Maafisa wa utawala nchini New
Zealand , wamemwambia mwanamume mmoja raia wa Afrika Kusini ambaye pia ni
mpishi kuwa ni mnene kupita kiasi kuweza kuruhusiwa kuishi nchini humo.
Maafisa wa uhamiaji walisema kuwa
Albert Buitenhuis, mwenye uzani wa kilo 130 hana afya nzuri.
Sasa anakabiliwa na tisho la
kufukuzwa kutoka nchini humo licha ya kupunguza uzani wake kwa kilo 30 tangu
kuhamia mjini Christchurch miaka sita iliyopita.
New Zealand ni mojawapo ya nchi
zenye idadi kubwa ya watu wenye unene kupita kiasi huku takriban asilimia 30 ya
watu wake wakiwa waathiriwa.
Bwana Buitenhuis na mkewe walihamia
nchini New Zealand, mwaka 2007. Wakati huo mwanamume huyo alikuwa na uzani wa
kilo 160.
Hadi sasa wamekuwa wakipokea Viza
zao zinazowaruhusu kufanya kazi nchini humo bila matatizo mengi kulingana na
mkewe.
''Tumekuwa tukiomba viza hizo kila
mwaka na hapajawahi kuwa na matatizo yoyote, '' alisema mkewe Albert
"hawajawahi kuzungumzia uzito
wa Albert wala afya yake wakati hata alipokuwa mnene kushinda sasa.''
Lakini mapema mwezi Mei, wanandoa
hao waliambiwa kuwa hawatapokea visa mpya kwa sababu ya unene wa bwana
Buitenhuis.
"nimeshangazwa sana kwa sababu
kwa sasa ameweza kupoteza kilo 30 tangu tuje hapa New Zealand, '' alisema mkewe
Buitenhuis.
Wawili hao wamemuomba waziri wa
uhamiaji wa nchi hiyo kuwaruhusu waendelee kuishi nchini humo kwani bwana
Buitenhuis ameweza kupoteza kilo.
Msemaji wa uhamiaji alisema kuwa
bwana Buitenhuis alinyimwa visa mpya kwa sababu ya tisho kwa afya yake kutokana
na uzani wake, kuwa anaweza kupatwa na kisiukari, shinikizo la damu na maradhi
ya moyo.
BBC SWAHILI