotokea vurugu juzi.

 Hapa ndipo Katoro, waislam na Wakristo walichinjana sababu ni nani ana ruhusa ya kuchinja wanyama.

 Njiani tukiuacha mji Geita tunautafuta mkoa wa Kagera, tulisimama kuchimba dawa. Nikaamua nijifotoe.                                                      Sidhani kama hii picha inahitaji maelezo.

Juzi nilisema nitazungumzia ziara yangu ya kanda ya ziwa niliyoifanya wiki iliyopita. Ziara hiyo ilinisaidia kukamilisha mkoa mmoja wa Mwanza ambao nilikuwa nikiutamani sana kuutembelea katika kanda ya ziwa.

Mpaka sasa nimeshatembea nusu ya Tanzania, kanda zote nimefika kasoro kanda ya kusini na nyanda za juu kusini. Hii inanipa faraja sana katika utanzania wangu, mara nyingi nikiwa njiani huwa naimba kimoyomoyo ule wimbo wa Tazama Ramani utaona nchi nzuri, yenye mito na mabonde mengi ya nafaka, nchi hiyo mashuhuri natamka Tanzania.

Awali Tanzania ilikuwa na mikoa 21 ukiondoa Unguja na Pemba. Ila sasa baada ya kuongezwa mikoa minne Tanzania bara sasa ina mikoa 25, na katikia mikoa hiyo 25 tayari nimefikisha nusu bado nusu.

Mikoa ambayo nimeshaitembelea ni Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Dodoma, Singida, Tabora, Mwanza, Arusha, Shinyanga, Morogoro, Kilimanjaro,Geita, Kagera, na Manyara.

Na mikoa ambayo bado sijakanyaga ni Mbeya, Iringa, Kigoma, Lindi, Ruvuma, Mtwara, Rukwa, Mara, Katavi, Njombe na Simiyu.

MIKOA MIPYA ILIYOANZISHWA  NI:
(i)  Mkoa wa Njombe, ambao unatokana na kumega na kuunganisha
Wilaya za Njombe, Ludewa na Makete kutoka Mkoa wa Iringa.
Mkoa huu utakuwa na Wilaya mpya ya Wanging’ombe ambayo
inatokana na kugawanywa kwa Wilaya ya Njombe.

(ii)  Mkoa wa Geita,  ambao unatokana na kumega na kuunganisha
Wilaya za Geita kutoka Mkoa wa Mwanza, Bukombe kutoka Mkoa
wa Shinyanga na Chato kutoka Mkoa wa Kagera. Mkoa huu
utakuwa na Wilaya mpya ya Nyang’hwale ambayo inatokana na
kugawanywa kwa Wilaya ya Geita.

(iii)  Mkoa wa Simiyu,  ambao unatokana na kumega na kuunganisha
Wilaya za Bariadi kutoka Mkoa wa Shinyanga, Maswa kutoka Mkoa
wa Shinyanga, Meatu kutoka Mkoa wa Shinyanga na Wilaya mpya
ya Busega kutoka Mkoa wa Mwanza. Mkoa huu utakuwa na Wilaya
nyingine mpya ya Itilima ambayo inatokana na kugawanywa kwa
Wilaya ya Bariadi.

(iv)  Mkoa wa Katavi,  ambao unatokana na kumega na kuunganisha
Wilaya za Mpanda kutoka Mkoa  wa Rukwa pamoja na Wilaya
mpya ya Mlele ambayo inatokana na kugawanywa kwa Wilaya ya
Mpanda.

MADHUMUNI YA KUANZISHWA MIKOA MIPYA
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza kuwa, kwa ajili ya
utekelezaji bora wa shughuli za Serikali, Mheshimiwa Rais anaweza kuigawa
Nchi katika Mikoa au Wilaya. Hivyo, madhumuni ya kuanzishwa kwa Mikoa hiyo
ni kuboresha utendaji wa  Serikali Kuu kwa kupunguza  ukubwa wa maeneo ya
Mikoa mama ili Wananchi wapate huduma za kiutawala ngazi ya Mikoa kwa
karibu.
Jumla ya Mikoa ya Tanzania Bara itakuwa  25  ambayo ni Arusha, Dar Es
Salaam, Dodoma, Iringa, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mara,
Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza,  Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga,
Singida, Tabora, Tanga, Njombe, Geita, Simiyu na Katavi.

HAFIDH KIDO
0713 593894
18 Feb, 2013-02-18
Dar es Salaam, Tanzania

No comments:

Post a Comment