Friday, July 12, 2013

Coastal Union U20 yatinga nusu fainali Rollingstone Cup.

Kampeni ya kuchukua ubingwa wa michuano ya Rollingstone bila kufungwa bao hata moja inazidi kukolea chumvi baada ya leo vijana wa Coastal Union wagosi wa kaya kutinga hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa 1-0 walipokutana na Dareda FC jijini Arusha katika uwanja wa General Tyre.
Bao hilo lililoingizwa kimiani kwa mkwaju wa adhabu ndogo baada ya mchungulia nyavu maarufu Ally Nassor ‘Ufudu’ kuchezewa madhambi nje kidogo ya D hivyo nahodha msaidizi Ayoub Semtawa akapiga faulo iliyoingia wavuni bila kipingamizi, hiyo ilikuwa ni dakika ya 64 kipindi cha pili.
Kipindi cha kwanza mambo yalikuwa magumu baada ya vuta nikuvute ya dakika 45 kuisha bila timu yoyote kuchungulia wavu wa mwenzake; lakini katika dakika ya 35 yuleyule bingwa wa mipira iliyokufa Ayoub Semtawa, alikosa faulo iliyogonga mwamba huku golikipa wa Dareda FC kuruka upande mwingine, wenyewe wanaita alimpeleka sokoni.
Kama kawaida yake Bakari Shime ‘Super Coach’ huwa anazitumia vema zile dakika chache za mapumziko kwa kukipanga upya kikosi chake, ndivyo alivyofanya leo baada ya kugundua ukuta wa Dareda haupitiki kwani Ally Ufudu alikumbana na zahma nyingi kila alipojaribu kuingia na mpira.
Sifa kubwa ya Ufudu ni kasi na kumiliki mpira, walichofanya mabeki wa Dareda ni kuharibu mipira anayopewa Ufudu ama kumchezea rafu mbaya, hivyo kocha Shime akampanga Semtawa awe mpigaji faulo ama penati huku akimsisitiza Ufudu kuendelea kukimbia na mipira bila kupiga mashuti ya mbali.
Ndipo ilipofika dakika ya 64 mbinu hiyo ikazaa matunda baada ya Ufudu kuchezewa madhambi hatua chache kutoka eneo la kujidai la golikipa wa Dareda. Kama kawaida Ayoub Semtawa aliutumbukiza kwa ufundi mkubwa mpira kasha Shime akawataka wachezaji wake kubadilisha mbinu wazuie au kupaki bus.
Shime aliwatumia vema mabeki wake hatari  Hamad Juma, Mwaita Saleh, Yusuf Chuma na Nzara Ndaro ambao walijipatia majina kwenye michuano hiyo iliyofanyika mwaka jana nchini Burundi na katika kombe la Uhai lililofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo katika michuano yote walifika hatua ya fainali na kutolewa kwa mikwaju ya penalt. Burundi walitolewa na Ecofoot ya Congo wakati Dar es salaam walitolewa na Azam FC ‘wana lambalamba’.
Mungu akipenda nusu fainali inachezwa kesho ambapo Coastal Union wanasubiri mshindi wa mechi namba 25 ambao ni Simba SC na JKT Oljoro, wanacheza leo asubuhi hii. Fainali itapigwa Julai 15 siku ya jumatatu.
Mungu ibariki Tanga, Mungu ibariki Coastal Union.
COASTAL UNION

No comments:

Post a Comment