Bi Zamaradi Kawawa (aliyesimama) ambaye ni naibu Mkurugenzi wa idara ya habari MAELEZO akiwafafanulia wanahabari juu ya baadhi ya majibu yaliyokanganya kutoka TRL.
Mkurugenzi mtendaji wa TRL, mhandisi Kipallo Aman Kisamfu amesema
wanataka kuhakikisha ifikapo mwaka 2015 shirika hilo liwe na uwezo wa
kusafirisha tani milioni 3 za mizigo kwa mwaka.
Akizungumza katika ukumbi wa idara ya habari MAELEZO jijini
Dar es Salaam leo asubuhi Kisamfu amesema Serikali imeamua kuuweka usafiri wa
reli katika vipaumbele vya taifa vilivyowekwa katika mpango wa taifa wa miaka
mitano unaoanzia 2011-2016.
“Mpango huu wa taifa umeongezewa nguvu kupitia mpango
mwingine wa miaka mitatu ambao ni mfumo mpya wa kusimamia utekelezaji,
ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo. Mpango huu umeanza kutekelezwa
kwa kutumia uzoefu wa ‘Performance Management and Delivery Unit’ (PEMANDU)
kutoka Malaysia.
“Katika mpango wa PEMANDU ambao unaendana na program ya
matokeo makubwa ya haraka (Big Results now ‘BRN’), TRL imepanga kusafirisha
mizigo kiasi cha tani milioni 3 kwa mwaka ifikapo mwaka 2015. Kiasi hiki ni
kikubwa ambacho hakijawahi kusafirishwa na reli ya kati tangu ilipojengwa miaka
mia moja iliyopita,” alisema KIsamfu.
Aidha katika bajeti ya Serikali mwaka wa fedha 2013/14 TRL
imetengewa Sh Bil 137.6 ili kukamilisha miradi iliyokwishaanza kupitia bajeti
ya mwaka jana. Miradi itakayokamilika kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14
ni pamoja nah ii ifuatayo: Kutengeneza upya vichwa vya treni 8, kununua vuchwa
vipya 13, kununua mabehewa mapya ya abiria 22, kununua mabehewa mapya ya mizigo
274, kununua mabehewa ya kubebea kokoto 25, kununua mabehewa ya breki 34, kununua mashine moja ya kushindilia
kokoto kwenye reli, na kupata kreni moja yenye uwezo wa tani 100 ya kunyanyulia
mabehewa na vichwa vya treni zinapotokea ajali.
Hata hivyo kwa mujibu wamkurugenzi mtendaji huyo wa TRL
mradi wa miaka mitatu wa kuiinua TRL unahitaji kiasi cha Sh trilioni 1.1 ili
kununua vichwa vipya vya treni 58, mabehewa ya mizigo 1960, mabehewa ya abiria
44 lengo likiwa ni kupata uwezo wa kubeba mizigo ya tani milioni 3 kwa mwaka
ifikapo mwaka 2015.
HAFIDH KIDO
9 Julai, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA
No comments:
Post a Comment