Thursday, July 4, 2013

Miraa yapigwa marufuku Uingereza.


Mmea unaotumika sana na unaoaminika kulewesha, Miraa au Khat , huenda ukapigwa marufuku nchini Uingereza kinyume na ushauri uliotolewa na baraza la kuchunguza matumizi mabaya ya madawa ya kulevya AMCD.
Mwezi Januari, baraza hilo lilisema kuwa Miraa haistahili kuharamishwa kwa sababu hakuna ushahidi wa kutosha kuonyesha unaathiri afya ya watu.
Lakini waziri wa mambo ya ndani Theresa May ameamua kuupiga marufuku akisema kuwa madhara yanayotokana nao ni makubwa kuliko inavyodhaniwa.
Khat sasa itakuwa katika kikundi cha C cha madawa kama ketamine na madawa mengine ya kusisimua misuli.
Tayari imepigwa marufuku katika nchi nyingi barani Ulaya na katika nchi zengine ikiwemo Marekani na Canada.
Uamuzi wa Uingereza kuchukua hatua hiyo unazingatia zaidi usalama na masharti ya kimataifa, hasa kuwa Uingereza inaweza kutumika kama kivukio cha mmema huo kuelekea katika nchi zingine za Ulaya.
''Ikiwa tutakosa kuchukua hatua kubadilisha sheria kwa upande wa Uingereza , huenda ikatishia nchi hii kwa sababu huenda ikatumika kama kivukio,'' alisema Bi May katika taarifa yake.
Lakini wanaharakati wanasema kuwa wamekasirishwa na hatua ya serikali kukosa kutilia maanani ushauri wa baraza lilaloshughulikia maswala ya utumizi mbaya wa madawa ya kulevya.
Khat hutumiwa na jamii za wasomalia, watu kutoka Yemen na Ethiopia.
Wizara ya mambo ya ndani ilisema kuwa mmea huo unalewesha kidogo kuliko madawa mengine ingawa baraza la kudhibiti utumizi mbaya wa madawa ya kulevya ilisema kuwa haikupata ushahidi wowote kuwa mmea huo unalewesha.
Makundi ya wasomali nchini Uingereza yaliambia baraza la AMCD kuwa Miraa husababisha matatizo makubwa ya kijamii na kusema inaleta matatizo ya kiafya na kuathiri familia nyingi.
KIDOJEMBE

No comments:

Post a Comment