Nicodemus Mushi akiwa na naibu mkurugenzi wa MAELEZO, Zamaradi Kawawa leo asubuhi.
Wanahabari wakifuatilia kwa makini maelezo ya ofisa habari na mawasiliano wa wizara ya viwanda na biashara.
Serikali imeamua kufufua viwanda vyote vilivyokufa wakati wa
kipindi cha kubinafsisha viwanda vya Serikali wakati wa awamu ya tatu ya
utawala wa Rais Benjamin Mkapa.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mendeleo ya
viwanda na biashara nchini ofisa habari na mawasiliano wa wizara ya viwanda na
biashara Tanzania, Nicodemus Mushi amesema wizara hiyo imedhamiria kuongeza
ajira na kukuza pato la taifa kupitia viwanda vya ndani.
Mushi aliweka wazi kuwa Wizara imekusudia kuifanya sekta ya
viwanda nchini kuendelea kuisaidia juhudi za Serikali katika kupambana na
tatizo la ajira nchini kwa kuajiri idadi kubwa zaidi ya watu hasa vijana wenye ujuzi
katika fani mbalimbali na kuzalisha bidhaa bora kwa kiwango kinachohitajika kwa
soko la ndani na nje ya nchi.
“Viwanda vilivyobinafsishwa chini ya sekta ya viwanda na
biashara ni 74 na kati ya hivyo ni viwanda 17 tu ndivyo havifanyi kazi. Juhudi za
kufufua viwanda hivyo zinafanyika chini ya Consolidated Holding Corporation
(CHC) iliyo chini ya wizara ya fedha, kwa kuzingatia utaratibu wa urekebishaji
wa mashirika ya umma,” alieleza Mushi.
Aidha wizara hiyo imelenga kuboresha vivutio kwa ajili ya
uwekezaji kwenye viwanda vinavyotumia malighafi mbalimbali zilizopo nchini
vikiwemo viwanda vya nguo, ngozi, usindikaji matunda, mbogamboga na usanifu wa
madini ya vito.
Katika hatua nyingine wataangalia wajasiriamali hasa wa
vijijini ili kuwaeweka katika program ya muunganisho wa ujasiriamali vijijini
kwa kutoa ushauri, mafunzo, mitaji na huduma za kiufundi kwa wajasiriamali.
“Tunawatazama wajasiriamali kama kundi maalum linalopewa
kipaumbele, lengo letu ni kuhakikisha sekta hii inaendelea kuwakomboa
watanzania kwa kuwapa ajira, kuwapa kipato na kuwaondolea umaskini. Ndiyo maana
SIDO na chuo chetu cha elimu ya biashara wapo pamoja nao wakati wote likiwapa
mafunzo, kukusanya katika vikundi na kuwapa mbinu za kupata mitaji na namna
bora ya kufanya shughuli zao kwa tija,” alieleza Mushi.
HAFIDH KIDO
10 Julai, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA
No comments:
Post a Comment