Thursday, July 4, 2013

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii yafungua kampeni ya wasemaji wa Wizara na wanahabari itakayodumu kwa wiki mbili.

 Afisa kutoka idara ya habari Maelezo bi Zamaradi (aliyesimama) akimtambulisha msemaji wa Wizara ya Afya Nsachris Mwamwaja (katikati) na kulia kwa Mwamwaja ni msemaji msaidizi wa wizara ya afya na ustawi wa jamii Catherine Sungura.

 Wanahabari wakifuatilia kwa makini ufunguzi wa mkutano wa wanahabari na wasemaji wa wizara nchini uliofanyika Idara ya habari Maelezo jijini Dar es Salaam leo ambapo mikutano hiyo itaendelea kwa muda wa wiki mbili mfululizo.

 Msemaji wa wizara ya afya na ustawi wa jamii Nsachris Mwamwaji akisikiliza kwa makini swali la mwanahabari (hayupo pichani) wakati wa kipindi cha maswali na majibu.

 Mwamwaja akifafanua jambo wakati wa mkutano na wanahabari leo, kulia ni msaidizi wake Catherine Sungura.

 Wanahabari wakihakikisha hawapitwi na neno hata moja wakati msemaji wa wizara ya afya akitoa ufafanuzi.

 Msemaji wa mamlaka ya chakula na dawa nchini TFDA, Gaudencia Simwanza akitoa ufafanuzi juu ya maabara ya mamlaka hayo, kuli ni Salum Kindoli ofisa mwandamizi uchunguzi wa maabara katika mamlaka hayo.

 Gaudencia Simwanza akifafanua jambo kwa umakini mbele ya wanahabari kwenye ukumbi wa MAELEZO.



Ofisa mwandamizi wa uchungizi maabara ya TFDA, Salum Kindoli akifafanua kitu mbele ya wanahabari.
 
Leo Serikali imeanza kampeni yake ya kuhakkisha wasemaji wa wizara wanazungumza na wanahabari kuelezea mafanikio na malengo ya wizara zao kwa mwaka wa fedha uliopita na unaoanza sasa.
Leo ilianza wizara ya afya na ustawi wa jamii ambapo msemaji wa wizara hiyo Nsachris Mwamaja alieleza jitihada za wizara yake katika kuimarisha huduma za afya kwa kuongeza watumishi kada za afya nchini.
Wakati Mwamwaja akizungumzia mpango wa maendeleo ya afya ya msingi (MMAM 2007-2017) alisema “Rasilimali watu, ujenzi na ukarabati wa vituo vya huduma, huduma za afya wilayani, afya ya uzazi, mama na mtoto, mapambano dhidi ya magonjwa, lishe, magonjwa yasiyopewa kipaumbele, huduma za ustawi pamoja na manunuzi ya dawa, vifaa, vifaa tiba na utendanishi, ni moja ya mkakati wa MMAM.”
Katika hatua nyingine Mwamwaja alieleza namna wizara itakavyoshughulikia tatizo la ajira kwa madaktari na wauguzi na kuweka wazi kuwa wizara inao mpango wa kuongeza watumishi wa kada mbalimbali za afya nchini kwa kuwapangia wataalamu wapya wanaotoka vyuoni sasa.
“Wizara katika mwaka wa fedha 2012/13 ilipata kibali cha kuwapangia vituo vya kazi wataalamu wa afya 8,869 kwa ajili ya mamlaka mbalimbali za ajira ikijumuisha Halmashauri, tawala za Mikoa, Hospitali za mashirika ya kujitolea, Wizara, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisis ya saratani Ocean Road, Hospitali ya Rufaa Bugando na CCBRT,” alisema.
Wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari msemaji huyo wa wizara ya afya na ustawi wa jamii aliweka wazi kuwa kwa sasa wizara inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa wataalamu wa afya kwa asilimia 47, hivyo wapo katika harakati za kuhakikisha vyuo vyote vinane vilivyoidhinishwa na Serikali kutoa wataalamu hao vinafanya hivyo kwa wakati na kuwapa ajira wahitimu mara wamalizapo mazoezi ili kuziba pengo hilo.
Nayo mamlaka ya chakula na dawa nchini (TFDA) ambao walihudhuria ufunguzi huo wa wazsemaji wa wizara walitoa mikakati yao hasa ikizingatiwa wapo chini ya wizara ya afya na ustawi wa jamii hivyo walikuwa na nafasi ya kutosha kutumia mwanya huo kuelezea majukumu yao.
Msemaji wa TFDA Bi Gaudencia Simwanza, aliwaeleza wanahabari kuwa taasisis hiyo ilianzishwa mwaka 2003 chini ya sheria namba 1 ya chakula, dawa na vipodozi sura 219 kwa  lengo la kudhibiti ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya za wananchi.
“Hivi sasa TFDA inatambuliwa kwa kufanya kazi kulingana na viwango vya kimataifa vya ISO 9001: 2008. Na maabara ya TFDA iliwahi kufanyiwa ukaguzi na shirika la afya duniani WHO mwezi Mei 2005 na Septemba 2010 hivyo ikakidhi viwango na kutambuliwa rasmi na shirika hilo tarehe 18 Januari 2011, maana yake TFDA inatambulika kimataifa,” alsiema Gaudencia.
Mbali ya shughuli za kupicha chakula, dawa na vipodozi TFDA inakabiliwa na wafanyabiashara wa vipodozi feki ambavyo vinaharibu miili ya watumiaji hasa vile vinavyoongeza sehemu nyeti za kinamama na kinababa na vile vinavyobadilisha ngozi kutoka ya asili na kuwa nyeupe,
Msemaji huyo wa TFDA alisema matumizi ya vipodozi ambavyo havijapitishwa na tasisi yake vina madhara makubwa ikiwemo kupata saratani na magonjwa mengine ya ngozi na kuzorota afya.
Kesho kutakuwepo na wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi ambapo taasisi waalikwa iytakuwa ni bodi ya mikopo ya elimu ya juu Tanzania. Mikutano yote itafanyika katika ukumbi wa idara ya habari (MAELEZO) mpaka wizara zote zitakapoisha.
HAFIDH KIDO
5 Julai, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA   

No comments:

Post a Comment