Hakuna shaka taifa la Brazil
linaanza kurudisha ufalme wa soka miguuni mwa wachezaji wao baada ya mwishoni
mwa wiki iliyopita kutwaa taji la mashindano ya mabara yaliyofanyika nchini
humo kwa kuwafunga Hispania 3-0.
Kwa muda mrefu Brazil imekuwa
ikifanya vibaya katika michuano mikubwa ya soka hasa walipokuja Afrika kwa
michuano ya kombe la dunia 2002 nchini Afrika Kusini, wachambuzi wa soka
wakaanza kutabiri mwisho wa soka la Brazil na kutupa turufu ya kwa Ujerumani na
Hispania.
Lakini kufanya vibaya kwa timu za
Hispania kwenye kombe la mabingwa barani Ulaya dhidi ya timu za Ujerumani
kuliamsha hisia kuwa Ujerumani inaweza kuchukua nafasi ya Brazil, lakini baada
ya kombe la mabara kufikia hatua ya nusu fainali kila mtu akaanza kuamini
Hispania imedhamiria, kilichotokea wakati wa fainali katika kiwanja cha
Maracana jijini Reo De Jeneiro ni kilio kwa walioichukia Brazil.
Mabao mawili ya Frederico Chaves
Guedes ‘Fred’ na moja la mshambuliaji aliyekuwa gumzo katika michuano hiyo
Neymar Junior, yaliwamaliza nguvu wachezaji wa Hispania kiasi Sergio Ramos wa
Hispania kushindwa kufunga penati katika kipindi cha pili.
Ambaye ameshuhudia fainali ile
lazima ataafiki kuwa Brazil waliutawala mchezo kwa dakika zote tisini kama hiyo
haitoshi walionekana kama wanacheza na wadogo zao tena kwenye mechi ya
kirafiki, Hispania hawakuonyesha uhai kabisa waliangusha matarajio ya mashabiki
wengi usiku ule.
Historia pia ilimkandamiza kocha wa
Hispania Vicente Del Bosque kwani Brazil hawajawahi kupoteza hata mechi moja ya
kiushindani katika ardhi yao tangu mwaka 1975 walipofungwa na Peru katika
michuano ya Copa America.
Aidha tangu mwaka 1934 Hispania
wamefanikiwa kuwafunga Brazil mechi mbili tu katika mechi tisa walizokutana
ambapo mwaka 1934 walipokutana kwenye kombe la dunia nchini Italia, Brazil
walilala kwa mabao 3-1 na mwaka 1990 katika mechi ya kimataifa Brazil walilala
kwa mabao 3-0 kwa hiyo ni kama Brazil wamejibu mapigo ya mwaka 1990.
Katika hatua nyingine Brazil pia
imeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kuwafunga Hispania katika mechi ya
ushindani tangu mwaka 2010, ambapo Hispania imecheza mechi 29 bila kufungwa na
taifa lolote mpaka jumapili iliyopita walipotulizwa na Brazil.
Wazungu wanasema: For Brazil, the
party has only just begun.
HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
July 3, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA
No comments:
Post a Comment