Rais wa TFF Leodger Chilla Tenga akifurahia jambo makao makuu ya TFF.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Leodegar Tenga amesema kikosi cha Taifa Stars sasa kina uwezo wa kushindana
katika mashindano yoyote, kwani tayari kimeiva.
Akizungumza na wachezaji wa timu hiyo kambini kwao
hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam, Rais Tenga aliwaambia kuwa kiwango
walichoonesha kwenye mechi zilizopita za mchujo za Kombe la Dunia dhidi ya
Morocco na Ivory Coast kimethibitisha hilo.
“Kiwango mlichoonyesha katika mechi hizo kila
Mtanzania anayewafuatilia amekiona, hivyo hatuna shaka kuwa mtatuwakilisha
vizuri kwenye mechi ya kesho dhidi ya Uganda,” amesema Rais Tenga na kuwataka
kupigana kwa ajili ya Tanzania.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager
kesho (Julai 13 mwaka huu) saa 9 kamili alasiri Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
itacheza na Uganda (The Cranes) katika mechi ya kwanza ya raundi ya mwisho
kuwania tiketi ya kucheza Fainali za CHAN zitakazofanyika mwakani nchini Afrika
Kusini.
Rais Tenga amesema TFF, mdhamini Kilimanjaro Premium
Lager, Kamati ya Ushindi na Watanzania kwa ujumla wanawaunga mkono kwani
wamekuwa wakiboresha kiwango chao kila wanavyozidi kucheza mechi tangu wake
chini ya Kocha Kim Poulsen, Mei mwaka jana.
Wakati huo huo, Rais Tenga ameahidi kumpatia tiketi ya
kwenda Uganda kwenye mechi ya marudiano mshabiki Wiseman Mwakyusa Luvanda
anayetembea kwa miguu kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam kushuhudia mechi ya
kesho.
“Kama ni kweli anakuja kwa kutembea, huyu ameonyesha
kiwango kikubwa cha uzalendo kwa timu ya Taifa, nitampatia tiketi ya kwenda
Kampala kuishangilia Taifa Stars kwenye mechi ya marudiano,” amesema Rais
Tenga.
…POULSEN, MICHO WATABIRI MECHI KALI
Makocha wa timu hizo Kim Poulsen wa Taifa Stars na
Sredojvic Micho wa The Cranes wamesema mechi ya kesho itakuwa ngumu kwa vile
kila mmoja amejiandaa kuhakikisha anafanya vizuri.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari leo, makocha wote
waliezea ubora wa wapinzani wao, lakini wakasisitiza kuwa wanaingia uwanjani
kuhakikisha wanashinda ili kujiweka katika mazingira mazuri kwa ajili ya mechi
ya marudiano itakayochezwa Kampala wiki mbili zijazo.
Kim alisema Uganda ndiyo inayoongoza kwa ubora wa
viwango vya FIFA katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo ni
changamoto kwao ingawa wachezaji wake tayari wamejipanga vizuri kwa ajili ya
mechi hiyo.
Naye Micho aliyefuatana na nahodha wake Hassan Wasswa
alisema Taifa Stars imekuwa ikifanya vizuri tangu iwe chini ya Kim, na itakuwa
na wachezaji tisa wa kikosi cha kwanza kinachocheza mechi za mchujo za Kombe la
Dunia wakati kwa upande wake atakuwa na wachezaji wawili tu.
Boniface
Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Julai 12, 2013
No comments:
Post a Comment