Wendawazimu wa mambo, na fujo za itikadi
Mawazo kunuka shombo, la chuki kwenye fuadi
Tofauti za majimbo, huchochea uhasidi
Hizi ndizo siasa zetu.
Wamekonda kimaumbo, weupe kwenye miundi
Kama wanywa zarambo, bongo zilivyo baridi
Badili yao makombo, mbali baidi kwa mandi
Hizi ndizo hadhi zao
Wengi hufuata mkumbo, wakitamani ushindi
Hawajui hata jambo, baraka ya ukaidi
Kutwa huimbishwa nyimbo, na kuchapishiwa kadi
Hawa ndiwo wafuasi wao
Ulimi kama ulimbo, na sura kama waridi
Wayaelezapo mambo, hudhani ni mahasidi
Wakishapata majimbo, kushukuru hawarudi
Hawa ndiwo wanasiasa
Vurugu na majigambo, kwa ulevi wa mtindi
Pesa za kunyweshwa tembo, na kuhonga makuwadi
Sera huzidiwa tambo, kuharibiwa marudi
Hizi ni chaguzi zetu
kuila rushwa ndo mambo, na kununua vikundi
kujivimbisha vitumbo, na kuua makusudi
kama ifumwapo bambo,
na mchele haurudi
hao diwo viongozi wetu
HAFIDH KIDO (TOTO LA BAKUNGWI)
TANGA, NGAMIANI
ST. 6
No comments:
Post a Comment