Wednesday, July 10, 2013

SOKA LA BONGO LITAOKOLEWA NA VIJANA.


Sasa imedhihirika wazi vijana wa Coastal Union wamekwenda jijini Arusha si kushiriki michuano ya soka la vijana Rollingstone Cup, bali kuchukua ubingwa wa michuano hiyo iliyoanzishwa tangu mwaka 1999 kwa kushirikisha vijana wenye umri chini ya miaka 20 na 15.
Ni baada ya kushinda mechi zote tatu za kundi A, bila kuruhusu bao hata moja kutikisa nyavu zao tangu mechi ya kwanza dhidi ya Young Life waliyoshinda 3-0, jana walicheza na JKT Oljoro wakawafunga 1-0 na leo wamehitimisha mzunguko wa kwanza ili kuingia hatua ya robo fainali kwa kuwachapa Testimony Academy 1-0.
Mfungaji wa bao la leo ni Ally Kipanga mnamo dakika ya 35 ya mchezo baada ya kupokea krosi murua kutoka kwa mshambuliaji hatari wa Coastal Union, Ally Nassor ‘Ufudu’ na kutumbukiza gozi hilo la ng’ombe kwa guu lake la kulia.
Mpaka mapumziko matokeo yaliendele kuwa 1-0 huku vijana wa Testimony Academy wakionekana kukata tamaa, katika kipindi cha pili kocha Bakari Shime, ambaye aliamua kuchezesha  kikosi cha pili na kuwapumzisha wachezaji wake hatari ili keshokutwa wacheze hatua ya robo fainali wakiwa na afya tele katika dakika 55 ya mchezo aliamua kumtoa kiungo Mohammed Issa ‘Banka’ na kumuingiza mshambuliaji Bakar Mwaita ili kujihakikishia ushindi mechi ya leo.
Baada ya Shime kuridhika na hali ya mchezo na kuona hakuna tena dalili ya kupata mabao ilipowadia dakika ya 70 aliamua kumpumzisha Ally Nassor ‘Ufudu’ na kumuingiza Suleiman Omary.
Mpaka mwamuzi anapuliza kipyenga cha mwisho kuashiria dakika 90 za kawaida zimefikia tamati ubao wa matokeo uliendelea kusomeka 1-0 maana yake Coastal Union walitimiza point 9 na kuwafanya kushika nafasi ya kwanza katika kundi A huku wakisubiri kundi B kukamilisha mechi zao leo ambapo mpaka sasa Simba SC ndiwo wanaoongoza katika kundi B wakifuatiwa na DAREDA kutoka Arusha.
Kundi B ambalo katika kundi hilo Coastal Union watacheza na mshindi wa pili siku ya Ijumaa Julai 12, lina timu zifuatazo: Simba SC, DAREDA, Future Star na CIDT.
Kikosi kilichoanza leo ni: 1. Adam mussa. 2. Mtenji Albano. 3. Mohamed Omar. 4. Halfan Mbarouk. 5. Mwaita saleh. 6.Hamis Rashid. 7.Mohamed Isa. 8. Behewa sembwana. 9. Ali kipanga. 10. Ali Nassor. 11. Ayoub semtawa.
Baadaye akatoka Mohammed Issa akaingia Bakari Mwaita, halafu akatoka Ally Ufudu na kuingia Suleiman Omary.
Mungu ibariki Tanga, Mungu ibariki Coastal Union.
Chanzo: COASTAL UNION Blog
10 Julai, 2013

No comments:

Post a Comment