Viongozi wa Friends Rangers
wakimhudumia mchezaji wao aliyefunga bao la kwanza jana, Robert Katabi
aliyeumia baada ya kufunga bao hilo jana katika mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi
ya Polisi Jamii kwenye Uwanja wa Azam Complex.
CHAMA ya Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar
es Salaam (DRFA), kimeipongeza timu ya Friends Rangers kwa kufuzu kucheza Ligi
Daraja la Kwanza msimu ujao baada ya jana Jumapili kuifunga Polisi Jamii ya
mkoani Mara mabao 3-1.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa
Julai 6 kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma, Polisi waliibuka na ushindi wa
bao 1-0.
Katika mechi ya marudiano
iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam
na kuchezeshwa na mwamuzi Hans Mabena kutoka Tanga, Rangers walipata mabao yao
kupitia kwa Robert Katabi katika dakika ya 53, Bakari Bakari dakika ya 67 na
Mick Castro dakika ya 87.
Bao la Polisi lilifungwa na Faustine
Faru katika dakika ya 68 na hivyo kuipa tiketi ya Friends Rangers kufuzu
kucheza Daraja la Kwanza kwa jumla ya mabao 3-2.
Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed
Mharizo, amesema ni faraja kwao kuona Friends Rangers imetinga Ligi Daraja la
Kwanza na kuuwakilisha vyema Mkoa wa Dar es Salaam.
“Kwa niaba ya DRFA nachukua fursa
hii kuwapongeza wachezaji, viongozi na mashabiki wa Friends Rangers kwa
uvumilivu na subra waliyokuwa nayo katika kipindi chote cha ushiriki wa Ligi ya
Mabingwa wa Mkoa, bado tupo pamoja nao katika kufanikisha timu hiyo inafanya
vizuri zaidi na hatimaye kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara,” alisema Mharizo.
Friends Rangers inaungana na Kimondo FC ya Mbeya na Stand United
ya Shinyanga kucheza Ligi Daraja la Kwanza.
Wawakilishi wengine kutoka Mkoa wa Dar es Salaam katika Ligi ya
Mabingwa wa Mikoa walikuwa Red Coast na Abajalo ambazo ziliaga michuano katika
hatua za awali.
kidojembe
No comments:
Post a Comment