Friday, July 19, 2013

Kivuli cha Maximo bado kinaishi Tanzania 
Mpaka sasa hakuna mtanzania mpenda michezo anayeweza kuingia uwanja wa Taifa kuangalia mechi ya Taifa Stars huku anakula pop corn ‘bisi’.
Ni kuwa bado hatukiamini kikosi chetu kufanya vizuri hata kwa michuano midogo ya Afrika Mashariki ama hii kampeni inayoendelea ya kushiriki kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani .
Wapo watu wanaoamini tatizo ni kocha, na wapo wanaoshikilia misimamo ya siasa za soka ndizo zinazoharibu soka la Tanzania. Wote wanaweza kuwa sahihi na wote wanaweza wasiwe sahihi kwa sababu tofautitofauti.
Binafsi bado naamini soka la Tanzania litapewa heshima na vijana ambao kwa sasa wana miaka kumi kushuka chini. Wao ndiwo wanaoona kiu na hamu ya watanzania kutaka kupaa katika nafasi za FIFA za kidunia.
Na hapo ndipo dhana ya kuamini kivuli cha kocha wa zamani wa Taifa Stars mbrazil Marcio Maximo, bado kinaishi Tanzania. Wakati anaanza kampeni ya kuwapa nafasi vijana na kuweka wazi kwa viongozi wa soka kuwa hawa ndiwo watakaowapa furaha, kila mmoja alimpinga na kumuona ameishiwa.
Lakini ndiye kocha aliyethubutu kushikilia msimamo wake wa kuibua vipaji vya vijana hata timu za chini ya miaka 17 zikaanza kuangaliwa kwa jicho la ‘jiko’ linalopika wachezaji wa Taifa Stars. Lakini ni baada ya kutukanwa na kudhalilishwa sana ndipo wapenzi wa soka wakaanza kuafiki sayansi yake.
Wapo wachezaji waliopatikana kupitia kampeni ya Maximo kama Jerry Tegete na Mrisho Ngasa, leo hii wanaheshimika sana ingawa hata baada ya kuondolewa Maximo mawazo yake yakawa yanafanyiwa kazi lakini si kwa kiasi kikubwa kama ambavyo angefanya yeye.
Maneno ya ucheshi ya mwanamichezo na mtangazaji wa kituo kimoja cha Radio na TV, Mbwiga wa Mbwiguke  yana maana kubwa zaidi ya kuchekesha  anasema mchezo wa soka ni sawa na mnazi unaupanda leo unakuja kuvuna nazi baada ya miaka mitano ama kumi.
Maximo ndiye aliyesisitiza wachezaji wadogo watiliwe maanani, ndiye aliyetoa wazo la kuwapeleka ziarani wachezaji wa Taifa Stars mpaka akakejeliwa kuwa ndiye kocha wa kwanza kuweka wachezaji kambini kwa zaidi ya miezi mitatu. Lakini lengo lake ni kuwatoa taka za macho wachezaji  ili siku watakapokutana na timu za mabara mingine yaliyoendelea kisoka wasiwe na wasiwasi.
Na ndiyo maana tuliwahi kupata sifa za ‘kijinga’ kuwa timu ya kwanza duniani kuvunja mwiko wa kutikisa nyavu za Brazil ambayo ilikuwa njiani kuelekea Afrika Kusini kushiriki kombe la dunia ingawa tulifungwa mabao mengi lakini tulifanikiwa kumfanya golikipa mahiri wa timu hiyo ya dunia kuokota mpira wavuni japo mara moja.
Watanzania wasihuzunishwe na matokeo mabaya ya timu yao bali wazingatie sana kuwapa furaha wajukuu wao, yaani wakubali kuumia sasa lakini wawape furaha watanzania watakaokuja baada ya miaka 20.
Kama ambavyo tunaona timu za Afrika magharibi ziliwekeza katika soka, Maximo akirudi leo nitaishawishi TFF imkabidhi timu ya vijana tena wa miaka 17 aisuke vilivyo, tofauti na sasa kocha mkuu wa Taifa Stars anakuwa na majukumu mawili ya kuangalia timu ndogo na kubwa.
Soka ni taasisi lazima iende kwa mipango, kuna michuano mingi sana ya vituo vya soka ‘Soccer Academy’ ambayo inaisha na mshindi anapatikana timu kubwa zinagombania baadhi ya wachezaji wanacheza misimu miwili kwisha habari yao, bila TFF kufikiria namna bora ya kuwatumia watoto wale. Tuanze sasa kujitoa mhanga kwa ajili ya furaha ya wajukuu wetu.
HAFIDH KIDO
KIDOJEMBE
19 JULAI, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA 

No comments:

Post a Comment